Mufti Mkuu wa Tanzania Sheikh Abubakar Zuberi ametangaza kupiga marufuku dufu na kaswida maarufu kama ”mziki moto” ambazo amesema kuwa, zinaaibisha na kuchafua sura ya Uislamu huku zikitoka nje ya utamaduni na maadili ya dini tukufu ya Kiislamu.
Akitangaza uamuzi huo hapo jana Mufti Mkuu Sheikh Abubakar Zuberi alisema kama ninavyomnukuu: Nikiwa Sheikh Mkuu na Mufti wa Tanzania, kwa niaba ya Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (BAKWATA) nachukua fursa hii adhimu kuzuilia na kupiga marufuku dufu na kaswida zinazojulikana kwa jina la mziki moto kote Tanzania ambazo zinaaibisha Uislamu na zimetoka nje ya maadili na utamaduni wa Kiislamu na ambazo zinachafua sura nzuri ya Uislamu na maadili yake.
Mufti Mkuu wa Tanzania Sheikh Abubakar Zuberi amesema kuwa, anawataka watu wanaofanya hivyo kuacha mara moja, kwani Uislamu ni dini ya akhlaq na maadiili mema na mafunzo sahihi yanayotokana na Qur'ani na mafunzo ya Mtume Muhammad SAW.
Mufti Abubabak Zuberi amewataka piia waalimu wa madrasa zote nchini Tanzania kufundisha misingi mizuri na kujenga vijana ili wawe watu wema na wacha Mungu ambao watakuwa viongozi bora wa baadaye.
Sheikh Abubakar Zuberi amewaagiza Masheikh wote nchini Tanzania wa mikoa, wilaya, kata na Maimamu wote kukemea vikali upigaji dufu na kaswida unaokiuka maadili.
Mufti Mkuu wa Tanzania ameonya kuwa, endapo hatua hizo za upigaji dufu na uimbaji kaswida zinazokiuka maadili utaendelea, basi hatua za kinidhamu zitachukuliwa dhidi ya wahusika.
Ikumbukkwe kuwa, Mufti Mkuu wa Tanzania ametangaza uamuzi huo baada ya hivi karibuni kuenea kwa kasi katika mitandao ya kijamii video zinazoonyesha watu waopiga dufu na kuimba kaswida katika mtindo unaokiuka maadili ya Uislamu na kuchafua sura nzuri ya Uislamu.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni