Translate

Jumatano, 3 Aprili 2019

Katazo la Mwanamke Kusafiri bila Maharimu

                                           Katazo la Mwanamke Kusafiri bila Maharimu



Mwanamke Muumini na Swaalihah haimpasi kwenda safari bila ya Maharimu wake kuwa pamoja naye hata ikiwa safari yenyewe ni ya kutekeleza ibada kama vile ibada ya Hijjah achilia mbali safari ya kutembea au kufanya biashara, kutalii na kadhalika.  

Safari ni safari iwe wakati wa Mtume Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) au wakati huu wa sayansi na ufundi wa hali ya juu; na iwe kwa chombo chochote kile; iwe kwa gari, treni, meli, ndege na kadhalika; bila ya shaka yoyote ile itakuwa ina mengi ndani yake baadhi yake ni ya hatari na mengine ni ya kashifa, fedheha na dhambi kuyaeleza.


Hekima ya Mjumbe wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) kumkataza mwanamke kusafiri peke yake bila ya kuwa na maharimu wake ni ya aina yake pekee, hivyo inawajibika kutekelezwa na kufuatwa na huko ndiko kumtii Mjumbe wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) kwenyewe, lengo au sababu yake iwe inaeleweka au haieleweki kwa kila mwenye macho, akili na uume kamili [si dayuwth: mwanamme dhaifu asiyejiheshimu na hajali kuhusu tabia chafu ama mavazi mabaya ya wanawake waliko chini yake] na kwa kila mwenye kupenda kuwa miongoni mwa wale wataoingia katika Kauli Yake Allaah:
Mwenye kumtii Mtume basi atakuwa amemtii Allaah.” [An-Nisaa 4: 80].

Na wala si kuwa miongoni mwa wale watoingia katika Kauli Yake Allaah:
Basi na watahadhari wanaokhalifu amri yake; isije ikawapata fitnah au[ikawapata] adhabu iumizayo” [An-Nuwr 24: 63].

Katika hali ya kawaida tu achilia mbali safari mwanamke huhitaji wa kumsaidia, kumshauri na kubwa kumhurumia kwa anayokutana nayo; na hakuna Arhamu na mwenye huruma na kuwahurumia wanawake zaidi ya Allaah na Mjumbe Wake (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam); kwani Allaah ni Arhamu kwa waja Wake kuliko mama kwa mtoto wake, na Mjumbe wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) hakutumwa isipokuwa awe Rahmah kwa viumbe vyote wakiwemo wanawake; Allaah Anasema:
Nasi Hatukukutuma ila ni Rahmah kwa viumbe wote.“ [Al-Anbiyaa 21: 107].
Aliyetumwa kuwa Rahmah kwa viumbe amemkataza mwanamke mwenye kuamini Allaah na Siku ya Qiyaamah kusafiri bila ya Maharimu wake.

Kutoka kwa Ibn ‘Abbaas (Radhiya Allaahu ‘anhu) amesema kwambaMjumbe wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:“Asisafiri mwanamke isipokuwa awe pamoja nae maharimu wake, na wala asiingie (katika Riwaayah: Asikae faragha) mwanamme kwa mwanamke isipokuwa awe na maharimu wake.” Mtu mmoja akauliza: ee Mjumbe wa Allaah, mimi natarajia kutoka katika jeshi [kwenda vitani] kadhaa wa kadhaa, na mke wangu anatarajia kwenda Hijjah?” Mjumbe wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) Akamwambia: Nenda ukahiji pamoja na mkeo.” [Imepokelewa na Al-Bukhaariykatika Kitabu cha Hajj, milango ya Muhswar na malipo ya kiwindo, mlango wa Hajj ya wanawake, Hadiyth namba 1739; na Muslim, katika Kitabu cha Hajj, mlango wa safari ya mwanamke pamoja na maharimu wake kwenda Hajj, Hadiyth namba 2801].

Na kutoka kwa Abu Sa’iyd Al-Khudriyy (Radhiya Allaahu ‘anhu) amesema kwamba Mjume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: “Si halali kwa mwanamke anayemwamini Allaah na Siku ya Mwisho kusafiri safari ya [katika Riwaayah: masafa ya siku mbili] siku tatu na kuendelea, isipokuwa awe pamoja nae baba yake, au mtoto wake [aliye baleghe] au mume wake, au ndugu/kaka yake au katika maharimu wake.” [Imepokelewa na Al-Bukhaariykatika Kitabu cha Hajj, milango ya Muhswar na malipo ya kiwindo, mlango wa Hajj ya wanawake, Hadiyth namba 1741; na Muslim, katika Kitabu cha Hajj, mlango wa safari ya mwanamke pamoja na maharimu kwenda Hajj, Hadiyth namba 2398 na lafdhi ni lake].

Na kutoka kwa Abu Sa’iyd Al-Khudriyy (Radhiya Allaahu ‘anhu) amesema kwamba Mjume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: “Asisafiri mwanamke (na katika Riwayah): zaidi ya masiku tatu[siku tatu] isipokuwa awe pamoja na maharimu.” [Imepokelewa na Muslim, katika Kitabu cha Hajj, mlango wa safari ya mwanamke pamoja na maharimu kwenda Hajj, Hadiyth namba 2398 na namba 2393].

Na  Allaah  anajua  zaidi


https://ift.tt/2Uz9rel i live islam

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni

20-Hakika Shirki Ni Dhulma Kubwa Mno! - Isti’aadhah Kwa Asiyekuwa Allaah

  إِنَّ الشِّرْكَ لَظُلْمٌ عَظِيم   Hakika Shirki Ni Dhulma Kubwa Mno!   20 - Isti’aadhah  (Kuomba Kinga) Kwa Asiyekuwa Allaah   ...