Hadiyth: Allaah Ndiye Mpangaji Bei
(Faida Na Sharh)
Imeandaliwa Na: 'Abdullaah Mu'aawiyah (Abu Baasim)
Imepokelewa na Anas (Radhwiya Allaahu 'anhu) kwamba kulitokea mfumuko wa bei ya bidhaa enzi ya Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam). Watu wakasema: “Ee Rasuli wa Allaah! Tupangie bei.” Akasema:
((إِنَّ اللَّهَ هُوَ الْمُسَعِّرُ الْقَابِضُ الْبَاسِطُ الرَّزَّاقُ، وَإِنِّي لَأَرْجُو أَنْ أَلْقَى رَبِّي وَلَيْسَ أَحَدٌ مِنْكُمْ يَطْلُبُنِي بِمَظْلِمَةٍ فِي دَمٍ وَلَا مَالٍ))
((Hakika Allaah Ndiye Mpangaji bei, Mwenye Kubana, Mwenye Kukunjua na Mwingi wa Kuruzuku. Na hakika mimi, bila shaka, ninataraji kukutana na Rabb wangu, na ilhali hakuna yeyote kati yenu anayenitafuta kwa dhulma katika damu wala mali)) [Imaam Ahmad na wengineo]
Faida Na Sharh:
Katika Hadiyth hii tukufu, kuna faida kadhaa:
Kwanza:
Mfumuko wa bei na ughali wa vitu, ni jambo ambalo liko Mkononi mwa Allaah ('Azza wa Jalla). Yeye Ndiye Akunjuaye na Abanae, na Ndiye Mwenye Kuongeza na Kupunguza. Anazikunjua riziki bei ya vitu ikashuka, na Anazibana na kuwa chache, na bei ya vitu ikapanda. Mvua zinapokosekana na mavuno kupungua, bei ya mazao hupanda, lakini zikinyesha katika wakati na kwa vipimo mwafaka, mazao huvunwa kwa wingi na bei hupungua. Na haya yote yako Mkononi Mwake Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa).
Na ikiwa mambo haya yako chini ya udhibiti wa Allaah ('Azza wa Jalla), basi ni juu ya waja kutegemeza nyoyo zao kwa Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) na kumwomba daima Awakunjuulie riziki zao, bei ya vitu ishuke na maisha yawe nafuu zaidi. Na ili kukubaliwa hili, ni lazima waja hawa wamridhishe Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) kwa kumtii, kuzishukuru neema Zake na kujiepusha na maasia. Wakifanya hivi, Allaah ('Azza wa Jalla) Atawafungulia milango ya Baraka za mbinguni na ardhini. Anatuambia:
وَلَوْ أَنَّ أَهْلَ الْقُرَى آمَنُوا وَاتَّقَوْا لَفَتَحْنَا عَلَيْهِمْ بَرَكَاتٍ مِنَ السَّمَاءِ وَالْأَرْضِ وَلَكِنْ كَذَّبُوا فَأَخَذْنَاهُمْ بِمَا كَانُوا يَكْسِبُون
Na lau watu wa kijiji wangeliamini na kucha, Tungeliwafungulia barakah toka mbinguni na ardhini, lakini walikadhibisha, Tukawaadhibu kwa sababu ya waliyokuwa wakiyachuma)). [Al-A’raaf: 96]
Pili:
Enzi bora kabisa na iliyotakasika zaidi ya Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Maswahaba wake, haikusalimika na tatizo la mfumuko wa bei. Hiki ni kiashirio kuwa jamii au nchi yoyote inaweza kukabiliwa na tatizo hili na misukosuko mingineyo hata kama watu wake ni wachaji, wema na waadilifu. Majaribio mara yanakuwa adhabu na wakati mwingine yanakuwa kwa ajili ya kufuta mabaya na kunyanyua daraja.
Tatu:
Unapotokea mfumuko wa bei, Muislamu anatakiwa asipaparike, bali atulize roho yake na kuwa na yakini kuwa Alichopangiwa na Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) ni lazima atakipata na ambacho hakupangiwa hatokipata vyovyote aendavyo mbio. Riziki yake imeandikwa tokea yuko tumboni mwa mama yake.
Nne:
Unapotokea mfumuko wa bei, haijuzu kuwatupia lawama viongozi wa nchi, kwani suala hili liko Mkononi mwa Allaah ('Azza wa Jalla) Peke Yake.
Tano:
المسعر ni moja kati ya Sifa za Sifa za Matendo ya Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) kama alivyosema Imaam Ibn ‘Uthaymiyn alipoulizwa [Liqaaul-Baab Al-Mafutwh]
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni