Maandamano hayo yamefanyika sambamba na kuanza kusikilizwa kesi kuhusu mauaji hayo iliyowasilishwa na Gambia katika Mahakama ya Kimataifa ya Uadilifu (ICJ) nchini Uholanzi kwa niaba ya nchi wanachama katika Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu (OIC).
Watetezi wa haki za binadamu walikusanyika jana na kufanya maandamano huko Hague wakati mahakama ya ICG ilipoanza kikao cha kwanza cha kusikiliza kesi ya mauaji ya kimbari dhidi ya Waislamu wa Myanmar. Aung San Suu Kyi ambaye ni kiongozi wa chama tawala nchini Myanmar na aliyewahi kuwa mshindi wa tuzo ya amani na Nobel ndiye anayeiwakilisha Myanmar katika kesi hiyo. Wakaguzi wa Umoja wa Mataifa wanasema kuwa, Mabudha na jeshi la Myamnar wamefanya mauaji ya halaiki na jinai kubwa dhidi ya Waislamu wa Rohingya ikiwa ni pamoja na kubaka wanawake, kuchoma moto nyumba na vijiji vyao na kuwaua kwa shabaha ya kuangamiza kizazi chao.
Kuanzia Agosti 25 mwaka 2017 Waislamu zaidi ya 740,000 wa jamii ya Rohingya walilazimika kuyahama makazi yao kwa umati katika jimbo lao la Rakhine na kukimbilia nchi jirani ya Bangladesh walikojiunga na wenzao wengine laki mbili waliokuweko nchini humo, baada ya vikosi vya jeshi la Myanmar na Mabudha wenye misimamo ya kufurutu ada kuanzisha wimbi kubwa la hujuma na ukandamizaji dhidi ya Waislamu hao.
Aliyekuwa Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa Zeid Ra'ad Al Hussein alisema kuwa uhalifu unaofanywa na Mabudha kwa himaya ya serikali nchini Myanmar dhidi ya Waislamu wa jamii ya Rohingya ni mauaji ya kimbari.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni