Translate

Jumatano, 3 Aprili 2019

Katazo la Mwanamke kumuasi Mume

                                                    Katazo la Mwanamke kumuasi Mume


Mke kumuasi au kumdharau mumewe ni katika madhambi makubwa; mke anatakiwa awe mnyenyekevu mbele ya mumewe, asimwangalie mumewe kwa jicho la ufedhuli, asimnunue wala asimgomee, amtii anapomwamrisha, anyamaze na kumsikiliza anapomsemesha, amsikilize anapozungumza, amkaribishe anapoingia nyumbani, amuage anapoondoka nyumbani, ampokee anapokuja na kitu, ajiepushe na mambo yanayoweza kumkasirisha au kumuudhi, aridhike na kidogo chochote anacholetewa, asimkalifishe kwa asiyoyaweza.

Allaah Anasema: “… Basi Swaalihaatu[wanawake wema] ni Qaanitaatu[wale wenye kutii] na ni Haafidhaatu[wanaohifadhi heshima zao na mali za waume zao] hata katika siri [wanapokuwa hawapo] kwa Aliyoyahifadhi Allaah [Aliyoyaamrisha Allaah kuhifadhiwa]. Na wale [wanawake] ambao mnachelea uasi wao, basi wapeni mawaidha [wanasihini], [wakiendelea na uasi, basi] muwahame katika malazi na muwapige. [Watakapo rejea katika twaa’ah] msiwatafutie njia ya kuwaudhi bure…” [An-Nisaa 4: 34].

Ni juu ya mwanamke swaalihah kumtendea wema mumewe na kukaa nae kwa ihsaan; kumsikiliza kama itakiwavo na kumtii katika mambo yasiyo ya maasi, kwani hakuna utiifu kwa kiumbe yeyote yule katika maasi; mke atakapoamrishwa na mumewe katika yenye kumghadhibisha Mola na katika yenye kwenda kinyume na maamrisho au mafundisho ya Mjumbe wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) huwa hatakiwi kutii wala kusikiliza katika hilo.

Kutoka kwa Ibn Mas’uud (Radhiya Allaahu ‘anhu) amesema kwamba Mjumbe wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema kumwambia yeye Ibn Mas’uud (Radhiya Allaahu ‘anhu): “Utakuwa na hali gani ee ‘Abdullaah! Mtakapokuwa na viongozi wenye kupuuza [kutojali] Sunnah na kuchelewesha Swalah na nyakati zake? Akasema: Nini unaniamrishwa ewe Mjumbe wa Allaahu (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam)! Akasema: Unaniuliza cha kufanya Ibn Umm ‘Abdi?! Hakuna kutii [amri yoyote yule ya] kiumbe katika yenye kumuasi Allaah…” [Imepokelewa na Ahmad, kitabu Musnad ya Kumi waliobashiriwa Jannah, Musnad Mukthiriyna katika Swahabah (Radhiya Allahu ‘anhum), Hadiyth ya Ibn Mas’uud (Radhiya Allahu ‘anhu), Hadiyth namba 3757 na kitabu Musnad ya Kumi waliobashiriwa Jannah, Awwalul Musnadul Baswariyyina, Hadiyth ya ‘Imraan bin Huswayn (Radhiya Allahu ‘anhu), Hadiyth namba 20150].

Amesema Ibn al-Jawziy: Kuhusu kuwajibika mke kumtii mumewe, ni kuwa haijuzu kwa mke kumtii mume katika yasiyokuwa halali, kama vile atakapo mtaka kumuingilia kwenye duburi [utupu wa nyuma] au kumuingilia wakati akiwa katika hedhi, au katika mchana wa Ramadhaan, au katika yasiyokuwa hayo katika maasi.

Mke hutarajiwa kumtii mumewe katika kila lenye kueleweka kuwa ni ma’aruuf; Mjumbe wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amewaamrisha wanawake kuwatendea wema waume zao na kukaa nao kwa ihsaan; na kuwasikiliza na pia Mjumbe wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amewakataza wanawake kuwaasi waume zao na kuwatendea maovu kwa sababu na hekima aijuayo yeye Mjumbe wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) hekima iliyompelekea [Allaahu A’alam] kufikia kusema: " …. lau kama ningelikuwa wa kumwamrisha mmoja yeyote amsujudie mmoja; basi ningelimwamrisha mwanamke kumsujudia mumewe, lau mumewe angelimwamrisha kuchukua [kitu]kutoka jabali manjano kupeleka jabalí jeusi na kutoka mlima mweusi kupeleka mlima mweupe, basi ingekuwa juu yake [mke] kutekeleza”[Imepokelewa Ahmad, katika Musnad ya Kumi waliobashiriwa Jannah, Saadis ‘Ashar Al-Answaar, Hadiyth ya mama wa Waumini ‘Aaishah (Radhiya Allahu ‘anhaa), Hadiyth namba 23912; na Ibn Maajah, katika Kitabu cha ndoa, mlango wa haki ya Mume juu ya ya mkewe, Hadiyth namba 1842].

Dada yangu katika iymaan ni hakika isiyokuwa na mjadala kuwa mwenye kumuasi mtu yeyote huwa hakuna njia ya aliyeasiwa kumpenda mtu huyo; hivyo basi utapomuasi mumeo kwa kwenda kinyume na matakwa yake si tu unakwenda kinyume na mafundisho aliyokuja nayo Mjumbe wa Allaah(Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na kuwa unastahiki anayostahiki kila mwenye kwenda kinyume na amri zake (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam); bali pia utakuwa umejitoa katika mapenzi ya huyo mume na kumpelekea kutokuwa na furaha yoyote ile wakati anapokutazama au kuona au hata kusikia sauti yako na huenda ukampelekea kuwa miongoni mwa wanaume wenye wake lakini wakati wao wote wanaupitisha nje ya nyumba zao kwa kutopenda kuwaona wake zao kwa maudhi yao, jambo ambalo huenda likakupelekea kujiondoa katika wenye kueleweka kuwa ni wanawake wazuri na bora miongoni mwa wanawake kama ilivyothibiti.

Kutoka kwa Abu Hurayrah (Radhiya Allahu ‘anhu) amesema kwamba aliulizwa Mjumbe wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) wanawake gani bora? Mjumbe wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akisema: Ambae humfurahisha [humpendezesha]anapomtazama, na humtii anapomwamrisha, mke humhifadhi katika nafsi yake na mali ya mumewe”[Imepokelewa na Ahmad, katika Musnad ya Kumi waliobashiriwa Jannah, Musnad waliobakia katika Mukthiriyna katika Swahaabah (Radhiya Allahu ‘anhum), Musnad Abi Hurayrah (Radhiya Allahu ‘anhu), Hadiyth namba 7245 na 9377 na 9445].

Pia Kutoka kwa ‘Abdullaah bin ‘Amr(Radhiya Allaahu ‘anhuma) kwambaMjumbe wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:“Allaah hamtazami mwanamke yeyote yule asiyekuwa na shukurani kwa mumewe, naye hawezi kujitosheleza bila ya huyo mume”  [Imepokelewa katika Mustadrak ya Swahiyhayn, katika Kitabu cha Imaamah na Swalah ya Jama’ah, mlango wa Taamiyn,Hadiyth namba 2696; na katika Kitabu cha kuwajua Swahaabah (Radhiya Allaahu ‘anhum), kutajwa kwa fadhila za makabila, Hadiyth namba 7416 na 7417; na An-Nasaaiy, katika Kitabu cha ‘Ish-ratun Nisaa, milango ya Mulaa’abah, Hadiyth namba 8803 na 8804; na Al-Bayhaqiy katika Kitabu cha Wasiya, Jimaa’u milango ya kuwaendea wanawake, Hadiyth namba 13637].

Ni juu ya kila mwanamke swaalihah kutafuta radhi za Mola wake kupitia radhi za mumewe kwa kumtii mumewe, na kutokwenda kinyume na amri zake kwa kumfanyia ujeuri, ufedhuli au usafihi au maovu yoyote yale, yawe ya kauli au vitendo; kwani mume huenda ikawa Jannah ya huyo mke au huenda ikawa Moto wake; kutoka kwa ‘Abdur-Rahmaan bin ‘Awf(Radhiya Allaahu ‘anhu) amesema kwamba Mjumbe wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:“Atakaposwali mwanamke Swalah zake tano; na akafunga mwezi wake [Ramadhaan]; na akahifadhi sehemu zake za siri; na akamtii mume wake; ataambiwa [Siku ya Qiyaamah]: Ingia Jannah kupitia mlango wowote uutakao katika milango ya Jannah” [Imepokelewa na Ahmad, katika Musnad ya Kumi waliobashiriwa Jannah, Musnad waliobaki katika kumi waliobashiriwa Jannah, Hadiyth ya ‘Abdur-Rahmaan bin ‘Awf (Radhiya Allahu ‘anhu), Hadiyth namba 1595; na Ibn Hibbaan, katika kitabu cha Ndoa, mlango wa mu’aasharah wanandoa wawili, Hadiyth namba 4252]

Na  Allaah  anajua  zaidi


https://ift.tt/2FUrcwg i live islam

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni

20-Hakika Shirki Ni Dhulma Kubwa Mno! - Isti’aadhah Kwa Asiyekuwa Allaah

  إِنَّ الشِّرْكَ لَظُلْمٌ عَظِيم   Hakika Shirki Ni Dhulma Kubwa Mno!   20 - Isti’aadhah  (Kuomba Kinga) Kwa Asiyekuwa Allaah   ...