Katazo la Mwanamke Kudai Talaka bila ya Sababu inayokubalika
Ndoa ni katika mambo Aliyoyaamrishwa Allaah na kuyahimizaMjumbe wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam), ndoa ni mafungamano ya kishari’ah baina ya mwanamme na mwanamke yenye mipaka, nidhamu, vidhibiti na kanuni maalumu; na inaathiri mengi; ima kujenga na kusimamisha familia ya Kiislamu yenye kuongozwa na kuongoka kwa uongofu wa Qur-aan na Sunnah za Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na kuwa miongoni mwa tofali la kuijenga jamiirabbaaniy [yenye kumuabudu Allaah pekee Mola wa viumbe vyote na yenye kufundisha Kitabu, kukisoma na kukifuata]; na ima kuvunja na kubomoa familia kwa kuivuruga vuruga na kuisambaratisha na kusababisha athari mbaya kwa jamii na watoto kwa kuachana kwa mume na mke.
Allaah Alipoweka shari’ah na utaratibu wa ndoa na kuiamrishwa [kwa kuwa Yeye Subhaanah ndie Muumba wetu na ni ‘Aalim wa hali zetu na uwezo wetu, Alielewa kuwa tabia na desturi zetu huenda zisikubaliane, na kwamba mawazo na fikra huenda yasifanane]; hivyo kwa Hikma Yake Akaweka utaratibu wa kuachana na kutengana [talaka] pale panaposhindikana kupatikana njia ya kusuluhisha na kupatanisha baina ya wanandoa wawili. Hata hivyo Allaah Ameiwekea talaka taratibu, nidhamu na mipaka yake; hatarajiwi kuivuka na kuivunja isipokuwa faasiq; na katika taratibu, nidhamu na mipaka ya talaka ni kuwahaifai kwa mke kumuomba mumewe talaka bila sababu yoyote ile yenye kukubalika kishari’ah.
Hii ni kwa kuwa Mjumbe wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: “Mwanamke yeyote yule ataemuomba mumewe talaka bila ya sababu yoyote ile, basi ni haramu juu yake harufu ya Jannah“[Imepokelewa na Ahmad, kitabu Musnad, Musnad ya Kumi waliobashiriwa Jannah, Musnadul Answaar, Hadiyth namba 21852 na 21789; na Ibn Maajah, katika Kitabu cha Atw-Twalaaq, mlango wa uchukivu wa kujikombowa kwa mwanamke, Hadiyth namba 2044 na 2045; na katika Mustadrak ya Swahiyhayn, katika Kitabu cha Imaamah na Swalah ya Jama’ah, mlango wa Ta-amiyn, Hadiyth namba 2735].
Lau mume atakuwa anamfanyia vitimbi na makruhi [kumpelekea mke kudai talaka] au hampendi lakini anamng’ang’ania na kumtundika kwa kisingizio kuwa anamtia adabu; hili ni kosa kwa upande wa mume. Katika hali hii pia mke hatakiwi kudai talaka yake bali atatakiwa apeleke lalamiko lake kwa Qaadhi au msimamizi wa mambo ya Kiislamu ili ichukuliwe hatua munasibu kwa kumuachisha na mume hatolipwa chochote kwa sababu yeye ndiye mkosa na haitokuwa halali kwa mume kuchukua chochote walaKhul'u haiswihi hapa kama Anavyosema Allaah:
“Wala msiwadhikishe ili muwapokonye baadhi ya mlivyowapa - isipokuwa wakifanya uchafu ulio wazi. Na kaeni nao kwa wema, na ikiwa mmewachukia, basi huenda mkakichukia kitu, na Allaah ametia kheri nyingi ndani yake.” [An-Nisaa 4: 19].
Na katika yaliyokatazwa ambayo yameenea na kuzagaa kwa wenye kupenda dunia na kuiweka kando Aakhirah ni kwa mwanamke kumtaka au kumghilibu mumewe; iwe kwa kumhadaa au vinginevyo kwa kumshurutisha amuache mkewe ili apate kuolewa yeye au abakie yeye pekee yake [kama ni mke mwenza] hili limekatazwa kama ilivyothibiti katika Hadiythi kuwa Mjumbe wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: “Mwanamke asitake (katika Riwayah: Si halali kwa mwanamke kudai kuachwa ukhti wake [mwanamke mwenzake] ili aichukue nafasi yake na kuolewa yeye; kwani hatopata isipokuwa yale aliyoandikiwa.” [Imepokelewa na Al-Bukhaariy, kitabu cha tafsiyr ya Qur-aan, Surat Qul A’uwdhu Birabbil Falaq, Hadiyth namba 6141 na 4782; na Muslim, katika Kitabu cha ndoa, mlango wa Uharamu wa kuwakusanya mwanamke na Shangazi yake, Hadiyth namba 2527; na Abu Daawuud, katika Kitabu cha atw-Twalaaq, mlango katika mwanamke anamtaka mumewe talaka ya mke wake, Hadiyth namba1865].
Na Allaah anajua zaidi
https://ift.tt/2OGpj9i i live islam
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni