Lu-ulu-un-Manthuwrun
(Mkusanyiko Wa Hadiyth Mbali Mbali Na Mafunzo Yake)
Hadiyth Ya 39
Tofauti Ya Kuandamana Na Rafiki Mwema Na Muovu
عَنْ أَبِي مُوسَى الأَشْعَرِيِّ (رضي الله عنه) عَنْ النَّبِيِّ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ قَالَ: ((إِنَّمَا مَثَلُ الْجَلِيسِ الصَّالِحِ وَالسَّوْءِ كَحَامِلِ الْمِسْكِ وَنَافِخِ الْكِيرِ. فَحَامِلُ الْمِسْكِ إِمَّا أَنْ يُحْذِيَكَ، وَإِمَّا أَنْ تَبْتَاعَ مِنْهُ، وَإِمَّا أَنْ تَجِدَ مِنْهُ رِيحًا طَيِّبَةً. وَنَافِخُ الْكِيرِ إِمَّا أَنْ يُحْرِقَ ثِيَابَكَ، وَإِمَّا أَنْ تَجِدَ مِنْهُ رِيحًا مُنْتِنَةً)) متفق عليه
Imepokelewa kutoka kwa Abuu Muwsaa Al-Ash-‘ariyyi (رضي الله عنه) kwamba Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema: ((Hakika mfano wa jalisi [rafiki] mwema na jalisi mbaya, ni kama mfano wa mbebaji miski na [mfua chuma] anayevuvia kipulizo. Mbebaji miski, ima atakupa, au utanunua kutoka kwake, au utapata harufu nzuri kwake. Na anayepuliza kipulizo, ima atachoma nguo zako, au utapata harufu mbaya kutoka kwake)). [Al-Bukhaariy na Muslim]
Mafunzo Na Mwongozo:
1. Umuhimu wa kuandamana na rafiki mwema, na tahadharisho la kuandamana na rafiki muovu.
2. Rafiki mwema ndiye mwenye kunufaisha ki-Dini na dunia, ama rafiki muovu ni mwenye kukhasirisha duniani na Aakhirah, na Siku ya Qiyaamah itakuwa ni majuto makubwa kuandama na rafiki muovu. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):
وَيَوْمَ يَعَضُّ الظَّالِمُ عَلَىٰ يَدَيْهِ يَقُولُ يَا لَيْتَنِي اتَّخَذْتُ مَعَ الرَّسُولِ سَبِيلًا ﴿٢٧﴾
Na siku dhalimu atakapotafuna mikono yake akisema: “Laiti ningeshika njia pamoja na Rasuli.
يَا وَيْلَتَىٰ لَيْتَنِي لَمْ أَتَّخِذْ فُلَانًا خَلِيلًا ﴿٢٨﴾
“Ee ole wangu! Laiti nisingelimfanya fulani kuwa rafiki mwandani.”
لَّقَدْ أَضَلَّنِي عَنِ الذِّكْرِ بَعْدَ إِذْ جَاءَنِي ۗ وَكَانَ الشَّيْطَانُ لِلْإِنسَانِ خَذُولًا ﴿٢٩﴾
“Kwa yakini amenipoteza mbali na Ukumbusho baada ya kunijia.” Na shaytwaan kwa insani daima ni mwenye kutelekeza. [Al-Furqaan (25: 27-29]
3. Rafiki mwema anamuathiri anayeandamana naye kwa tabia zake njema, na rafiki muovu pia anamuathiri anayeandamana naye kwa tabia zake mbovu.
4. Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) amefananisha harufu nzuri na mbaya kama tabia ambayo inamfikia haraka mtu puani kuisikia. Hivyo basi, haraka mno mtu anaweza kuathirika kwa tabia za mwenziwe zikiwa ni njema au tabia ovu.
5. Hakuna atakayemfaa mwenziwe Siku ya Qiyaamah kwa lolote, hata rafiki mwema hatoweza kumfaa mwenzake kila mmoja siku hiyo atakuwa analo la kumshughulisha mwenyewe. Seuze basi iwe ni rafiki muovu? Rejea: Ghaafir (40: 18), Al-Haaqah (69: 35), Al-Ma’aarij (70 : 10).
Rejea Hadiyth Namba (47).
Pia Hadiyth ya Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم):
عَنْ عائِشَةَ رَضِيَ اللهُ عَنْها أَنَّ رَسُولَ اللهِ صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وسَلَّمَ قالَ: ((يُبْعَثُ النّاسُ يَوْمَ القِيامَةِ حُفاةً عُراةً غُرْلاً)) فَقالَتْ عائِشَةُ: فَكَيْفَ بِالعَوْراتِ قالَ (لِكُلِّ امْرِئٍ مِّنْهُمْ يَوْمَئِذٍ شَأْنٌ يُغْنِيهِ)
Kutoka kwa ‘Aaishah (رضي الله عنها) kwamba Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema: ((Watu watafufuliwa siku ya Qiyaamah bila ya viatu, uchi na bila ya kutahiriwa)) Akasema ‘Aaishah: Vipi watakuwa uchi? Akasema: ((Kila mtu miongoni mwao siku hiyo atakuwa na hali ya kumtosheleza)) [Aayah Suwrah ‘Abasaa (80: 37), Hadiyth katika An-Nasaaiy na ameisahihisha Al-Albaaniy katika Swahiyh An-Nasaaiy (2082)]
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni