Translate

Ijumaa, 29 Machi 2019

Usidharau katika wema jambo lolote hata bashasha kwa ndugu yako

Siku moja Hudhaifa (Allah amridhie) alimsikia Mtume (rehema za Allah na amani zimshukie) akisema: “Hakika mtu mmoja miongoni mwa wale waliokuwapo kabla yenu (katika umati zilizopita) alijiwa na Malaika kwa ajili ya kuchukua roho yake, akasema, ‘Je, kuna kheri yoyote umeifanya?’ Akasema, ‘Sijui.’ Malaika akamuambia, ‘Tazama,’ akasema, ‘Sijui kitu chochote (nilichokifanya) isipokuwa duniani nilikuwa nikiwauzia watu vitu, nikimpa tajiri muda wa ziada kulipa deni na ninamsamehe maskini. Allah akamuingiza peponi,” [Bukhari].

Mafunzo ya tukio hili

Watu wataingia peponi kwa fadhila za Allah
Muislamu hatakiwi kudanganyika na wingi wa matendo anayoyafanya kwa kuona kuwa amali anazozifanya zinatosha kumuingiza peponi. Watu wataingia peponi kwa fadhila za Allah Mtukufu kupitia njia zake, yaani sababu zinazopelekea kupata fadhila za Allah. Yapo mambo lukuki ambayo Mwenyezi Mungu ametuamuru kuyafanya ili tuvune thawabu nyingi na hatimaye atuingize peponi kwa huruma yake na fadhila zake.

Kukithirisha matendo mema
Tukio hili linatupa hamasa ya kukithirisha kufanya mambo mema hasa ikizingatiwa kuwa Muislamu hajui ni aina gani ya ibada ambayo akiifanya itapelekea kupata fadhila za Allah na hatimaye kuingia peponi.

Katika tukio hili, tumeshuhudia mmoja wa waja wa Allah akiwapa watu muda wa kutosha wa kulipa madeni na kuwasamehe watu masikini na wale walioshindwa kuyalipa. Jambo hili lilimpendeza mno Allah hadi akamuingiza mja wake huyo peponi.

Na hayo ndiyo makusudio na shabaha ya Sharia ya Kiislamu, ambayo licha ya kuwahimiza watu kusaidiana pia inazingatia hali na mazingira yao na si kung’ang’ania makubaliano pekee. Mwenyezi Mungu anasema “Na akiwa [mdaiwa] ana shida, basi [mdai] angoje mpaka atakapojiweza. Na mkilifanya deni kuwa ni sadaka, basi ni bora kwenu, ikiwa mnajua.” [Qur’an, 2:280].

Kuwa na nyoyo za huruma
Duniani kuna watu wapole wenye imani, na ambao Allah amewapa ukarimu wa kuwasaidia wanyonge, maskini na wenye uhitaji. Kupitia kwao watu wengi wanajikwamua na hali ngumu ya maisha. Allah Mtukufu anawapenda watu wa aina hii kutokana na kujitolea kwao katika kuwanufaisha waja wake.

Katika kulibainisha hilo, Mtume (rehema za Allah na amani zimshukie) amesema: “Mtu anayependwa zaidi kwa Allah Mtukufu ni yule mwenye kuwanufaisha watu, na matendo yanayopendeza sana kwa Allah ni furaha unayoiingiza kwa Muislamu au kumuondoshea tatizo, au kumlipia deni,” [Twabraniy].

Kuwa mwema au muovu
Katika maisha yake hapa ulimwenguni, mwanadamu hufanya mambo mema yatakayobaki katika kumbukumbu nzuri hata baada ya kufa. Kwa upande mwingine, mwanadamu hufanya mambo maovu ambayo baada ya kufa yataacha kumbukumbu mbaya kwa walimwengu.

Katika tukio hili tunaona namna mja huyu wa Allah alivyofanya matendo mema yenye kuwanufaisha watu hadi Allah akamfanya kielelezo cha watu wema na matendo yake kubaki katika kumbukumbu nzuri hata baada ya kufa kwake. Kadri mali yake ilipoongezeka ndivyo alivyomshukuru Mola wake kwa kauli na matendo.

Kutokana na wingi wa mali yake watu walikuwa wakimuendea na kumueleza shida zao, akawa anawakopesha na ulipofika muda wa kulipa madeni alikuwa akitazama hali ya wale anaowadai, akiwapa watu muda wa ziada kulipa madeni yao na kuwasamehe wanyonge, maskini na walioshindwa kulipa.

Huruma ya Allah
Tukio hili pia linatupa mwangaza juu ya huruma ya Allah juu ya waja wake. Pamoja na mja wake huyu kufanya amali njema chache, Allah alimruzuku pepo kutokana na tabia yake ya kuwahurumia watu.

Ni jambo jema mtu kufanya kheri kwa ajili ya manufaa binafsi na ya jamii nzima. Mfano wa kheri hizo ni kama vile kutoa sadaka, kuwalingania watu, kulea yatima, kusaidia maskini na mafukara na kutoa ufadhili wa masomo.

Fadhila za kusaidia watu
Zimethibiti fadhila nyingi ndani ya Qur’an Tukufu na Sunna (Hadithi) za Mtume (rehema za Allah na amani zimshukie) kwa mtu mwenye kuwasaidia watu pindi wanapokabiliwa na shida na matatizo mbalimbali. Mtume (rehema za Allah na amani zimshukie) amesema: “Yeyote atakayemfanyia wepesi mtu aliyepatwa na uzito (shida) Allah atamfanyia wepesi duniani na Akhera.” [Muslim].

Na katika riwaya ya Imam Ahmad, Mtume amesema: “Atakayemuondoshea yule anayemdai, au kumuondoshea kabisa deni lake, basi Siku ya Kiyama atakuwa chini ya kivuli cha arshi.” Hizi ni fadhila kubwa ambazo aghalabu watu wengi huzikosa kutokana na nyoyo zao kuegemea zaidi matamanio ya kidunia na kusahau njia za kheri zenye kujenga upendo katika maisha ya kijamii.



from TIF https://ift.tt/2FM0E0m
via IFTTT

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni

20-Hakika Shirki Ni Dhulma Kubwa Mno! - Isti’aadhah Kwa Asiyekuwa Allaah

  إِنَّ الشِّرْكَ لَظُلْمٌ عَظِيم   Hakika Shirki Ni Dhulma Kubwa Mno!   20 - Isti’aadhah  (Kuomba Kinga) Kwa Asiyekuwa Allaah   ...