Translate

Alhamisi, 24 Septemba 2020

15-Hakika Shirki Ni Dhulma Kubwa Mno! - Kuapa Kwa Asiyekuwa Allaah

 

إِنَّ الشِّرْكَ لَظُلْمٌ عَظِيمٌ

Hakika Shirki Ni Dhulma Kubwa Mno!

15- Kuapa Kwa Asiyekuwa Allaah

Alhidaaya.com

 

 

 

Haijuzu Muislamu kuapa isipokuwa kwa Jina la Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) kwa sababu kuapia kwa yeyote au chochote ni kumshirikisha Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa). Inavyopasa kuapa ni ima kusema: “Wa-Allaahi”, au “BiLLaahi” au “Ta-Allaahi” kama ilivyothibiti katika Qur-aan. Na Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amekataza kuapia chochote isipokuwa kwa Jina la Allaah akasema:

 

 مَنْ حَلَفَ بِغَيْرِ اللَّهِ فَقَدْ كَفَرَ أَوْ أَشْرَكَ

((Atakayeapa pasi na Allaah, atakuwa amekufuru na amemshirikisha Allaah) [Abu Daawuwd, At-Tirmidhiy, Ibn Hibbaan, Al-Haakim na wengineo na ameipa daraja ya Swahiyh Al-Albaaniy]

 

Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Pekee Ndiye Mwenye haki kuapia Atakacho kwani Yeye ni Muumba wa kila kitu. Ndio maana Anaapia katika Qur-aan vitu vingi; Wa-Tiyni waz-Zaytuni, Wal-‘Aswr, Wadh-Dhwuhaa, Wash-Shamsi, Wal-Layli, Wal-Fajr, Wal-‘Aadiyaat n.k.

 

Hata Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) haikumpasa kuapia chochote, na ndio maana tunaona anapotaka kuapa, mara nyingi husema:

 

وَالَّذِي نَفْسِي بِيَدِهِ

Naapa kwa Yule Ambaye nafsi yangu imo Mikononi Mwake… [Akimkusudia Allaah]

 

 

Na akakataza katika Hadiyth mbali mbali zifuatazo kuapia kwa yeyote au kwa chochote isipokuwa kuapia kwa Allaah pekee:

 

عَنْ عَبْدِ اللَّهِ بْنِ عُمَرَ رَضِي اللَّه عَنْهمَا أَنَّ رَسُولَ اللَّهِ صَلَّى اللَّه عَلَيْهِ وَسَلَّمَ أَدْرَكَ عُمَرَ بْنَ الْخَطَّابِ وَهُوَ يَسِيرُ فِي رَكْبٍ يَحْلِفُ بِأَبِيهِ فَقَالَ : أَلَا إِنَّ اللَّهَ يَنْهَاكُمْ أَنْ تَحْلِفُوا بِآبَائِكُمْ مَنْ كَانَ حَالِفًا فَلْيَحْلِفْ بِاللَّهِ أَوْ لِيَصْمُتْ

Imepokelewa kutoka kwa ‘Abdullaahi bin ‘Umar (Radhwiya Allaahu ‘anhumaa) kwamba Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alikutana na ‘Umar bin Al-Khattwaab akiwa katika msafara wa ngamia akawa ameapia kwa baba yake. Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akasema: ((Tanabahi Allaah Anawakatezeni kuapia kwa baba zenu. Anayetaka kuapa basi aapie kwa Allaah au anyamaze kimya)) [Al-Bukhaariy, Muslim na Ahmad]

 

Pia:

 

عَنْ أَبِي هُرَيْرَةَ - رضي الله عنه: لَا تَحْلِفُوا بِآبَائِكُمْ, وَلَا بِأُمَّهَاتِكُمْ, وَلَا بِالْأَنْدَادِ, وَلَا تَحْلِفُوا إِلَّا بِاللَّهِ, وَلَا تَحْلِفُوا بِاللَّهِ إِلَّا وَأَنْتُمْ صَادِقُونَ

Imepokelewa kutoka kwa Abuu Hurayrah (Radhwiya Allaahu ‘anhu) amesema Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam): ((Msiapie kwa baba zenu wala mama zenu, wala kwa mnaowalinganisha na Allaah. Na wala msiape isipokuwa kwa Allaah, wala msiape kwa Allaah isipokuwa mnapokuwa mnasema ukweli)) [Abuu Daawuwd na An-Nasaaiy]

 

Amekataza pia kuapia kwa uaminifu akasema Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam:

 

 عَنْ عَبْدِ اللَّهِ بْنِ بُرَيْدَةَ عَنْ أَبِيهِ قَالَ: قَالَ رَسُولُ اللَّهِ صلى الله عليه وسلم: (لَيْسَ مِنَّا مَنْ حَلَفَ بِالأَمَانَةِ

Imepokelewa kutoka kwa ‘Abdullaah bin Buraydah kutoka kwa baba yake kwamba Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: ((Si miongoni mwetu anayeapia kwa amana)) [Ahmad (5/325) na ameisahihisha Al-Albaaniy katika As-Silsilah Al-Hadiyth Asw-Swahiyhah (1/325)]

 

 

Na Hadiyth ya Abuu Hurayrah (Radhwiya Allaahu ‘anhu) kwamba Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:

 

مَن حلَف فقال في حَلِفه: باللات والعُزَّى، فليقل: لا إله إلا الله

((Yeyote atakayeapa akasema katika kiapo chake: “Naapa kwa Al-Laata, na Al-’Uzzaa” basi aseme: “Laa ilaaha illa-Allaah”)) [Al-Bukhaariy na Muslim]

 

 

Na Ibn Mas-‘uwd (Radhwiya Allaahu ‘anhu) amesema:

 

لأَنْ أَحْلِفَ بِاللَّهِ كَاذِبًا أَحَبُّ إِلَيَّ مِنْ أَنْ أَحْلِفَ بِغَيْرِهِ صَادِقًا

“Ni bora kwangu kuapa kwa Jina la Allaah wakati naongopa kuliko kuapa kwa asiyekuwa Allaah kwa jambo la kweli.” [Majm’a Az-Zawaaid (4/180), na ameisahihisha Al-Albaaniy katika Swahiyh At-Targhiyb (2953)]

 

 

 

Aina za viapo ni vitatu: 

 

 

1- Al-Yamiyn Al-Ghamuws (Kiapo cha uongo):

 

Ni kula kiapo huku kukusudia kuongopa, kama vile kusema: “Wa-Allaahi nimenunua kitu kadhaa kwa gharama ya fedha kadhaa”, na hali si kweli kuwa umenunua bei hiyo. Au kusema: “Wa-Allaahi nimefanya kadhaa”, na hali hakufanya. Kuapa hivi ni miongoni mwa madhambi makubwa kama alivyosema Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam):

 

عَنْ عَبْدِ اللَّهِ بْنِ عَمْرٍو بْن الْعاص (رضي الله عنهما) عَنْ النَّبِيِّ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ َقَالَ: ((الْكَبَائِرُ الإِشْرَاكُ بِاللَّهِ وَعُقُوقُ الْوَالِدَيْنِ وَقَتْلُ النَّفْسِ وَالْيَمِينُ الْغَمُوسُ)) البخاري

Imepokelewa kutoka kwa ‘Abdullaah bin ‘Amri bin Al-‘Aasw (Radhwiya Allaahu ‘anhumaa)  ambaye amesema: Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: ((Al-Kabaair [Madhambi makubwa] ni kumshirikisha Allaah,  kuwaasi wazazi wawili, kuua nafsi na yamini [kiapo] ya uongo)) [Al-Bukhaariy]

 

Na katika riwaya nyingine:

 

أنَّ أَعْرَابِياً جَاءَ إِلَى النَّبِيِّ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ فَقَالَ: يَا رَسُولَ اللَّه,ِ مَا الْكَبَائِر؟ ُ قَالَ: ((الإشْرَاكُ بِاللَّهِ)) قَالَ: ثُمَّ مَاذَا؟ قَالَ: ((الْيَمِينُ الْغَمُوسُ)) قُلْتُ: وَمَا الْيَمِينُ الْغَمُوسُ؟  قَالَ: ((الَّذِي يَقْتَطِعُ مَالَ امْرِئٍ مُسْلِمٍ!)) يَعْنِ: بِيَمِينٍ هُوَ فِيهَا كَاذِبٌ

Alikuja Bedui mmoja kwa Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akamuuliza: Ee Rasuli wa Allaah! Ni yepi Al-Kabaair [madhambi makubwa]?” Akasema: ((Kumshirikisha Allaah)) Akasema: Kisha yepi? Akasema: ((Yamini ya uongo)). Nikauliza: Ni ipi yamini ya uongo? Akasema: ((Ni ambayo mtu hujichukulia mali ya Muislamu!)) yaani akaapa kwa uongo. [Al-Bukhaariy]

 

Imeitwa Yamiyn Al-Ghamuws (kiapo cha uongo) kwa sababu yamzamisha mwenye yamini hiyo ndani ya dhambi na yamini hii ndiyo iliyokusudiwa katika kauli ya Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam):

 

مَنْ حَلَفَ يَمينٍ صَبْرٍ لِيَقْتَطِعَ بِها مَالَ امْرِىءٍ مُسْلِمٍ، لَقِيَ اللهَ وَهُوَ عَلَيْهِ غَضْبانُ

((Atakayekula yamini hali yeye katika yamini hiyo anaongopa ili apate kwa yamini hiyo kumega mali ya mtu mwengine Muislamu basi mtu huyo atakutana na Allaah hali Amemghadhibikia)). [Al-Bukhaariy na Muslim]

 

Hukmu yake:  Kuna kauli mbili,

 

i) Yamiyn Al-Ghamuws haina kafara bali mtu atubie tawbah ya kwelikweli. Ni rai ya Imaam Abiy Haniyfah, Imaam Maalik na Imaam Ahmad bin Hanbal (Rahimahumu-Allaah). Pia Fatwa ya Al-Lajnatud-Daaimah (23/133) wamefutu: ”Al-Yamiyn Al-Ghamuws ni katika madhambi makubwa na haihitaji kafara kwa sababu ya ukubwa wa dhambi yake, bali inahitaji tawbah na kuomba maghfirah na ndio ilivyo sahihi kutokana na kauli za ‘Ulamaa.”

 

Na Shaykh Al-Islaamiy Ibn Taymiyyah amesema katika Majmuw’ Al-Fataawaa (34/139) baada ya kutaja ikhtilafu kuhusu kiapo cha Ghamuws….

“Wameafikiana kwamba dhambi haianguki kwa ajili ya kufanya kafara”. 

Amesema pia:

Ikiwa amemdhulumu mja mwenziwe basi amrudishie haki yake pamoja na kumuomba msamaha.

 

ii) Ama Imaam Ash-Shaafi’iy ameona inapasa kafara.  

 

 

2-Al-Yamiyn Al-Laghw (Kiapo cha upuuzi):

 

Hiki ni kile kiapo kipitacho katika ulimi wa Muislamu bila kukusudia, kama yule ambaye katika mazungumzo yake hujitokeza kwa wingi mno wa neno: “Wa-Allaahi hapana”. Hii ni kufuatia kauli ya Mama wa Waumini ‘Aaishah (Radhwiya Allaahu ‘anhaa):

لغو اليمين كقول الرجل لا والله وبلى والله،

 “Upuuzi katika yamini ni maneno anayozungumza mtu, “Hapana Wa-Allaahi, Ndio Wa-Allaahi.” [Al-Bukhaariy]

 

Hukumu ya yamini aina hii ni kuwa haina dhambi wala kafara kwa mhusika, kwa kauli yake Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) katika Suwrah Al-Maaidah (5: 89):

 

لَا يُؤَاخِذُكُمُ اللَّـهُ بِاللَّغْوِ فِي أَيْمَانِكُمْ

Allaah Hatokuchukulieni kwa viapo vyenu vya upuuzi, [Al-Maaidah: 89]

 

 

 

3-Al-Yamiyn Al-Mun’aqidah (Kiapo cha kufungika):

 

Ni kukusudia jambo la baadae. Kama vile Muislamu kusema: “Wa-Allaahi nitalifanya jambo kadhaa” Au “Wa-Allaahi sitolifanya…” kisha akafanya kinyume chake.

 

Hukmu yake ni katika Suwrat Al-Maaidah (5: 89):

 

وَلَـٰكِن يُؤَاخِذُكُم بِمَا عَقَّدتُّمُ الْأَيْمَانَ

lakini Atakuchukulieni kwa (kuvunja) viapo mlivyoapa kwa niyyah mlioifunga thabiti. [Al-Maaidah: 89]

 

ambayo inampasa afanye kafara:

 

فَكَفَّارَتُهُ إِطْعَامُ عَشَرَةِ مَسَاكِينَ مِنْ أَوْسَطِ مَا تُطْعِمُونَ أَهْلِيكُمْ أَوْ كِسْوَتُهُمْ أَوْ تَحْرِيرُ رَقَبَةٍ ۖ فَمَن لَّمْ يَجِدْ فَصِيَامُ ثَلَاثَةِ أَيَّامٍ ۚ ذَٰلِكَ كَفَّارَةُ أَيْمَانِكُمْ إِذَا حَلَفْتُمْ ۚوَاحْفَظُوا أَيْمَانَكُمْ ۚ كَذَٰلِكَ يُبَيِّنُ اللَّـهُ لَكُمْ آيَاتِهِ لَعَلَّكُمْ تَشْكُرُونَ ﴿٨٩﴾

Basi kafara yake ni kulisha maskini kumi chakula cha wastani mnachowalisha ahli zenu, au kuwavisha nguo, au kuacha huru mtumwa. Lakini asiyeweza kupata (katika hayo), basi afunge Swiyaam siku tatu. Hiyo ndio kafara ya viapo vyenu mnapoapa. Na hifadhini yamini zenu. Hivyo ndivyo Allaah Anavokubainishieni Aayaat (na hukmu) Zake ili mpate kushukuru.  [Al-Maaidah: 89]

 

 

Vinavyoapiwa kimakosa:

 

1- Kuapia vitu kadhaa:

 

Unapoapa kimakosa kwa kutumia vitu kuapia huhitaji kafara bali inakupasa urudi kutubia kwa Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa). ‘Ulamaa wamekubaliana hivyo kama alivyosema Shaykh Al-Islaam Ibn Taymiyyah katika Al-Fataawa Al-Kubraa (3/222): 

“Kuapia vitu viliyvoumbwa kama Al-Ka’bah, Malaika, mashekhe, wafalme, wazazi, makaburi ya wazazi n.k haihitajiki kafara kama ilivyokuwa ni rai ya Wanavyuoni. Bali imeharamishwa na Wanavyuoni na haramisho hili ni haraam kutokana na rai iliyo na nguvu kabisa”.

 

 

2- Kuapia kwa Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam):

 

Baadhi ya watu huapa kwa tamshi la: “Wan-Nabiy!”, “Haki ya Mtume!” n.k.

 

 

3- Kuapia kwa Msahafu:

 

Imaam Ibn 'Uthaymiyn (Rahimahu Allaah) aliulizwa kuhusu hukmu ya kuapia Msahafu alijibu:

"Hairuhusiwi kuweka nadhiri au kuapa isipokuwa kwa Allaah au moja ya Sifa Zake. Ikiwa mtu ataapa kwa jina la Allaah, basi hakuna haja tena kuleta Msahafu kwa ajili ya kuapa kwa sababu kuapa kwa Msahafu haikufanyika zama za Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Maswahaba. Hata baada ya Qur-aan kukusanywa katika Kitabu kimoja hawakuwa wakiapia Msahafu bali mtu alikuwa akiapa kwa Allaah bila ya kushika Msahafu."

[Fataawaa Nuwr 'Alaa Ad-Darb]

 

 

4- Kuapia kwa Al-Ka’bah:

 

Baadhi ya Waislamu hufikishana Makkah kuapizana kwa Al-Ka’bah jambo ambalo halijuzu bali ni kuvuka mipaka ya ‘Ibaadah, na kupoteza muda na mali ya kuwapeleka huko.

 

 

5- Kuapia wazazi, watoto:

 

Makatazo katika Hadiyth zilotanguliwa kutajwa juu.

 

 

6- Kuapia ‘amali njema kama Swiyaam (funga), Swadaqah n.k.

 

 

 



Hakuna maoni:

Chapisha Maoni

20-Hakika Shirki Ni Dhulma Kubwa Mno! - Isti’aadhah Kwa Asiyekuwa Allaah

  إِنَّ الشِّرْكَ لَظُلْمٌ عَظِيم   Hakika Shirki Ni Dhulma Kubwa Mno!   20 - Isti’aadhah  (Kuomba Kinga) Kwa Asiyekuwa Allaah   ...