Translate

Ijumaa, 5 Julai 2019

Marufuku ya Niqab itazuia Ugaidi?

“Niqaab, Silaha Stop Sabasaba”, liliandika gazeti moja litokalo kila siku nchini Tanzania. Maana yake ni kwamba, tukiweza kuzuia uvaaji wa Niqaab na watu wasiporuhusiwa kuingia na silaha Viwanja vya Maonesho ya Sabasaba, vilivyopo Barabara ya Kilwa; hapo tunakuwa tumefanikiwa kuzuia ugaidi.

Kwanza niipongeze serikali kwa kujali usalama wa raia na mali zao na kuhakikisha kuwa shughuli za kiuchumi, kijamii na maisha ya kawaida ya Watanzania yanaendelea pasina matukio ya kuhatarisha amani.

Vazi la Niqaab halihusishwi sio tu kwenye maonesho ya biashara ya Sabasaba bali pia katika viwanja vya ndege, bandarini, benki, hospitali na katika ofisi zote za umma. Kama nilivyotaja, marufuku hii imelenga kuimarisha usalama wa raia na mali zao dhidi ya vitendo vya kigaidi.

Ni kweli watu waovu wanapotaka kufanya uovu wao hufunika nyuso zao kwa soksi au chohote kile katika kile kiitwacho maarufu kama ‘Ninja’. Lakini vazi la Niqaab ni vazi linalovaliwa na wanawake wa Kiislamu ambalo asili yake haikukusudiwa kutumika katika vitendo viovu au vya kihalifu kama vile ujambazi na ugaidi.

Ni kuzuka kwa matukio ya kigaidi duniani na kutumika kwa wanawake waliovaa Niqaab katika matukio hayo ndiko kulikolifikisha vazi la Niqaab katika hali ya sasa kuwa ni kihatarishi cha amani. Makundi ya kigaidi kama vile Boko Haram, Daesh au Islamic State, Al-Shabaab na mengineyo yamekuwa yakiwashawishi wanawake kutekeleza matukio ya kigaidi kwa kuamini kwamba wakiwa wamevaa Niqaab, hawawezi kugunduliwa kiurahisi na maafisa wa usalama.

Mwaka 2014, Mwalimu mmoja mwanamke Mmarekani alidungwa kisu na mwanamke aliyekuwa amevalia Niqaab katika katika chumba cha kupumzikia kwenye moja ya maduka (Mall) mjini Dubai.

Nchini Malaysia nako serikali ilipiga marufuku uvaaji wa Niqaab katika vyuo vikuu kufuatia matukio ya kigaidi nchini humo mwaka 2013. Mwaka huu Sri Lanka pia ilipiga marufuku uvaaji wa Niqaab kwa sababu za kiusalama. Kwa hiyo imekuwa ni jambo la kawaida kwa uvaaji Niqaab kupigwa marufuku kwa sababu hizo za kiusalama.

Waislamu wagawanyika

Kufuatia marufuku hii, Waislamu wanawazuoni kwa wasio wanawazuoni wamegawanyika. Wako wanaopinga moja kwa moja marufuku ya uvaaji Niqaab iwe ni shuleni, vyuoni au maeneo ya umma na wako pia wanaokubali kwa sababu za kiusalama. 

Chimbuko la kugawanyika huku ni kutofautiana kwa wanawazuoni kuhusu hukumu ya uvaaji Niqaab. Aliyekuwa Mufti wa Saudi Arabia, Sheikh Ibn Baaz (Allah amrehemu) alinukuliwa akisema: “Niqaab ni faradhi (lazima) juu ya wanawake isipikuwa katika kipindi cha Hijja na Umrah kwa sababu ni sitara kwao dhidi ya fitna.”

Sheikh akatolea dalili Aya ya Allah isemayo: “Na pindi mtakapowauliza kitu waulizeni kwa kutokea nyuma ya pazia, kufanya hivyo ndiyo utakasifu kwa nyoyo zenu na nyoyo zao.” [Qur’an, 33:53]. Kwa upande mwingine, Sheikh Mkuu wa Al-Azhar, Dkt. Ahmad Twayyib, anasema: “Hakika uvaaji wa Niqaab siyo faradhi wala Sunna lakini ni jambo ambalo siyo Makruuh (linalochukiza) au lililokatazwa.”

Kwa msimamo wa kwanza kwamba Niqaab ni faradhi (lazi
ma), hatua yoyote ile ya kumlazimisha mwanamke Muislamu asivae Niqaab anapokuwa hayuko katika Hijja au Umrah ni kumzuia jambo la kidini hivyo katazo hilo ni katazo batili. Kwa wanaoona uvaaji wa Niqaab si lazima wala Sunna, katazo la kuzuia wanawake wasivae Niqaab halina athari yoyote kwao. Kwa hiyo kwa kugawika kwa Maulamaa juu ya hukmu ya Niqaab kunapelekea Waislamu wa kawaida nao kugawanyika.

Mjadala mkali juu ya kuzuiwa Niqaab

Kufuatia serikali za nchi mbali mbali duniani kuzuia wanawake wasivae Niqaab, kumezuka mjadala mkali kati ya Waislamu kuhusu marufuku ya Niqaab. Wapo wanaosema kwa kuwa, uvaaji wa Niqaab si jambo la lazima kwa wanawake, marufuku ya uvaaji Niqaab kwa sababu za kiusalama ni katazo linalokubalika iwapo litatolewa na serikali.

Sheikh Ahmad Al-Qubaisi, mmoja wa wanawachuoni nchini Dubai anasema: “Niqaab siyo lazima, kwa hiyo ikiwa ni lazima kuipiga marufuku kwa usalama wa nchi na watu wake, serikali inaweza kuamua kuwataka wanawake wasivae Niqaab.”

Al-Qubaisi anasema: “Katika nchi mbali mbali za Kiislamu, wanafunzi wa kike katika vyuo vikuu mbali mbali hutakiwa kuvua Niqaab ili kuwawezesha wasimamizi wajiridhishe kama kweli mwanafunzi anayefanya mtihani ndiye mwanafunzi husika na si mwingine.”

Mwanawachuoni mwingine, Sheikh Khaleeq Ahmad Mufti wa Dubai huko huko yeye akasema ingawa kwa upande mwingine Niqaab inaweza kuzuiliwa kwa mujibu wa hali itakavyohitaji, lakini haipaswi kuigwa marufuku moja kwa moja: “Kwa mujibu wa masomo yangu, wanawazuoni wa Kiislamu hawajakubaliana kuhusu kama Niqaab ni lazima au si lazima. Katika hali fulani, hasa inapikuja kuhusu kulinda uhai wa watu na mali zao na usalama wa nchi, wanawake wanaweza kutakiwa wasivae Niqaab.”

“Kwa mfano, wanawake wanatakiwa kuonesha nyuso zao kwa ajili ya picha za hati za kusafiria (passport) na wanapokuwa katika ukaguzi viwanja vya ndege. Lakini sikubaliani na fikra ya kuipiga marufuku Niqaab moja kwa moja. Njia mbadala zinaweza kutumika”, aliongeza Sheikh.

Hata hivyo, raia wa Uingereza Jamie G mwenye umri wa miaka thelathini na tano alipohojiwa na Aljazeera kuhusu marufuku ya Niqaab alisema marufuku ya Niqaab ni kumvunjia heshima wale wanaovaa Niqaab: “Hatua hii itakuwa kuwavunjia heshima wale wanaoamini juu ya kufunika nyuso zao kwa sababu za kidini na kimaadili hasa katika nchi ambayo uvaaji Niqaab ni jambo lilizoeleka. Kama mtu yuko tayari kumdunga kisu mwanadamu mwingine hadi kufa, kukatazwa kuziba nyuso zao nyuma ya Niqaab hakuwezi kuwazuia kuua.”

Naye kijana Ali Bashar kutoka Palestina, alisema: “Kila mmoja anapaswa kuwa na haki ya kuvaa chochote atakacho. Jambazi yeyote au muuaji anaweza kufunika uso wake kabla ya kutenda uhalifu, lakini wanaweza kupatikana kutiwa hatiani kwa upelelezi kupitia alama za vidole vyao (finger prints). Kwa hiyo kwa nini tubague watu kundi la watu?”

Wakishindwa kuvaa Niqaab, watavaa misalaba!

Mmoja wa Waislamu waliohoji nguvu kubwa kuelekezwa katika upoigaji marufuku uvaaji wa Niqaab ambalo ni vazi alama ya Uislamu kutokea Zanzibar, Fatma Khamis Ubwa alisema kwa staili hii watu waovu wana upenyo rahisi sana.

“Kwa kuelekeza nguvu zote kuzuia uvaaji wa Niqaab, serikali yetu inapaswa kutia maanani kwamba watu waovu wanaweza kuamua kutumia alama nyingine za kidini na kufanikiwa kutenda uhalifu kama vile kuvaa shungi za masista au hata misalaba ambapo hawatoitiliwa mashaka”.

Wakosoaji wa hatua ya marufuku ya Niqaab wanasema hatua hii imelenga kuwanyima haki wanawake Waislamu wanaovaa Niqaab. Hoja yao iko katika ukweli kwamba hatua za kiusalama za zama hizi ni madhubuti kiasi kwamba mtu akikusudia kutenda uhalifu akiwa amevaa Niqaab hawezi kufaulu kufanya uovu wake kabla hajakamatwa.

Vifaa vya kung’amua vitu hatarishi (metal detectors) vikitumika ipasavyo na askari wa kike katika kukagua (body search) hatua hizi zingeweza kuwapa fursa wanawake waliovaa Niqaab kuruhusiwa kuingia mahali popote. Hatua hizi hufuatwa na benki za Kiislamu duniani kote hata hapa nchini pia na wanawake wavaa Niqaab wakapata haki yao.

Pia, kuipiga marufuku Niqaab ni kutoa fursa kwa wanaokusudia uovu kuitumia marufuku ya Niqaab kama kichocheo cha kuwarubuni vijana, kwamba dini yenu inakandamizwa. Hadi hapo suala hili la marufuku ya uvaaji Niqaab ambalo linajenga picha watu wa dini moja wananyanyaswa litakapoangaliwa kwa jicho la tatu, mjadala wa marufuku ya Niqaab utaendelea kutawala anga za kimataifa.

Ndiyo maana tunauliza, je marufuku ya uvaaji Niqaab kweli itazuia ugaidi nchini au ndiyo inaweza kuchochea kwa waovu kuitumia kama sababu (Motivational factor) kuhamissisha ugaidi?



Hakuna maoni:

Chapisha Maoni

20-Hakika Shirki Ni Dhulma Kubwa Mno! - Isti’aadhah Kwa Asiyekuwa Allaah

  إِنَّ الشِّرْكَ لَظُلْمٌ عَظِيم   Hakika Shirki Ni Dhulma Kubwa Mno!   20 - Isti’aadhah  (Kuomba Kinga) Kwa Asiyekuwa Allaah   ...