Translate

Jumatano, 13 Novemba 2019

Hadiyth Kuhusu: Watu Ambao Allaah Hatowatazama Wala Kuongea Nao Wala Hatowatakasa Na Watapata Adhabu Iumizayo Siku Ya Qiyaamah: (Faida Na Sharh)


Hadiyth Ya Kwanza:

Mzee Mzinzi, Mfalme Mwongo, Na Masikini Mwenye Kibri:


 عن أبي هريرة قالقال رسول الله صلى الله عليه وسلم: ((ثلاثةٌ لا يكلمهم الله يوم القيامة، ولا يزكيهم، ولا ينظر إليهم، ولهم عذابٌ أليمٌشيخٌ زانٍ، وملكٌ كذابٌ، وعائلٌ مستكبرٌ))  رواه مسلم.
Imepokelewa toka kwa Abuu Hurayrah (Radhwiya Allaahu ‘anhu) ambaye amesema: Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: ((Wa tatu, Allaah Hatozungumza nao Siku ya Qiyaamah, wala Hatawatakasa, wala Hatawaangalia, na watapata adhabu iumizayo: Mzee mzinzi, mfalme mwongo, na masikini mwenye kibri)). [Imesimuliwa na Muslim]

Faida Na Sharh:

Makusudio ya Allaah ('Azza wa Jalla)  kutozungumza nao ni kuwa Hatozungumza nao mazungumzo ya kuwa radhi nao na kuwafurahikia, bali Atazungumza nao mazungumzo ya hasira na kutowafurahikia.

Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa)  Anasifika na sifa hii ya kuzungumza. Huzungumza wakati wowote Atakapo na kwa namna yoyote Aitakayo. Alizungumza na Nabiy Muwsaa ('Alayhis-Salaam)  Akazungumza na Nabiy wetu Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam)  usiku wa Mi’iraaj, na pia Atazungumza na Nabiy ‘Iysaa  ('Alayhis-Salaam)  Siku ya Qiyaamah Amuulize:

   وَإِذْ قَالَ اللَّـهُ يَا عِيسَى ابْنَ مَرْيَمَ أَأَنتَ قُلْتَ لِلنَّاسِ اتَّخِذُونِي وَأُمِّيَ إِلَـٰهَيْنِ مِن دُونِ اللَّـهِ ۖ قَالَ سُبْحَانَكَ مَا يَكُونُ لِي أَنْ أَقُولَ مَا لَيْسَ لِي بِحَقٍّ ۚ إِن كُنتُ قُلْتُهُ فَقَدْ عَلِمْتَهُ ۚ تَعْلَمُ مَا فِي نَفْسِي وَلَا أَعْلَمُ مَا فِي نَفْسِكَ ۚ إِنَّكَ أَنتَ عَلَّامُ الْغُيُوبِ  
((Na pindi Allaah Atakaposema: “Ee ‘Iysaa mwana wa Maryam!  Je, wewe uliwaambia watu: ‘Nifanyeni mimi na mama yangu kuwa ni waabudiwa wawili badala ya Allaah?” (‘Iysaa) Atasema: “Utakasifu ni Wako hainipasi mimi kusema yasiyo kuwa haki kwangu; ikiwa nimesema hayo basi kwa yakini Ungeliyajua; Unayajua yale yote yaliyomo katika nafsi yangu; na wala mimi sijui yale yaliyomo katika Nafsi Yako; hakika Wewe ni Mjuzi wa ghayb)). [Al-Maaidah (5:116)]

Aidha, Atazungumza mazungumzo makali ya hasira na magombesho kwa makafiri na waasi Siku ya Qiyaamah. Atawaambia watu wa motoni kwa mfano:

قَالَ اخْسَئُوا فِيهَا وَلَا تُكَلِّمُونِ ﴿١٠٨﴾
108. Wataambiwa: “Hizikeni humo! Na wala msinisemeshe!”   [Al-Muuminuwn: 108]


Ama kutakaswa,  ni kutwaharishwa. Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa)  Huwatwaharisha  Waja Wake wema hapa duniani kwa kuzizidishia nyoyo zao iymaan, matendo mema na taqwa. Anatuambia:
قَدْ أَفْلَحَ مَن تَزَكَّىٰ ﴿١٤﴾
14. Hakika amefaulu ambaye amejitakasa.


وَذَكَرَ اسْمَ رَبِّهِ فَصَلَّىٰ ﴿١٥﴾
15. Na akadhukuru Jina la Rabb wake na akaswali. [Al-A’laa: 14-15]


Na huko Aakhirah inakuwa kwa kuwasafisha kutokana na uchafu wa makosa wakatakata kabisa na kisha kuwaingiza Peponi, kwani Peponi haingii mtu mchafu.

Ama kuwaangalia, makusudio yake ni kuwaangalia kwa jicho la ridhaa na furaha. Kwani Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Anawaangalia viumbe Vyake vyote bila kukiacha hata kimoja.

Watu hao watakaokumbana na mkasa huu:

Mtu wa kwanza: Mzee, ajuza na kikongwe mzinifu na mzinzi. 

Mzee kama huyu ambaye umri wake umesonga mbele, anachotakiwa ni kujikurubisha zaidi kwa Allaah ('Azza wa Jalla)  badala ya kumwasi kwa kosa hili ambalo Allaah ('Azza wa Jalla)  Amelielezea kama ni uchafu na njia mbaya kabisa. Mzee kama huyu inaonyesha kwamba mizizi ya madhambi imejikita hadi kwenye kina cha mwisho cha moyo wake.


Mtu wa piliNi mfalme mwongo.

Mwana Aadam kawaida husema uongo kutokana na unyonge wake na udhaifu wake na kushindwa kuwakabili wenye nguvu kwa haki na ukweli, na hapo hulazimika kuongopa. Ama mfalme, yeye anamwogopa nani? Watu wote ni raia wake, na vyombo vyote vya dola viko chini yake. Na ikiwa anaongopa, basi ni dalili kuwa mfalme huyo ni mchafu kimaadili, fisadi, mwenye uchu, na ubaya wa kila aina umejikita ndani ya nafsi yake.

Hii ni kama mzazi kuwaongopea watoto wake. Ni kwa nini afanye hivyo? Anaweza kuwaambia ukweli kwenye kila kitu, nao wakafahamu, wakavaana na hali iliyopo na wakakulia katika mazingira ya usemaji kweli. Na baba anapowaongopea watoto, inakuwa ni dhambi kubwa ambalo wengi hawalihisi. Na baba huyu anaweza kuwa sawa na mfalme huyo, na akaingia kwenye makamio haya ya Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa).


Mtu wa tatuNi masikini jeuri mwenye kibr.

Kibr mara nyingi huchochewa na utajiri alionao mtu ambapo watu hujipendekeza kwake na kumwonyesha kuwa wanamheshimu na kumtukuza kwa ajili ya maslaha. Hali hii mara nyingi humfanya mtu kuwa na kibr. Allaah ('Azza wa Jalla)  Anatuambia:
((كَلَّا إِنَّ الْإِنسَانَ لَيَطْغَىٰ))
((Laa hasha! Hakika mwana Aadam bila shaka amepindukia mipaka kuasi ))
((أَن رَّآهُ اسْتَغْنَىٰ ))
((Kwa kuwa amejiona amejitosheleza)) [Al-‘Alaq 96: 6 - 7]


Basi ikiwa mtu masikini na mlalahoi, na akawa na kibr, hii bila shaka inaonyesha kuwa uovu na uhabithi umejikita ndani ya nafsi yake. Mtu huyu bila shaka anaishi maisha ya taabu, dhiki na kubahatisha hapa duniani, na huko Aakhirah atakwenda kukumbana na makamio hayo ya Allaah (‘Azza wa Jalla). Anakuwa amekhasirika hapa duniani na huko aakhirah.

مستكبر anaweza pia kuwa mtu anayependa kujionyesha kwa watu kinyume na uwezo wake. Anaweza hata kuazima nguo, au kununua kitu cha ghali kwa kukopa, au kufanya harusi kubwa kwa madeni, ili tu mradi aonekane na yeye ni katika watu wa hadhi ya juu nailhali hana chochote. Hili wanalo wengi sana katika jamii.

Au hata akina mama wanapoalikwa kwenye harusi na kadhalika, hujitahidi kununua nguo ya ghali isiyopatikana nchini mwake na kuiagizia nje ili tu aonekane yeye tu aliyevaa nguo hiyo pasina mwengine.




Hadiyth Ya Pili:

Mwenye Kuburuza Nguo Yake (Isbaal), Msimbuliaji,
Na Mchuuzi Wa Bidhaa Yake Kwa Kiapo Cha Uongo



عن أبي ذر، عن النبي صلى الله عليه وسلم قال(( ثلاثةٌ لا يكلمهم الله يوم القيامة، ولا ينظر إليهم، ولا يزكيهم، ولهم عذابٌ أليمٌ)) ، قالفقرأها رسول الله ثلاث مرارٍ، قال أبو ذرخابوا وخسروا، من هم يا رسول الله؟ قالالمسبل إزاره، والمنان، والمُنَفِّقُ سلعته بالحلف الكاذب)) رواه مسلم.
Imepokelewa toka kwa Abuu Dharr (Radhwiya Allaahu 'anhu) toka kwa Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam)   akisema: ((Watatu (wa aina tatu) Allaah Hatozungumza nao Siku ya Qiyaamah, wala Hatowaangalia, wala Hatowatakasa, na watapata adhabu iumizayo)). Akasema: Rasuli akayasema hayo mara tatu. Abu Dharr akasema: Wamepita utupu na wamekula hasara. Ni nani hao ee Rasuli wa Allaah? Akasema: ((Mwenye kuburuza nguo yake, msimbuliaji, na mchuuzi wa bidhaa yake kwa kiapo cha uongo)). [Imesimuliwa na Muslim].


Faida Na Sharh:


Hadiyth hii tukufu inaonyesha hatari kubwa kabisa inayowakabili watu wa sampuli hizi tatu za madhambi yanayozingatiwa kuwa ni katika madhambi makubwa kufikia ngazi ya kunyimwa na kuyakosa mambo hayo matatu muhimu kabisa katika siku hiyo ya hisabu, na hata kumfanya Abuu Dharr kusema hayo aliyoyasema na kutaka kuwajua ni akina nani hao ili awajue na aepukane na makosa hayo. Na kutokana na ubaya na ukubwa wa hasara, Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam)  amelikariri neno hilo mara tatu kuonyesha uhatari wake na umuhimu wa kujiepusha na mambo hayo.

Mtu wa kwanza: Mwenye kuburuza nguo (Isbaal)

Ni mtu mwenye kuiachia na kuiteremsha nguo yake ikashuka chini ya vifundo viwili vya miguu. Sheikh Ibn Baaz (Rahimahu-Allaah) amesema: "Ni wajibu kwa mwanamume Muislamu amche Allaah, na anyanyue nguo yake ikiwa ni kanzu, au kikoi, au suruali na kadhalika, isishuke chini ya vifundo viwili vya miguu. Na ubora zaidi kwake iwe nguo yake kati ya nusu muundi hadi kwenye vifundo.”

Hata kuna baadhi ya Mafuqahaa wametanua wigo wa hilo kufikia kwenye mikono ya nguo. Wanasema kuwa mikono ya nguo isivuke kifundo cha mkono na kufunika sehemu ya kiganja. Wengine hata kilemba kuwa kisidizi sana urefu na upana, na mikia yake isidizi zaidi ya nchi moja (shibr). Hawa wanaitegemea Hadiyth nyingine ya Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam)  isemayo:

((الإسبال في الإزار والقميص والعمامة، من جَرَّ شيئًا خيلاء لم ينظُرِ الله إليه يوم القيامة)).
(("Isbaal" iko katika izari, kanzu na kilemba. Yeyote  mwenye kuburuza chochote (katika hivyo) kwa kibr, basi Allaah Hatomtizama Siku ya Qiyaamah)). [Imepokelewa toka kwa Saalim bin ‘Umar toka kwa baba yake toka kwa Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam)]

Kisha Mafuqahaa wamezitoa hali nne nje ya makhitilafiano, kwa maana kwamba wamekubaliana wote katika hali hizo.

Ya kwanza: Kuburura nguo kimakusudi kwa kibr. Hili ni haraam, na ni katika madhambi makubwa.

Ya pili: Kuburuza kutokana na dharura iliyompata mtu kama kuficha ugongwa kwenye makanyagio yake au mfano wake. Hili linajuzu. Ni kama kuvaa hariri kwa mwanamume kutokana na ugonjwa wa ngozi.

Ya tatu: Kuburuza wanawake maabaya na mabaibui yao na kadhalika. Hili limeruhusiwa na Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam)  kwa kiasi cha inchi moja ili kusitiri makanyagio yao. Hili pia halina mahitalifiano.

Ya nne: Kuburuza kutokana na dharura ya ghafla iliyomtokezea mtu kama tukio la kutisha, au hasira kali, au kusahau na kadhalika. Hili halina mahitalifiano pia.

Ama kwa upande wa hukmu ya Isbaal bila kusudio la kibr, Mafuqahaa wamekhitalifiana kwa kauli mbili:


Kauli ya kwanza:

Kufanya isbaal bila kukusudia kibr si haraam. Hii ni kauli ya Jamhuri ya ‘Ulamaa wa madhehebu manne ingawa wametofautiana katika nukta ya kuwa makruwh (chukizo) hu au jaaiz (kukubalika), lakini haifikii mpaka wa kuwa ni haraam. Wametolea dalili hili kwa baadhi ya Hadiyth ikiwemo ile ambayo Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam)  alimwambia Abu Bakr: ((Wewe si katika wenye kufanya hilo kwa kibr)).

Ibn Qudaamah amesema kwenye Al Mughniy (2/298):
“Ni makruhu kuburuza kanzu, izari na suruwali. Ikiwa atafanya hivyo kwa njia ya kibr, basi ni haraam.”


Na An Nawawiy katika Sharh Muslim (14/62) amesema: “Haijuzu kuiteremsha chini ya mafundo mawili ya mguu ikiwa ni kwa kibr. Na kama ni kwa jinginelo, basi ni makruwh (chukizo).


Kauli ya pili:

“Isbaal ni haraam  kwa hali yoyote. Na kama ni kwa kibr, basi uharamu wake ni mkubwa zaidi.”

Kauli hii imeungwa mkono na ‘Ulamaa wa kale kama Ibn Al-‘Arabiy, Ibn Hajar, Asw- Swan-‘aaniy na wengineo.

Pia ‘Ulamaa wengineo   kama Masheikh Ibn Baaz, Ibn ‘Uthaymiyn, Ibn Jabriyn, Al Fawazaan na ‘Ulamaa wa Al-Lajnah Ad-Daaimah (Tume Ya Kudumu ya Utoaji Fatwa).

Hawa  wametolea dalili baadhi ya Hadiyth ambazo baadhi yake ni mutwlaq (jumuishi)  ambazo hazikutaja kibr, na nyingine muqayyad (ainishi), ambazo zimeainisha kibr kuwa sababu.


Mtu wa pili: Ni msimbuliaji

 "المنان" . "المنان"  linanyambulika toka kisoukomo  (maswdar)"المن" ambalo lina maana nne.


Kwanza: Katika vita, neno hili lina maana ya kamanda au mkuu wa jeshi kumwachalia huru mateka wa kikafiri bila kuchukua fidia yoyote. Ni kama Kauli Yake Ta’alaa:

((فَإِمَّا مَنًّا بَعْدُ وَإِمَّا فِدَاءً حَتَّىٰ تَضَعَ الْحَرْبُ أَوْزَارَهَا))
((Kisha ima (wafanyieni) ihsaan baada ya hapo au wajifidie mpaka vita vitue mizigo yake)) [Muhammad 47: 4]

Pili: Ni Jina kati ya Majina ya Allaah (Al-Mannaan) lenye maana ya Mtoaji hisani na Mpaji wa neema zote kiasili. Kwa maana kwamba neema zote zinatoka Kwake hata kama zitafikishwa au kuwasilishwa au kufanywa na watu. Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa)  Anatuambia:

(( لَقَدْ مَنَّ اللَّهُ عَلَى الْمُؤْمِنِينَ ))
((Hakika Allaah Amewafanyia Waumini hisani kubwa)) [Aal- ‘Imraan (4:164)]

Na pia:
كَذَلِكَ كُنْتُمْ مِنْ قَبْلُ فَمَنَّ اللَّهُ عَلَيْكُمْ

((Hivyo ndivyo mlivyokuwa kabla na Allaah Akakufanyieni ihsaan basi hakikisheni)). [An Nisaa (5:94)]

Na katika Sunnah, Hadiyth ya Anas inasema:

((اللهم إني أسألك بأن لك الحمد، لا إله إلا أنت المنان، بديع السموات والأرض...))
((Ee Allaah! Hakika mimi nakuomba kwa kuwa Himdi ni Yako. Hapana mwabudiwa wa haki ila Wewe Mhisani na Mpaji wa neema, Muumbaji wa mbingu na ardhi bila ruwaza)). [Imesimuliwa na wanne, pamoja na Al Haakim aliyesema ni Swahiyh. Adh-Dhahabiy amewafikiana naye, na Al-Albaaniy kasema ni Swahihy]


Tatu: Ni aina ya chakula mithili ya asali ambayo Banu Israaiyl waliteremshiwa na Allaah ('Azza wa Jalla).


Nne: Ni mtu kuelezea hisani, wema, huduma au msaada aliomfanyia mtu mwingine kwa njia ya masimango, na kumsababishia anayesimangwa adha na kutahayuri. Maana hii ndiyo iliyokusudiqwa katika Hadiyth hii Tukufu.


Masimango ya aina yoyote yakiwa makubwa au madogo ni katika madhambi makubwa yatakayomwingiza mtu ndani ya makamio hayo matatu yaliyokuja kwenye Hadiyth hii ya Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam).


Masimbulizi kama haya hufuta thawabu zote za msimbuliaji. Mtu akitoa swadaqah, kisha akamsimbulia anayempa, basi thawabu zake zote huyeyuka. Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Anatuambia:
( يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا لَا تُبْطِلُوا صَدَقَاتِكُمْ بِالْمَنِّ وَالْأَذَى ))
((Enyi walioamini! Msiharibu swadaqah zenu kwa kusimbulia na maudhi)). [Al-Baqarah (2:264)]

Ibn ‘Abbaas (Radhwiya Allaahu ‘anhumaa) amesema: “Wema hautimu ila kwa mambo matatu: Kwa kuuharakisha, kuudogesha na kuusitiri.”

Masimbulizi mtu anaweza kuyaona ni jambo dogo, kumbe madhara yake ni makubwa mno.



Mtu wa tatu: Ni mfanya biashara au mchuuzi mwenye kutumia kiapo ili kuvutia biashara yake.


Hili ni janga baya na mtihani mkubwa unaowakabili wachuuzi na wafanya biashara wengi. Huwaapia wateja kwa viapo vyote kwamba bidhaa ni nzuri, ina ubora, haina tatizo lolote na kadhalika ili ima kuongeza thamani yake au kumvuta mteja ainunue. Wengine huapa kwamba wameinunua kwa bei kadhaa na bei wanayouzia haishuki hata kidogo wakati ni kinyume na hivyo. Na hapa hutumia Jina la Allaah ('Azza wa Jalla)  kwa ajili ya kuwalaghai wateja, na hichi ndicho kiini cha hayo yatakayomsibu Siku hiyo ya Qiyaamah, kwa kuwa mchezo huu ni haraam, na dhambi kati ya madhambi makubwa. Na hii ni kutokana na haya yafuatayo:

1- Ni kudharau kwake Jina la Allaah ('Azza wa Jalla)  katika kiapo hicho na kukhalifu amri ya Allaah ('Azza wa Jalla)  ya kuhifadhi kiapo Aliposema:
(( وَاحْفَظُوا أَيْمَانَكُمْ ))
((Na hifadhini viapo vyenu)).  [Al-Maaidah (5:89)]


2-Kusema kwake uongo, kwa kuwa bidhaa iko kinyume na anavyoinadia. Uongo ni katika sifa mbaya kabisa zisilolaikiana na Muislamu na ambazo inabidi Muislamu ajiepushe nazo ili asije kusajiliwa kwenye buku la wasemao uongo.


3-Kula kwake mali anayoichuma kwa njia ya kiapo hicho kwa batili, na kiapo chake hicho ni katika viapo vyenye kubeba madhambi makubwa zaidi.

Kiapo hiki ni kile kiitwacho الغموس. Imekuja katika Swahihy mbili kwamba Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam)  amesema:

(( من حلف على يمين هو فيها فاجر يقتطع بها مال امرئ مسلم، لقي الله وهو عليه غضبان))
((Mwenye kuapa juu ya kiapo ambacho yeye ni mwongo ili amege kwacho mali ya mtu Muislamu, atakutana na Allaah Akiwa Amemghadhibikia)). [Imepokelewa na ‘Abdullaah bin Mas’uwd (Radhwiya Allaahu ‘anhu).
  

Ama mchuuzi kuapa kila anapouza au kununua hata kama ni mkweli, hili pia ni haraam, na ni moja kati ya madhambi makubwa. Ni kutokana na Hadiyth ya Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam)

((ثلاثة لا يكلمهم الله يوم القيامة ولا يزكيهم ولهم عذاب أليمأشيمط زان، وعائل مستكبر، ورجل جعل الله بضاعته لا يشتري إلا بيمينه ولا يبيع إلا بيمينه))
((Watu watatu Allaah Hatozungumza nao Siku ya Qiyaamah, wala Hatowatakasa, na watapata adhabu iumizayo: Kikongwe mzinzi, masikini mwenye kibri, na mtu ambaye Amemfanya Allaah bidhaa yake; hanunui ila kwa kumwapia, na hauzi ila kwa kumwapia)). [Imesimuliwa na Atw-Twabaraaniy katika Hadiyth ya Sulaymaan]

Sheikh Ibn ‘Uthaymiyn (Rahimahu-Allaah) amesema: “Maana yake ni kuwa kila anaponunua huapa, na kila anapouza huapa ili kupata faida zaidi. Na huyu amestahiki adhabu hii, kwa kuwa, kama ni mkweli, basi viapo vyake vinaonyesha kuwa havina tena thamani wala uzito kwake, ni kama kitu cha mchezo tu, na kukhalifu kwake Kauli Yake Ta’alaa:
  واحفظوا أَيْمَانَكُمْ   

Na hifadhini viapo vyenu [Al-Maaidah:

Na kama ni mwongo, basi anakuwa amekusanya mambo manne yaliyotolewa onyo.”


Ama hukmu ya kuapa kwenye manunuzi na mauzaji bila kuwa ni tabia ya muuzaji au mnunuzi, ‘Ulamaa wanasema kuwa kiasili ni makruwh (chukizo) Ni kutokana na ujumuishi wa Kauli Yake Ta’alaa:

  إِنَّ الَّذِينَ يَشْتَرُونَ بِعَهْدِ اللَّهِ وَأَيْمَانِهِمْ ثَمَنًا قَلِيلًا أُولَئِكَ لَا خَلَاقَ لَهُمْ فِي الْآخِرَةِ وَلَا يُكَلِّمُهُمُ اللَّهُ وَلَا يَنْظُرُ إِلَيْهِمْ يَوْمَ الْقِيَامَةِ وَلَا يُزَكِّيهِمْ وَلَهُمْ عَذَابٌ أَلِيمٌ)
((Hakika wale wanaobadilisha ahadi ya Allaah na viapo vyao kwa thamani ndogo; hao hawana sehemu yoyote katika Aakhirah na wala Allaah Hatowasemesha na wala Hatowatazama Siku Ya Qiyaamah na wala Hatowatakasa na watapata adhabu iumizayo)) [Aal ‘Imraan (3:77)]

Na kwa Hadiyth isemayo:
((الحلف منفقة للسلعة.. ممحقة للبركة))
((Kuapa kunapromoti bidhaa, kunafuta barkah)). [Hadiyth Marfu’u iliyopokelewa na Abuu Hurayrah (Radhwiya Allaahu ‘anhu) [Imesimuliwa na Al-Bukhaariy na Muslim]

Ama kuapa kwa haja bila kukithirisha, hili halina ubaya.




Hadiyth Ya Tatu:

03-Mtu Mwenye Maji Ya Ziada Jangwani Anayazuia Kwa Mpita Njia, Na Mtu Aliyepatana Na Mtu Kumuuzia Bidhaa Baada Ya Alasiri Akamwapia Kwa Allaah Kwamba Ameinunua Kwa Thamani Kadha Wa Kadha Akamsadiki, Naye Yuko Kinyume Na Hilo, Na Mtu Aliyempa (imaam) Kiongozi Bay’ah, Hampi Bay’ah Hiyo Ila Kwa Ajili Ya Dunia Tu.



 عن أبي هريرة قالقال رسول الله صلى الله عليه وسلم ((ثَلَاثٌ لَا يُكَلِّمُهُمُ اللَّهُ يَوْمَ الْقِيَامَةِ ، وَلَا يَنْظُرُ إِلَيْهِمْ ، وَلَا يُزَكِّيهِمْ وَلَهُمْ عَذَابٌ أَلِيمٌ : رَجُلٌ عَلَى فَضْلِ مَاءٍ بِالْفَلَاةِ يَمْنَعُهُ مِنَ ابْنِ السَّبِيلِ ، وَرَجُلٌ بَايَعَ رَجُلًا بِسِلْعَةٍ بَعْدَ الْعَصْرِ فَحَلَفَ لَهُ بِاللَّهِ لَأَخَذَهَا بِكَذَا وَكَذَا فَصَدَّقَهُ وَهُوَ عَلَى غَيْرِ ذَلِكَ ، وَرَجُلٌ بَايَعَ إِمَامًا لَا يُبَايِعُهُ إِلَّا لِدُنْيَا فَإِنْ أَعْطَاهُ مِنْهَا وَفَى ، وَإِنْ لَمْ يُعْطِهِ مِنْهَا لَمْ يَفِ)).
Imepokelewa toka kwa Abuu Hurayrah akisema: “Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa Sallam) amesema: ((Watatu (wa aina tatu) Allaah Hatozungumza nao Siku ya Qiyaamah, wala Hatowaangalia, wala Hatowatakasa, na watapata adhabu iumizayo. Mtu mwenye maji ya ziada jangwani anayazuia kwa mpita njia, na mtu aliyepatana na mtu kumuuzia bidhaa baada ya Alasiri, akamwapia kwa Allaah kwamba ameinunua kwa thamani kadha wa kadha akamsadiki, naye yuko kinyume na hilo, na mtu aliyempa (imaam) kiongozi bay’ah, hampi bay’ah hiyo ila kwa ajili ya dunia tu. Akimpa kitu katika hiyo dunia, hutekeleza ipasavyo, na kama hakumpa kitu katika hiyo dunia, hatekelezi chochote)). [Al-Bukhaariy, Muslim na wengineo]


Faida Na Sharh:


Mtu wa kwanza: Mtu mwenye maji ya ziada jangwani anayazuia kwa mpita njia.

Mtu huyo ni mwenye maji shambani kwake, au kwenye kisima chake, au kwenye tanki, au kwenye bomba lake na kadhalika, na huko aliko ni ardhi mahame isiyo na watu. Lakini watu wanapopita hapo ili wanywe au wateke anawazuia kwa roho mbaya, au chuki, au ubaguzi na kadhalika. Huyu atastahiki makamio hayo matatu Siku hiyo.


Mtu wa pili:  Ni mtu aliyeuza bidhaa baada ya Alasiri, akaapa kwa mnunuzi kuwa ameinunua kwa thamani fulani ili amuuzie kwa bei ya juu zaidi

Anafanya hivyo ilhali anasema uongo, na mteja akamsadiki na akainunua kwa mujibu wa kiapo chake huku mambo ni kinyume, basi huyu anaingia pia kwenye makamio hayo. 

‘Ulamaa wamejaribu kuelezea sababu ya Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam)  kuuhusisha hapa wakati wa Alasiri kinyume na nyakati nyinginezo. Sababu zenyewe ni:

1- Wakati huu ndio wakati bora kabisa ambapo Malaika wa usiku na mchana hukutana.

2-Alasiri ni “Asw-Swaalatul-Wustwaa” (Swalaah ya katikati) ambayo Allaah ('Azza wa Jalla)  Ameipa umahususi wa kipekee wa kuilinda baada ya ujumuishi wa Swalaah nyinginezo Aliposema:

((حَافِظُوا عَلَى الصَّلَوَاتِ وَالصَّلَاةِ الْوُسْطَى))
((Hifadhini Swalaah, na Swalaah ya kati)). [Al-Baqarah (2:283)]

3-Ni wakati wa kuhitimishwa amali.

4-Ni wakati wa kupandishwa amali.

Hivyo kufanya uhalifu huo katika wakati huo inakuwa ni vibaya zaidi. Na hii haimaanishi kuwa nyakati nyingine inafaa kufanya uhalifu huo, bali ni haraam nyakati zote.


Mtu wa tatuNi mtu aliyetangaza utiifu wake kwa kiongozi, na hafanyi hivyo ila kwa ajili ya maslahi ya kidunia, na si kwa ajili ya Allaah.

Hii ni aina ya unafiki mbaya kabisa. Kutangaza utiifu kwa kiongozi ni wajibu kwa kila Muislamu, na kila Muislamu ni lazima awe na kiongozi, sawasawa akiwa kiongozi mkuu wa nchi, au kiongozi katika eneo analoishi. Na utiifu kwa kiongozi au imaam ni wajibu kwa kila linalomridhisha Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa). Ama linalomghadhibisha, basi ni wajibu kuliepuka.

Na utiifu huu ni lazima uwe juu ya Qur-aan na Sunnah. Atatangaza utiifu wake kuwa atende haki, atekeleze adhabu za ki-shariy’ah (huduwd), aamrishe mema na akataze munkari.

Nukta hii inatukumbusha pia kuwa amali yoyote ambayo haimkusudii Allaah ('Azza wa Jalla) bali kwa maslahi ya kidunia, basi imeharibika na mfanyaji wake anachuma madhambi.



Hakuna maoni:

Chapisha Maoni

20-Hakika Shirki Ni Dhulma Kubwa Mno! - Isti’aadhah Kwa Asiyekuwa Allaah

  إِنَّ الشِّرْكَ لَظُلْمٌ عَظِيم   Hakika Shirki Ni Dhulma Kubwa Mno!   20 - Isti’aadhah  (Kuomba Kinga) Kwa Asiyekuwa Allaah   ...