Translate

Jumapili, 20 Januari 2019

Watu ambao Allaah hatowatizama wala Kuongea nao siku ya Qiyamah - sehemu ya 1

                   Watu ambao Allaah hatowatizama wala Kuongea nao siku ya Qiyamah.



Hadiyth ya Kwanza

Mzee Mzinzi, Mfalme Mwongo, na Masikini Mwenye Kibri


 عن أبي هريرة قالقال رسول الله صلى اللهعليه وسلم: ((ثلاثةٌ لا يكلمهم الله يومالقيامة، ولا يزكيهم، ولا ينظر إليهم، ولهمعذابٌ أليمٌشيخٌ زانٍ، وملكٌ كذابٌ، وعائلٌمستكبرٌ))  رواه مسلم.
Imepokelewa toka kwa Abuu Hurayrah (Radhwiya Allaahu ‘anhu) ambaye amesema: Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: ((Wa tatu, Allaah Hatozungumza nao Siku ya Qiyaamah, wala Hatawatakasa, wala Hatawaangalia, na watapata adhabu iumizayo: Mzee mzinzi, mfalme mwongo, na masikini mwenye kibri)). [Imesimuliwa na Muslim]


Faida na Sharh ya Hadiyth.

Makusudio ya Allaah ('Azza wa Jalla)  kutozungumza nao ni kuwa Hatozungumza nao mazungumzo ya kuwa radhi nao na kuwafurahikia, bali Atazungumza nao mazungumzo ya hasira na kutowafurahikia.

Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa)  Anasifika na sifa hii ya kuzungumza. Huzungumza wakati wowote Atakapo na kwa namna yoyote Aitakayo. Alizungumza na Nabiy Muwsaa ('Alayhis-Salaam)  Akazungumza na Nabiy wetu Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam)  usiku wa Mi’iraaj, na pia Atazungumza na Nabiy ‘Iysaa  ('Alayhis-Salaam)  Siku ya Qiyaamah Amuulize:

   وَإِذْ قَالَ اللَّـهُ يَا عِيسَى ابْنَ مَرْيَمَ أَأَنتَ قُلْتَ لِلنَّاسِ اتَّخِذُونِي وَأُمِّيَ إِلَـٰهَيْنِ مِن دُونِ اللَّـهِ ۖ قَالَ سُبْحَانَكَ مَا يَكُونُ لِي أَنْ أَقُولَ مَا لَيْسَ لِي بِحَقٍّ ۚ إِن كُنتُ قُلْتُهُ فَقَدْ عَلِمْتَهُ ۚ تَعْلَمُ مَا فِي نَفْسِي وَلَا أَعْلَمُ مَا فِي نَفْسِكَ ۚ إِنَّكَ أَنتَ عَلَّامُ الْغُيُوبِ  
((Na pindi Allaah Atakaposema: “Ee ‘Iysaa mwana wa Maryam!  Je, wewe uliwaambia watu: ‘Nifanyeni mimi na mama yangu kuwa ni waabudiwa wawili badala ya Allaah?” (‘Iysaa) Atasema: “Utakasifu ni Wako hainipasi mimi kusema yasiyo kuwa haki kwangu; ikiwa nimesema hayo basi kwa yakini Ungeliyajua; Unayajua yale yote yaliyomo katika nafsi yangu; na wala mimi sijui yale yaliyomo katika Nafsi Yako; hakika Wewe ni Mjuzi wa ghayb)). [Al-Maaidah (5:116)]

Aidha, Atazungumza mazungumzo makali ya hasira na magombesho kwa makafiri na waasi Siku ya Qiyaamah. Atawaambia watu wa motoni kwa mfano:

قَالَ اخْسَئُوا فِيهَا وَلَا تُكَلِّمُونِ ﴿١٠٨﴾
108. Wataambiwa: “Hizikeni humo! Na wala msinisemeshe!”   [Al-Muuminuwn: 108]


Ama kutakaswa,  ni kutwaharishwa. Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa)  Huwatwaharisha  Waja Wake wema hapa duniani kwa kuzizidishia nyoyo zao iymaan, matendo mema na taqwa. Anatuambia:
قَدْ أَفْلَحَ مَن تَزَكَّىٰ ﴿١٤﴾
14. Hakika amefaulu ambaye amejitakasa.


وَذَكَرَ اسْمَ رَبِّهِ فَصَلَّىٰ ﴿١٥﴾
15. Na akadhukuru Jina la Rabb wake na akaswali. [Al-A’laa: 14-15]


Na huko Aakhirah inakuwa kwa kuwasafisha kutokana na uchafu wa makosa wakatakata kabisa na kisha kuwaingiza Peponi, kwani Peponi haingii mtu mchafu.

Ama kuwaangalia, makusudio yake ni kuwaangalia kwa jicho la ridhaa na furaha. Kwani Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Anawaangalia viumbe Vyake vyote bila kukiacha hata kimoja.

Watu hao watakaokumbana na mkasa huu:

Mtu wa kwanza: Mzee, ajuza na kikongwe mzinifu na mzinzi. 

Mzee kama huyu ambaye umri wake umesonga mbele, anachotakiwa ni kujikurubisha zaidi kwa Allaah ('Azza wa Jalla)  badala ya kumwasi kwa kosa hili ambalo Allaah ('Azza wa Jalla)  Amelielezea kama ni uchafu na njia mbaya kabisa. Mzee kama huyu inaonyesha kwamba mizizi ya madhambi imejikita hadi kwenye kina cha mwisho cha moyo wake.


Mtu wa piliNi mfalme mwongo.

Mwana Aadam kawaida husema uongo kutokana na unyonge wake na udhaifu wake na kushindwa kuwakabili wenye nguvu kwa haki na ukweli, na hapo hulazimika kuongopa. Ama mfalme, yeye anamwogopa nani? 

Watu wote ni raia wake, na vyombo vyote vya dola viko chini yake. Na ikiwa anaongopa, basi ni dalili kuwa mfalme huyo ni mchafu kimaadili, fisadi, mwenye uchu, na ubaya wa kila aina umejikita ndani ya nafsi yake.

Hii ni kama mzazi kuwaongopea watoto wake. Ni kwa nini afanye hivyo? 

Anaweza kuwaambia ukweli kwenye kila kitu, nao wakafahamu, wakavaana na hali iliyopo na wakakulia katika mazingira ya usemaji kweli. Na baba anapowaongopea watoto, inakuwa ni dhambi kubwa ambalo wengi hawalihisi. 

Na baba huyu anaweza kuwa sawa na mfalme huyo, na akaingia kwenye makamio haya ya Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa).


Mtu wa tatuNi masikini jeuri mwenye kibr.

Kibr mara nyingi huchochewa na utajiri alionao mtu ambapo watu hujipendekeza kwake na kumwonyesha kuwa wanamheshimu na kumtukuza kwa ajili ya maslaha. Hali hii mara nyingi humfanya mtu kuwa na kibr. Allaah ('Azza wa Jalla)  Anatuambia:
((كَلَّا إِنَّ الْإِنسَانَ لَيَطْغَىٰ))
((Laa hasha! Hakika mwana Aadam bila shaka amepindukia mipaka kuasi ))
((أَن رَّآهُ اسْتَغْنَىٰ ))
((Kwa kuwa amejiona amejitosheleza)) [Al-‘Alaq 96: 6 - 7]


Basi ikiwa mtu masikini na mlalahoi, na akawa na kibr, hii bila shaka inaonyesha kuwa uovu na uhabithi umejikita ndani ya nafsi yake. Mtu huyu bila shaka anaishi maisha ya taabu, dhiki na kubahatisha hapa duniani, na huko Aakhirah atakwenda kukumbana na makamio hayo ya Allaah (‘Azza wa Jalla). Anakuwa amekhasirika hapa duniani na huko aakhirah.

مستكبر anaweza pia kuwa mtu anayependa kujionyesha kwa watu kinyume na uwezo wake. Anaweza hata kuazima nguo, au kununua kitu cha ghali kwa kukopa, au kufanya harusi kubwa kwa madeni, ili tu mradi aonekane na yeye ni katika watu wa hadhi ya juu nailhali hana chochote. Hili wanalo wengi sana katika jamii.

Au hata akina mama wanapoalikwa kwenye harusi na kadhalika, hujitahidi kununua nguo ya ghali isiyopatikana nchini mwake na kuiagizia nje ili tu aonekane yeye tu aliyevaa nguo hiyo pasina mwengine.


Na  Allaah  anajua zaidi

Inaendelea usikose sehemu ya 2 In Shaa Allaah.....................


from fisabilillaah.com http://bit.ly/2RBqdZr
via IFTTT

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni

20-Hakika Shirki Ni Dhulma Kubwa Mno! - Isti’aadhah Kwa Asiyekuwa Allaah

  إِنَّ الشِّرْكَ لَظُلْمٌ عَظِيم   Hakika Shirki Ni Dhulma Kubwa Mno!   20 - Isti’aadhah  (Kuomba Kinga) Kwa Asiyekuwa Allaah   ...