Mwenyezi Mungu Aliyetukuka ndiye aliyeumba ulimwengu wote na viumbe vyote bila usaidizi wa mtu yoyote na yeye ndiye anayeuendesha ulimwengu huu. Kwa hivyo, ni Yeye ndiye anayestahiki kuadudiwa kwa sababu hakuna yoyote aliyemsaidia katika uumbaji.
Ndugu katika imani! Jueni ya kwamba viumbe vyote ambavyo vinapatikana ulimwenguni havijileti vyenyewe bali Mwenyezi Mungu Aliyetukuka ndiye aliyeviumba viumbe hivyo. Kuna viumbe wengi mno ulimwenguni. Wapo tunaowafahamu na tusiowafahamu. Si jambo la ajabu kusikia kila uchwao wavumbuzi wanaleta taarifa ya uwepo wa viumbe wapya. Viumbe hawa walikuwepo, laini pengine macho yetu ndiyo bado hayakudiriki kuwaona.
Baada ya utangulizi huo, leo tumtazame mdudu kupe, namna Mbora wa Waumbaji, Mola aliyetakasika na sifa zote, alivyomuumba kipekee alivyoumbwa kipekee. Hivyo, kila unavyojifunza kuhusu kupe na kuona hatari aliyokuwa nayo, kumbuka pia ukubwa wa huyo aliyemuumba kwani nirudie kusisitiza, kupe/papasi hajajileta mwenyewe duniani.
Kupe ni wadudu wadogo wanaoishi kwa kula damu ya ndege, wanyama, nyoka, mamba na hata binadamu. Wadudu hawa wamejaaliwa kuwa na miguu nane, upande wa kulia minne na kushoto minne. Wataalamu wa elimu ya wadudu wanasema kwamba, kupe/papasi wapo wa aina nyingi sana. Miongoni mwao ni wale wenye ngozi ngumu na wenye ngozi laini.
Wadudu hawa Kingereza wanaitwa ‘ticks’ ila Waswahili wamewagawanya katika makundi mawili. Wapo wale wanaodanda katika mwili wa binadamu wakiitwa ‘papasi’ na wengine ni wale wanaodanda kwa wanyama tunawaita ‘kupe.’ Wote hao kwa kiingereza ni ‘ticks.’ Kupe hupenda sana kuwadanda wanyama, hasa ng’ombe, sehemu zile laini kama katika matiti au masikioni.
Makazi na uzazi
Wadudu hawa wasumbufu kwa wanyama na binadamu, hupatikana maeneo mengi duniani na kwa kawaida wanapenda sana kukaa kwenye manyasi, vichaka, na hata kwenye matobo ya nyumba za udongo.
Kupe ni miongoni mwa wadudu ambao wanataga kama ilivyo tu kwa wadudu wengine. Katika uzazi, kupe, kama ilivyo kwa wadudu wengine, hupitia hatua kadhaa katika utaratibu au mfumo ulioratibiwa
na Mwenyewe Allah Muumba Mbingu na Ardhi na vilivyomo baina ya viwili hivyo.
Kupe jike linataga yai ambalo baaadae linabadilika na kuwa kiwavi au lava. Kisha, kiwavi kinabadilika na kuwa nyimphi ambaye naye hatimaye anabadilika na kuwa kupe mdogo na kisha kuwa kupe kamili. Hizi ndiyo hatua za ukuaji wa kupe/ papasi.
Mambo usiyoyajua kuhusu kupe.
- Kupe hawezi kuruka wala kupaa.
- Kupe au papasi huwa hakai muda mrefu katika mwili wa binadamu. Kupe huwa anamuuma binadamu na kuondoka, lakini kwa wanyama huweza kukaa kwa masiku kadhaa.
- Kupe au papasi anaponyonya damu na kushiba huwa anavimba na kuwa mkubwa zaidi ya umbo lake la kawaida kitu ambacho huwezi kukiona kwa wadudu wengine walao damu.
- Kupe au papasi ni wadudu hatari kwa sababu wanasambaza maradhi ya aina nyingi ikiwemo homa ya vipindi, kwa kiingereza huitwa, ‘Tick born replasing fever.’ Lakini kupe pia husambaza virusi, bakteria na vimelea vyingine kwa binadamu na wanyama.
- Ugonjwa unaosambazwa na kupe hupita hadi kwenye vizazi vyao tofauti na chawa na kiroboto. Mfano ikitokea kupe amenyonya damu ya mnyama mwenye ugonjwa anabeba ugonj w a huo hadi kweny e vizazi vyake (yai, kiwavi, nyimphi). Hivyo, kupe akimnyonya mnyama au binadamu humuambukiza ni tofauti kabisa kwa chawa na kiroboto ambao wao vimelea huwa huishia kwao wenyewe tu.
- Kupe anaweza kukaa muda mrefu bila kula. Wataalamu wa elimu ya wadudu wanasema, anaweza kukaa hadi miaka mitatu bila kula. Kipindi chote hicho anaweza kusubiri mtu au mnyama amnyonye, wakati kwa mdudu kama chawa akikaa nje ya mwili wa binadamu masaa 24 hufa.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni