Hivi karibuni, serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imeanza kutoza ushuru wa asilimia 10 kwa nywele bandia au kwa jina maarufu mawigi, zinazotengenezwa hapa nchini na asilimia 25 kwa mawigi yanayoingizwa kutoka nje ya nchi.
Hatua hiyo ya serikali imeibua mjadala mkubwa huko mitaani na katika mitandao ya kijamii, huku baadhi ya wananchi wakipendekeza kupigwa marufuku kwa nywele hizo kama ilivyokuwa kwa mifuko ya sandarusi (plastiki).
Hili ni wazo zuri na lenye faida kwa wananchi hasa ikizingatiwa kuwa kusuka/ kuunganisha nywele kuna madhara makubwa kiafya. Kwa mujibu wa wataalamu wa afya, kubandika au kusuka nywele bandia kwa kutumia gundi ni chanzo kimojawapo cha saratani ya ngozi na ile ya damu.
Mbali na saratani, madhara mengine ya kuunganisha/ kubandika nywele bandia ni mhusika kupata michubuko wakati wa ubanduaji wa nywele hizo, kunyonyoka nywele na kuumwa kichwa mara kwa mara.
Hata hivyo, madhara haya yanaweza kuepukika endapo watu watafuata mafundisho ya Uislamu na ushauri wa wataalamu wa afya. Ukiachilia mbali jukumu la viongozi wa dini na wataalamu wa afya, wajibu wa kwanza ni wanawake wenyewe kuchukua tahadhari kwa kuepuka kunganisha nywele.
Uislamu unakataza kuunga nywele
Na hili la ubaya wa kuunganishwa nywele limeshazungumzwa na Mwenyezi Mungu katika Qur’an [4: 117–119)] kuwa: “…wala hawamuombi ila shetani aliyeasi. Allah amemlaani. Naye Shetani alisema, ‘Kwa yakini nitawachukua sehemu maalumu katika waja wako. Na hakika nitawapoteza na nitawatia matamanio, na nitawaamrisha, basi watakata masikio ya wanyama, na nitawaamrisha, basi watabadili maumbile ya Allah.’ Na mwenye kumfanya Shetani kuwa ni mlinzi wake badala ya Allah, basi huyo amepata hasara ya dhahiri.” [Qur’ an, 4: 117–119].
Na katika Hadithi sahihi, Mtume (rehema za Allah na amani zimshukie) amesema: “Mwenyezi Mungu amemlaani mwenye kuunganisha nywele zake (au nywele za mwingine kwa nywele nyingine) na mwenye kuungwa (au kuvaa nywele hizo).” [Bukhari na Muslim].
Aidha, Mtume ameonya kwa kusema: “Hakika waliangamizwa wana wa Israil pale wake zao walipoichukua tabia hii (ya kuunganisha nywele).” [Bukhari, Muslim, Abu Daud, Tirmidhiy na Nasaiy].
Wakati tukielekea kuhitimisha, tunatoa wito kwa serikali kuangalia upya uamuzi wake wa kuruhusu uuzwaji na usambazaji wa nywele za bandia.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni