Translate

Ijumaa, 29 Novemba 2019

Masuala Kumi Yanayoeleweka Vibaya Katika Uislam - 4

Suala Nambari 4 Linaloeleweka Vibaya

Uislamu unakubaliana zaidi na Waarabu tu kwa sababu:
·                     Waislamu wengi ni Waarabu
·                     Qur-aan ipo kwa Kiarabu

JIBU
Hoja ya mwanzo kuhusu suala hili linaloeleweka vibaya ipo mbali na ukweli. Waislamu walio zaidi ya bilioni moja duniani, basi kati ya asilimia 18 tu ni Waarabu. Nchi zilizo na idadi kubwa ya Waislamu duniani ni Indonesia. Nchi ya pili yenye idadi kubwa ya Waislamu ni Bangladesh. Sio nchi hata moja kati ya hizi ni ya Kiarabu.

Uislamu ni dini yenye kukua kwa kasi duniani (Encyclopedia Britannica). Ina wafuasi kwenye mabara yote yenye idadi kubwa ya watu, na pia inakubalika kwa Waarabu na wasio Waarabu. Waislamu hadi itakapofikia mwisho mwa karne, wanatarajiwa kuwa ni dini kubwa kabisa kati ya dini zenye wafuasi wachache largest religious minority nchini Marekani, wakiwashinda Mayahudi.

Lalamiko la ulimwengu la Uislamu kwa Waarabu na wasiokuwa Waarabu linafuatia ingawa Qur-aan ni ya Kiarabu. Allaah Anaelezea ndani ya Qur-aan kwamba njia hii ya maisha inayoitwa Uislamu ni ya watu wote (tafsiri inafuata):
 [21:107]

 [34:28]

Juu ya hivyo, Muumba Hatumii kigezo cha rangi au lugha ya mama mother tongue kuwahukumu, wawe ni Waarabu au sio. Badala yake, ni kiwango cha kumtambua Allaah ndicho kigezo.

 [49:13]

Uchaguzi wa Kiarabu kuwa ni lugha ya Qur-aan umeelezwa kiurahisi na kiuwazi (tafsiri inafuata):
 [41:44]

Hata hivyo, ni muhimu pia kutilia mkazo kwamba Qur-aan ikiwa na uteremsho wa mtindo wa Kiarabu ni Neno sanifu la Muumba, lakini tafsiri yoyote sio (Qur-aan). Kila tafsiri kiusahihi inaitwa kuwa ni tafsiri na fafanuzi, kwani kila mfasiri anaingiza matashi/ upendeleo (bias) wake.

Itaendelea in Shaa Allaah....


MAWAIDHA : Sheikh Nassor Bachu - Njama za Makafiri [ Listen/ Download]


OMBI LETU KWAKO

Kwa yoyote yule mwenye Muhadhara wa Sheikh Nassor Bachu basi anaweza kukutumia kwa Email hii ili wengi wanufaike kwayo muislamublog@gmail.com



Umuhimu Wa Swalah

Bismillahi-Rrahmani-Rrahim. Alhamdulillahi Rabbil Aalamiyn, waswalatu wassalam ‘alaa RasuliLlaahi. Amma ba’ad.
Assalamu ‘Alaykum wa RahmatuLlaahi wa Barakaatuh.
Anasema Allaah Subhaanahu wa Ta'ala:

}}وَأَقِمِ الصَّلاَةَ طَرَفَيِ النَّهَارِ وَزُلَفًا مِّنَ اللَّيْلِ إِنَّ الْحَسَنَاتِ يُذْهِبْنَ السَّـيِّئَاتِ ذَلِكَ ذِكْرَى لِلذَّاكِرِينَ (11:114)
}}وَاسْتَعِينُواْ بِالصَّبْرِ وَالصَّلاَةِ وَإِنَّهَا لَكَبِيرَةٌ إِلاَّ عَلَى الْخَاشِعِينَ (2:45)
Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) ameturuzuku zawadi kubwa ambayo thamani yake haina mfano. Lakini kwa ajili ya uzoefu wetu juu yake, mara nyingi hatuipi cheo na heshima inayostahiki zawadi hiyo. Zawadi hiyo yenye thamani kubwa ni Swalah. Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam)  alituletea zawadi hii kutoka kwa Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) alipopelekwa kwenye mbingu saba katika safari yake ya Mi’raaj. Kama tujuavyo, kwanza Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam)   alipewa Swalah khamsini ambazo zilipunguzwa mpaka tano, zile tunazoziswali sasa; na kwa Ukarimu Wake Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) tunapata fadhila ya zile Swalah khamsini vile vile, ilihali tunaswali tano. Subhana Allaah!
Kwa hivyo Swalah yetu, ambayo wengi wetu tunaichukulia kwa wepesi na kuipuuza, ina utukufu wa kukutana kwa Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) Inasemekana kuwa yale maneno tunayoyasema katika tashahhud ni kumbukumbu ya mawasiliano yaliyotokea baina ya Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Mola wake wakati huo wa Mi’raaj. Wa Allaahu A’alam. Kwa hivyo, kila tunapokaa kwenye tashahhud, inatupasa tuwe ni wenye kuzingatia utukufu wa kikao hicho.
Swalah ni mojawapo ya njia kubwa ambayo Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) Ametutolea iwe ni hakikisho kuwa tunabaki kwenye njia ya Uislamu ambayo inaongoza kwenye Rehma Yake na Msamaha Wake, na kila zuri duniani na Aakhira. Kwa hakika, Swalah inatuunganisha na Mola wetu. Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amelinganisha Swalah na mto ambao mtu akioga ndani yake mara tano kwa siku, Hakika mtu huyo hatokuwa mchafu. Hivyo basi, Swalah zetu tano zinazuia kufungika kwa uhusiano baina yetu na Allaah. Kwa hivyo kuswali kwetu, daima kunafuta madhambi madogo yaliyotendeka baina ya kila Swalah. Allaah  (Subhaanahu wa Ta'ala)  Ametufaradhishia Swalah ili daraja zetu zipande, thawabu zetu zizidishwe, na madhambi yetu yadondoke kutoka kwetu, na kwa ajili yake Atutie Peponi na Atuokoe na Moto.
Walakini, Swalah ni kama upanga wenye makali pande zote mbili. Tukiihifadhi, itatupa mwangaza kwenye nyoyo zetu, makaburi yetu, na siku ya Kiama. Itatushuhudia wakati ambao tunahitaji shahidi ili tuokoke na adhabu ya Moto, kama tujuavyo kutoka kwa Yahya ibn Sa'id kwenye Muwatta: “kitendo cha kwanza kutizamwa siku ya Kiama ni Swalah, ikikubaliwa, basi vitendo vyengine vitaangaliwa, lau sio hivyo, basi vitendo vyote pia havitoangaliwa.” Lakini tukiipuza na kuitoa thamani, basi nayo itatoa ushahidi dhidi yetu, wakati ambao tunahitajia shahidi zaidi. Lazima tujihadhari tusiwe miongoni mwa watu wale ambao Allaah  (Subhaanahu wa Ta'ala) anawazungumzia katika Surat Maryam:
}}فَخَلَفَ مِن بَعْدِهِمْ خَلْفٌ أَضَاعُوا الصَّلَاةَ وَاتَّبَعُوا الشَّهَوَاتِ فَسَوْفَ يَلْقَوْنَ غَيًّا (19:59)
Na tuzingatie maneno ya Mtume Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) : Jabir amesema, “nimemsikia Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam)  akisema,
((Kitu ambacho kinasimama baina ya binaadamu na kutokuamini na shirki, ni kuacha Swalah)) [Muslim]
Cheo cha Swalah katika dini ni kama mfano wa mlingoti wa nyumba, ukiwepo, nyumba itakuwa madhubuti na vifaa vyake vyote vitalingana mahali pake. Lakini isipokuweko, basi jengo lote litabomoka na kuwa halina maana.
Kulingana na hayo, ni muhimu kukumbuka kuwa Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) Hatuamrishi kuswali tu, bali Anatuamrisha tuimarishe Swalah, ambapo Mufassirun wote wamekubaliana kuwa kuimarisha Swalah, ina uzito zaidi kuliko kuswali tu rakaa tulizoambiwa. Kuimarisha Swalah ina maanisha shuruti zote za twahara, mahali pa kuswali, nguo, kibla, na mengineyo, yote ni lazima yatimizwe.
'Abdullaah bin Mas'uud amesema, "Yeyote anayetamani kukutana na Allaah  (Subhaanahu wa Ta'ala)  kesho, basi atunze Swalah hizi tano wakati muadhini unapoadhini Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala)  Alimuonesha Mtume Wake (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam)  Sunnah zote za muongozo, na kuimarisha Swalah ni moja wapo. Ukiswali nyumbani kwako kama wanao kosa kuswali jama’a, umetupilia mbali Sunnah ya Mtume Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) . Na ukitupa Sunnah ya Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) , huwezi kuongoka. Mumetuona sisi, na hakuna kati yetu ambao walikosa Swalah ya jama’ah isipokuwa wale wanafiki ambao unafiki wao ulikuwa unajulikana, au wale waliokuwa wagonjwa. Watu walikuwa wanakuja kuswali jama’ah huku wameshikiliwa na watu wawili mpaka wakasimamishwa kwenye safu”.
Swalah ni kitu ambacho hakiwezi kumalizwa kuzungumziwa, na vitabu vingi vimeandikwa juu yake, lakini ningependa kumalizia kwa kauli zifuatazo walizosema  baadhi ya Maulamaa waliotangulia,  kuhusu Swalah:
1)
"Kwa vile Allaah Anajua kuwa munachokeshwa na kitu mara moja,
Amezifanya namna kwa namna ibada zenu juu Yake.
Kwa vile Anajua kuwa muna pupa,
Amewakataza kuzifanya Ibada wakati mwengine.
Amefanya hivyo ili matamanio yenu yawe ni kuimarisha Swalah,
Sio kuswali tu!
Sio wote wenye kuswali wanaimarisha Swalah.
Swalah ni utakaso wa nyoyo,
Na mahali pa mazungumzo ya undani,
Baina ya mja na Mola wake.
 Viwanja vya siri vinaenea ndani yake,
Mianga  inaangaza na kumulika nuru zake.
Allaah Anajua nyinyi ni dhaifu,
Basi Amezifanya idadi za Swalah kidogo tu!
Anajua kuwa nyinyi ni wahitaji wa Rehma Zake nyingi.
Kwa hivyo amezidisha Neema Zake kwenu ndani yake"

2)
"Yeyote anayetamani kujiokoa nafsi yake, kujifurahisha moyo wake, kusitiriwa makosa yake, kupata Radhi za Mola wake, na moyo wake kupata uhai, lazima ampe heshima Anayostahiki Mola wake na asicheleweshe Swalah wakati unapoingia, na asijiruhusu kufanya hivyo. Wala asiswali peke yake wakati ambao anaweza kuswali jama’ah. Na bado tunaona watu wakichelewesha Swalah na kuswali peke yao ilihali wanaweza kuswali jama’a. Ni ubaya ulioje wanaoufanya hao. Tunawaona wamezama ndani ya mhangaiko, huzuni, taabu, na mateso. Hakika, chanzo cha yanayowapata ni kupuuza kwao kwa dini. Pia tunaona kuwa hawajui tofauti ya kuswali safu ya mbele wala ya nyuma. Sio kwa sababu hawajui, bali ni kwasababu ya kutojali dini. Hawajali kuhusu twahara pia.  Lakini ukweli ni kuwa, yeyote mwenye najisi, hana udhu, na ambae hana udhu, hana Swalah, na ambae hana Swalah, hana mazuri yoyote. Wa Allaahu A’alam"   

3)
"Kuna nuru kubwa katika Swalah ambayo inaangaza ndani ya nyoyo za wale wanaoimarisha swala na wale wanaomakinika na kunyenyekea kwenye Swalah zao. Kwa hivyo, ukija kuswali, komboa moyo wako kutokana na dunia na vilivyomo ndani yake; jihusishe na kumakinika na hudhurio la Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala)   Ambaye Swalah hiyo ni kwa ajili Yake.  Lazima ujue kwamba msingi wa Swalah ni unyenyekevu na kumtii Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala)  kwa kusimama, kurukuu, na kusujudu mbele Yake, na Kumtukuza kwa takbir, tasbih, na dhikri.
Kwa hivyo tunza Swalah yako kwa sababu ni ibada kubwa kabisa miongoni mwa ibada. Usimuache shetani acheze na moyo wako na kukupurukusha katika Swalah ili usipate utamu wa nuru ya Swalah. Na muombe Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) kwani Yeye ndiye Mbora wa Wasaidizi".

Tunamuomba Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) Atujaaliye tuwe miongoni mwa waja wake ambao wanathamini ile zawadi Aliyotupa ndani ya Swalah. Tunamuomba Atuongezee unyenyekevu na utulivu ndani ya Swalah ili tuwe ni wenye kufaidika nayo. Tunaumuomba Allaah Atulete pamoja ndani yake (Swalah) na atuzidishie idadi ya safu na atupe nguvu ndani yake (Swalah) ili tutoke ndani yake ilihali tumenufaika. Aamiyn.


Jumatano, 27 Novemba 2019

Atakayemtimizia Haja Nduguye Na Kumsitiri Atapata Faraja Na Sitara Siku Ya Qiyaama

Hadiyth Ya 23
 Atakayemtimizia Haja Nduguye Na Kumsitiri Atapata Faraja Na Sitara Siku Ya Qiyaama


 عن ابْنَ عُمَرَ (رضي الله عنهما)  أَنَّ رَسُولَ اللَّهِ (صلى الله عليه و آله وسلم) قَالَ: ((الْمُسْلِمُ أَخُو الْمُسْلِمِ لاَ يَظْلِمُهُ ولاَ يُسْلِمُهُ، وَمَنْ كَانَ فِي حَاجَةِ أَخِيهِ كَانَ اللَّهُ فِي حَاجَتِهِ، وَمَنْ فَرَّجَ عَنْ مُسْلِمٍ كُرْبَةً فَرَّجَ اللَّهُ عَنْهُ كُرْبَةً مِنْ كُرُبَاتِ يَوْمِ الْقِيَامَةِ، وَمَنْ سَتَرَ مُسْلِمًا سَتَرَهُ اللَّهُ يَوْمَ الْقِيَامَةِ)) متفق عليه
Imepokelewa kutoka kwa Ibn ‘Umar (رضي الله عنهما)  kwamba Rasuli  wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema: ((Muislamu ni ndugu wa Muislamu, hamdhulumu wala hamsalimishi [kwa adui]. Na atakayemtimizia haja nduguye, Allaah Atamtimizia haja yake. Na atakayemfariji [atakayemuondoshea] Muislamu dhiki yake, Allaah Atampa faraja ya dhiki zake Siku ya Qiyaamah. Na atakayemsitiri Muislamu mwenzake [aibu zake], Allaah Atamsitiri [aibu zake] Siku ya Qiyaamah)). [Al-Bukhaariy na Muslim]


Mafunzo Na Mwongozo:


1. Waislamu ni ndugu wanapasa kutendeana mema. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):

إِنَّمَا الْمُؤْمِنُونَ إِخْوَةٌ فَأَصْلِحُوا بَيْنَ أَخَوَيْكُمْ ۚ وَاتَّقُوا اللَّـهَ لَعَلَّكُمْ تُرْحَمُونَ﴿١٠﴾
Hakika Waumini ni ndugu, basi suluhisheni baina ya ndugu zenu. Na mcheni Allaah ili mpate kurehemewa. [Al-Hujuraat: 10]

Pia rejea: Al-Maaidah (5: 2).
Rejea pia Hadiyth namba (20), (21).



2. Uislamu unakataza kufanyiana dhulma.

Rejea Hadiyth namba (19).

Pia Allaah (سبحانه وتعالى) Anasema katika Hadiyth Qudsiy: ((Enyi waja Wangu! Mimi Nimejiharamishia dhuluma juu ya Nafsi Yangu na Nikaifanya ni haramu baina yenu basi msidhulumiane)). [Muslim]


3. Waislamu wanapasa kusaidiana dhidi ya adui.


4. Himizo la kusaidiana wakati wa dhiki na shida.


5. Himizo la kusitiriana aibu na onyo kali la kuieneza aibu, kashfa, uzushi n.k. kwa wengineo. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):

 إِنَّ الَّذِينَ يُحِبُّونَ أَن تَشِيعَ الْفَاحِشَةُ فِي الَّذِينَ آمَنُوا لَهُمْ عَذَابٌ أَلِيمٌ فِي الدُّنْيَا وَالْآخِرَةِ ۚ وَاللَّـهُ يَعْلَمُ وَأَنتُمْ لَا تَعْلَمُونَ ﴿١٩﴾
Hakika wale wanaopenda uenee uchafu wa kashfa kwa wale walioamini; watapata adhabu iumizayo duniani na Aakhirah. Na Allaah Anajua nanyi hamjui [An-Nuwr (24: 19)]
         

6. Malipo ya Aakhirah ni makubwa zaidi kuliko ya duniani. Rejea An-Nahl (16: 41).


7. Rahma ya Allaah (سبحانه وتعالى) kuwalipa waja wanapotendeana wema.  


8. Muislamu akhiari kumwondoshea dhiki nduguye duniani apate kuondoshewa dhiki Siku ya Qiyaamah, kwani huko ndiko kwenye dhiki na shida kubwa zaidi.

Rejea: Al-Hajj (22: 1-2).


Masuala Kumi Yanayoeleweka Vibaya Katika Uislam - 3

Muislamublog.com

 

Ndani ya Uislamu, wanawake ni duni kuliko wanaume kwasababu:
·        mwanaume anaweza kuoa hadi wake wanne, mwanamke anaweza kuolewa na mwanaume mmoja tu.

·        sehemu ya urithi wa mwanamme ni kubwa kuliko ya mwanamke.

·        mwanamme anaweza kuoa mwanamke asiye Muislamu, mwanamke hawezi

·        mwanamke ni lazima avae hijaab.

JIBU
Suala hili pana halielekei kufuatana kwa mnasaba wa hoja zinazotolewa. Tathmini ya mwanzo na muhimu zaidi ya kuifanya ni kuhusu suala maarufu “Je wanaume ni sawa na wanawake?” Ni suala ambalo limetengenezwa vibaya, lisiloweza kujibika. Tatizo ambalo watu wengi wanatumia kuliepuka ni kutolitafsiri neno “usawa”. Hii ni nukta inayohitaji kuupambanua usawa ambao ni lazima uelezwe kwa hali inayopimika. Kwa mfano, wanawake kwa kiwango fulani wapo juu kuliko wanaume kama tutauliza nani ni mfupi kwa (kupambanisha na) urefu kuliko mwengine (“Ukuaji na Maendeleo” Encyclopaedia Britannica, 1992). Wanawake pia wapo juu kwa kiwango fulani kama tutauliza watoto wana mapenzi zaidi na nani, mama au baba? Wanawake pia wapo juu kwa kiwango fulani kama tutauliza nani ana tabia ya kujiweka kwenye jamii zaidi. Kwa upande mwengine, wanaume wapo juu kwa kiwango fulani kama tutauliza nani ni mrefu kwa (kupambanisha na) ufupi kuliko mwengine. Na mambo mengineyo: kila suala linaweza kugeuzwa upande mwengine, na muhimu zaidi ni kuwa hali hizi hazina mnasaba.
Je, kinachofuata, ni hali gani muhimu ambayo tuna wasiwasi nayo kuhusiana na usawa wa jinsia? Kiasili, kutokana na uoni wa Qur-aan na Sunnah, hali iliyokuwa muhimu zaidi ni nani aliyekuwa mtiifu kwa Allaah, wanaume au wanawake? Suala hili bila ya shaka linajibiwa ndani ya Qur-aan (iliyotafsiriwa):
 [4:124]

 [33:35]
Qur-aan na Sunnah zinarudia tena na tena kwamba Allaah Anampendelea mtu mmoja dhidi ya mtu mwengine kwa kigezo chake cha hamasa, unyenyekevu, khofu, mapenzi, na matarajio ya Allaah (neno la kiarabu la ‘Taqwa’ ‘ucha Mungu’ ni gumu kulipatia tafsiri yake halisi). Sifa nyengine zote zimetenguliwa: jinsia, kabila, taifa, asili, n.k.
Kwa vile Allaah Hapendelei jinsia moja dhidi ya nyengine ndani ya matakwa Yake kwetu sisi (na inasaidia kukumbuka kwamba Allaah sio mwanamume wala mwanamke), na sasa tunaweza kuelezea tofauti baina ya jinsia ndani ya Uislamu.
Kwanza, wanaume na wanawake hawapo sawa kama tunavyoelewa. Muumba Anaelezea ndani ya Qur-aan (iliyotafsiriwa):
 [3:36]
Wanaume na wanawake ni tofauti kwenye tabia, na kwenye majukumu yao ndani ya Uislamu. Hata hivyo, wote wana ulazima wa uwajibikaji kwa mwenziwe, hususan nukta hii muhimu inayofuata ambayo ni lazima ieleweke ndani ya mjadala wowote kuhusu wanaume na wanawake.
 [24:32]
Ndani ya Aayah hii, Muumba Anatilia mkazo kwamba ndoa ni lazima ifungwe mapema na Waislamu: tabia ya kuwa pweke isikuwepo. Kwa kuwepo hili akilini, tunaweza kuanza kuelewa hoja nne zilizotajwa hapo juu kwa hitimisho lisilo na kosa lolote.
Wanaume na wanawake ni tofauti kwenye kuwajibika kwao kwa familia ambazo wanahimizwa sana kuzisimamisha. Wanawake hawawajibiki kufanya kazi, wakati wanaume wanalazimika. Mwanamume ni lazima atoe mahitaji kwa familia, lakini mwanamke hana haja ya kutumia pesa yake kwa ajili hiyo, ingawa anapata malipo kwa kufanya hivyo. Allaah Anasema ndani ya Qur-aan (iliyotafsiriwa):
 [4:34]

Kutokana na Sunnah, hususan ndani ya somo la Sunnah linaloitwa Swahiyh al-Bukhaariy, tunaona:
Amesimulia ‘Amr bin Al-Haarih: Zaynab, mke wa ‘Abdullaah alisema: “Nilikuwa Msikitini nikamuona Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akisema: ‘Enyi wanawake! Toeni sadaka hata kama kutoka kwenye mapambo yenu’ Zaynab alikuwa akimpatia ‘Abdullaah na mayatima walio chini ya hifadhi yake. Hivyo alimwambia ‘Abdullaah, “Je unaweza kumuuliza Mtume wa Allaah iwapo naweza kutumia sehemu ya Zakaat kwako na mayatima walio chini ya hifadhi yangu?” Alijibu “Je, utamuuliza mwenyewe Mtume wa Allaah?” (Zaynab akaongeza): Hivyo nilienda kwa Mtume na hapo nikamuona mwanamke wa ki-Aanswari aliyekuwa amesimama mlangoni (kwa Mtume) aliyekuwa na tatizo lililo sawa na langu. Bilaal alipita mbele yetu na tukamuomba, “Muulize Mtume wa Allaah iwapo naweza kutumia sehemu ya Zakaat kwa mume wangu na mayatima walio chini ya hifadhi yangu” Na tukamuomba Bilaal kutomtaarifu Mtume kuhusu sisi. Hivyo Bilaal aliingia ndani na kumuuliza Mtume kuhusiana na tatizo letu. Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) aliuliza, “Hao wawili ni kina nani?” Bilaal alijibu kwamba alikuwa ni Zaynab. Mtume alisema, “Zaynab gani?” Bilaal alisema, “Mke wa ‘Abdullaah (bin Mas’uud)”. Mtume akasema, “Ndio, (inawezekana kwake), na atapata malipo mara mbili yake (kwa tendo hilo): Kwanza kwa kusaidia jamaa zake, na pili kwa kutoa Zakaat.”
Kutokana na waume kulazimishwa kuwahudumia wake, na kwamba ndoa ni pendekezo lililotiliwa mkazo (sana) la Uislamu, ni rahisi kuona kwanini urithi wa wanawake ni nusu ya wanaume. Pia tunatambua kwamba, katika ndoa ni wanaume wanaolazimishwa kuwapatia wanawake mahari yaliyo muafaka. Ni kweli, na inafaa kwa sasa kuzungumza misamiati ya waume na wake kuliko wanaume na wanawake. Allaah Anasema ndani ya Qur-aan (iliyotafsiriwa):
 [4:4]

Allaah Anasema ndani ya Qur-aan (iliyotafsiriwa):
 [2:228]

Hali hii haimuathiri (hata chembe) wadhifa wa Muumba ambaye Ameeleza kwamba Hawaangalii wanawake kuwa ni bora Kwake kuliko wanaume, au kinyume chake. Isipokuwa kwa njia nyepesi ya kugawa majukumu ndani ya nyumba yenye watu wazima wawili: mtu mmoja ni lazima awe na kauli ya mwisho katika masuala ya kila siku. Kama itakavyooneshwa hapa chini ndani ya sehemu kwenye masuala tofauti yanayoeleweka vibaya, ingawa kauli ya mwisho inaangukia kwa mume, ni kwa kupitia njia ya mashauriano kwamba amri zilizo nzuri zinafikiwa.

Wakati wanaume wanaruhusiwa kuoa hadi wake wanne, pia wanalazimika kabla yake kutimiza masharti ya kuweza kuwahudumia kifedha. Pia wamtumikie kila mke kwa haki na usawa pamoja na majukumu ya ndoa na uchumi. Allaah Anasema ndani ya Qur-aan (iliyotafsiriwa):
 [4:3]

Juu ya hivyo, wanawake wanaruhusiwa kukataa posa yoyote iliyofanywa kwake na mposaji aliye tayari (kuoa), hivyo kama atahisi kwamba hawezi kutimiza kanuni za Qur-aan na Sunnah ikiwa ataolewa na mtu fulani, anaweza kukataa posa yake (mposaji). Ingawa (tuhuma hizi) si sahihi kwa Uislamu, ni vyema ikabainishwa kwamba dini zote mbili; Uyahudi na Ukristo unakubali ndoa ya mke zaidi ya mmoja. Fikra hii sio kwamba ni ngeni kwa wasiokuwa Waislamu kama inavyodaiwa.

Mwisho, uvaaji wa hijabu kwa wanawake ni jambo lisilo na mantiki kudai kwamba wanawake wapo chini kuliko wanaume. Ni bora kuikemea jamii inayokubali picha za uchi pornography kuliko kuikemea jamii inayokubali hijabu. Ikiangaliwa kwamba Allaah sio mwanamume wala mwanamke, na ikiangaliwa kwamba Hawatukuzi watu Kwake kwa kigezo cha jinsia zao, ikiangaliwa kwamba Muumba Anatujali sote wanaume kwa wanawake, ikiangaliwa kwamba shahawa za kimwili na shinikizo la mahitaji ya wanaume yapo juu kuliko yale ya wanawake….yakiangaliwa yote haya, basi hakuna maana yoyote kuvurumisha maelezo mabaya kwenye kanuni inayofuata iliyomo ndani ya Qur-aan (iliyotafsiriwa):
 [24:30-31]

 [33:59]

Kwenye suala hili linaloeleweka vibaya, kuna maelezo marefu ya kuendelea kuandika, mengi yao yakuonesha namna matendo ya sasa ya ardhi zilizo nyingi za Waislamu yanavyokwenda kinyume na amri za Qur-aan na Sunnah, ardhi ambazo wanawake wanafanywa kama vile ni bidhaa (huu sio Uislamu), hawana elimu (huu sio Uislamu), wanazuiwa haki zao za uchumi (huu sio Uislamu), na mengineyo. Hakika katika nukta hii, tunamuhimiza kila mmoja kushauriana na Qur-aan na Sunnah kabla ya kuukosoa Uislamu. Daima kumbuka kwamba Uislamu ni njia kamili ya maisha inayotoka kwa Muumba, na kwamba Waislamu ni watu wanaodai kuifuata njia hiyo ya maisha. Muislamu anaweza kudai kufuata Uislamu, lakini akawa ana makosa.

Itaendelea in shaa Allaah...


Jumanne, 26 Novemba 2019

Kukafini Maiti

Yampasa kumkafini maiti na vile vile yapasa gharama za sanda zitokane na mali ya maiti mwenyewe kama alivyosema Mtume صلى الله عليه وآله وسلم wakati alipofariki mtu akiwa katika hali ya kuhirimia, “Mkafinini kwa nguo yake” [Al-Bukhaariy na Muslim] yaani vazi lake la ihraam na huko kumkafini (kumpamba) maiti kunatangulizwa kabla ya deni lake kulipwa kama analo na hata kabla ya kuutekeleza wasiya wake wa Mirathi.

·         Sanda huwa ni shuka tatu (3) tu, na si zaidi, kutokana na Hadiyth iliyosimuliwa na Mama wa Waumini ‘Aaishah رضي الله عنها: “Alikafiniwa Mtume صلى الله عليه وآله وسلم katika nguo tatu nyeupe, hakuna kanzu wala kilemba katika sanda hizo.” [Imaam Ahmad na Abu Daawuud]. Hili la sanda vipande vitatu ni kwa wanaume na kwa wanawake kwani Hadiyth hapo juu inaweka kanuni ya jumla na hakuna kauli iliyokuja kutofautisha baina yao. Ama Hadiyth inayoeleza kuwa mwanamke anakafiniwa kwa vipande tano, hiyo ni Dhaifu.

·         Ni wajibu kumvika sanda nzuri maiti, au thamani ya sanda itokane na mali ya maiti, ndugu zake, jamaa zake, na isiwe sanda ya thamani kubwa, na avikwe maiti sanda hiyo kwa utaratibu alofundisha Mtume صلى الله عليه وآله وسلم bila kuzidisha chochote, na amesema Mtume صلى الله عليه وآله وسلم “Mmoja wenu anapomvika sanda ndugu yake, basi amvike sanda iliyo nzuri akiweza.” [Muslim, Abu Daawuud, na Ahmad]. Na makusudio ya sanda nzuri ni ile sanda ilio safi na yenye kutosha kumsitiri maiti mwili wake wote, na sio kufanya israfu katika sanda kwa kununua sanda ya thamani kubwa kama alivyofafanua Imaam ‘Abdullaah bin Mubaarak.

·         Endapo maiti huyo hakuwa na uwezo wa kuwa na sanda basi jamaa zake wenye kuhusiana naye watakuwa na wajibu wa kuandaa sanda kwa ajili yake. Nao ni watu wake kama baba yake, babu, mwanae wa kiume au mtoto wa mwanae (mjukuu). Na endapo wote hao watashindwa au atakuwa hana jamaa, basi litakuwa jukumu la ‘Baytul Maal’, yaani litatolewa fungu kutoka katika hazina ya Waislam kama ipo, na kama haipo basi litakuwa jukumu la Muislam yeyote aifahamuye hali ya huyo maiti.

·         Kinachopasa kumkafini maiti ni nguo itakayomsitiri mwili mzima.

·         Sanda inapendeza iwe nyeupe kwa Hadiyth isemayo: “Vaeni nguo nyeupe kwani ni vazi bora katika mavazi yenu, na mkafiniane kwazo” [Abu Daawuud, At-Tirmidhiy, na Ibn Maajah kaisahihisha].

·         Vipande hivyo vya sanda hutiwa harufu nzuri ya aina ya ubani uliosagwa, kisha hukunjwa moja juu ya nyingine na pia hutiwa kwenye sanda hiyo ‘Hanuut’ aina ya unga wenye harufu nzuri ambayo ni maalum kwa maiti na kisha baada ya hapo maiti hulazwa juu ya hiyo sanda iliyotiwa vitu hivyo, na hulazwa chale.  

·         Ukubwa wa shuka hizo za sanda unatakiwa uzidi kimo cha maiti kutegemea na urefu na upana wa maiti. Kuongezwe futi mbili kuzidi kile kimo cha maiti, kwa mfano kama maiti ana urefu wa futi sita, basi urefu wa shuka uwe futi nane na upana uwe futi sita ili stara iwe nzuri zaidi.

·         Baada ya kutandikwa sanda, maiti atalazwa juu yake akiwa amefunikwa sehemu zake za siri; juu ya kitovu hadi chini ya magoti yake. Itachukuliwa ncha ya upande wa kulia na iletwe hadi kifuani mwake, na ncha ya kushoto itafanywa hivyo hivyo, akishafunikwa na sanda hizo wakati huo huo itachomolewa ile shuka au taulo aliyokuwa amesitiriwa nayo sehemu zake za siri. Utaratibu huo utafuatwa kwa shuka ya pili na ya tatu. Kisha sanda hiyo husokotwa mwisho wake na kuanza kufungwa ili isije ikaachia sehemu yeyote na kulegea; husokotwa ncha ya hivyo vipande vya sanda upande wa kichwani na miguuni na kufungwa kwa kamba zilizotayarishwa. Na hufungwa nchani na katikati ya mwili hizo kamba kuweka himaya tu sanda zisiachie na kufunuka maiti, bila kukazwa kamba hizo. Na anawezwa maiti kufungwa mafundo matatu hadi saba kulingana na uimara na mahitajio.

·         Mpaka hapa, maiti itakuwa tayari kwa ajili ya kutekelezewa jambo la tatu ambalo ni kuswaliwa. 

·         Maiti ikishafikishwa kaburini na kuingizwa kwenye mwanandani, zinaweza kamba hizo kufunguliwa au kuachwa hakuna neno.

·         Kukikosekana vitambaa kama ilivyotajwa juu, huruhusiwa kumkafini maiti kwa vazi la kawaida kama shuka ya chini (kikoi) na nguo ya juu kama kanzu au shati ila ni bora zaidi kutumia mfumo uliotajwa mbeleni.

·         Na kukikosekana kabisa sanda atakafiniwa kwa vazi lake alilonalo au vazi lolote la kuweza kumsitiri, na ikiwa kakosa cha kumsitiri mfano yuko jangwani au porini, basi atasitiriwa na kitakachopatikana kama majani, matawi au chochote cha stara.

·         Mwanamke anakafiniwa kwa nguo au vitambaa vitatu kama tulivyotangulia kutaja huko nyuma, na hakuna dalili inayothibitisha kuwa anakafiniwa kwa vipande vitano kama baadhi ya mapokezi dhaifu yanavyoonyesha. Kuna wanaosema kuwa mwanamke anakafiniwa kwa vipande vitano. Nao wanategemea Hadiyth ya Layla bint Qaaif Ath-Thaqafiy inayoeleza kuwa sanda ya kike ni nguo tano zikiwa shuka ‘Izaar’ mbili, kikoi, kanzu ‘Qamiys’, na kilemba‘Khimaar’. Hadiyth hii upokezi (isnadi) yake ni dhaifu. Ndani ya msururu wa wapokezi (isnadi) kuna mtu mmoja, anaitwa Nuuh bin Haakim Ath-Thaqafiy, ambaye hajulikani zaidi ya jina lake tu, kama alivyoelezea al-Haafidh bin Hajar na wengineo. Hivyo itabaki kuwa mwanamke hukafiniwa kama mwanaume kwa vipande vitatu maadam hakuna dalili sahihi ya kutofautisha mwanaume na mwanamke katika kafan.



YASIYOFAA

  • Kutumia zaidi ya sanda tatu.

  • Kutumia sanda za ghali.

  • Kuandika jina la maiti kwenye kikaratasi au maneno mbalimbali kisha kukitia ndani ya sanda azikwe nayo.

  • Kutumia kipande cha sanda cha ziada kuzungushia sehemu za siri za maiti.

  • Kuandika baadhi ya du’aa au Aayah za Qur-aan juu ya sanda.


20-Hakika Shirki Ni Dhulma Kubwa Mno! - Isti’aadhah Kwa Asiyekuwa Allaah

  إِنَّ الشِّرْكَ لَظُلْمٌ عَظِيم   Hakika Shirki Ni Dhulma Kubwa Mno!   20 - Isti’aadhah  (Kuomba Kinga) Kwa Asiyekuwa Allaah   ...