Kujifunza elimu ya Kishari´ah ni nuru
Kwa hali yoyote, kujifunza elimu ni jambo lisilokuwa na shaka kwamba ndio maisha na nuru iliyoamrishwa na Allaah (Jalla wa ´Alaa), ikaamrishwa na Mtume Wake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na wakakokoteza kwayo. Amesema (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):
“Mwenye kushika njia akitafuta humo elimu, basi Allaah humsahilishia njia ya kuelekea Peponi. Hawakusanyiki watu katika nyumba miongoni mwa nyumba za Allaah, wakikisoma Kitabu cha Allaah na wakadarasishana baina yao, isipokuwa huteremka juu yao utulivu, rehema huwafunika, Malaika huwazunguka na Allaah huwataja kwa wale walioko pamoja Naye.”[1]
Amesema (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):
“Malaika hukunjua mbawa zao kwa mwenye kutafuta elimu hali ya kuridhia kile anachokifanya.”
Haya ni makokotezo juu ya kujifunza elimu na kuikimbilia ili dini ya mja iweze kunyooka, anufaike mwenyewe na pia awanufaishe wengine. Ni jambo lisilokuwa na shaka ya kwamba ikitoweka elimu na wakatoweka wanachuoni, basi Ummah utaangamia. Amesema (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):
“Hakika Allaah hatoiondoa elimu hii kwa kuinyakua kutoka kwenye vifua vya wanachuoni, lakini ataiondoa elimu kwa kufa kwa wanachuoni, mpaka pasibakie mwanachuoni yoyote ndipo watu watawachukua viongozi wajinga. Watawauliza maswali wafutu bila ya elimu. Matokeo yake watapotea na kuwapoteza wengine.”[2]
Kutoa fatwa pasi na elimu ni kupotea na kuwapoteza wengine. Ni lazima fatwa iwe juu ya elimu katika Qur-aan na Sunnah. Vinginevyo inakuwa ni upotevu na maangamivu. Haya hayawezi kupatikana isipokuwa kwa kusoma na mtu awe na hima ya kusoma kabla ya muda kupita midhali wanachuoni wapo. Utafika wakati ambapo hakuna mwanachuoni hata mmoja, hapo ndipo watu watawaelekea wajinga, wenye kujifanya ni wanachuoni na wasomaji ambapo watatoa fatwa pasi na elimu na matokeo yake wapotee wao na wapotoshe wengine.
[1] Ameipokea Muslim (2699).
[2] Ameipokea al-Bukhaariy (100) na Muslim (2673).
Rejea kitab Sharh Nawaaqidh-il-Islaam, uk. 196-197
https://ift.tt/2WqZ0qb i live islam
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni