Akizungumza Jumatano ya juzi tarehe 11 Disemba katika Mahakama ya Kimataifa ya Uadilifu mjini The Hague Uholanzi, Aung San Suu Kyi alitetea hatua ya serikali ya Myanmar ya kuwakandamiza Waislamu wa jamii ya Rohingya. Kiongozi huyo wa chama tawala nchini Myanmar amekana kutokea 'mauaji ya umati' dhidi ya Waislamu Warohingya na kudai kwamba, kukimbia mamia ya malefu ya Waislamu wa jamii ya Rohingya ilikuwa natija ya vita na waasi.
Akizungumza kwa utulivu kabisa San Suu Kyi alikana pia tuhuma dhidi ya jeshi la Myanmar kwamba, mwaka 2017 liliua maelfu ya Waislamu wa jamii ya Rohingya katika jimbo la Rakhine, kama ambavyo alikanusha ripoti kwamba, wanajeshi wa nchi hiyo walifanya vitendo vya ubakaji dhidi ya Waislamu hao sambamba na kuchoma moto nyumba zao.
Mahakama ya Kimataifa ya Uadilifu ICJ, Jumanne iliyopita, ilianza kusikiliza faili la kesi ya mauaji ya umati yaliyofanywa na wanajeshi wa Myanmar mwaka 2017 dhidi ya Waislamu Warohingya ambayo iliwasilishwa katika mahakama hiyo na serikali ya Gambia kwa niaba ya nchi 57 za Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu (OIC).
Matamshi ya uongo ya San Suu Kyi kuhusiana na kile kilichowalazimisha Waislamu wa jimbo la Rakhine wayakimbie makazi yao na kuelekea Bangladesh, ni kukana ukweli wa mambo ambao jamii ya kimataifa inaufahamu vyema.
Licha ya serikali ya Myanmar kuweka vizingiti dhidi ya makundi ya kutafuta ukweli na wanaharakati wa vyombo vya habari wanaoelekea nchini humo kwa ajili ya kujionea kwa karibu hali wanayokabiliwa nayo Waislamu Warohingya katika jimbo la Raghine la magharibi mwa nchi hiyo, lakini ripoti mbalimbali zilizotolewa na taasisi za kimataifa za haki za binadamu na Umoja wa Mataifa zote zimefichua na kuweka wazi jinai kubwa zilizofanywa na jeshi la nchi hiyo dhidi ya Waislamu hao.
Umoja wa Mataifa ulitangaza katika ripoti yake mwaka uliopita wa 2018 kwamba, jeshi la Myanmar limefanya mauaji ya kizazi nchini humo na kwamba, hilo ndilo jeshi katili zaidi duniani.
Anthony Kartaluchi, mtaalamu na mweledi wa jiopolitiki ya kisiasa anasema kuwa: Kile ambacho kinatajwa katika sheria za kimataifa kama 'mauaji ya kizazi' kinatokea katika mkoa wa Rakhine dhidi ya Waislamu Warohingya, na San Suu Kyi amefumbia macho hilo. Kundi ambalo linafanya mauaji ya kizazi dhidi ya jamii ya wachache ya Rohingya, limeweka suala la mauaji ya kizazi kama malengo yake ya awali.
Kuanzia Agosti 25 mwaka 2017 Waislamu zaidi ya 740,000 wa jamii ya Rohingya walilazimika kuyahama makazi yao katika jimbo lao la Rakhine na kukimbilia katika nchi jirani ya Bangladesh walikojiunga na wenzao wengine laki mbili waliokuweko nchini humo, baada ya vikosi vya jeshi la Myanmar na Mabudha wenye misimamo ya kufurutu ada kuanzisha wimbi kubwa la hujuma na ukandamizaji dhidi ya Waislamu hao.
Licha ya upinzani mkali wa serikali ya Myanmar, lakini kuingilia kati Mahakama ya Kimataifa ya Uadilifu na kuanza kushughulikia faili la mauaji ya jeshi la nchi hiyo dhidi ya Waislamu Warohingya inaweza kuwa hatua nzuri ya kulifanya faili hilo kuwa la kimataifa, na hivyo mkono wa sheria kuwafuatilia watenda jinai katika jimbo la Rakhine ambapo kilio cha fikra za waliowengi ulimwenguni ni kufuatilia faili la mauaji hayo na sheria kufuata mkondo wake.
Fikra za waliowengi ulimwenguni ni kuona Mahakama ya Kimataifa ya Uadilifu inashughulikia kwa umakini mkubwa faili la mauaji ya kimbari ya Waislamu Warohingya ambapo sambamba na kutoa hukumu izingatie ulazima wa kurejea wakimbizi wa Kirohingya walioko nchini Bangladesh kwa kuilazimisha serikali ya Myanmar iandae mazingira ya kurejea wakimbizi hao.
Hata hivyo kuna wasiwasi huu kwamba, kurejea kunakotarajiwa kwa wakimbizi hao kunasadifiana na duru mpyya ya vitendo vya utumiaji mabavu dhidi yao. Ni kutokkana na sababu hiyo ndiyo maana kupatikana hakikisho kutoka kwa serikali ya Myanmar kwa ajili ya kudhamini usalama wa wakimbizi hao ni dharura ya kimataifa.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni