Translate

Jumapili, 7 Julai 2019

'Amali Inayotaqabaliwa

Kabla ya kuchukua hata hatua moja, Ewe kaka yangu na dada yangu uliye Muislamu, ni muhimu kwako kuijua njia ambayo maokozi yako yatapokuwa. Usijichokeshe kwa kutekeleza mambo mengi (ambayo ndani yake hamna Ikhlaas). 


Kwani inaweza kuwa ya kwamba mtu atatenda matendo mengi, lakini hafaidiki na chochote isipokuwa kupata machofu kutokana na matendo hayo hapa duniani na kupata adhabu katika Akhera. 


Haya yanatolewa mfano  katika kauli ya Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam):“Inawezekana mtu anayefunga asipate chochote katika funga yake isipokuwa njaa na yule anayesimama usiku kuswali asipate chochote isipokuwa machofu” Imesimuliwa na Ibn Maajah kutoka kwa Abu Hurayrah na Shaykh Al-Albaaniy kasema kwamba ni sahihi katika Swahiyh al-Jaami’, no.3482. [Na tunajikinga na Allaah kutokana na kuwa miongoni mwa watu kama hawa]. 

Allaah Aliyetukuka Anasema:

Na Tutayaendea yale waliyoyatenda katika ‘amali Tuzifanye mavumbi yaliyotawanywa. (Suratul al- Furqaan 25: 23)
Akasema pia:
“Ambaye ameumba mauti na uhai ili kukujaribuni (kukufanyieni mtihani); ni nani miongoni mwenu mwenye kufanya vitendo vizuri zaidi…” (Suratul Mulk 67: 2)

Kwa hiyo, fahamu kabla ya kitu chochote kile chengine masharti ya lazima ya ‘amali kabla ya kukubaliwa kwao. Ni muhimu sana ya kwamba mambo mawili makubwa yatekelezwe kwa ajili ya kila tendo.

La kwanza: Ya kwamba yule ambaye aliyetenda amali njema asitamani kupata chochote isipokuwa Wajhi wa Allaah ‘Azza wa Jalla kwa ‘amali ile.
Ya Pili: Ya kwamba ‘amali hiyo iwe inakubaliana na yale ambayo Allaah Aliyetukuka Ameyaruhusu katika Kitabu Chake au Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amefafanua katika Sunnah.

Fudhayl bin Ayyaad, ambaye ni Taabi’iy, alisema kuhusu Aayah hii:“... ili kukujaribuni (kukufanyieni mtihani); ni nani miongoni mwenu mwenye kufanya vitendo vizuri zaidi...} [Suratul Mulk, 11: 7)“Ambayo yana Ikhlaas na yako sahihi”. Wale ambao walio mzunguka wakasema “Na yapi hayo ambayo yana Ikhlaas na yako sahihi?” Akajibu “Amali, ikiwa iko sahihi lakini haina Ikhlaas ndani yake, basi haitakubaliwa, na kama ina Ikhlaas lakini si sahihi hatakubaliwa mpaka iwe na vyote, iwe sahihi na ina Ikhlaas.  Ikhlaas inamaanisha ya kwamba hamna kitu chochote ambacho kinatafutwa isipokuwa Wajhi wa Allaah na sahihi inamaanisha ya kwamba kinaendana na Sunnah”.

Na Masalaf (watu wema waliopita) walikuwa wakisema: Hamna kitendo, japokuwa kama ni kidogo vipi, isipokuwa kitawekewa maswali mawili: Kwanini umekifanya? Na: Vipi umekifanya?

Swali la kwanza ni kuhusu sababu ya kutenda kitendo hicho na Niyah yake. Ikiwa Niyah ilikuwa kwa ajili ya madhumuni miongoni mwa madhumuni ya kidunia kama vile kutafuta kusifiwa au cheo au malengo yoyote yale ya kidunia, (kitendo) hicho kitakuwa ni kitendo kiovu na kitarembewa kwa yule aliyekifanya. Ikiwa Niyah ya kufanya hicho kitendo ni kutekeleza Haki ya Allaah ya kujiweka katika hali halisi ya utumwa Kwake na kutafuta njia ya kumkaribia, basi kitakuwa ni kitendo chema na kitakubaliwa, Allaah Akipenda.

Swali la pili ni kuhusu kumfuata na kumuigiza Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam). Je hicho kitendo kilikuwa ni miongoni mwa vitendo vilivyoruhusiwa katika Shari’ah au kilikuwa kutokana na bid’aa zinazotoka kwako wewe?  Ikiwa kinatokana na muongozo wa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), basi kitakuwa ni kitendo chema na ikiwa kilikuwa ni kinyume na matendo ya Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), basi kitakuwa ni kitendo kiovu na hakitakubaliwa kutoka kwa yule aliyekitenda kama ilivyothibitishwa katika Hadiyth ya ‘Aaishah ( Radhiya Allaahu ‘anha) ambaye alisema: Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alisema:“Yeyote atakayeleta katika jambo (Diyn) letu hili kitu ambacho hakimo basi hakitakubaliwa.” (Al-Bukhaariy na Muslim)
Na pia anasimulia ya kwamba Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alisema: “Yeyote atakayetenda kitendo ambacho hatukikuamrisha basi hakitakubaliwa.”(Muslim)

Ikiwa kama moja kati ya masharti mawili (yaliyokwishatajwa) juu haijakamilishwa, kitendo kinakuwa si chema wala chenye kukubalika. Haya yanathibitishwa katika kauli ya Tabaaraka wa Ta’aala:
“Na yeyote ambaye anatarajia kukutana na Mola wake na atende vitendo vyema na asimrikishe yeyote katika ibada ya Mola wake” (Suratul Kahf 18: 110) 
Allaah Mtukufu katika Aayaah hii Anaonyesha ulazima wa kitendo kuwa chema, kwa maana, kiwe kinakubaliana na Shari’ah. Kisha Akaamrisha ya kwamba mtu akitende kwa Ikhaas kwa ajili ya Allaah, bila ya kutaraji kitu chengine isipokuwa Yeye tu.

Al-Haafidh Ibn Kathiyr (Allaah Amrehemu) kasema:
“Hizi ni nguzo mbili za ‘amali zinazokubaliwa. Inahitajika ya kwamba kitendo kiwe na Ikhlaas na pia kiwe sahihi katika Shari'ah ya Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam). Mfano wa haya yamekwisha simuliwa kutoka kwa al-Qaadhi Iyyaad (Allaah Amrehemu) na wengine.

Allaah Ta’aala pia Anasema:
“Na nani ni mbora kwa Diyn kuliko yule ambaye anaunyeyekesha uso wake kwa Allaah na ni mtendaji wa vitendo mema…” (Suratun Nisaa 4: 125)

Maana ya mtu kuunyenyekesha uso wake kwa Allaah ni: Mtu kuweka Niyah na kutenda vitendo vyake kwa ajili ya Allaah. Na maana ya kutenda vitendo vyema ni: Kuiigiza na kuifuata Sunnah ya Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam).

*
Ikhlaas- Kufanya kitendo kwa dhati kwa ajili ya Allaah (Subhaanahu wa Ta’aala).


Hakuna maoni:

Chapisha Maoni

20-Hakika Shirki Ni Dhulma Kubwa Mno! - Isti’aadhah Kwa Asiyekuwa Allaah

  إِنَّ الشِّرْكَ لَظُلْمٌ عَظِيم   Hakika Shirki Ni Dhulma Kubwa Mno!   20 - Isti’aadhah  (Kuomba Kinga) Kwa Asiyekuwa Allaah   ...