Hadiyth ya Pili
Mwenye Kuburuza Nguo yake (Isbaal), Msimbuliaji,
na Mchuuzi wa Bidhaa yake kwa kiapo cha Uongo
عن أبي ذر، عن النبي صلى الله عليه وسلمقال: (( ثلاثةٌ لا يكلمهم الله يوم القيامة، ولاينظر إليهم، ولا يزكيهم، ولهم عذابٌ أليمٌ)) ،قال: فقرأها رسول الله ثلاث مرارٍ، قال أبوذر: خابوا وخسروا، من هم يا رسول الله؟قال: المسبل إزاره، والمنان، والمُنَفِّقُ سلعتهبالحلف الكاذب)) رواه مسلم.
Imepokelewa toka kwa Abuu Dharr (Radhwiya Allaahu 'anhu) toka kwa Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akisema: ((Watatu (wa aina tatu) Allaah Hatozungumza nao Siku ya Qiyaamah, wala Hatowaangalia, wala Hatowatakasa, na watapata adhabu iumizayo)). Akasema: Rasuli akayasema hayo mara tatu. Abu Dharr akasema: Wamepita utupu na wamekula hasara. Ni nani hao ee Rasuli wa Allaah? Akasema: ((Mwenye kuburuza nguo yake, msimbuliaji, na mchuuzi wa bidhaa yake kwa kiapo cha uongo)).[Imesimuliwa na Muslim].
Faida na Sharh ya Hadiyth
Hadiyth hii tukufu inaonyesha hatari kubwa kabisa inayowakabili watu wa sampuli hizi tatu za madhambi yanayozingatiwa kuwa ni katika madhambi makubwa kufikia ngazi ya kunyimwa na kuyakosa mambo hayo matatu muhimu kabisa katika siku hiyo ya hisabu, na hata kumfanya Abuu Dharr kusema hayo aliyoyasema na kutaka kuwajua ni akina nani hao ili awajue na aepukane na makosa hayo.
Na kutokana na ubaya na ukubwa wa hasara, Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amelikariri neno hilo mara tatu kuonyesha uhatari wake na umuhimu wa kujiepusha na mambo hayo.
Mtu wa kwanza: Mwenye kuburuza nguo (Isbaal)
Ni mtu mwenye kuiachia na kuiteremsha nguo yake ikashuka chini ya vifundo viwili vya miguu. Sheikh Ibn Baaz (Rahimahu-Allaah) amesema: "Ni wajibu kwa mwanamume Muislamu amche Allaah, na anyanyue nguo yake ikiwa ni kanzu, au kikoi, au suruali na kadhalika, isishuke chini ya vifundo viwili vya miguu. Na ubora zaidi kwake iwe nguo yake kati ya nusu muundi hadi kwenye vifundo.”
Hata kuna baadhi ya Mafuqahaa wametanua wigo wa hilo kufikia kwenye mikono ya nguo. Wanasema kuwa mikono ya nguo isivuke kifundo cha mkono na kufunika sehemu ya kiganja. Wengine hata kilemba kuwa kisidizi sana urefu na upana, na mikia yake isidizi zaidi ya nchi moja (shibr). Hawa wanaitegemea Hadiyth nyingine ya Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) isemayo:
((الإسبال في الإزار والقميص والعمامة، منجَرَّ شيئًا خيلاء لم ينظُرِ الله إليه يوم القيامة)).
(("Isbaal" iko katika izari, kanzu na kilemba. Yeyote mwenye kuburuza chochote (katika hivyo) kwa kibr, basi Allaah Hatomtizama Siku ya Qiyaamah)). [Imepokelewa toka kwa Saalim bin ‘Umar toka kwa baba yake toka kwa Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam)]
Kisha Mafuqahaa wamezitoa hali nne nje ya makhitilafiano, kwa maana kwamba wamekubaliana wote katika hali hizo.
Ya kwanza Kuburura nguo kimakusudi kwa kibr. Hili ni haraam, na ni katika madhambi makubwa.
Ya pili Kuburuza kutokana na dharura iliyompata mtu kama kuficha ugongwa kwenye makanyagio yake au mfano wake. Hili linajuzu. Ni kama kuvaa hariri kwa mwanamume kutokana na ugonjwa wa ngozi.
Ya tatu Kuburuza wanawake maabaya na mabaibui yao na kadhalika. Hili limeruhusiwa na Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) kwa kiasi cha inchi moja ili kusitiri makanyagio yao. Hili pia halina mahitalifiano.
Ya nne Kuburuza kutokana na dharura ya ghafla iliyomtokezea mtu kama tukio la kutisha, au hasira kali, au kusahau na kadhalika. Hili halina mahitalifiano pia.
Ama kwa upande wa hukmu ya Isbaal bila kusudio la kibr, Mafuqahaa wamekhitalifiana kwa kauli mbili:
Kauli ya kwanza
Kufanya isbaal bila kukusudia kibr si haraam. Hii ni kauli ya Jamhuri ya ‘Ulamaa wa madhehebu manne ingawa wametofautiana katika nukta ya kuwa makruwh (chukizo) hu au jaaiz (kukubalika), lakini haifikii mpaka wa kuwa ni haraam. Wametolea dalili hili kwa baadhi ya Hadiyth ikiwemo ile ambayo Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alimwambia Abu Bakr: ((Wewe si katika wenye kufanya hilo kwa kibr)).
Ibn Qudaamah amesema kwenye Al Mughniy (2/298):
“Ni makruhu kuburuza kanzu, izari na suruwali. Ikiwa atafanya hivyo kwa njia ya kibr, basi ni haraam.”
Na An Nawawiy katika Sharh Muslim (14/62) amesema: “Haijuzu kuiteremsha chini ya mafundo mawili ya mguu ikiwa ni kwa kibr. Na kama ni kwa jinginelo, basi ni makruwh (chukizo).
Kauli ya pili
“Isbaal ni haraam kwa hali yoyote. Na kama ni kwa kibr, basi uharamu wake ni mkubwa zaidi.”
Kauli hii imeungwa mkono na ‘Ulamaa wa kale kama Ibn Al-‘Arabiy, Ibn Hajar, Asw- Swan-‘aaniy na wengineo.
Pia ‘Ulamaa wengineo kama Masheikh Ibn Baaz, Ibn ‘Uthaymiyn, Ibn Jabriyn, Al Fawazaan na ‘Ulamaa wa Al-Lajnah Ad-Daaimah (Tume Ya Kudumu ya Utoaji Fatwa).
Hawa wametolea dalili baadhi ya Hadiyth ambazo baadhi yake ni mutwlaq (jumuishi) ambazo hazikutaja kibr, na nyingine muqayyad (ainishi), ambazo zimeainisha kibr kuwa sababu.
Mtu wa pili: Ni msimbuliaji
"المنان" . "المنان" linanyambulika toka kisoukomo (maswdar)"المن" ambalo lina maana nne.
Kwanza Katika vita, neno hili lina maana ya kamanda au mkuu wa jeshi kumwachalia huru mateka wa kikafiri bila kuchukua fidia yoyote. Ni kama Kauli Yake Ta’alaa:
((فَإِمَّا مَنًّا بَعْدُ وَإِمَّا فِدَاءً حَتَّىٰ تَضَعَ الْحَرْبُ أَوْزَارَهَا))
((Kisha ima (wafanyieni) ihsaan baada ya hapo au wajifidie mpaka vita vitue mizigo yake)) [Muhammad 47: 4]
Pili Ni Jina kati ya Majina ya Allaah (Al-Mannaan) lenye maana ya Mtoaji hisani na Mpaji wa neema zote kiasili. Kwa maana kwamba neema zote zinatoka Kwake hata kama zitafikishwa au kuwasilishwa au kufanywa na watu. Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Anatuambia:
(( لَقَدْ مَنَّ اللَّهُ عَلَى الْمُؤْمِنِينَ ))
((Hakika Allaah Amewafanyia Waumini hisani kubwa)) [Aal- ‘Imraan (4:164)]
Na pia:
كَذَلِكَ كُنْتُمْ مِنْ قَبْلُ فَمَنَّ اللَّهُ عَلَيْكُمْ
((Hivyo ndivyo mlivyokuwa kabla na Allaah Akakufanyieni ihsaan basi hakikisheni)). [An Nisaa (5:94)]
Na katika Sunnah, Hadiyth ya Anas inasema:
((اللهم إني أسألك بأن لك الحمد، لا إله إلاأنت المنان، بديع السموات والأرض...))
((Ee Allaah! Hakika mimi nakuomba kwa kuwa Himdi ni Yako. Hapana mwabudiwa wa haki ila Wewe Mhisani na Mpaji wa neema, Muumbaji wa mbingu na ardhi bila ruwaza)). [Imesimuliwa na wanne, pamoja na Al Haakim aliyesema ni Swahiyh. Adh-Dhahabiy amewafikiana naye, na Al-Albaaniy kasema ni Swahihy]
Tatu Ni aina ya chakula mithili ya asali ambayo Banu Israaiyl waliteremshiwa na Allaah ('Azza wa Jalla).
Nne Ni mtu kuelezea hisani, wema, huduma au msaada aliomfanyia mtu mwingine kwa njia ya masimango, na kumsababishia anayesimangwa adha na kutahayuri. Maana hii ndiyo iliyokusudiqwa katika Hadiyth hii Tukufu.
Masimango ya aina yoyote yakiwa makubwa au madogo ni katika madhambi makubwa yatakayomwingiza mtu ndani ya makamio hayo matatu yaliyokuja kwenye Hadiyth hii ya Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam).
Masimbulizi kama haya hufuta thawabu zote za msimbuliaji. Mtu akitoa swadaqah, kisha akamsimbulia anayempa, basi thawabu zake zote huyeyuka. Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Anatuambia:
( يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا لَا تُبْطِلُوا صَدَقَاتِكُمْبِالْمَنِّ وَالْأَذَى ))
((Enyi walioamini! Msiharibu swadaqah zenu kwa kusimbulia na maudhi)). [Al-Baqarah (2:264)]
Ibn ‘Abbaas (Radhwiya Allaahu ‘anhumaa) amesema: “Wema hautimu ila kwa mambo matatu: Kwa kuuharakisha, kuudogesha na kuusitiri.”
Masimbulizi mtu anaweza kuyaona ni jambo dogo, kumbe madhara yake ni makubwa mno.
Mtu wa tatu: Ni mfanya biashara au mchuuzi mwenye kutumia kiapo ili kuvutia biashara yake.
Hili ni janga baya na mtihani mkubwa unaowakabili wachuuzi na wafanya biashara wengi. Huwaapia wateja kwa viapo vyote kwamba bidhaa ni nzuri, ina ubora, haina tatizo lolote na kadhalika ili ima kuongeza thamani yake au kumvuta mteja ainunue. Wengine huapa kwamba wameinunua kwa bei kadhaa na bei wanayouzia haishuki hata kidogo wakati ni kinyume na hivyo. Na hapa hutumia Jina la Allaah ('Azza wa Jalla) kwa ajili ya kuwalaghai wateja, na hichi ndicho kiini cha hayo yatakayomsibu Siku hiyo ya Qiyaamah, kwa kuwa mchezo huu ni haraam, na dhambi kati ya madhambi makubwa. Na hii ni kutokana na haya yafuatayo:
1- Ni kudharau kwake Jina la Allaah ('Azza wa Jalla) katika kiapo hicho na kukhalifu amri ya Allaah ('Azza wa Jalla) ya kuhifadhi kiapo Aliposema:
(( وَاحْفَظُوا أَيْمَانَكُمْ ))
((Na hifadhini viapo vyenu)). [Al-Maaidah (5:89)]
2-Kusema kwake uongo, kwa kuwa bidhaa iko kinyume na anavyoinadia. Uongo ni katika sifa mbaya kabisa zisilolaikiana na Muislamu na ambazo inabidi Muislamu ajiepushe nazo ili asije kusajiliwa kwenye buku la wasemao uongo.
3-Kula kwake mali anayoichuma kwa njia ya kiapo hicho kwa batili, na kiapo chake hicho ni katika viapo vyenye kubeba madhambi makubwa zaidi.
Kiapo hiki ni kile kiitwacho الغموس. Imekuja katika Swahihy mbili kwamba Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:
(( من حلف على يمين هو فيها فاجر يقتطعبها مال امرئ مسلم، لقي الله وهو عليهغضبان))
((Mwenye kuapa juu ya kiapo ambacho yeye ni mwongo ili amege kwacho mali ya mtu Muislamu, atakutana na Allaah Akiwa Amemghadhibikia)). [Imepokelewa na ‘Abdullaah bin Mas’uwd (Radhwiya Allaahu ‘anhu).
Ama mchuuzi kuapa kila anapouza au kununua hata kama ni mkweli, hili pia ni haraam, na ni moja kati ya madhambi makubwa. Ni kutokana na Hadiyth ya Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam)
((ثلاثة لا يكلمهم الله يوم القيامة ولا يزكيهمولهم عذاب أليم: أشيمط زان، وعائلمستكبر، ورجل جعل الله بضاعته لا يشتريإلا بيمينه ولا يبيع إلا بيمينه))
((Watu watatu Allaah Hatozungumza nao Siku ya Qiyaamah, wala Hatowatakasa, na watapata adhabu iumizayo: Kikongwe mzinzi, masikini mwenye kibri, na mtu ambaye Amemfanya Allaah bidhaa yake; hanunui ila kwa kumwapia, na hauzi ila kwa kumwapia)). [Imesimuliwa na Atw-Twabaraaniy katika Hadiyth ya Sulaymaan]
Sheikh Ibn ‘Uthaymiyn (Rahimahu-Allaah) amesema: “Maana yake ni kuwa kila anaponunua huapa, na kila anapouza huapa ili kupata faida zaidi. Na huyu amestahiki adhabu hii, kwa kuwa, kama ni mkweli, basi viapo vyake vinaonyesha kuwa havina tena thamani wala uzito kwake, ni kama kitu cha mchezo tu, na kukhalifu kwake Kauli Yake Ta’alaa:
واحفظوا أَيْمَانَكُمْ
Na hifadhini viapo vyenu [Al-Maaidah:
Na kama ni mwongo, basi anakuwa amekusanya mambo manne yaliyotolewa onyo.”
Ama hukmu ya kuapa kwenye manunuzi na mauzaji bila kuwa ni tabia ya muuzaji au mnunuzi, ‘Ulamaa wanasema kuwa kiasili ni makruwh (chukizo) Ni kutokana na ujumuishi wa Kauli Yake Ta’alaa:
إِنَّ الَّذِينَ يَشْتَرُونَ بِعَهْدِ اللَّهِ وَأَيْمَانِهِمْ ثَمَنًاقَلِيلًا أُولَئِكَ لَا خَلَاقَ لَهُمْ فِي الْآخِرَةِ وَلَايُكَلِّمُهُمُ اللَّهُ وَلَا يَنْظُرُ إِلَيْهِمْ يَوْمَ الْقِيَامَةِ وَلَايُزَكِّيهِمْ وَلَهُمْ عَذَابٌ أَلِيمٌ)
((Hakika wale wanaobadilisha ahadi ya Allaah na viapo vyao kwa thamani ndogo; hao hawana sehemu yoyote katika Aakhirah na wala Allaah Hatowasemesha na wala Hatowatazama Siku Ya Qiyaamah na wala Hatowatakasa na watapata adhabu iumizayo)). [Aal ‘Imraan (3:77)]
Na kwa Hadiyth isemayo:
((الحلف منفقة للسلعة.. ممحقة للبركة))
((Kuapa kunapromoti bidhaa, kunafuta barkah)). [Hadiyth Marfu’u iliyopokelewa na Abuu Hurayrah (Radhwiya Allaahu ‘anhu) [Imesimuliwa na Al-Bukhaariy na Muslim]
Ama kuapa kwa haja bila kukithirisha, hili halina ubaya.
Na Allaah anajua zaidi
Inaendelea....Usikose sehemu ya 2
from fisabilillaah.com http://bit.ly/2RXumpL
via IFTTT
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni