Swali 01: Ni jambo linalojulikana kwamba mgonjwa baada ya kufanyiwa operesheni anabaki katika hali ya kutokuwa na fahamu mpaka pale atapoamka. Baada ya hapo anabaki akiwa na maumivu kwa masaa kadhaa. Je, aswali kabla ya kufanyiwa operesheni ilihali wakati bado hujaingia au acheleweshe swalah mpaka pale atapokuwa na uwezo wa kuiswali akiwa amehudhurisha hisia hata kama hayo yanaweza kuchukua zaidi ya siku moja?
Jibu: Kwanza ni lazima kwa madaktari kulitazama jambo hili. Wakiweza kuchelewesha upasuaji mpaka ukaingia kwa mfano wakati wa swalah ya Dhuhr na hivyo mgonjwa akaweza kuswali Dhuhr pamoja na ´Aswr kwa kuksuanya kipindi cha wakati wa swalah ya Dhuhr. Kadhalika wakati wa jioni aswali Maghrib na ´Ishaa kwa pamoja pindi jua litakapozama kabla ya kuanza operesheni. Ama operesheni ikiwa wakati wa asubuhi basi mgonjwa ni mwenye kupewa udhuru. Atakapoamka basi atatakiwa kulipa zile swalah anazodaiwa hata kama ni baada ya siku moja au mbili. Punde tu atakapopata fahamu basi atapaswa kulipa zile swalah anazodaiwa na hakuna dhambi juu yake. Ni kama mfano wa mwenye kulala akiamka, akazindukana na fahamu zake zikarudi basi ataswali vile vipindi vilivyompita kwa mpangilio Dhuhr, ´Aswr na nyenginezo mpaka alipe zile swalah anazodaiwa. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:
“Mwenye kupitiwa na usingizi swalah ikampita au akaisahau, basi aiswali atapokumbuka. Hakuna kafara yake isipokuwa hiyo.”
Ameipokea al-Bukhaariy na Muslim.
Kupoteza fahamu kwa sababu ya maradhi au matibabu hukumu yake ni kama ya aliyepitiwa na usingizi midhali haujarefuka muda. Muda ukirefuka zaidi ya siku tatu basi zimeanguka zile swalah anazodaiwa na mtu huyo anakuwa na hukumu kama ya mwendawazimu mpaka pale zitakaporudi akili zake. Hapo ndipo ataanza kuswali baada ya kuwa fahamu zake zimerudi. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:
“Kalamu imenyanyuliwa kwa watu aina tatu; aliyelala mpaka anapoamka, mtoto mpaka anapobaleghe na mwendawazimu mpaka anapopata akili.”
Kulipa hakukutajwa kwa mdogo na mwendawazimu. Jambo la kulipa limethibiti kwa aliyepitiwa na usingizi na aliyesahau.
from Firqatu Nnajia http://bit.ly/2J4Oj9F
via IFTTT
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni