Hadiyth ya Tatu
ن أبي هريرة قال: قال رسول الله صلى اللهعليه وسلم ((ثَلَاثٌ لَا يُكَلِّمُهُمُ اللَّهُ يَوْمَ الْقِيَامَةِ ، وَلَا يَنْظُرُ إِلَيْهِمْ ، وَلَا يُزَكِّيهِمْ وَلَهُمْ عَذَابٌ أَلِيمٌ : رَجُلٌ عَلَى فَضْلِ مَاءٍ بِالْفَلَاةِ يَمْنَعُهُ مِنَ ابْنِ السَّبِيلِ ، وَرَجُلٌ بَايَعَ رَجُلًا بِسِلْعَةٍ بَعْدَ الْعَصْرِ فَحَلَفَ لَهُ بِاللَّهِ لَأَخَذَهَا بِكَذَا وَكَذَا فَصَدَّقَهُ وَهُوَ عَلَى غَيْرِ ذَلِكَ ، وَرَجُلٌ بَايَعَ إِمَامًا لَا يُبَايِعُهُ إِلَّا لِدُنْيَا فَإِنْ أَعْطَاهُ مِنْهَا وَفَى ، وَإِنْ لَمْ يُعْطِهِ مِنْهَا لَمْ يَفِ)).
Imepokelewa toka kwa Abuu Hurayrah akisema: “Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa Sallam) amesema: ((Watatu (wa aina tatu) Allaah Hatozungumza nao Siku ya Qiyaamah, wala Hatowaangalia, wala Hatowatakasa, na watapata adhabu iumizayo. Mtu mwenye maji ya ziada jangwani anayazuia kwa mpita njia, na mtu aliyepatana na mtu kumuuzia bidhaa baada ya Alasiri, akamwapia kwa Allaah kwamba ameinunua kwa thamani kadha wa kadha akamsadiki, naye yuko kinyume na hilo, na mtu aliyempa (imaam) kiongozi bay’ah, hampi bay’ah hiyo ila kwa ajili ya dunia tu. Akimpa kitu katika hiyo dunia, hutekeleza ipasavyo, na kama hakumpa kitu katika hiyo dunia, hatekelezi chochote)). [Al-Bukhaariy, Muslim na wengineo]
Faida na Sharh ya Hadiyth
Mtu wa kwanza: Mtu mwenye maji ya ziada jangwani anayazuia kwa mpita njia.
Mtu huyo ni mwenye maji shambani kwake, au kwenye kisima chake, au kwenye tanki, au kwenye bomba lake na kadhalika, na huko aliko ni ardhi mahame isiyo na watu. Lakini watu wanapopita hapo ili wanywe au wateke anawazuia kwa roho mbaya, au chuki, au ubaguzi na kadhalika. Huyu atastahiki makamio hayo matatu Siku hiyo.
Mtu wa pili: Ni mtu aliyeuza bidhaa baada ya Alasiri, akaapa kwa mnunuzi kuwa ameinunua kwa thamani fulani ili amuuzie kwa bei ya juu zaidi
Anafanya hivyo ilhali anasema uongo, na mteja akamsadiki na akainunua kwa mujibu wa kiapo chake huku mambo ni kinyume, basi huyu anaingia pia kwenye makamio hayo.
‘Ulamaa wamejaribu kuelezea sababu ya Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) kuuhusisha hapa wakati wa Alasiri kinyume na nyakati nyinginezo. Sababu zenyewe ni:
1- Wakati huu ndio wakati bora kabisa ambapo Malaika wa usiku na mchana hukutana.
2-Alasiri ni “Asw-Swaalatul-Wustwaa” (Swalaah ya katikati) ambayo Allaah ('Azza wa Jalla) Ameipa umahususi wa kipekee wa kuilinda baada ya ujumuishi wa Swalaah nyinginezo Aliposema:
((حَافِظُوا عَلَى الصَّلَوَاتِ وَالصَّلَاةِ الْوُسْطَى))
((Hifadhini Swalaah, na Swalaah ya kati)). [Al-Baqarah (2:283)]
3-Ni wakati wa kuhitimishwa amali.
4-Ni wakati wa kupandishwa amali.
Hivyo kufanya uhalifu huo katika wakati huo inakuwa ni vibaya zaidi. Na hii haimaanishi kuwa nyakati nyingine inafaa kufanya uhalifu huo, bali ni haraam nyakati zote.
Mtu wa tatu: Ni mtu aliyetangaza utiifu wake kwa kiongozi, na hafanyi hivyo ila kwa ajili ya maslahi ya kidunia, na si kwa ajili ya Allaah.
Hii ni aina ya unafiki mbaya kabisa. Kutangaza utiifu kwa kiongozi ni wajibu kwa kila Muislamu, na kila Muislamu ni lazima awe na kiongozi, sawasawa akiwa kiongozi mkuu wa nchi, au kiongozi katika eneo analoishi. Na utiifu kwa kiongozi au imaam ni wajibu kwa kila linalomridhisha Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa). Ama linalomghadhibisha, basi ni wajibu kuliepuka.
Na utiifu huu ni lazima uwe juu ya Qur-aan na Sunnah. Atatangaza utiifu wake kuwa atende haki, atekeleze adhabu za ki-shariy’ah (huduwd), aamrishe mema na akataze munkari.
Nukta hii inatukumbusha pia kuwa amali yoyote ambayo haimkusudii Allaah ('Azza wa Jalla) bali kwa maslahi ya kidunia, basi imeharibika na mfanyaji wake anachuma madhambi.
Ukiwa na Swali kuhusu Dini, Maoni au Ushauri, Tafadhali wasiliana na Imaam Masjid Tawbah kwa Call/Sms/Whatssap namba 0714974397 au tuma ujumbe http://bit.ly/2LDVR23
Na Allaah anajua zaidi
from fisabilillaah.com http://bit.ly/2RE12Wg
via IFTTT
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni