Translate

Jumanne, 10 Desemba 2019

03-Matendo Mema Na Athari Yake Katika Utajiri Na Ukunjufu Wa Rizki: Athari Ya Matendo Mema Katika Rizki


B.    Athari Ya Matendo Mema Katika Riziki
 
 
1. Taqwa (Uchaji Allaah) Na Matunda Yake
 
 
 (a) Kufarijika Baada Ya Huzuni Na Kupata Riziki Pasina Kutarajia
 
“Na anayemuogopa Allaah Humtengenezea njia ya kuokoka (katika kila balaa).
 Na Humpa riziki kwa namna asiyoitazamia. Na anayemtegemea Allaah Yeye humtoshea.” Atw-Twalaaq: 2-3
 
Katika aya hii dalili kwamba Allaah Mtukufu Anawafariji wenye matatizo na Anawapa sababu za kupata riziki pasina ya kutegemea na kwa njia wasiyopanga akilini mwao kutokana ucha Allaah wao.
 
 
 (b) Riziki Nyingi Na Pana
 
 Anasema Allaah:
 
“Na kama watu wa miji wangaliamini na kuogopa kwa yakini tungeliwafungulia baraka za mbingu na ardhi, lakini walikadhibisha tukawapatiliza kwa sababu ya yale waliyokuwa wakiyachuma.” Al-A’araaf: 96
 
Alitoka ‘Umar (Radhiya Allaahu ‘anhu) anaomba mvua na hakuzidisha zaidi ya kuomba msamaha, aliporudi mvua ikanyesha, wakamwambia hatukukuona ukiomba du’aa ya mvua, akasema hakika nimeomba mvua kwa mawingu yanayoshusha mvua angani kisha akasoma Suratun Nuuh 10-11
 
“Ombeni msamaha kwa Mola wenu hakika Yeye ni mwingi wa msamaha. Atakuleteeni mawingu yanyeshayo mvua nyingi.”
 
 
2. ISTIGHFAAR
 
Matunda Ya Kuomba Msamaha
 
(a) Kukunjuliwa Rizki
 
Anasema Allaah:
 
“Na ili muombe msamaha kwa mola wenu kisha mtubie (mrejee) Kwake. Atakustarehesheni kwa starehe nzuri mpaka muda maalum (mtapoondoka ulimwenguni). Na Atampa (Akhera) kila mwenye fadhila fadhila yake. Na kama mtakengeuka basi nakuhofieni adhabu ya (hiyo) siku kubwa.” Huud: 3
 
Amewaamrisha kuomba msamaha kutokana na dhambi zilizopita na kutubia kwa Allaah, Atawastarehesheni duniani na Akhera.
 
 
(b) Mvua Kunyesha Kwa Mfululizo
 
Anasema Allaah:
 
Na enyi watu wangu ombeni msamaha kwa Mola wenu (kwa mabaya yenu yaliyopita), kisha mtubie Kwake (kwa kufanya mema sasa na kuacha mabaya, Atakuleteeni mawingu yateremshayo mvua tele, na Atakuzidishieni nguvu juu ya nguvu zenu (mlizonazo). Wala msikengeuke kuwa waovu.” Huud: 52
 
 
(c) Kuongezekewa Mali Na Watoto
 
Anasema Allaah:
 
“Nikawaambia, ombeni msamaha kwa Mola wenu hakika Yeye ni Mwingi wa msamaha. Atakuleteeni mawingu yanyeshayo mvua nyingi. Na Akakupeni mali na watoto, na Atakupeni mabustani, na Atakufanyieni mito.” Nuuh: 10-12
 
 
(d) Kupata Riziki Bila Ya Kutarajia
 
Amesema Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam):
 
“Mwenye kujilazimisha na kuomba msamaha Atamjalia Allaah kwa kila dhiki utatuzi na katika kila shida faraja na Atamruzuku pasina kutarajia.” Abu Daawuud
 
 
3. KUUNGA UDUGU
 
Amesema Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) kutoka kwa Allaah “Iliambiwa udugu, hivi huridhii nikimuunga anayekuunga na ninamkata anayekukata? akasema ndio naridhia Ee Mola wangu, akamwambia basi ni hivyo.” Al-Bukhaariy
 
Na kutoka kwa Abu Hurayrah (Radhiya Allahu ‘anhu) amesema, amesema Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam):
“Mwenye kufurahi kukunjuliwa katika riziki na kuongezewa umri (kwa kutenda mema) basi na aunge udugu wake.” Al-Bukhaariy
 
 
4. KUMTEGEMEA Allaah
 
Nayo ni sababu muhimu ya kurahisisha rizki.
 
Kutoka kwa ‘Umar bin Al-Khattwaab (Radhiya Allahu ‘anhu) amesema, nimemsikia Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) akisema:
 
“Lau nyinyi mngemtegemea Allaah ukweli wa kumtegemea Angewaruzuku kama Anavyomruzuku ndege, anatoka asubuhi na njaa anarudi jioni ameshiba.”
 
Katika Hadiyth hii, inatuwekea wazi (Allaah Anajua) kwamba Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) amekataza kukaa na kutotafuta maisha, bali amehimiza kutafuta riziki kwani ndege anatoka asubuhi mapema kutafuta riziki.
 
 
5. SWALAAH
 
Hakika Swalaah inampa Muumini raha na utulivu na furaha. Nayo pamoja na subra ina athari nzuri ya kutatua vikwazo, tabu, na matatizo anayokumbana navyo mwanaadamu.
 
Anasema Allaah:
 
“Enyi mlioamini jisaidieni (katika mambo yenu) kwa subira na Swalaah: bila ya shaka Allaah Yupo pamoja na wanaosubiri.” Al-Baqarah: 153
 
Amesema Sa’iyd bin Jubayr:
“Subra ni kukiri mja kwa Allaah kwa yaliyompata na kutaraji malipo, thawabu kwa Allaah, huenda mtu akafadhaika naye ana haraka asione subira.”
 
Anasema Allaah:
 
“Na waamrishe watu wako kuswali, na uendelee mwenyewe kwa hayo. Hatukuombi riziki bali Sisi ndiyo tunakuruzuku. Na mwisho mwema utawathubutukia wamchao Allaah.” Twaahaa: 132
 
 
6. KUTOA KATIKA NJIA YA ALLAAH
 
Kutoa katika njia (ajili) ya Allaah kuna malipo duniani na Akhera, duniani unapewa badala, baraka, kukunjuliwa katika riziki, ama Akhera ni kupata pepo kwa fadhila na rehma za Allaah.
 
Anasema Allaah:
 
“Enyi mlioamini toeni katika vile vizuri mlivyovichuma, na katika vile Tulivyokutoleeni katika ardhi.Wala msikusudie kutoa vilivyo vibaya hali nyinyi wenyewe msingevipokea isipokuwa kwa kuviangalia (basi Allaah Atapokea vibaya?) basi jueni kwamba Allaah ni Mkwasi na asifiwaye.
Shetani anakuogopesheni ufakara na anakuamrisheni ubakhili,na Mwenyezi Anakuahidini msamaha utokao kwako na ihsani (kubwa pindi mkitoa) na Allaah ni mwenye wasaa mkubwa na mwenye kujua.” Al-Baqarah: 267-268
 
Kwani Shaytwaan anakuogopesheni ufakiri na kuwakhofisha nayo ili mzuie msitoe kwa ajili ya Allaah mlivyo navyo, pia anawaamrisha uovu, maasi, mambo machafu, na Allaah Anakuahidini msamaha.
 
Anasema Allaah:
 
“Sema: “kwa hakika Mola wangu Humkunjulia riziki Amtakaye katika waja Wake, na Humdhikishia (Amtakaye) na chochote mtakachotoa basi Yeye Atakilipa na Yeye ni mbora wa wanaoruzuku.” Sabaa: 39         
 
Chochote mtoacho mtalipwa duniani na Akhera.
 
 
7. HAJJ NA ‘UMRAH
 
 Ibn Mas’uud amesema, amesema Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wasallam):
 
“Fuatisheni baina ya Hija na ‘Umrah kwani inaondosha umaskini na madhambi kama kutu inavyoondoshwa katika dhahabu na fedha, na Hija iliyokubaliwa thawabu yake ni pepo.”
 
 
8. KUWASAIDIA MADHAIFU NA KUWAJALI
 
Kutoka kwa Mas’ab bin Sa’ad amesema, aliona Sa’ad yeye ni bora kuliko walio chini yake, akasema Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam): “Je, (hamjui kuwa) mnapata ushindi na riziki ila kwa ajili ya madhaifu wenu?”
 
Kutoka kwa Abu Dardaa amesema, nimemsikia Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) akisema: “Kwa madhaifu wenu hakika mnaruzukiwa na kupewa ushindi kwa ajili yao.”
 
Amebainisha Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) kuwasaidia madhaifu na kuwaheshimu ni sababu ya kuwepesishiwa riziki na kupata ushindi.
 
 
9. DU’AA
 
 Anasema Allaah:
 
“Na kumbukeni (habari hii nayo) aliposema Ibraahiym: “Ee Mola wangu ufanye mji huu (wa Makkah) uwe na salama na uwape wakazi wake matunda wale wanaomwamini Allaah na siku ya mwisho.” (Allaah) Akasema na mwenye kukufuru (pia) nitamstarehesha kidogo kisha nitamsukumiza katika adhabu ya moto napo ni mahali pabaya kabisa pa kurejea." Al-Baqarah: 126
 
Anasema Allaah:
 
“Ee Allaah Mola wetu tuteremshie chakula kutoka mbinguni ili kiwe sikukuu kwa ajili ya mwanzo wetu (nao ni sisi) na wa mwisho wetu (nao ni wafuasi wetu watakaokuja baada yetu wakasikia haya) na kiwe ishara itokayo kwako basi turuzuku kwani Wewe ndie Mbora wa wanaoruzuku.” Al-Maaidah: 114
 
Kutoka kwa Abu Dhari kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wasallam) katika aliyopokea kutoka kwa Mola wake Mtukufu amesema:
 
“Enyi waja wangu Mimi nimeharamisha dhulma juu Yangu na Nimejaalia baina yenu haramu msidhulumiane, Enyi waja Wangu, nyote mmepotea ila Niliyemuungoza niombeni uongofu Nitawaongoza,
Enyi waja Wangu nyote mna njaa ila Niliyemlisha, niombeni chakula Nitawapeni,
Enyi waja Wangu nyote mpo tupu ila Niliyemvisha niombeni mavazi Nitawavisheni…” Muslim
 
 
Kutoka kwa Abu Ja’afar kwamba amemsikia Abu Hurayrah akisema, amesema Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wasallam):
 
“Itakapobakia theluthi ya usiku Anashuka Allaah Mtukufu katika uwingu wa dunia Anasema: “Nani ananiomba Nimjibu, nani ananiomba msamaha Nimsamehe, nani ananiomba riziki Nimpe, nani anataka kuondolewa matatizo Nimuondolee? Anaendelea hivyo mpaka alfajiri.”
 
Kutoka kwa Jaabir bin ‘Abdillaah amesema, amesema Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wasallam):
 
“Je, niwajulisheni itakayowaokoa na adui zenu, na itakayowafanyia nzuri rizki zenu? Ni kumuomba Allaah katika usiku wenu na mchana kwani du’aa ni silaha ya Muumin.” Ibn Maajah


Hakuna maoni:

Chapisha Maoni

20-Hakika Shirki Ni Dhulma Kubwa Mno! - Isti’aadhah Kwa Asiyekuwa Allaah

  إِنَّ الشِّرْكَ لَظُلْمٌ عَظِيم   Hakika Shirki Ni Dhulma Kubwa Mno!   20 - Isti’aadhah  (Kuomba Kinga) Kwa Asiyekuwa Allaah   ...