Translate

Ijumaa, 22 Novemba 2019

Vipi Kupata Unyenyekevu Kamili Katika Swalah?


SWALI:

Assalam alaykum
Swali ambalo kwa muda mrefu linanisumbuwa ni je swala inakuwa haipandi kama ukiwaza ndani yake. Kila siku najaribu nisiwaze katika swala lakini najikuta nikiwaza bila ya kutarajia. Nimefikia hata ya kutia nia ya kutowaza mapema zaidi tangu wakati wa kutia udhu lakini haijasaidia. Kuna wakati huwa nasimama mbele ya mswala najisemea mwenyewe kutowaza lakini hasaidii na sasa nistop. hata saa nyingine nikitafsiri suratul fat-ha kimoyo moyo huku naisoma kwa kiarabu huwa inaleta mawazo mengine kabisa. Si mawazo mabaya, kawaida huwa nakumbuka mijadala juu ya suratul fat-ha ambayo  inasemekana kuwa inatoshelezea kusoma katika kila swala bila ya sura nyingine au kadhalika. Na nyakati mbaya zaidi huwa napitawa na mawazo katika sura nyingine, mara nyingine yanakuwa mawazo ambayo hayana maana. Najua hii ni kazi ya ibilisi lakini sijui nimuepuke vipi kwani najaribu kufikiria kwamba Mungu yuko mbele yangu, na pia kukumbuka kwamba kila nikisoma suratul_fat-ha Yeye hujibu. Kawaida wakati wa sala ya isha huwa afadhali kwani nafanikiwa kufikiria kwamba kwapengine swala ninayoswali ni swala yangu ya mwisho. Lakini swala zote hata sekunde basi lazima mawazo yangu yatoke katika swala. Na mimi huwa sipendi nataka akili isifanye chochote ila kufocus katika maneno ninayoyasema au katika  kupata maghfira.Sifikiri mtu yeyote atapendezewa kuongea na mtu ambaye hajaweka akili katika anachosema. Ndio hivyo hivyo naona M/Mungu hatoridhika ikiwa sijaweza kuituliza swala yangu. Mungu anizidishe subira labda nikiendelea kuomba kuwa mnyenyekevu nitafanikiwa kuinusuru swala yangu. Naomba nasaha juu ya tatizo hili kwani nahofia kwamba swala zangu zitakuwa hazina thamani.  
Jazaka Allah Kheri


JIBU:

AlhamduliLLaah - Himidi Anastahiki Allaah (Subhaanahu wa Ta’aala) Rabb wa walimwengu, Swalaah na salamu zimshukie Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhwiya Allaahu 'anhum) na waliowafuata kwa wema mpaka Siku ya Mwisho.

Al-Khushuw’ (unyenyekevu) ni katika yaliyokuwa ni waajib  katika Swalaah na bila shaka ni jambo gumu kulitimiza kwa vile shaytwaan anapenda kumtia mtu wasi wasi katika Swalaah, ndio maana Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) ametutaka  tuwe tunajikinga na shaytwaan kabla ya kuanza Swalaah na pindi anapomtia mtu wasiwasi ndani ya Swalaah.  


Khushuw’ ni jambo la kuazimiwa kwa sababu Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Ameahidi waja Wake wenye kumiliki sifa hiyo, kuwaingiza katika Jannatul-Firdaws. Anasema Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa):      

 بِسْمِ اللَّـهِ الرَّحْمَـٰنِ الرَّحِيمِ ﴿١﴾


قَدْ أَفْلَحَ الْمُؤْمِنُونَ ﴿١﴾
Kwa yakini wamefaulu Waumini.


الَّذِينَ هُمْ فِي صَلَاتِهِمْ خَاشِعُونَ ﴿٢﴾
Ambao katika Swalaah zao huwa wananyenyekea. [Al-Muuminuwn: 1]


Aayah zinaendelea mpaka kauli Yake Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa):

 أُولَـٰئِكَ هُمُ الْوَارِثُونَ ﴿١٠﴾
Hao ndio warithi.

الَّذِينَ يَرِثُونَ الْفِرْدَوْسَ هُمْ فِيهَا خَالِدُونَ ﴿١١﴾
Ambao watarithi (Jannah) ya Al-Firdaws, wao humo ni wenye kudumu.  [Al-Muuminuun: 10-11]

Zifuatazo ni baadhi ya njia ambazo zitaweza In Shaa Allaah kukusaidia kupata khushuw’ (unyenyekevu) katika Swalaah:


1-Kwenda msalani kukidhi haja kubwa na ndogo kabla ya Swalaah.


2-Kula kama una njaa kabla ya kuswali


3-Kutia vizuri wudhuu.  


4-Kuweka Sutrah (Kizuizi) mbele yako.


5-Kutokuvaa nguo za rangi au zenye maneno hasa kama unaswali Jamaa  ili isiwashughulishe wengineo. 


6-Kukumbuka mauti.  


7-Kwa wanawake wanaoswali nyumbani, kutokuswali mbele ya watu   wanaozungumza, watoto na kutokuweko sauti za televisheni, radio n.k.


8-Kuanza kwa du’aa za kufungulia Swalaah na kujikinga na shatywaan kama ilivyothibiti katika Sunnah.

 أَعـوذُ بِاللهِ مِنَ الشَّـيْطانِ مِنْ نَفْخِـهِ وَنَفْـثِهِ وَهَمْـزِه
Najikinga na Allaah kutokana na shaytwaan, na kibri yake, na kupulizia kwake na kutia kwake wasiwasi (katika nyoyo za binaadamu) [Hadiyth ya Jubayr bin Mutw-‘im (رضي الله عنه) - Abu Daawuwd (1/203), Ibn Maajah (1/265), Ahmad (4/85), na Muslim kutoka kwa ibn ‘Umar (رضي الله عنهما) kama hivyo na mna kisa humo (1/420)]


9-Kujikinga na shaytwaan ndani ya Swalaah anapokupotezea khushuw’, nayo ni kutema mate kidogo kama kupuliza upande wa bega la kushoto mara tatu na kuomba kinga.  


10-Kuweka mkono wa kulia juu ya kushoto kwenye kifua vizuri.


11-Kutambua kwamba upo mbele ya Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) na unaposoma Al-Faatihah Anakujibu.


12-Kutazama sehemu ya kusujudu unaposimama.


13-Kuzingatia Quraan unapoisoma.


14-Kusoma Qur-aan kwa sauti nzuri katika katika Swalaah za jahriyyah (kisoma cha sauti).


15-Kunong'ona kwenye Swalaah za Sirriyah (Swalah za kimya) bila ya kutoa sauti sana au bila ya kuswali kimya sana.


16-Kuswali kwa twumaaninah: ni utulivu na kwa vituo na kutimiza kila kitendo bila ya kuharakisha kwa kupumzika kiasi hadi uhakikishe kila sehemu ya kiungo kimetulia mahala pake wakati wa kurukuu, kusimama baada rukuu, kusujudu, baina ya sijda mbili, ukitoka kusujudu kabla hujanyanyuka n.k.1-    


Na muhimu zaidi ni kumuomba Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Akuruzuku khushuw' katika Swalaah hasa kwa kuomba du'aa aliyotufunza Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam)  tuiombe tunapomaliza kila Swalaah baada ya tashahhud  kabla ya kutoa salaam: 

اللّهُـمَّ أَعِـنِّي عَلـى ذِكْـرِكَ وَشُكْـرِك ، وَحُسْـنِ عِبـادَتِـك
Ee Allaah nisaidie juu Kukudhukuru, na kukushukuru na kukuabudu kwa uzuri utakikanao. 

Na Allaah Anajua zaidi.


Hakuna maoni:

Chapisha Maoni

20-Hakika Shirki Ni Dhulma Kubwa Mno! - Isti’aadhah Kwa Asiyekuwa Allaah

  إِنَّ الشِّرْكَ لَظُلْمٌ عَظِيم   Hakika Shirki Ni Dhulma Kubwa Mno!   20 - Isti’aadhah  (Kuomba Kinga) Kwa Asiyekuwa Allaah   ...