Translate
Alhamisi, 28 Februari 2019
Madhambi Makubwa Na Madogo
Madhambi Makubwa:
Madhambi makubwa ni yale ambayo yametajwa katika Qur-aan na Sunnah za Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) nayo ni yale ambayo mja anapoyafanya huwa na hukmu zifuatazo:
1-Madhambi ambayo Allaah Anaalaani kitendo chake.
2-Madhambi ambayo yamewekewa adhabu kali kama mfano mwenye kuzini na hali ameoa au ameolewa kupigwa mawe hadi kufa au kupigwa bakora 100 kwa asiyeoa au asiyeolewa.
3-Madhambi ambayo Anaghadhibika nayo Allaah (Subhaanahu wa Ta'aala).
4-Madhambi ambayo Allaah Anamnyima Rahmah Yake mwenye kuyatenda.
Hadiyth ifuatayo imeyaelezea baadhi ya madhambi hayo makubwa ambayo yanajulikana Sab'ul-Muwbiqaat (saba yenye kuangamiza).
عَنْ أَبِي هُرَيْرَةَ (رضي الله عنه) عن النَّبِيِّ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ قَالَ: ((اجْتَنِبُوا السَّبْعَ الْمُوبِقَاتِ)) قَالُوا: يَا رَسُولَ اللَّهِ وَمَا هُنَّ؟ قَالَ: ((الشِّرْكُ بِاللَّهِ وَالسِّحْرُ وَقَتْلُ النَّفْسِ الَّتِي حَرَّمَ اللَّهُ إِلاَّ بِالْحَقِّ وَأَكْلُ الرِّبَا وَأَكْلُ مَالِ الْيَتِيمِ وَالتَّوَلِّي يَوْمَ الزَّحْفِ وَقَذْفُ الْمُحْصَنَاتِ الْمُؤْمِنَاتِ الْغَافلاَتِ)) متفق عليه
Imepokelewa kutoka kwa Abuu Hurayrah (رضي الله عنه) kwamba Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema: ((Jiepusheni na mambo saba yanayoangamiza!)) Wakauliza: Ni yepi hayo ee Rasuli wa Allaah? Akasema: ((Ni kumshirikisha Allaah, sihri [uchawi], kuua nafsi Aliyoiharamisha Allaah isipokuwa kwa haki, kula ribaa, kula mali ya yatima, kukimbia wakati wa kupambana na adui na kuwatuhumu uzinifu wanawake Waumini waliohifadhika walioghafilika)). [Al-Bukhaariy, Muslim, An-Nasaaiy, Abu Daawuud]
Madhambi hayo makubwa ni haya yafuatayo ambayo yametajwa katika Hadiyth hiyo juu na mengine mengi ambayo baadhi ya ‘Ulamaa wamejaribu kuyaorodhesha kwa kuyanyambua kutoka katika Qur-aan na Sunnah kulingana na makatazo, makemeo, laana, na adhabu zake, kama vile madhambi 70 aliyoyaorodhesha mwanachuoni mkubwa Imaam Muhammad bin ‘Uthmaan Adh-Dhahabiy kwenye kitabu chake Al-Kabaair:
1-Kumshikirika Allaah
2-Kuua
3-Uchawi
4-Kuacha Swalaah
6-Kuacha kufunga Swawm ya Ramadhwaan bila udhuru
7-Kutokuhiji kwa mwenye uwezo
8-Kutokuwatii wazazi
9-Kuwahama na kuwakata jamaa na ndugu; kutengana nao
10-Uzinzi (kufanya zinaa)
11-Liwati (matendo ya kaumu Luwt; watu kuingiliana nyuma) mwenye kufanya na kufanywa wote wanaingia
12-Kula ribaa
13-Kula mali ya yatima na kumdhulumu
14-Kumsingizia Allaah na Rasuli Wake uongo
15-Kukimbia vitani
16-Kiongozi kuwa mdanganyifu kwa raia wake na kutokuwa muadilifu
17-Kiburi, majivuno na kujitukuza
18-Kutoa ushuhuda wa uongo
19-Kunywa pombe
20-Kamari
21-Kumsingizia mwanamke mtwaharifu tuhuma ya uzinifu
22-Kuiba ngawira za vita
23-Wizi
24-Ujambazi
25-Kutoa kiapo cha uongo
26-Dhulma (Kudhulumu)
27-Chumo la haramu
28-Kupata utajiri kwa njia za haramu
29-Kujiua
30-Kusema uongo (kila mara)
31-Kutohukumu kwa uadilifu
32-Kutoa na kupokea rushwa
33-Mwanamke kujifananisha na mwanamme na mwanamme kujifananisha na mwanamke kimavazi, kutembea, kuzungumza na mengineyo
34-Udayuthi, ukuwadi, na kutokuwa mwaminifu katika ndoa
35-Kumuoa mwanamke aliyeachika kwa talaka tatu ili awe halali kwa mume aliyemuacha kumrudia
36-Kutojilinda kurukiwa na mikojo
37-Riyaa (kujionyesha matendo mema)
38-Kutafuta elimu kwa maslahi ya dunia, na kuificha elimu uliyonayo
39-Kufanya khiyana
40-Kutangazia na kuhesabu mema uliyoyatenda
41-Kupinga Qadar
42-Kusikiliza siri za watu
43-Kuhamisha maneno (umbea)
44-Kulaani wengine
45-Kuvunja ahadi
46-Kuwaamini makuhani, watabiri, wapiga ramli (watazamiaji)
47-Mke kutomtii mumewe
48-Kutengeneza masanamu, vinyago, na picha
49-Kupiga mayowe, kuchana nguo, kujipiga na kujikatakata wakati wa msiba
50-Kutokuwa muadilifu kwa watu
51-Kutokuwa na huruma na kuwafanyia ujeuri mke, wafanyakazi, madhaifu na wanyama
52-Kumuudhi jirani
53-Kuwaudhi na kuwatukuna Waislamu
54-Kuwaudhi na kuwafanyia ujeuri watu
55-Isbaal (mwanamme kuvaa nguo ndefu inayovuka viwiko vya miguu kwa kiburi au ufakhari)
56-Mwanaume kuvaa hariri
57-Mtumwa kumkimbia bwana wake
58-Kutokuchinja mnyama kwa ajili ya Allaah
59-Kumwita mtu kwa ubini wa baba asiyekuwa wake huku unajua (kwa makusudi)
60-Kugombana na kupigana
61-Kuzuilia (watu) maji
62-Kupunja kipimo
63-Kujilinda na Aliyoyapanga Allaah
64-Kuwaudhi waja wema vipenzi vya Allaah
65-Mwanaume kuacha kuswali Swalaah ya jama’aah (Msikitini) na kuswali pekee bila udhuru
66-Kuacha kuswali Ijumaa kwa makusudi au kutotilia umuhimu na kupuuzia
68-Kupanga njama na kufanya hila
69-Kuwapeleleza Waislamu kwa ajili ya makafiri na maadui
70-Kuwatukana Maswahaba (Radhwiya Allaahu ‘anhum)
Hayo ni madhambi 70 aliyojaaliwa Imaam Adh-Dhahabiy (Rahimahu Allaah) kuyakusanya kutoka katika Qur-aan na Sunnah.
Madhambi makubwa mengineyo:
71-Kusherehekea sikukuu za makafiri
72-Kunyoa nyusi
73-Kuunga nywele za bandia
74-Kujichora tattoo
75-Kuvunja mkataba (bila sababu ya ki-shariy’ah)
76-Kula nguruwe, nyamafu na damu
77-Kutoa kiapo cha uongo kwenye biashara
78-Kudharau na kuzikebehi Sunnah za Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kama ndevu, mswaki wa mti, kupunguza nguo isiburuze kwa wanaume n.k.
79-Kuwakebehi na wakuwapa majina mabaya wale wanaozifuata Sunnah za Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam)
80-An-Namiymah (Kufitinisha watu)
81-Ghiybah (kusengenya)
82-Kuamini nuksi (superstition), na kutabiri kwa nyota (horoscope), kutundika vitu na kuvaa kwa kuitakidi kuwa vinamlinda mtu na shari
83-Bid-ah za aina zote katika Dini
84-Kudanganya watu kupata maslahi ya kidunia
85-Kufanya israfu ya chakula na israfu katika sherehe ambayo inadhihirisha riyaa (kujionyesha kwa watu)
86-Kukufuru neema za Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa)
87-Kuisoma Qur-aan kimakosa kwa kubadilisha maana za Maneno ya Allaah
88-Kuapa uongo kama kuapia kwa ajili ya kumvutia mteja biashara
89-Kughushi katika biashara kama kupunja au kuuza bidhaa mbovu
90-Mwanamke kutokujisitiri vizuri kwa hijaab ya ki-shariy’ah
Madhambi Madogo:
Madhambi madogo ni yale ambayo hayamo katika fungu hilo hapo juu nayo ni yale ambayo yamekusudiwa katika kauli ya Allaah (Subhanaahu wa Ta'aalaa):
الَّذِينَ يَجْتَنِبُونَ كَبَائِرَ الْإِثْمِ وَالْفَوَاحِشَ إِلَّا اللَّمَمَ ۚ
Wale wanaojiepusha na madhambi makubwa na machafu isipokuwa makosa madogo-madogo. [An-Najm: 32]
Madhambi hayo ambayo Allaah Humghfuruia mja maadam mja hatoendelea kuyatenda kila mara kwani kuyaendeleza husababisha kugeuka kuwa ni madhambi makubwa. Mfano kuchanganyika wanawake na wanaume, mtu kuzungumza na asiye Mahram wake bila ya sababu ya ki-shariy’ah, husababisha kukaribia zinaa na huenda yakampeleka mja kutumbukia katika maasi hayo makubwa.
Madhambi madogo kama ilivyo dalili katika Qur-aan na Sunnah kwamba kila jema alifanyalo mja hufuta ovu lake kama Anavyosema Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa):
وَأَقِمِ الصَّلَاةَ طَرَفَيِ النَّهَارِ وَزُلَفًا مِّنَ اللَّيْلِ ۚ إِنَّ الْحَسَنَاتِ يُذْهِبْنَ السَّيِّئَاتِ ۚ ذَٰلِكَ ذِكْرَىٰ لِلذَّاكِرِينَ﴿١١٤﴾
Na simamisha Swalaah katika ncha mbili za mchana na sehemu ya kwanza ya usiku; hakika mema yanaondosha maovu. Hivyo ni ukumbusho kwa wanaokumbuka. [Huwd: 114]
Mfano kufanya wudhuu vizuri, madhambi madogo hupuputika.
Madhambi hayo pia yanaweza kuwa ni kama, kutazama picha na sinema chafu zisizofaa, kusikiliza maovu, kusikiliza na kuimba muziki, kutamka maneno maovu kama kutukana, kuwa na ghadhabu, na mengi mengineyo ambayo hayakuwekewa adhabu kali au laana, au ghadhabu ya Allaah.
from Uislamu Wangu https://ift.tt/2XDI6pY
via IFTTT
'Ibaadah Zipasazo Kutekelezwa Siku Ya Ijumaa
Ijumaa ni siku tukufu kwa Waislamu. ‘Ibaadah kadhaa zenye fadhila adhimu zinapasa kutekelezwa siku hiyo kama ifuatavyo pamoja na dalili zake:
1-Ghuslu (Kuoga)
حديث أَبِي سَعِيدٍ الْخُدْرِيِّ، عَنِ النَّبِيِّ صلى الله عليه وسلم قَالَ: الْغُسْلُ يَوْمَ الْجُمُعَةِ وَاجِبٌ عَلَى كُلِّ مُحْتَلِمٍ.أخرجه البخاري
Kutoka kwa Abu Sa'iyd Al-Khudriyy (Radhwiya Allaahu 'anhu) ambaye alisema: Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: ((Ghuslu (kukoga kwa kujitia twahara) siku ya Ijumaa ni wajibu kwa kila Muislamu aliyebaleghe)) [Al-Bukhaariy]
Pia, inapendekezwa kwa kila anayekwenda kuswali kujisafisha, kupiga mswaki, kujitia mafuta mazuri (isipokuwa mwanamke) na kuvaa nguo iliyo nzuri kabisa. Muislamu akitimiza adabu ya Swalaah ya Ijumaa hufutiwa madhambi yake ya wiki.
عَنْ سَلْمَانَ الْفَارِسِيِّ، قَالَ قَالَ النَّبِيُّ صلى الله عليه وسلم " لاَ يَغْتَسِلُ رَجُلٌ يَوْمَ الْجُمُعَةِ، وَيَتَطَهَّرُ مَا اسْتَطَاعَ مِنْ طُهْرٍ، وَيَدَّهِنُ مِنْ دُهْنِهِ، أَوْ يَمَسُّ مِنْ طِيبِ بَيْتِهِ ثُمَّ يَخْرُجُ، فَلاَ يُفَرِّقُ بَيْنَ اثْنَيْنِ، ثُمَّ يُصَلِّي مَا كُتِبَ لَهُ، ثُمَّ يُنْصِتُ إِذَا تَكَلَّمَ الإِمَامُ، إِلاَّ غُفِرَ لَهُ مَا بَيْنَهُ وَبَيْنَ الْجُمُعَةِ الأُخْرَى ". رواه البخاري
Kutoka kwa Salmaan Al-Faarisiy (Radhwiya Allaahu 'anhu) kwamba Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: ((Muislamu atakayekoga (Ghuslu) siku ya Ijumaa, akajisafisha vizuri awezavyo, akatia rangi (nywele zake) (isiyo nyeusi), au akajipaka mafuta mazuri aliyonayo nyumbani kwake, kisha akaenda Msikitini bila ya kufarikisha (kuwapangua akipita) watu wawili (ambao wameshakaa kitako msikitini), akaswali aliyofaridhishwa, kisha akasikiliza (khutbah) kimya, hufutiwa madhambi yake yaliyo baina ya Ijumaa hiyo na Ijumaa ijayo. [Al-Bukhaariy na Ahmad]
2-Swalaah Ya Ijumaa
Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Ametuamrisha kwenda kuswali Swalaah ya Ijuma Anaposema:
يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا إِذَا نُودِيَ لِلصَّلَاةِ مِن يَوْمِ الْجُمُعَةِ فَاسْعَوْا إِلَىٰ ذِكْرِ اللَّـهِ وَذَرُوا الْبَيْعَ ۚ ذَٰلِكُمْ خَيْرٌ لَّكُمْ إِن كُنتُمْ تَعْلَمُونَ﴿٩﴾
Enyi walioamini! Inaponadiwa kwa ajili ya Swalaah siku ya Ijumaa, kimbilieni kumdhukuru Allaah na acheni kuuza na kununua. Hivyo ni kheri kwenu mkiwa mnajua. [Al-Jumu’ah 62: 9]
Ni wajibu kwa kila mwanamme Muislamu kwenda kuswali Ijumaa, na hatari ya kutokwenda kuswali bila ya kuwa na sababu inayoruhusu shariy’ah ni kuwa Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Humpiga muhuri mtu moyoni mwake kwa kauli ya Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam):
مَنْ تَرَكَ ثَلاَثَ جُمَعٍ تَهَاوُنًا بِهَا طَبَعَ اللَّهُ عَلَى قَلْبِهِ -رواه أحمد وأصحاب السنن
((Atakayeacha (kuswali Swalaah ya) Ijumaa mara tatu bila ya sababu yeyote, Allaah humpiga muhuri katika moyo wake)) [Ahmad na wapokezi wa Hadiyth wengine wenye vitabu vya ‘Sunnan’]
Kupigwa muhuri huo inamaanisha kwamba Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Ameshampa chapa huyu mtu kuwa ni 'Aasi na amekwishatumbukia katika makemeo ya Allaah kwamba ni katika walioghafilika kama alivyotutahadharisha Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam):
ابن عمر وأبي هريرة أَنَّهُمَا، سَمِعَا رَسُولَ اللَّهِ صلى الله عليه وسلم يَقُولُ عَلَى أَعْوَادِ مِنْبَرِهِ " لَيَنْتَهِيَنَّ أَقْوَامٌ عَنْ وَدْعِهِمُ الْجُمُعَاتِ أَوْ لَيَخْتِمَنَّ اللَّهُ عَلَى قُلُوبِهِمْ ثُمَّ لَيَكُونُنَّ مِنَ الْغَافِلِينَ "
Kutoka kwa Ibn 'Umar na Abu Hurayrah (Radhwiya Allaahu ‘anhumaa) kwamba wamemsikia Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akisema: “Wasiohudhuria Swalaah ya Ijumaa wabadilishe mtindo wao huo au sivyo Allaah Atawapiga mihuri katika nyoyo zao na watakuwa miongoni wa walioghafilika.” [Muslim]
3-Kufika Mapema Msikitini
Kila atakapofika mtu mapema Msikitini huwa amepata daraja fulani na muhimu kabisa ni kufika kabla ya khutba kuanza, akichelewa mtu kufika akakosa khutba atakuwa amekosa Swalaah ya Ijumaa.
حديث أَبِي هُرَيْرَةَ رضي الله عنه، أَنَّ رَسُولَ اللهِ صلى الله عليه وسلم قَالَ: مَنِ اغْتَسَلَ يَوْمَ الْجُمُعَةِ غُسْلَ الْجَنَابَةِ ثُمَّ رَاحَ فَكَأَنَّمَا قَرَّبَ بَدَنَةً، وَمَنْ رَاحَ فِي السَّاعَةِ الثَّانِيَةِ فَكَأَنَّمَا قَرَّبَ بَقَرَةً، وَمَنْ رَاحَ فِي السَّاعَةِ الثَّالِثَةِ فَكَأَنَّمَا قَرَّبَ كَبْشًا أَقْرَنَ، وَمَنْ رَاحَ فِي السَّاعَةِ الرَّابِعَةِ فَكَأَنَّمَا قَرَّبَ دَجَاجَةً، وَمَنْ رَاحَ فِي السَّاعَةِ الْخَامِسَةِ فَكَأَنَّما قَرَّبَ بَيْضَةً، فَإِذَا خَرَجَ الإِمَامُ حَضَرَتِ الْمَلاَئِكَةُ يَسْتَمِعُونَ الذِّكْرَ. أخرجه البخاري
Kutoka kwa Abu Hurayrah (Radhwiya Allaahu 'anhu) kwamba Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: “Atakayekoga (Ghuslu) siku ya Ijumaa kisha akaenda Msikitini, itakuwa kama mfano ametoa (kafara ya) ngamia. Akienda saa ya pili yake, itakuwa kama katoa (kafara ya) nġ’ombe. Akienda saa ya tatu yake, itakuwa kama katoa (kafara ya) kondoo mwenye pembe. Akienda saa ya nne yake, itakuwa kama katoa kuku. Akienda saa ya tano yake itakuwa kama katoa yai. Imaam akifika, Malaika watatoka kuja kusikiliza dhikr”[Al-Bukhaariy]
4-Kusoma Suwrah Al-Kahf:
‘Ulamaa wengi wanaonelea kuisoma Suwratul-Kahf siku ya Ijumaa kutokana na Hadiyth ifuatayo chini, lakini Wanachuoni wa Hadiyth wamesema hakuna Hadiyth iliyothibiti kwa lafdhi ya kuisoma siku ya Ijumaa kama zinavyotaja Hadiyth hizo. Bali ni siku yoyote kama ilivyokuja katika Hadiyth ya mwisho ya mlango huu.
Walioonelea inafaa kusomwa Ijumaa, wametolea ushahidi kwa Hadiyth hii:
عن أبي سعيد الخدري رضي الله عنه أن النبي صلى الله عليه وسلم قال: من قرأ سورة الكهف يوم الجمعة أضاء له من النور ما بين الجمعتين. رواه الترمذي
Kutoka kwa Abu Sa'iyd Al-Khudriyy (Radhwiya Allaahu 'anhu) ambaye amesema: Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: Atakayesoma Suwratul-Kahf siku ya Ijumaa atakuwa katika mwangaza baina ya Ijumaa mbili.” [At-Tirmidhiy]
Pamoja na kusemwa kuwa Hadiyth hiyo imetoka kwa Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) lakini Wanachuoni wa Hadiyth wengi wamesema ni Hadiyth 'Mawquuf' ambayo haijaelezwa na Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) bali ni kutoka kwa Maswahaba, na kwa nyongeza ya neno 'atakayeisoma Ijumaa' haikuthibiti kwa Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) , na maelezo hayo hapo juu ni ya kutoka kwa Abu Sa'iyd Al-Khudriyy na yeye ndiye aliyekuwa akiisoma Suwrah hiyo katika siku ya Ijumaa, na Wanachuoni wanasema kuwa maadam Maswahaba walikuwa wakiisoma Suwrah hiyo siku ya Ijumaa, basi hakuna neno kuisoma Ijumaa, japo kuisoma siku yoyote ni sawa na mtu atapata fadhila zilizotajwa kwenye Hadiyth hiyo. Ama kutoka kwa Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam), Wanachuoni wamesema haikuja na lafdhi ya 'kuisoma Ijumaa', bali imekuja kwa ujumla wake wa kuisoma Suwrah hiyo siku yoyote ile kama ilivyokuja hapa chini:
قال صلى الله عليه وسلم: ((من قرأ سورة الكهف كما أنزلت كانت له نورا يوم القيامة، من مقامه إلى مكة ، و من قرأ عشر آيات من آخرها ثم خرج الدجال لم يضره...)) صححه الألباني في سلسلة الأحاديث الصحيح
Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: atakayesoma Suwratul-Kahf kama ilivyoteremshwa, atakuwa na mwangaza siku ya Qiyaamah pale alipo mpaka Makkah, na atakayesoma Aayah kumi za mwisho kisha akitokea Dajjaal hatomdhuru)) [Swahiyh kama alivyoeleza Shaykh Al-Albaaniy katika Silsilatul-Ahaadiyth As-Swahiyhah]
5-Suwrah Ya Kusoma Katika Swalaah Ya Alfajiri
حديث أَبِي هُرَيْرَةَ رضي الله عنه، قَالَ: كَانَ النَّبِيُّ صلى الله عليه وسلم يَقْرَأُ فِي الْجُمُعَةِ، فِي صَلاَةِ الْفَجْرِ، آلَم تَنْزيلُ، السَّجْدَةَ، وَ هَلْ أَتَى عَلَى الإِنْسَانِ. أخرجه البخاري
Kutoka kwa Abu Hurayrah (Radhwiya Allaahu 'anhu) ambaye alisema: Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa akisoma Suwrah ya Alif-Laam-Tanziylu (Suwratus Sajdah) na Hal-Ataa 'Alal-Insaan (Suwratul Insaan)” [Al-Bukhaariy]
6-Kumswalia Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) kwa wingi:
عَنْ أَوْسِ بْنِ أَوْسٍ (رضي الله عنه) قَالَ: قَالَ رَسُولُ اللهِ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ: ((إِنَّ مِنْ أَفْضَلِ أَيَّامِكُمْ يَوْمَ الْجُمُعَةِ، فَأَكْثِرُوا عَلَيَّ مِنْ الصَّلاةِ فِيهِ، فَإِنَّ صَلاَتَكُمْ مَعْرُوضَةٌ عَلَيَّ)) قَالوا: يَا رَسُولَ اللَّهِ وَكَيْفَ تُعْرَضُ صَلاتُنَا عَلَيْكَ وَقَدْ أَرَمْتَ؟ قَالَ: يَقُولُ: بَلِيتَ قَالَ: ((إِنَّ اللَّهَ تَبَارَكَ وَتَعَالَى حَرَّمَ عَلَى الأَرْضِ أَجْسَادَ الأَنْبِيَاءِ)) رواه ابو داوُود بِاِسنادٍ صحيح
Imepokelewa kutoka kwa Aws bin Aws (رضي الله عنه) ambaye amesema: Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم ) amesema: ((Hakika siku zenu zilizo bora mno ni siku ya Ijumaa, basi kithirisheni kuniswalia siku hiyo, hakika Swalaah zenu huwa naletewa)). Maswahaba wakauliza: “Ee Rasuli wa Allaah! Vipi Swalaah zetu kuwa unaletewa na ilihali wakati huo utakuwa umeshaoza?” Akajibu: ((Hakika Allaah Ameiharamisha ardhi kula viwiliwili vya Manabii)). [Abu
Pia:
عَنْ أَبِي هُرَيْرَةَ، أَنَّ النَّبِيَّ صلى الله عليه وسلم قَالَ: (( خَيْرُ يَوْمٍ طَلَعَتْ عَلَيْهِ الشَّمْسُ يَوْمُ الْجُمُعَةِ فِيهِ خُلِقَ آدَمُ وَفِيهِ أُدْخِلَ الْجَنَّةَ وَفِيهِ أُخْرِجَ مِنْهَا وَلاَ تَقُومُ السَّاعَةُ إِلاَّ فِي يَوْمِ الْجُمُعَةِ))
Imepokelewa kutoka kwa Abuu Hurayrah (رضي الله عنه) kwamba Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema: ((Siku bora kabisa iliyochomoza jua ni siku ya Ijumaa, na hiyo ndio ameumbwa Aadam na hiyo ndio aliingizwa Jannah (Peponi) na akatolewa humo. Na Qiyaamah hakitosimamia siku yoyote isipokuwa siku ya Ijumaa)) [Muslim]
7-Kumdhukuru Allaah ('Azza wa Jalla) Kwa Wingi Khasa Nyakati Za Jioni:
Anasema Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa):
يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا إِذَا نُودِيَ لِلصَّلَاةِ مِن يَوْمِ الْجُمُعَةِ فَاسْعَوْا إِلَىٰ ذِكْرِ اللَّـهِ وَذَرُوا الْبَيْعَ ۚ ذَٰلِكُمْ خَيْرٌ لَّكُمْ إِن كُنتُمْ تَعْلَمُونَ﴿٩﴾
Enyi walioamini! Inaponadiwa kwa ajili ya Swalaah siku ya Ijumaa, kimbilieni kumdhukuru Allaah na acheni kuuza na kununua. Hivyo ni kheri kwenu mkiwa mnajua.
فَإِذَا قُضِيَتِ الصَّلَاةُ فَانتَشِرُوا فِي الْأَرْضِ وَابْتَغُوا مِن فَضْلِ اللَّـهِ وَاذْكُرُوا اللَّـهَ كَثِيرًا لَّعَلَّكُمْ تُفْلِحُونَ﴿١٠﴾
Na inapomalizika Swalaah, tawanyikeni katika ardhi, na tafuteni katika fadhila za Allaah, na mdhukuruni Allaah sana ili mpate kufaulu.
وَإِذَا رَأَوْا تِجَارَةً أَوْ لَهْوًا انفَضُّوا إِلَيْهَا وَتَرَكُوكَ قَائِمًا ۚ قُلْ مَا عِندَ اللَّـهِ خَيْرٌ مِّنَ اللَّـهْوِ وَمِنَ التِّجَارَةِ ۚ وَاللَّـهُ خَيْرُ الرَّازِقِينَ﴿١١﴾
Na wanapoona tijara au pumbao wanaikimbilia, na wanakuacha umesimama. Sema: “Yaliyoko kwa Allaah ni bora zaidi kuliko pumbao na tijara, na Allaah ni Mbora wa wenye kuruzuku. [Al-Jumu’ah (62: 9-11)]
8-Kuomba Du’aa Khasa Baada Ya Swalaah Ya Alasiri Kwani Ni Wakati Du’aa Inatakabaliwa:
عَنْ أَبِي هُرَيْرَةَ (رَضِيَ اللَّهُ عَنْهُ) أَنَّ رَسُولَ اللَّهِ (صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ) ذَكَرَ يَوْمَ الْجُمُعَةِ فَقَالَ: ((فِيهِ سَاعَةٌ لاَ يُوَافِقُهَا عَبْدٌ مُسْلِمٌ وَهُوَ قَائِمٌ يُصَلِّي يَسْأَلُ اللَّهَ تَعَالَى شَيْئًا إلاَّ أَعْطَاهُ إِيَّاهُ)) وَأَشَارَ بِيَدِهِ يُقَلِّلُهَا
Imepokelewa kutoka kwa Abuu Hurayrah (رضي الله عنه) kwamba Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) ametaja Siku ya Ijumaa akasema: ((Humo mna saa haimwafikii mja Muislamu akiwa amesimama anaswali anamwomba Allaah تعالىkitu ila Anampa)). Akaashiria kuonyesha ukaribu wake [Al-Bukhaariy (935), Muslim (852) na wengineo]
Rai za ‘Ulamaa kuhusu Saa katika siku ya Ijumaa inayotakabaliwa du’aa zimetajwa nyakati kadhaa, ila waliyokubaliana zaidi yao ni saa ya mwisho kabla ya Swalaah ya Magharibi:
عَنْ جَابِرِ بْنِ عَبْدِ اللَّهِ (رضي الله عنه) عَنْ رَسُولِ اللَّهِ (صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ) قَالَ: ((يَوْمُ الْجُمُعَةِ اثْنَتَا عَشْرَةَ سَاعَةً ،لاَ يُوجَدُ فِيهَا عَبْدٌ مُسْلِمٌ يَسْأَلُ اللَّهَ شَيْئًا إلاَّ آتَاهُ إِيَّاهُ ، فَالْتَمِسُوهَا آخِرَ سَاعَةٍ بَعْدَ الْعَصْر))
Imepokelewa kutoka kwa Jaabir bin ‘Abdillaah (رضي الله عنه) kwamba Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema: ((Siku ya Ijumaa kuna masaa kumi na mbili ambayo hapatikani mja Muislamu anayemwomba Allaah kitu ila Anampa, basi itafuteni baada ya Swalaah ya Alasiri)) [Swahiyh Abiy Daawuwd (1048), Swahiyh An-Nasaaiy (1388), Swahiyh Al-Jaami’ (8190)]
from Uislamu Wangu https://ift.tt/2SAE65M
via IFTTT
Jisajili kwenye:
Machapisho (Atom)
20-Hakika Shirki Ni Dhulma Kubwa Mno! - Isti’aadhah Kwa Asiyekuwa Allaah
إِنَّ الشِّرْكَ لَظُلْمٌ عَظِيم Hakika Shirki Ni Dhulma Kubwa Mno! 20 - Isti’aadhah (Kuomba Kinga) Kwa Asiyekuwa Allaah ...
-
Assallaam Aleykum WarahmatulLaah Wabarakatuh YAFUATAYO NI MAJINA YA MASWAHABA WANAWAKE (RADHI ZA ALLAAH...
-
Dalili 18 zinazoashiria una ujauzito wa mtoto wa kiume Awali ya yote nitoe pongezi kwa mama K na Baba K wote popote walipo kwa kazi nzuri ...
-
Assallaaam Aleykum WarahmatulLaah Wabarakatuh Naam, Ndugu zangu katika Imaani, Siku chache zimebaki kwa ajili ya Vijana wetu wanaosoma Elim...