Assallaam Aleykum WarahmatulLaah Wabarakatuh
Kufunga mwezi wa Ramadhwaan ni moja katika nguzo za Dini yetu ya Kiislamu na moja katika mambo ya lazima yampasayo kila Muislamu. Allaah (Subhanahu wa Ta’ala) Anasema:
يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا كُتِبَ عَلَيْكُمُ الصِّيَامُ كَمَا كُتِبَ عَلَى الَّذِينَ مِن قَبْلِكُمْ لَعَلَّكُمْ تَتَّقُونَ
“Enyi mlioamini! Mmeandikiwa Swawm kama ilivyoandikwa kwa wale ambao wa kabla yenu mpate kuwa na taqwa.” [Suwratul Baqarah 02: 183].
Baada ya Aayah hii Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala) Anasema tena:
شَهْرُ رَمَضَانَ الَّذِيَ أُنزِلَ فِيهِ الْقُرْآنُ هُدًى لِّلنَّاسِ وَبَيِّنَاتٍ مِّنَ الْهُدَى وَالْفُرْقَانِ فَمَن شَهِدَ مِنكُمُ الشَّهْرَ فَلْيَصُمْهُ وَمَن كَانَ مَرِيضًا أَوْ عَلَى سَفَرٍ فَعِدَّةٌ مِّنْ أَيَّامٍ أُخَرَ يُرِيدُ اللّهُ بِكُمُ الْيُسْرَ وَلاَ يُرِيدُ بِكُمُ الْعُسْرَ وَلِتُكْمِلُواْ الْعِدَّةَ وَلِتُكَبِّرُواْ اللّهَ عَلَى مَا هَدَاكُمْ وَلَعَلَّكُمْ تَشْكُرُونَ
“Mwezi wa Ramadhwaan ambao imeteremshwa humo Qur-aan ili iwe Hudan (Uongofu) kwa watu na hoja bayana za Al-Hudaa (Uongofu) na Al-Furqaan (Upambanuzi). Basi atakayeshuhudia miongoni mwenu mwezi na afunge. Na atakayekuwa mgonjwa au safarini basi (atimize) idadi katika siku nyinginezo. Allaah Anakutakieni mepesi na wala Hakutakieni magumu; ili mkamilishe idadi na ili mumkabbiri Allaah (mseme: Allaahu Akbar) kwa kukuhidini na mpate kushukuru..” [Suwratul Baqarah 02: 185].
Ibn ´Umar (Radhiya Allaahu ´anhuma) alimsikia Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa Sallam) akisema:
“Uislamu umejengewa katika (nguzo) tano: Kuthibitisha kidhati kuwa hakuna Mola apasae kuabudiwa kwa Haqq ila Allaah, na kuthibitisha kidhati kuwa Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa Sallam) ni Mtume Wake, kusimamisha Swalah, kutoa Zakaah, kutekeleza ´Ibaadah ya Hajj kwa mwenye uwezo, na kufunga mwezi mtukufu wa Ramadhwaan.”[Imeripotiwa na Al-Al-Bukhaariy na Muslim].
Waislamu wote wamekubaliana kuwa kufunga mwezi wa Ramadhwaan ni wajibu wa kila Muislamu na kuwa ni moja katika (nguzo) za Uislamu na ni jambo lenye kujulikana katika Dini yetu kwa kutekelezwa kwake. Yeyote atakayekanusha ´Ibaadah hii ya Kufunga mwezi wa Ramadhwaan kuwa si wajibu kwa kila Muislamu atakuwa amekufuru Kufru ambayo inamtoa katika Uislam.
Uzuri Wa Kutekeleza ´Ibaadah Ya Kufunga Mwezi Wa Ramadhwaan
Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu ´anhu) alimsikia Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa Sallam) akisema:
“Yeyote atakayefunga mwezi wa Ramadhwaan kwa Imani na kutarajia malipo kutoka kwa Allaah basi Allaah Atamsamehe madhambi yake yote yaliyopita.” [Imeripotiwa na Al-Al-Bukhaariy na Muslim, An-Nasaaiy na Ibn Maajah].
Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu ´anhu) amesema tena, alimsikia Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa Sallam) akisema:
“Allaah amesema: “Kila ‘Amali ya mwanaadam ni yake yeye mja Wangu ila Swawm. Ni yangu Mimi na mimi ndiye Nitakayemlipa mja Wangu.”
Swawm ni kinga. Itakapofikia siku mmoja wenu amefunga ajiepushe na kufanya kitendo cha jimai na mabishano na watu. Na yeyote atakayetaka kupigana naye basi amwambie “Mimi nimefunga.” Naapa kwa jina la Allaah, Harufu inayotoka katika mdomo wa mwenye kufunga ni nzuri kwa Allaah kuliko harufu ya Misk. Kwa Mwenye kufunga ana furaha mbili: Furaha anapofungua Swawm yake na furaha pale atakapoonana na Mola Ameridhika kwa kufunga kwake.” [Imeripotiwa na Al-Al-Bukhaariy na Muslim na An-Nasaaiy]
Sahl ibn S’ad (Radhiya Allaahu ´anhu) alimsikia Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa Sallam) akisema:
‘’Peponi kuna mlango unaitwa Ar-Rayyaan. Wale wenye kufunga wataingia peponi kupitia lango huu siku ya Qiyaamah na hakuna mwengine atakayepita katika mlango huu ila (wafungaji). Itaambiwa: ‘’Wako wapi waliokuwa wakifunga?” Watasimama na watapita katika mlango huu na watakapomalizika kuingia wote (wafungaji) utafungwa na hakuna mwengine atakayepita hapo tena.“ [Imeripotiwa na Al-Al-Bukhaariy na Muslim, At-At-Tirmidhiy, Ibn Maajah na An-Nasaaiy].
Kufunga Mwezi Wa Ramadhwaan Ni Wajibu Pale Mwezi Unapoonekana
Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu ´anhu) amemsikia Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa Sallam) akisema:
“Fungeni kwa kuona au kuandama mwezi wa Ramadhwaan na fungueni (malizeni) kufunga mwezi wa Ramadhwaan kwa kuona mwezi na msipouona mwezi basi timizeni siku thelathini.” [Imeripotiwa na Al-Al-Bukhaariy, Muslim, na An-Nasaaiy].
Mwezi Wa Ramadhwaan Unathibitishwaje Kuonekana Kwake?
Mwezi wa Ramadhwaan unathibitishwa kuonekana kwake na mtu mmoja mwenye kujulikana kwa ukweli na kumcha kwake Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) au kwa kutimiza siku thelathini za mwezi wa Sha’abaan.
Ibn ´Umar amesema watu walikuwa wakitafuta kuandama kwa mwezi. nikamjulisha Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa Sallam) kuwa mimi nimeuona mwezi. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa Sallam) akafunga na akaamrisha watu wafunge.” [Hadiyth Swahiyh. Angalia Kitaab I’rwa al-Ghaliyl na. 908 na Imeripotiwa na Abu Daawuwd].
Ikiwa mwezi haukuandama, kwa sababu ya kufunikwa na mawingu au kwa sababu nyingine basi hapo mwezi wa Sha’abaan utatimizwa kwa siku thelathini kama alivyoripoti Abu Hurayrah katika Hadiyth iliyo hapo juu.
Lakini mwezi wa Shawwaal unatangazwa kuonekana kwa mashahidi wawili.’ ´Abdur-Rahmaan bin Zayd bin Al-Khattwaab amesema: “Nilipokuwa nikikhutubia siku ambayo ni ya shaka (kama mwezi wa Ramadhwaan kama umekwisha ama la), nikasema: “Nilikaa na Maswahaba zake Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa Sallam) nikawauliza wao. Wakaniambia mimi kuwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa Sallam) alisema:
‘’Fungeni kwa kuonekana mwezi na fungueni kwa kuonekana mwezi na tekelezeni ´Ibaadah ya Hajj kwa haki zake. Ikiwa kuna mawingu basi timizeni siku thelathini. Na Ikiwa Waislamu wawili watachukua kiapo kwa kuonekana kwa mwezi basi fungeni na mfungue kwa kushuhudia kwao mwezi.’’ [Hadiyth Swahiyh. Angalia Kitaab cha Shaykh Al-Albaaniy, Swahiyh al-Jamiy’ Asw-Swaghiyr na. 3811. Pia Imeripotiwa na Imaam Ahmad na An-Nasaaiy bila kipande kinachosema ‘’Waislamu wawili.’’].
Mtawala wa Makkah, Al-Haarith bin Hatwiyb amesema:
“Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa Sallam) alituambia sisi tekelezeni ´Ibaadah ya Hajj kwa haki zake munapouona mwezi. Na ikiwa hamkuuona mwezi lakini mashahidi wawili wa kuaminika wakishuhudia kwa kuona mwezi tunatekeleza ´Ibaadah ya Hajj kutokana na ushahidi wao.’’ [Hadiyth Swahiyh angalia Shaykh Al-Albaaniy, Swahiyh Sunan Abiy-Daawuwd, na. 205. Imeripotiwa na Abu Daawuwd].
Tukiangalia ripoti mbili hizi,
’’Ikiwa waislamu wawili watachukua kiapo kwa kuona mwezi, basi fungeni na fungueni’’ katika Hadiyth ya Abdur-Rahmaan bin Zayd na:
‘’Na ikiwa hamkuuona mwezi lakini watu wawili wenye kujulikana kwa ukweli wakasema wameuona mwezi tunatimiza haki za ´Ibaadah ya Hajj kutokana na ushahidi wao.’’ katika Hadiyth ya Al-Haarith wanaonyesha kwa kutilia mkazo, kuwa haifai kuanza kufunga au kumaliza kufunga kutokamana na ushahidi wa mtu mmoja pekee. Juu ya hilo, tangu kuanza kwa kufunga imeondolewa uzito kutokana na ushahidi (uliotolewa hapo juu), inawacha suala la kumaliza kufunga, ambalo halina ushahidi kwamba linatoshelezwa kwa ushahidi wa mtu mmoja pekee. Huu ni ufupi wa mjadala unaopatikana katika Kitabu ‘Tuhfah Al-Ahwadhiy’ [Mjalada wa 3, uk. 373-3749].
Tanbihi: Ikiwa mtu atauona mwezi yeye peke yake, hafungi mpaka watu wafunge na hamalizi kufunga mpaka watu wamalize kufunga kama ilivyoripotiwa na Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu ´anhu), kwamba amesema Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa Sallam):
‘’Swawm (kufunga) ni siku ambayo watu wanafunga. Na kumaliza kufunga ni siku ambayo watu wanamaliza kufunga. Na kuchinja ni katika siku ambayo watu wanachinja.’’ [Hadiyth Swahiyh. Angalia Swahiyh Al-Jami’ Asw-Swaghiyr, na. 3869]. Imehifadhiwa na Imaam At-At-Tirmidhiy ambaye amesema: ‘’Baadhi ya Maulamaa wanaifasiri Hadiyth hii kwa maana: “Kuanza kufunga na kumaliza kufunga kunatekelezwa na watu wote kwa pamoja na wakati mmoja.”
Nani Anawajibika Kufunga
Maulamaa wamekubaliana kufunga ni wajibu kwa mwenye akili timamu, Baleghe, mwenye afya na mkazi wa mji. Tukiongezea wanawake waliotwaharika na hedhi na nifasi.
Kwa wale ambao Swawm si wajibu juu yao ni wale ambao hawana akili timamu, hawajabaleghe.
Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa Sallam) amesema:
“Kalamu (kurekodiwa ‘amali) imeinuliwa (hairekodi) kwa watu watatu: anayepatwa na usingizi mpaka aamke, mtoto mpaka afike umri wa kubaleghe, na aliorukwa na akili mpaka atakapopata akili timamu.”[Hadiyth imesahihishwa na Shaykh Al-Albaaniy katika Swahiyh Al-Jami´, na. 3513 na Imerikodiwa na Abu Daawuwd].
Ama kwa wale wasioweza kufunga ni kutokamana na maneno Yake Allaah:
فَمَن شَهِدَ مِنكُمُ الشَّهْرَ فَلْيَصُمْهُ وَمَن كَانَ مَرِيضًا أَوْ عَلَى سَفَرٍ فَعِدَّةٌ مِّنْ أَيَّامٍ أُخَرَ
“Basi atakayekuwa mgonjwa miongoni mwenu, au yuko safarini (akafunga baadhi ya siku); basi (akamilishe) idadi (ya siku anazotakiwa kufunga) katika siku nyinginezo.” [Suwratul-Baqarah 02: 184].
Ikiwa mgonjwa au msafiri atafunga basi inawatosheleza, ama wakichukua ruhsa ya kula hapo wameondolewa uzito. Ama wakiamua kufunga kwa kuwa wanataka kufunga hapo pia wako sawa.
Ni kupi bora: Kutofunga au Kufunga?
Ikiwa mgonjwa au msafiri hawatoona tabu yoyote katika kufunga, basi kufunga kunapendekezwa. Ama wakikhofia kupata tabu kutokamana na kufunga, basi hapo kutofunga kunapendekezwa.
Abu Sa’iyd al-Khudriy ameelezea:
‘’Tulikuwa vitani na Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa Sallam) wakati wa Ramadhwaan. Wengine katika sisi walikuwa wamefunga na wengine walivunja Swawm zao. Wale waliofunga hawakuwaona waliovunja Swawm zao kuwa wako makosani na waliokula pia hawakuwaona waliofunga kuwa wako na makosa. Waliona wenye uwezo wa kufunga (walifunga) na hilo ni jambo zuri. Na ambao hawakuweza kufunga walivunja Swawm zao kwa udhaifu wa kufunga (hawakufunga) na hili pia ni jambo zuri.’’ [Imesahihishwa na Shaykh Al-Albaaniy katika Swahiyh Sunan At-At-Tirmidhiy na. 574. Pia imerikodiwa na Imaam Muslim].
Ushahidi wa wanawake wasio Twahara kuwa hawafungi ni Hadiyth ya Abu Sa´iyd ambayo Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa Sallam) amesema:
’’Je, si kwa kesi kwamba anapopatwa na damu yake ya mwezi, haswali wala hafungi? huo ni upungufu katika Dini yake.’’ [Imesahihishwa na Shaykh Al-Albaaniy, katika Mukhtaswar Swahiyh Al-Al-Bukhaariy na. 951. Imerikodiwa na Imaam Al-Al-Bukhaariy].
Ikiwa mwanamke asiyo Twahara atafunga basi swawm yake haikubaliki kwani katika masharti ya kukubalika swawm ya mwanamke ni awe katika Twahara. Mwanamke pia itamlazimu alipe siku alizokosa kufunga. ´Aaishah (Radhiya Allaahu ´anhu) amesema:
“Tulipokuwa tukipatwa na siku zetu za ada wakati wa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa Sallam) tuliamrishwa kulipa Swawm za siku tuliokosa kufunga na hatukuamrishwa kulipa Swalah tulizokosa.’’ [Imesahihishwa na Shaykh Al-Albaaniy katika Swahiyh Sunan At-Tirmidhiy na.630. Imerikodiwa na Imaam Muslim, Abu Dawuud, At-Tirmidhiy na An-An-Nasaaiy].
Yanayomlazimu Mtu Mzima Na Mwenye Ugonjwa Wa Kuendelea
Asioweza kufunga, kwa ajili ya utu uzima au kwa ajili sababu nyenginezo, hatofunga badili yake atalisha maskini mmoja kwa kila siku aliokosa kufunga. Allaah (Subhanahu wa Ta’ala) Amesema:
وَعَلَى الَّذِينَ يُطِيقُونَهُ فِدْيَةٌ طَعَامُ مِسْكِينٍ
“Na wale wasioweza, watoe fidiya kwa kumlisha masikini. (kwa kila siku).”(Suuratul Baqarah 02 : 184)
‘Atwaa’ amesema alimsikiya Ibn ´Abbaas akisoma Aayah hii kisha akasema ‘’Haikuondolewa. Inawahusu watu wazima waume kwa wake ambao hawawezi kufunga. Ndio watalisha masikini mmoja kwa kila siku ambayo hawakufunga.” [Imesahihishwa na Shaykh Al-Albaaniy katika I’rwa al-Ghaliyl na.912 na Imerikodiwa na Imaam Al-Bukhaariy].
Mwanamke Mja Mzito (Mwenye Mimba) Au Mwenye Kunyonyesha
Mwanamke mwenye mimba au mwenye kunyonyesha ambaye hana uwezo wa kufunga ama ambaye anahofia afya ya mtoto wake anaweza asifunge, atalisha maskini mmoja na hawajibiki kuilipa siku aliyokula. Ibn ´Abbaas amesema:
“Ruhusa amepewa mtu mzima mume au mke ambapo wataoneleya tabu kufunga, hawatofunga ambapo hawatopendeleya kufunga na watalisha maskini mmoja kwa kila siku ya kufunga. Kisha hawatalipa siku walizokosa kufunga hii iliondolewa baada ya Aayah hii:
وَعَلَى الَّذِينَ يُطِيقُونَهُ فِدْيَةٌ طَعَامُ مِسْكِينٍ
“Na wale wasioweza, watoe fidiya kwa kumlisha masikini. (kwa kila siku).”(Suuratul Baqarah 02 : 184)
Baada ya hapo ikahakikishwa kuwa mtu mzima mume au mke ambao hawawezi kufunga na mwanamke mwenye mimba au mwenye kunyonyesha, ikiwa watahofia, hawatafunga na watalisha maskini kwa kila siku ambayo hawakufunga. [Msururu wa Riwaayah hii ni madhubuti imeripotiwa na Al-Bayhaqiy]. Pia imerikodiwa kuwa alisema, ikiwa wakati wa Ramadhwaan mwanamke mwenye mimba anahofia afya yake, au mwenye kunyonyesha anahofia afya ya mtoto wake, hawatafunga na watalisha maskini mmoja kwa kila siku ambayo hawakufunga na hawatalipa siku hizo kwa kufunga. [Imesahihishwa na Shaykh Al-Albaaniy katika I’rwa al-Ghaliyl mjallad 4 uk.19].
Nafi’iy alisema ‘’Mmoja katika mabanati wa Ibn ´Umar aliolewa na mwanamume wa ki-Quraysh. Akapata mimba na wakati wa Ramadhwaan anashikwa na kiu sana. Ibn ´Umar akamwambiya funguwa swawm yako na ulishe masikini kwa kila siku.’’[Msururu wa Riwaayah ni Swahiyh na Imesahihishwa na Shaykh Al-Albaaniy katika I’rwa al-Ghaliyl mjallad 4 uk.20. Imerikodiwa na ad-Daraqutniy].
Kiwango gani cha chakula anawajibika kulisha?
Imeelezwa kwamba Anas Ibn Malik alidhoofika sana na hakuweza kufunga mwaka mzima akatayarisha sufuriya THARIYD (Mkate na nyama uliolowana katika supu) kisha akaalika masikini thelathini akawalisha mpaka wakaridhika’’. [Msururu wa Riwaayah hii ni Swahiyh pia imesahihishwa na Shaykh Al-Albaaniy katika I’rwa al-Ghaliyl, mjallad 4 uk.21 imerikodiwa na ad-Daraqutniy].
Yaliyo Muhimu Kwa Ujumla Wa Kutekeleza ´Ibaadah Ya Swawm (Kufunga)
1. Niyyah.
Allaah (Subhanahu wa Ta’ala) Amesema:
وَمَا أُمِرُوا إِلَّا لِيَعْبُدُوا اللَّهَ مُخْلِصِينَ لَهُ الدِّينَ حُنَفَاء وَيُقِيمُوا الصَّلَاةَ وَيُؤْتُوا الزَّكَاةَ وَذَلِكَ دِينُ الْقَيِّمَةِ
“Nao hawakuamrishwa kitu ila wamuabudu Allaah kwa kumtakasia Dini, wawe waongofu, na washike Swalah, na watoe Zakaah. Na hiyo ndiyo Dini madhubuti.” (Suuratul Bayyinah 98 : 05)
Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa Sallam) amesema:
’’Kila kitendo hulipwa (kutokana na) niyyah na kila mtu ni lili alilonuwiya.’’
Na niyyah mahala pake ni moyoni. Niyyah ya kufunga ni lazima iwe moyoni kila usiku kabla ya wakati wa Fajr kuingiya.
Hafsah (Radhiya Allaahu ´anha) amesema mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa Sallam) amesema:
‘’Hana swawm asiyenuwia kufunga kabla ya fajr.’’ [Imesahihishwa na Shaykh Al-Albaaniy katika Swahiyh al-Jamiy´ as-Saghiyr, na.6238. Pia imerikodiwa na Abu Dawuud, At-Tirmidhiy na An-Nasaaiy].
2. Kujiepusha katika masiku ya kuamka na swawm na chochote chenye kubatilisha swawm yako (tangu wakati wa adhaana ya pili) na usiku mpaka kutakapopambauka (Jua kuchomoza).
Amesema Allaah (Subhanahu wa Ta’ala):
وَكُلُواْ وَاشْرَبُواْ حَتَّى يَتَبَيَّنَ لَكُمُ الْخَيْطُ الأَبْيَضُ مِنَ الْخَيْطِ الأَسْوَدِ مِنَ الْفَجْرِ ثُمَّ أَتِمُّواْ الصِّيَامَ إِلَى الَّليْلِ
“Na kuleni na kunyweni mpaka ubainike kwenu weupe wa alfajiri katika weusi wa usiku. Kisha timizeni swawm mpaka usiku.” (Suuratul-Baqarah: 187).
Mambo Sita Yanayobatilisha Swawm
1. na 2. Kula au kunywa kwa kukusudia.
3. Kujitapisha kusudi.
4. na 5. Mwanamke atakapopata ada yake mwezi akiwa katika swawm.
6. Kitendo cha Jimai.
Mambo Yaliyopendekezwa Kwa Mwenye Kufunga
Imependekezwa kwa mwenye kufunga afuate Sunnah za Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa Sallam) katika kujitayarisha na swawm yake nayo ni haya yafuatayo;
1. Kula daku
Amehadithia Anas (Radhiya Allaahu ´anhu) Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wasallam) amesema:
‘’Kuleni daku, kwani kula huko daku kuna baraka.” [Imeripotiwa na Imaam Al-Bukhaariy, Muslim, At-Tirmidhiy na Nasaa’y na Ibn Maajah].
Na ‘’kuleni daku’’ hata kama kwa kunywa maji inatosheleza. ´Abdullaah Ibn ´Amr amehadithia Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa Sallam) amesema:
’’Kuleni daku japo kwa kunwa tama la maji.’’ [Imesahihishwa na Shaykh Al-Albaaniy katika Swahiyh al-Jamiy´ as-Swaghiyr na.2945 imeripotiwa na Ibn Hibbaan].
Pia Imependekezwa kuchelewesha kula daku. Amehadithiya Anas kutoka kwa Zayd ibn Thabit ambaye amesema:
‘’Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa Sallam) alikula daku kisha akatoka kwenda kuswali. Anas akamuuliza “Kulikuwa na muda gani baina chakula cha daku na adhaana?” Akajibu: “Ilikuwa kiasi cha kusoma Aayah khamsini za Qur-aan". [Imeripotiwa na Imam Al-Bukhaariy na Muslim].
Pia ameruhusiwa amalize chakula chake anaposikia Adhaana ya Fajr. Abu Hurayrah amehadithia Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa Sallam) amesema:
“Endapo mmoja wenu atasikiya adhaana na mkononi mwake ana kinywaji, asirudishe kinywaji hicho mpaka aridhike nacho.’’[yaani anywe mpaka amalize haja yake].[Imesahihishwa na Shaykh al-Albaaniy katika al-Jami' as-Swaghiyr na.607].
2. Kujiepusha na maneno ya Upuuzi na mambo yasofaidisha Swawm yako.
Amehadithia Abu Hurayrah Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa Sallam) amesema:
’’Ikiwa mmoja wenu yuko ndani ya swawm ajiepushe na kitendo cha jimai na mabishano. Na kukitoka mmoja anataka kupigana nawe basi mwambiye ‘’Mimi Nimefunga’’.[Imeripotiwa na Imaam Al-Bukhaariy na Muslim na An-Nasaaiy]. Tena amehadithiya Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa Sallam) amesema:
’’Yeyote ambaye hatowacha kusema uongo na kutenda kwa uongo basi Allaah (SubhanaHu wa Ta’ala) hana haja yake kwa kuwacha chakula chake na kinywaji chake’’. [Imesahihishwa na Shaykh Al-Albaaniy katika mukhtasar Swahiyh Al-Al-Bukhaariy na.921].
3. Kuwa na moyo kutoa na kujifunza Kusoma Qur-aan
Ibn ´Abbaas amesema: ’’Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa Sallam) alikuwa mwenye moyo wa kutoa mali katika watu wote na akifanya vizuri kabisa. Alikuwa akitoa zaidi katika mwezi wa Ramadhwaan anapoonana na Malaika wa Allaah Jibriyl (´alayhis-Salaam). Jibriyl anaonana naye kila usiku wa Ramadhwaan mpaka mwezi umalizike. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa Sallam) atasoma naye Qur-aan. Anapoonana na Jibriyl, alikuwa na moyo zaidi wa kufanya mema kuliko kuifadisha swawm yake’’. [Imeripotiwa na Imaam Al-Bukhaariy na Muslim].
4. Kukimbilia (kuharakisha) kufungua swawm
Sahl Ibn Sa'd amehadithiya Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa Sallam) amesema:
’’Watu watakuwa katika kheri endapo watakimbilia kufungua swawm zao’’.
5. Kufungua Swawm na yale yaliotajwa katika Hadiyth ikiwa ni rahisi kufanya hivo.
Anas amehadithia Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa Sallam) alikuwa akifunguwa swawm yake na Tende zilioiva kabla kusali. Kama si zilioiva alikuwa akifungua na Tende kavu. Kama hiyo pia haikupatikana basi alikuwa akifunguwa na kinywaji cha maji. [Ni Hadiyth Hasan Swahiyh katika al-Jamiy´ as-Swaghiyr na.2065]
Mambo Yanayofaa Kufanywa Na Mwenye Kufunga
1. Anaruhusiwa kujisuuza kichwa na maji ya baridi.
2. Kusukutua na maji bila kuyamiza na kutiya maji puani bila kuingiya ndani ya mwili.
3. Kuumikwa ama kutoa damu kwa ajili ya matibabu.
4. Kumbusu au kumgusa mke wako bila matamanio kwa mwenye kuweza kujizuwiya.
5. Mwenye kuamka asubuhi na akiwa katika janaba.
6. Kuchelewesha kufungua swawm mpaka saa ya kula daku.
7. Kutumia mswaki, manukato, wanja, dawa ya macho na kudungwa sindano kwa ajili ya matibabu.
Na Allaah anajua zaidi
http://bit.ly/2UJhYac i live islam
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni