Translate

Jumatano, 3 Aprili 2019

Katazo la Mwanamke kukaa Faragha na Mwanaume asiye kuwa Maharim

                     Katazo la Mwanamke kukaa Faragha na Mwanaume asiye kuwa Maharim


Uislamu unapendelea mahusiano yoyote yale baina ya mwanamme na mwanamke wenye kuweza kuoana yawe na mipaka na udhibiti wenye kuchunga heshima na kujiweka mbali na yenye kuweza kutokea ambayo ni haramu pindi tu wawili hawa wenye jinsi tofauti na wenye maumbile yaliyopambiwa na kupandikizwa kupenda matamanio ya kila mmoja kutaka kuelemea kwa jinsi iliyo tofauti na yake watapokuwa faragha; Allaah Anasema:
“Watu wamepambiwa kupenda matamanio ya wanawake, na wana, na mirundi ya dhahabu na fedha, na farasi asili, na mifugo, na mashamba. Hayo ni starehe ya maisha ya duniani; na kwa Allaah ndio kwenye marejeo mema” [Aal-‘Imraan 3: 14].

Ni katika yenye kupendwa na wengi ukaaji wa faragha kwa wawili wenye jinsiya tofauti na wenye uwezo wa kuoana huku wakielewa fika kuwa ukaaji wao huo unaweza kuwapelekea kutenda kila lililokatazwa na Allaah na Mtumewe litalo wapelekea kufikia kuwa wenye kustahiki adhabu ilyowekwa na Allaah hapa duniani au huko Aakhirah.

Kutoka kwa Ibn ‘Abbaas (Radhiya Allahu ‘anhu) amesema kwamba alimsikia Mjumbe wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akihutubia kwa kusema:“Asikae faragha mwanamme na mwanamke isipokuwa [mwanamke huyo]awe na maharimu wake...”  [Imepokelewa na na Al-Bukhaariy, kitabu cha Tafsiyr ya Qur-aan, Suwrat Qul A’uwdhu Birabbil Falaq, Hadiyth namba 4860; na Muslim, kitabu Kitabu cha Hajj, mlango wa Safari ya mwanamke pamoja na Maharimu wake kwenda Hajj, Hadiyth namba 2399].

Na kutoka kwa Jaabir bin ‘Abdillaah (Radhiya Allahu ‘anhu) amesema kwamba Mjumbe wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:Mwenye kumuamini Allaah na Siku ya Mwisho asiingie katika Hammaam [mahodhi ya kuogea]isipokuwa awe amevaa miizar[shuka]; na mwenye kumuamini Allaah na Siku ya Mwisho asimuingize khaliylah wake [mkewe] katika Hammaamna mwenye kumuamini Allaah na Siku ya Mwisho asikae kwenye meza yenye kunywewa ulevi; na mwenye kumuamini Allaah na Siku ya Mwisho asikae faragha [peke yake]na mwanamke asiyekuwa na maharimu wake pamoja naye, kwani watatu wao huwa shaytwaan [Imepokelewa na Ahmad, katika Musnad, Musnad Kumi waliobashiriwa Jannah, iliyobaki Musnad Mukthiriyna katika Swahaba (Radhiya Allahu ‘anhum), Hadiyth namba 14356].

Na katika desturi yenye kwenda kinyume na mafundisho ya Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ni hii desturi ya watu kukaa faragha na shemeji zao;aliulizwa Mjumbe wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam)kuhusu shemeji na majibu yalikuwa kwamba shemeji ndio hasa hatari [mauti] kubwa kwa kukaa faragha na mke wa ndugu yake, kwani yeye huwa na nafasi kubwa asiyokuwa nayo mtu mwingine wa nje asiyekuwa shemeji; Mjumbe wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:Tahadharini kuwaingilia[kuingia majumbani mwao] wanawake; akasema mtu mmoja miongoni mwa Answaar: Ee Mjumbe wa Allaah, vipi kuhusu Hamuu [shemeji]?! Mjumbe wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akasema: Hamuu ni mauti.[Hamuu” Katika hali hii kunamaanishwa ndugu za mume (wa kiume). Haafidh Ibn Hajar (Rahimahu Allaah) kasema: "Atw-Twabariy kasema: "Maana yake ni kwamba kuwepo kwa mwanamke katika nyumba au chumba na kaka wa mume au binamu ya mke wawili peke yao ni kama kifo, kwa kuwa Waarabu huzoea kuita kila kitu chenye hatari “kifo”]. [Imepokelewa na Al-Bukhaariy, kitabu cha Ndoa, mlango asikae faragha mwanamme na mwanamke isipokuwa awepo maharimu, Hadiyth namba 4859; na Muslim, katika Kitabu cha Salamu, mlango uharamu wa kukaa faragha na mwanamke asiyekuwa maharimu wako na kuingia nyumbani kwake, Hadiyth namba 4044.].

Ni vyema ieleweka kuwa shemeji wa mtu, binamu ya mke wa mtu si miongoni mwa Maharimu zake kwa kuwa wao wanaweza kumuoa hali kadhalika wengi wa jamaa za mume si Maharimu wa mke.

Pia katika kawaida zenye kwenda kinyume na mafundisho ya Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ni hii desturi ya watu kulala kwenye nyumba za wanawake wajane; kutoka kwa Jaabir bin ‘Abdillaah(Radhiya Allahu ‘anhu) amesema kwambaMjumbe wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: “Asilale mwanamme yeyote yule kwa mwanamke mjane (na katika Riwaayah): [katika nyumba] isipokuwa awe mwenye kumuoa au maharimu wake.” [Imepokelewa na Muslim, katika Kitabu cha Salaam, mlango uharamu wa kukaa faragha na mwanamke asiyekuwa maharimu wako na kuingia nyumbani kwake, Hadiyth namba 4043.].

Na katika mazoea na mila walizonazo watu zenye kwenda kinyume na mafundisho ya Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ni haya mazoea ya kwenda au kuingia kwenye nyumba za watu ambao waume hawapo na kukaa kupiga domo [soga] au kutoa stori za kweli na uongo na mke wa mtu.

Kutoka kwa ‘Abdullaah bin ‘Amru bin Al-‘Aasw (Radhiya Allahu ‘anhu) amesema kwamba: “Watu kutoka bani Haashim waliingia kwenye nyumba ya Asmaa bint ‘Umays; basi akaingia Abu Bakr (Radhiya Allahu ‘anhu)... alipowaona hao watu hakufurahi [alichukizwa], akamuelezaMjumbe wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam); Abu Bakr (Radhiya Allahu ‘anhu) akasema: Sikuona isipokwa kheri. Mjumbe wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akasema: “Hakika Allaah Amemuepusha [Asmaa] na hayo. Kisha akasimama Mjumbe wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kwenye minbar akasema: Asiingie mwanamme yeyote yule baada ya siku ya leo kwa maghiybah [mwanamke aliyekuwa mumewe hayupo] isipokuwa awe pamoja nae mwanamme mwingine au wanaume wawili.” [Imepokelewa na Muslim, katika Kitabu cha Salaam, mlango uharamu wa kukaa faragha na mwanamke asiyekuwa maharimu wako na kuingia nyumbani kwake, Hadiyth namba 4046.].

Hadiyth hizi za Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ziko wazi katika kutufahamisha kuwa ni haramu kukaa faragha mwanamme na mwanamke wenye uwezo wa kuoana na kwenda au kuingia katika nyumba ambayo mume hayupo.

Dada yangu Muislamu huu pia ni uwanja mwengine wenye kufanywa mwepesi kufikiwa na kila mtu kwa madai tofauti yakiwemo ya kuwa ni mwenzangu katika kazi, au ni mwanafunzi mwenzangu, au mengineyo.

Hivyo ni wajibu kwa mwanamke Swaalihah (mwema) kutomruhusu kuingia katika nyumba yake isipokuwa yule anayemridhia mumewe wakati yupo huyo mume, na atakaporuhusiwa iwe kukaa kwake kwa vidhibiti vya kishari’ah; ikiwemo kutokaa naye faragha au kukaa naye bila ya kuvaa hijabu ya kishari’ah; au bila ya haja yenye kukubalika; hivyo haitakiwi kukaa pamoja na asiyekuwa maharimu yake [hata akiwepo mumewe au akiwepo mmoja kati ya maharimu zake] kwa kuzungumza tu na kuhadithiana yaliyopo au habari zilizopo.

Kinachojitokeza siku hizi [ambacho hakikubaliki pia] ni kwa wanawake kukaa faragha na wasiokuwa maharimu zao kwa kisingizio kuwa wako watoto wao wa kiume wadogo wadogo [wasio kuwa baleghe], hivyo hudai kuwa faragha imetoweka kwa kuwepo hao watoto wake wadogo; hii si sahihi, kwani kuwepo kwa mtoto mdogo na kutokuwepo ni sawa, kwani hakuna anayewaonea hayaa kwa sababu ya umri wao mdogo; na katika yanayofanywa pia ambayo yanakwenda kinyume na mafundisho ya Mtume Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na kuwa miongoni mwa jumla ya yasiyokubalika katika Uislamu ambayo ni miongoni mwa namna fulani ya kukaa faragha kwa mwanamke na asiyekuwa maharimu wake, ni huku kwa baadhi ya watu [wenye kujiita au kuitwa mustaadh] kwenda kuwaombea [kuwazinguwa] wasichana wanaotarajiwa kuolewa au kuwasomea mabibi arusi huku wakiwa wamepambika kisawa sawa, ukaaji wa aina hii kwa hali yoyote ile ikiwa hakuna maharamu ni ukaaji faragha wa wanaume wengi na mwanamke mmoja pia hakukubaliki.

Ama mwanamme akimkuta mwanamke aliyepotea njia, itajuzu kwake kufuatana naye kwa vidhibiti vya kishari’ah, miongoni mwake ni kwa yule mwanamke kuwa nyuma ya yule mwanamme katika kwenda kwao na si kwenda sambamba au bega kwa bega huku wakizungumza na kucheka kama mke na mumewe.

 Na  Allaah  anajua  zaidi


https://ift.tt/2K5lzQ2 i live islam

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni

20-Hakika Shirki Ni Dhulma Kubwa Mno! - Isti’aadhah Kwa Asiyekuwa Allaah

  إِنَّ الشِّرْكَ لَظُلْمٌ عَظِيم   Hakika Shirki Ni Dhulma Kubwa Mno!   20 - Isti’aadhah  (Kuomba Kinga) Kwa Asiyekuwa Allaah   ...