Swali 1: Swawm ya Ramadhaan inamuwajibikia nani? Ni upi ubora wa kuifunga na kufunga swawm ya sunnah?
Jibu: Ni wajibu kwa kila muislamu ambaye ´ibaadah ni zenye kumuwajibikia kufunga Ramadhaan. Ni mamoja awe mwanaume au mwanamke. Imependekezwa kwa yule ambaye amefikisha miaka saba na zaidi ya hapo na akaweza kufunga katika wavulana na wasichana. Ni wajibu kwa wasimamizi wao kuwaamrisha jambo hilo wakiweza kama wanavyowaamrisha kuswali. Msingi wa hilo ni maneno ya Allaah (´Azza wa Jall):
يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا كُتِبَ عَلَيْكُمُ الصِّيَامُ كَمَا كُتِبَ عَلَى الَّذِينَ مِن قَبْلِكُمْ لَعَلَّكُمْ تَتَّقُونَ أَيَّامًا مَّعْدُودَاتٍ ۚ فَمَن كَانَ مِنكُم مَّرِيضًا أَوْ عَلَىٰ سَفَرٍ فَعِدَّةٌ مِّنْ أَيَّامٍ أُخَرَ
“Enyi mlioamini! Mmefaradhishiwa kufunga kama ilivyofaradhishwa kwa waliokuwa kabla yenu ili mpate kumcha Allaah. [Kufunga ni] siku za kuhesabika. Yule atakayekuwa mgonjwa miongoni mwenu au safarini, basi akamilishe idadi [ya siku zilizompita] katika siku nyinginezo.”[1]
Mpaka pale aliposema:
شَهْرُ رَمَضَانَ الَّذِي أُنزِلَ فِيهِ الْقُرْآنُ هُدًى لِّلنَّاسِ وَبَيِّنَاتٍ مِّنَ الْهُدَىٰ وَالْفُرْقَانِ ۚ فَمَن شَهِدَ مِنكُمُ الشَّهْرَ فَلْيَصُمْهُ ۖ وَمَن كَانَ مَرِيضًا أَوْ عَلَىٰ سَفَرٍ فَعِدَّةٌ مِّنْ أَيَّامٍ أُخَرَ
“Mwezi wa Ramadhaan ambao imeteremshwa humo Qur-aan ili iwe mwongozo kwa watu na hoja bayana za mwongozo na pambanuo la batili. Basi atakayeshuhudia miongoni mwenu mwezi mpya na afunge . Atakayekuwa mgonjwa au safarini basi atimize idadi katika siku nyinginezo.”[2]
Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:
”Uislamu umejengwa juu ya mambo matano; kushuhudia ya kwamba hapana mungu wa haki isipokuwa Allaah na kwamba Muhammad ni Mtume wa Allaah, kusimamisha swalah, kutoa zakaah, kufunga Ramadhaan na kuhiji nyumba.”
Ameipokea al-Bukhaariy na Muslim kupitia kwa Ibn ´Umar (Radhiya Allaahu ´anhumaa).
Vilevile amesema (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):
”Uislamu ni kushuhudia ya kwamba hapana mungu wa haki isipokuwa Allaah na kwamba Muhammad ni Mtume wa Allaah, kusimamisha swalah, kutoa zakaah, kufunga Ramadhaan na kuhiji Nyumba kwa yule mwenye kuweza.”
Ameipokea Muslim katika ”as-Swahiyh” kupitia kwa ´Umar bin al-Khattwaab (Radhiya Allaahu ´anh). Mashaykh wawili wamepokea maana yake kupitia kwa Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu ´anh).
Katika ”as-Swahiyh” mbili kupitia kwa Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu ´anh) ambaye amesimulia kuwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:
”Mwenye kufunga Ramadhaan kwa imani na kwa matarajio basi atasamehewa madhambi yake yaliyotangulia.”
Imethibiti pia kutoka kwake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kwamba amesema:
“Kila kitendo cha mwanadamu kinalipwa maradufu tendo jema moja mara kumi mfano wake mpaka mara mia saba. Allaah (Ta´ala) amesema: “Isipokuwa swawm. Hiyo ni Yangu mimi na mimi Ndiye nitailipa. Anaacha matamanio yake na chakula chake kwa ajili Yangu. Mfungaji ana furaha mbili: furaha ya kwanza ni pale anapokata swawm na furaha nyingine ni pale atapokutana na Mola wake. Ile harufu ya mfungaji ni nzuri zaidi kuliko harufu ya miski.”
Ameipokea al-Bukhaariy na Muslim.
Kuna Hadiyth nyingi juu ya fadhilah za kufunga Ramadhaan na ubora wa kufunga swawm za Sunnah na zinatambulika.
[1] 02:183
[2] 02:185
from Firqatu Nnajia https://ift.tt/2OBXkHO
via IFTTT
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni