Translate

Jumapili, 7 Julai 2019

Umuhimu wa Kuchunga Wakati Kwa Muislamu

                          Umuhimu wa Kuchunga Wakati Kwa Muislamu



Makala hii muhimu itagusia sana umuhimu wa Muislamu kuchunga muda wake na kutokuuangamiza kwa kufanya mambo ya kipuuzi ambayo hayatomsaidia si duniani wala Akhera. Waislamu wengi tunashinda siku kutwa na kujishughulisha na mambo ya kipuuzi ambayo mengi katika hayo hayamridhishi Allaah.

Kwanza kabla ya kuendelea tungelipenda kurudi nyuma kidogo tukumbushane lengo la sisi kuwa hapa duniani ni lipi, kwa nini Allaah ametuumba. Allaah anasema katika Qur-aan:
وَمَا خَلَقْتُ الْجِنَّ وَالْإِنسَ إِلَّا لِيَعْبُدُونِ
”Nami sikuwaumba majini na watu ila waniabudu Mimi”

Hapa tumeona kuwa lengo kubwa la Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) kutuumba ni sisi kumuabudu Yeye, na kama tunavyosimuliwa na Wanachuoni wetu maana ya ”Ibaadah” kijumla ni kila Anachokipenda Allaah na kukiridhia basi hiyo ni Ibaadah bila shaka.

Moja kwa moja tukirudi katika mada yetu ya kuhusu umuhimu wa kuchunga wakati, tutaona kwamba wengi wetu tumeghafilika na kupuuzia risala hii ambayo ndio lengo kuu la Allaah kutuumba. Na tumesahau kwamba kila Muislam hatopiga hatua moja mpaka mbili siku ya Qiyaamah mpaka ajibu maswali manne, na moja kati ya hayo ni ”Muda wako uliutumia katika mambo gani.”

Ndugu Muislamu tuzingatie kuwa kila mmoja wetu ataulizwa kwa kila dakika yake moja aliitumia katika mambo ya kheri au ya shari. Utamkuta Muislamu amekaa tu na kulalamika kwamba anahisi uvivu kisa hana la kufanya. Inashangaza sana kwa Muislamu kulalamika kwamba anahisi uvivu kana kwamba hana Qur-aan aweze kusoma Aayah kadhaa katika Mus-haf ambapo endapo atasoma Aayah moja tu katika Qur-aan basi atapata ujira kumi kwa kila herufi moja.

Muislamu kana kwamba hana vitabu vya Dini ambavyo anaweza kusoma na kujikurubisha zaidi kwa Mola wake. Mambo muhimu sana kwa Muislamu ni mengi endapo tutayataja basi hatuwezi kuyamaliza yote, ndo maana haifai hata kid ogo Muislamu kusema kwamba anahisi uvivu au hana cha kufanya.

Waislamu wengi sana takriban asilimia hamsini tunapoteza muda wetu katika mambo ya kipuuzi na kilichochangia zaidi ni mitandao hii ya kisasa ya kiteknolojia ambayo imetengenezwa na Mayahudi kwa lengo kubwa la kumshuhulisha Mwanaadamu kutokufanya mambo yake yenye faida na yeye hapa duniani na huko Akhera. Inasikitisha sana kuona Waislamu wengi tunaangamiza muda wetu mwingi katika kuangalia filamu za kipuuzi, wengine tunapoteza muda wetu mwingi kwenye kompyuta na kufanya mambo ya kipuuzi, wengine tunapoteza muda katika kuangalia video za muziki na kusikiliza nyimbo za taarabu na michezo ya kuigiza ambazo zinapoteza muda na zisizo na maadili wala faida, na wengine tunapoteza muda wetu katika mambo fofauti ambayo hayaafikiani hata kidogo na Dini yetu wala hayachangii hata kidogo katika kuueneza Uislamu duniani.

Ndugu yangu Muislamu, tujue kwamba kuchunga muda ni katika mambo muhimu sana katika Uislamu, na ndio maana Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) kaapa mahali pengi sana kwa muda katika Qur-aan kutuonyesha umuhimu wa muda. Na Allaah Anapotueleza jambo fulani katika Qur-aan basi linakuwa na umuhimu na faida kubwa sana kwa Mwanaadamu. Tukiangalia Kitabu kitukufu cha Allaah chatueleza nini kuhusu wakati, basi tutaona kwamba Allaah Kaapia kuhusu muda kuanzia asubuhi mpaka pale usiku unapoingia, na lengo ni kutuonyesha umuhimu na na utukufu wa muda kwa Muislam.

Tuangalie Allaah Anatuambia nini kuhusu muda:  
Allaah Ameapia muda wa asubuhi kwa kusema:
وَالْفَجْرِ
1.     Naapa kwa alfajiri

Baada ya hapo Ameapa muda wa mchana kwa kusema:
وَالضُّحَى
2.     Naapa kwa nyakati za mchana

Baada ya hapo Ameapa kwa mchana unapofunuka wazi.
وَالنَّهَارِ إِذَا جَلَّاهَا
3.     Na kwa mchana unapolidhihirisha!
 وَاللَّيْلِ إِذَا يَغْشَى
4.     Naapa kwa usiku unapofunika!

Viapo vyote hivi haina maana Allaah Amependa tu Kuapa bila sababu au maana, Amependa kutuonesha umuhimu na utukufu wa wakati. Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) hajaapa kwa kitu chochote mara nyingi sana kuliko wakati. Allaah Kaapa mara nyingi sana na zile tulizotaja ni baadhi ya viapo tu katika Qur-aan, ila viapo ni vingi sana Kaapia juu ya wakati. Ameapa kwa kila wakati kuanzia asubuhi mpaka usiku wakati wenyewe Amekuumbia umfanyie Ibada na si vinginevyo au kuangamiza bure tu.

Tukumbuke kwamba kila dakika moja inapotoweka basi hairudi nyuma na wakati wako wa maisha unazidi kupunguka. Kwahio inafaa tuzingatie sana na kutumia mda wetu katika mambo mema na mazuri tu ambayo yatatukurubisha zaidi kwa Mola wetu.

Tusipoteze mda wetu kwa mambo ya kipuuzi ilihali tuko na mambo mengi ambayo yanaweza kutushughulisha yenye faida na sisi hapa Duniani na huko Akhera. Panga muda wako vizuri kwa siku usikose kusoma Qur-aan, usikose kuongea na watoto wako na mama watoto, usikose kujifunza moja au mawili ambayo yatakusogeza zaidi kwa Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala).

Tupunguze kazi zetu na shuhuli zetu fulani na tupangilie muda fulani kudumisha malezi na tarbiyah ya Kiislamu katika majumba yetu ili tuweze kuisogeza mbele jamii yetu ya Kiislam.

Kumbuka kwamba Malaika wa kutoa roho (Malakul Mawt) atapokuja na kuchukua roho yako, utatamani akupe angalau dakika chache ili uweze kuswali rakaa mbili, muda wako utakuwa umekwisha na hutopewa hata dakika moja. Kwa hiyo chunga sana Muislamu na acha kuangamiza na kuponda muda wako, ikiwa ni ujana wako na nguvu zako ndizo unazojivunia, wangapi wameiaga dunia hii huku wakiwa  na nguvu na uwezo wa kukushinda.

Tunamuomba Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) Atujalie tuwe miongoni mwa wale wenye kusikia machache na kuyazingatia. Na Atujalie katika umri wetu wote uliobakia tuweze kutumia muda wetu kwa yale Anayoyapenda na Kuyaridhia.



Hakuna maoni:

Chapisha Maoni

20-Hakika Shirki Ni Dhulma Kubwa Mno! - Isti’aadhah Kwa Asiyekuwa Allaah

  إِنَّ الشِّرْكَ لَظُلْمٌ عَظِيم   Hakika Shirki Ni Dhulma Kubwa Mno!   20 - Isti’aadhah  (Kuomba Kinga) Kwa Asiyekuwa Allaah   ...