Tofauti ya Rasuli na Nabiy
Assallaam Aleykum WarahmatulLaah Wabarakatuh
‘Ulamaa wamesema mengi kuhusu tofauti baina ya Rasuli na Nabiy. Wakakubaliana wengi wao kwamba Rasuli ni ambaye ameteremshiwa shariy’ah na akaamrishwa kubalighisha. Ama Nabiy ni ambaye ametumwa na Allaah ('Azza wa Jalla) bila kuteremshiwa shariy’ah mpya naye hutumia shariy’ah ya Rasuli aliyemtangulia.
Shaykhul-Islaam ibn Taymiyyah amesema: “Rasuli ni ambaye aliyetumwa kwa kaumu makafiri waliokanusha. Nabiy ni aliyetumwa kwa Waumini kwa shariy’ah ya Rasuli wa kabla yake awafunze na awahakumu baina yao kama Anavyosema Allaah ('Azza wa Jalla):
إِنَّا أَنزَلْنَا التَّوْرَاةَ فِيهَا هُدًى وَنُورٌ ۚ يَحْكُمُ بِهَا النَّبِيُّونَ الَّذِينَ أَسْلَمُوا لِلَّذِينَ هَادُوا
Hakika Tumeteremsha Tawraat humo mna mwongozo na nuru; ambayo kwayo, Nabiy waliojisalimisha (kwa Allaah), waliwahukumu Mayahudi... [Al-Maaidah: 44]
Kwa ufupi ni kuwa kila Rasuli ni Nabiy lakini si kila Nabiy ni Rasuli. Na ‘Ulamaa wamekubaliana kwamba Rasuli ni bora kuliko Nabiy. Hivyo Rasuli ana daraja kubwa kuliko Nabiy.
Na katika ambao Allaah ('Azza wa Jalla) Amewafadhilisha juu ya wengine ni ambao wanaojulikana kwa Ulul-‘Azmi (wenye azimio la subira katika da'wah [ulinganiaji]) kama Anavyosema Allaah ('Azza wa Jalla):
فَاصْبِرْ كَمَا صَبَرَ أُولُو الْعَزْمِ مِنَ الرُّسُلِ
Basi subiri (ee Muhammad صلى الله عليه وآله وسلم) kama walivyosubiri wenye azimio madhubuti miongoni mwa Rusuli [Al-Ahqaaf: 38]
Na walio mashuhuri kama walivyokubaliana baadhi ya 'Ulamaa ni ambao wametajwa katika kauli ya Allaah ('Azza wa Jalla):
وَإِذْ أَخَذْنَا مِنَ النَّبِيِّينَ مِيثَاقَهُمْ وَمِنكَ وَمِن نُّوحٍ وَإِبْرَاهِيمَ وَمُوسَىٰ وَعِيسَى ابْنِ مَرْيَمَ ۖ وَأَخَذْنَا مِنْهُم مِّيثَاقًا غَلِيظًا ﴿٧﴾
Na pale Tulipochukua kutoka kwa Manabii fungamano lao na kutoka kwako (ee Muhammad صلى الله عليه وآله وسلم) na kutoka kwa Nuwh, na Ibraahiym, na Muwsaa, na ‘Iysaa mwana wa Maryam; na Tukachukua kutoka kwao fungamano gumu. [Al-Ahzaab: 7]
Na Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amefadhilishwa kwa fadhila adhimu na nyingi mno kama Anavyosema Allaah (‘Azza wa Jalla) katika kauli Yake:
وَكَانَ فَضْلُ اللَّـهِ عَلَيْكَ عَظِيمًا ﴿١١٣﴾
Na fadhila za Allaah juu yako daima ni adhimu. [An-Nisaa: 113]
Na Allaah anajua zaidi
from fisabilillaah.com http://bit.ly/2LCy1DU
via IFTTT
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni