Translate

Jumapili, 24 Novemba 2019

Kumpenda Mtume صلى الله عليه وآله وسلم Ni Kumtii Na Kumfuata


Sifa zote njema anastahiki Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala), Swalah na salamu zimshukie Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), ahli zake na Maswahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema baada yao mpaka siku ya Malipo.
Nawausia kaka na dada zangu pamoja na kuiusia nafsi yangu katika kumcha na kumpenda Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala).

Ndugu zangu wapenzi, Waislam wengi wamejenga ada ya kumkumbuka Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kwa kumsherehekea mazazi (MAWLID) yake, na kutenga siku maalum kwa sherehe hiyo na kukesha kwa kuzitaja sifa zake na kuimba na wengine kucheza na kuandaa vyakula kwa kuiadhimisha siku hiyo. Ingawa ushahidi wa kuzaliwa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) katika siku hiyo iliyozoeleka kusherehekewa, ina utata! Vitabu mbalimbali vya kihistoria vinataja tarehe mbalimbali na hata mwaka tofauti wa kuzaliwa kwake.

Kinachokubaliwa ni siku ambayo ni ya Jumatatu kama alivyosema mwenyewe wakati Maswahaba zake watukufu walipomuuliza kwanini hufunga Swawm katika siku hiyo.
Imetoka kwa Abu Qataadah (Radhiya Allaahu ‘anhu) kwamba aliulizwa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kuhusu kufunga Jumatatu akasema: ((Hiyo ni siku niliyozaliwa na siku ulioteremshwa kwangu [Utume])) [Imaam Muslim]

Lengo letu hapa si kueleza yafanywayo katika siku hiyo na kwanini yanafanywa, bali ni kueleza njia sahihi zilizothibiti zinazopaswa kudhihirisha mapenzi ya umpendaye. Na mapenzi ya kumpenda Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) yanayotakikana na ambayo yanamridhisha Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) ni kutekeleza yale aliyotuamrisha kuyafanya, na kuyaacha yale aliyotukataza kuyatenda. Pia kujipamba na yote aliyokuja nayo na aliyokuwa amepambika nayo.

Iweje usome Barzanji na kuimba kwa madaha na umsifie Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) uzuri na urefu wa ndevu zake na hali wewe wanyoa au kuzichonga mistari kama ramani kwa kuwaiga wanamuziki na wacheza mipira?


Iweje utaje na kuimba sifa za uaminifu, ukweli, uadilifu wake kwa wake zake (Radhiya Allaahu ‘anhunna), na hali wewe ni khaini, muongo na mwenye kunyanyasa wake zako au kutoa mapenzi zaidi na haki zaidi kwa mmoja na wengine huwajali?


Iweje Mawlid kwako ni ‘Ibaadah na Swalah huzitekelezi kwa wakati au huziswali kabisa?

Iweje wayatukuza mazazi ya Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na unazibeza na kuzipuuza Sunnah zake?
Hayo hayawezi kuwa mapenzi. Na mifano ni mingi tunayoiona kwa wenye kusherehekea hayo Mawlid na kuyaadhimisha.
Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) Anasema:
“Enyi Mlioamini! Mcheni Allaah haki ya kumcha na msife isipokuwa mmekwisha kuwa Waislamu kamili” (3: 102)

Tuitazame vizuri qadhiyah hii muhimu sana nayo ni “Kumtii na Kumfuata Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam)”.
Hakika Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) Amemchagua Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kwa kumpatia Unabii na Utume na Akateremshiwa Kitabu (Qur-aan) na Hikma (Sunnah) na Akaamrishwa kufuata aliyoteremshiwa na kufikisha ujumbe kutoka kwa Allaah. Alisimama Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kufikisha ujumbe na kutekeleza amana. Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) Anasema:
“Kama Tulivyomleta Mtume kwenu anayetokana na nyinyi, anakusomeeni aya zetu na kukutakaseni na kukufundisheni Kitabu na hikima na kukufundisheni mliyokuwa hamyajui” (2: 151)
Kitabu hapa ina maana ya Qur-aan na Hikma ni mafunzo yake Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam).
Allaah Amemshuhudia yeye kuwa ni mkweli na ameshikamana vilivyo kwa amri Zake (Allaah) kama Alivyomshuhudilia kwa uongofu katika nafsi Yake na kuwa yeye Anawaongoza wanaomfuata. Allaah Anasema:
“Na namna hivi Tumekufunulia Wahyi kwa amri yetu. Ulikuwa hujui Kitabu ni nini wala imani; lakini tumefanya kitabu hiki (Qur-aan) ni nuru, ambayo kwa (nuru) hiyo Tunamuongoza Tumtakaye katika waja wetu. Na kwa yakini wewe unaongoza katika njia iliyonyooka. Njia ya Allaah ambaye ni vyake (peke yake vyote) vilivyomo mbinguni na vilivyomo katika ardhi. Jueni kuwa mambo yote yanarudi kwa Allaah” (42: 52-53)
Na hiki ni cheo na daraja ya Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) katika Dini. Yeyote atakayemuamini, hivyo amemuamini Allaah na yeyote atakayemtii basi amemtii Allaah. Kwa ajili ya hili, Allaah Amewaamrisha waja wake kumtii Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Akawalazimisha wao kufuata amri Zake na kusadikisha habari Anazotupasha, na Akatutahadharisha kutomhalifu wala kumuasi. Anasema Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala):
“Msifanye wito wa Mtume baina yenu kama wito wa nyinyi kwa nyinyi. Hakika Allaah Anawajua miongoni mwenu wale waondokao kwa utoro wakijificha. Basi wajihadhari wale wanaokaidi amri Yake, Usije ukawapata msiba au ikawafika adhabu iumizayo” (24: 63)
Allaah Akajaalia kuwa kumtii Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ni faradhi ya lazima kwa kila anayemuamini Allaah, wala hakujaalia kwa muumini khiyari kwa amri yoyote baada ya kuwa Allaah na Mtume Wake wamepitisha. Allaah Anasema:

“Haiwi kwa mwanaume aliyeamini wala kwa mwanamke aliyeamini, Allaah na Mtume Wake wanapokata shauri, wawe na khiyari katika shauri lao. Na mwenye kumuasi Allaah na Mtume Wake, hakika amepotea upotofu ulio wazi kabisa” (33: 36)

Anasema tena Allaah:
“Enyi Mlioamini! Mtiini Allaah na Mtume wake, wala msijiepushe naye na hali mnasikia” (8: 20)

Anasema tena:
“Enyi Mlioamini! Mtiini Allaah na mtiini Mtume, wala msiviharibu vitendo vyenu” (47: 33)
Na tena:

“Sema: ‘Mtiini Allaah na mtiini Mtume, na kama mkikengeuka, basi ni juu yake (huo) mzigo alioutwika. Na juu yenu (huo mzigo) mliotwikwa – (kutii). Na mkimtii mtaongoka; hapana juu ya Mtume ila kufikisha ujumbe wake wazi wazi” (24: 54)

Na Anasema tena Allaah kwa yule mwenye kumuasi Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam):
“Na anayemuasi Allaah na Mtume Wake, na kuiruka mipaka yake, (Allaah) Atamwingiza Motoni, humo atakaa milele, na atapata adhabu zifedheheshazo” (4: 14)
Amebainisha Allaah baada hii amri ya kumtii Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kuwa ni sababu ya uongofu na rehma, kama alivyobainisha Aliyetukuka ya kwamba hakuna kufaulu kwa waja na wala 'kunali saada' (kupata furaha) kwao wao katika ahadi isipokuwa kwa kufuata maagizo ya Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na kumtii.
Anasema Allaah:
“Enyi Mlioamini! Muogopeni Allaah na semeni maneno ya haki.  Atakutengenezeeni vizuri vitendo vyenu na Atakusameheni madhambi yenu; Na anayemtii Allaah na Mtume Wake, bila shaka amefanikiwa mafanikio makubwa” (33: 70-71)

Na Anasema Allaah:
“Hiyo ni mipaka ya Allaah. Na anayemtii Allaah na Mtume Wake, (Allaah) Atamwingiza katika Bustani zipitazo mito mbele yake; wakae humo milele. Na huko ndiko kufaulu kukubwa” (4: 13)

Allaah Amefanya wajibu juu ya waumini kurudisha mambo na mizozano yao kwa Allaah na Mtume Wake. Na Akajaalia Aliyetukuka kuwa hilo ni katika Imani na ulazima wake. Akasema:

“Enyi mlioamini! Mtiini Allaah na mtiini Mtume na wenye madaraka katika nyinyi. Na mkizozana katika jambo basi lirudisheni kwa Allaah na Mtume, ikiwa mnamuamini Allaah na Siku ya Mwisho. Hayo ndiyo bora zaidi na ndiyo yenye mwisho mwema” (4: 59)
Kama hivyo hivyo Alivyowajibisha Allaah kwa Waumini kurudi kwa Kitabu chake na Sunnah za Mtume Wake. Ameifanya hukumu ya Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ni wajibu kufuatwa na kuisalimisha nafsi kikamilifu kwa hukumu yake. Na Akajaalia hilo ni katika ulazima wa mtu kuwa na Imani, pale aliposema (Subhaanahu wa Ta’ala):
“La! Naapa kwa Mola wako Mlezi! Hawataamini mpaka wakufanye wewe ndiye muamuzi katika yale wanayokhitalifiana, kisha wasione uzito katika nyoyo zao juu ya hukumu utakayoyatoa, na wanyenyekee kabisa” (4: 65)
Allaah Ametuamrisha kumfuata Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kwa anayotuamrisha na kuacha anayotukataza. Amesema (Subhaanahu wa Ta’ala):
“Na anachokupeni Mtume chukueni, na anachokukatazeni jiepusheni nacho. Na mcheni Mwenyeezi Mungu. Hakika Mwenyeezi Mungu ni Mkali wa kuadhibu” (59: 7)
Katika Hadiyth zifuatazo ambazo zinatupatia mwelekeo wa mada hii yetu. Amepokea Al-Bukhaariy kuwa Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu ‘anhu) amesema kuwa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:
“Ummah wangu wote utaingia Peponi isipokuwa kwa anayekataa”. Pakasemwa: “Na ni nani atakayekataa, ewe mjumbe wa Allaah?” Akasema: “Mwenye kunitii mimi ameingia peponi na anayeniasi amekataa” .
Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu ‘anhu) amesema ya kwamba Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema“Yeyote atakayenitii mimi basi amemtii Allaah, na anayeniasi mimi amemuasi Allaah” (Al-Bukhaariy).
Na hivyo hivyo, kama Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alivyowaamuru Waislamu kumtii, amewaonya wasitoke katika Sunnah zake wala kuzipuuza.


Amesema katika Hadiyth ya Al-Bukhaariy kutoka kwa Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu ‘anhu) na Muslim kutoka kwa Anas bin Maalik (Radhiya Allaahu ‘anhu) ya kwamba: “Yeyote atakayekengeuka kutoka katika Sunnah zangu si katika mimi”.

Na Mama wa Waumini ‘Aaishah (Radhiya Allaahu ‘anha) amesema ya kwamba Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:
“Mwenye kuzua katika jambo letu hili (la dini) ambalo halipo basi litarudishwa” (Al-Bukhaariy na Muslim).

Na katika riwaya ya Muslim: “Yeyote atakayefanya amali ambayo haina hukumu yetu basi itarudishwa”.
Usikose kusoma maudhui nyingine hapa chini kuhusiana na Mawlid,




Ee Mola wetu! Tujaalie ni wenye kusikiliza maneno na utupatie hima na moyo wa kuyafuata yaliyo mazuri na mema. Ee Mola wetu! Tujaalie ni wenye kufuata Sunnah na kumtii Mtume wetu (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kwa kauli na matendo.


Hakuna maoni:

Chapisha Maoni

20-Hakika Shirki Ni Dhulma Kubwa Mno! - Isti’aadhah Kwa Asiyekuwa Allaah

  إِنَّ الشِّرْكَ لَظُلْمٌ عَظِيم   Hakika Shirki Ni Dhulma Kubwa Mno!   20 - Isti’aadhah  (Kuomba Kinga) Kwa Asiyekuwa Allaah   ...