Lu-ulu-un-Manthuwrun
(Mkusanyiko Wa Hadiyth Mbali Mbali Na Mafunzo Yake)
Hadiyth Ya 51
Muumin Anahimiza Jeneza Lake, Kafiri Anakhofia Na Kupiga Mayowe!
عَنْ أَبِي سَعِيدٍ الْخُدْرِيَّ (رضي الله عنه) أَنَّ رَسُولَ اللَّهِ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ قَالَ: ((إِذَا وُضِعَتْ الْجِنَازَةُ وَاحْتَمَلَهَا النَّاسُ – أوِ الرِّجَالُ عَلَى أَعْنَاقِهِمْ، فَإِنْ كَانَتْ صَالِحَةً قَالَتْ: قَدِّمُونِي. وَإِنْ كَانَتْ غَيْرَ صَالِحَةٍ قَالَتْ: يَا وَيْلَهَا! أَيْنَ يَذْهَبُونَ بِهَا؟ يَسْمَعُ صَوْتَهَا كُلُّ شَيْءٍ إلاَّ الإِنْسَانَ وَلَوْ سَمِعَهُ صَعِقَ)) البخاري
Imepokelewa kutoka kwa Abuu Sa’iyd Al-Khudriyy (رضي الله عنه) kwamba Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema: ((Linapowekwa jeneza na likabebwa na watu au wanaume shingoni mwao, basi anapokuwa [maiti] ni mwema husema: Nikadimisheni [nitangulizeni]. Lakini ikiwa si mtu mwema husema: Ole wake! Wanalipeleka wapi? Sauti yake inasikika na kila kitu isipokuwa binaadamu. Na lau angeisikia angelizimia)). [Al-Bukhaariy]
Mafunzo Na Mwongozo:
1. Muumin anatamani ayafikie mema aliyoahidiwa na Allaah (سبحانه وتعالى) baada ya kufariki kama Anavyosema Allaah (سبحانه وتعالى):
وَعَدَ اللَّـهُ الْمُؤْمِنِينَ وَالْمُؤْمِنَاتِ جَنَّاتٍ تَجْرِي مِن تَحْتِهَا الْأَنْهَارُ خَالِدِينَ فِيهَا وَمَسَاكِنَ طَيِّبَةً فِي جَنَّاتِ عَدْنٍ ۚوَرِضْوَانٌ مِّنَ اللَّـهِ أَكْبَرُ ۚ ذَٰلِكَ هُوَ الْفَوْزُ الْعَظِيمُ﴿٧٢﴾
Allaah Amewaahidi Waumini wanaume na Waumini wanawake Jannaat zipitazo chini yake mito, ni wenye kudumu humo na makazi mazuri katika Jannaat za kudumu milele. Na radhi kutoka kwa Allaah ndio kubwa zaidi. Huko ndiko kufuzu adhimu. [At-Tawbah (9: 72)]
Rejea pia: An-Nisaa (4: 122), Al-Maaidah (5: 9), At-Tawbah (9: 111), Luqmaan (31: 8-9), Az-Zumar (39: 20)
2. Kafiri au mtu muovu anakhofia adhabu aliyotishiwa nayo ambayo hakuiamini duniani. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):
وَلَوْ تَرَىٰ إِذِ الظَّالِمُونَ فِي غَمَرَاتِ الْمَوْتِ وَالْمَلَائِكَةُ بَاسِطُو أَيْدِيهِمْ أَخْرِجُوا أَنفُسَكُمُ ۖ الْيَوْمَ تُجْزَوْنَ عَذَابَ الْهُونِ بِمَا كُنتُمْ تَقُولُونَ عَلَى اللَّـهِ غَيْرَ الْحَقِّ وَكُنتُمْ عَنْ آيَاتِهِ تَسْتَكْبِرُونَ ﴿٩٣﴾
Na lau ungeliona madhalimu pale wakiwa katika mateso makali ya mauti, na Malaika wamenyosha mikono yao (wakiwaambia): “Toeni nafsi zenu! Leo mnalipwa adhabu ya kudhalilisha kwa yale mliyokuwa mkiyasema juu ya Allaah pasi na haki, na mlikuwa mkitakabari kuhusu Aayaat Zake.” [Al-An’aam (6: 93)]
Na pia:
وَعَدَ اللَّـهُ الْمُنَافِقِينَ وَالْمُنَافِقَاتِ وَالْكُفَّارَ نَارَ جَهَنَّمَ خَالِدِينَ فِيهَا ۚ هِيَ حَسْبُهُمْ ۚ وَلَعَنَهُمُ اللَّـهُ ۖ وَلَهُمْ عَذَابٌ مُّقِيمٌ﴿٦٨﴾
Allaah Amewaahidi wanafiki wanaume na wanafiki wanawake na makafiri moto wa Jahannam, ni wenye kudumu humo; unawatosheleza Na Allaah Amewalaani, na watapata adhabu ya kudumu. [At-Tawbah (9: 68)]
Rejea pia: Al-Jaathiyah (45: 28)
3. Ni Sunnah kuharakiza Jeneza.
4. Jeneza linabebwa na wanaume na si wanawake.
5. Baadhi ya sauti zinasikika kwa viumbe isipokuwa binaadamu na pia vitu vinginevyo visivyokuwahai. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):
فَإِنَّكَ لَا تُسْمِعُ الْمَوْتَىٰ وَلَا تُسْمِعُ الصُّمَّ الدُّعَاءَ إِذَا وَلَّوْا مُدْبِرِينَ ﴿٥٢﴾
Basi hakika wewe huwezi kusikilizisha wafu, na wala huwezi kusikilizisha viziwi wito wanapokengeua wakigeuza migongo yao. [Ar-Ruwm (30: 52)]
Rejea pia: An-Naml (27: 80)
6. Dalili kwamba maiti anasikia ila hawezi kuongea.
7. Uthibitisho wa hali ya maisha ya Barzakh na matokeo ya adhabu za kaburi au neema zake.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni