إِنَّ الشِّرْكَ لَظُلْمٌ عَظِيمٌ
Hakika Shirki Ni Dhulma Kubwa Mno!
12 -Kuchinja Kwa Niyyah Ya Asiyekuwa Allaah
Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Anaharamisha:
حُرِّمَتْ عَلَيْكُمُ الْمَيْتَةُ وَالدَّمُ وَلَحْمُ الْخِنزِيرِ وَمَا أُهِلَّ لِغَيْرِ اللَّـهِ بِهِ وَالْمُنْخَنِقَةُ وَالْمَوْقُوذَةُ وَالْمُتَرَدِّيَةُ وَالنَّطِيحَةُ وَمَا أَكَلَ السَّبُعُ إِلَّا مَا ذَكَّيْتُمْ وَمَا ذُبِحَ عَلَى النُّصُبِ وَأَن تَسْتَقْسِمُوا بِالْأَزْلَامِ ۚ ذَٰلِكُمْ فِسْقٌ
Mmeharamishiwa nyamafu, na damu, na nyama ya nguruwe, na kilichotajiwa asiyekuwa Allaah katika kuchinjwa kwake, na aliyenyongwa au aliyepigwa akafa, au aliyeporomoka, au aliyepigwa pembe, na aliyeliwa na mnyama mwitu, isipokuwa mliyewahi kumchinja kihalali (kabla ya kufa); na waliochinjwa kwa ajili ya ‘ibaadah ya waabudiwa, na kupiga ramli kwa mishale. Hayo kwenu ni ufasiki. [Al-Maaidah: 3]
Sababu kuchinja ni ‘ibaadah tukufu kabisa Ameamrisha Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) ichinjwe kwa ajili Yake Pekee.
فَصَلِّ لِرَبِّكَ وَانْحَرْ ﴿٢﴾
Basi swali kwa ajili ya Rabb wako na chinja kwa ajili Yake. [Al-Kawthar: 2]
Na Anasema Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa):
قُلْ إِنَّ صَلَاتِي وَنُسُكِي وَمَحْيَايَ وَمَمَاتِي لِلَّـهِ رَبِّ الْعَالَمِينَ ﴿١٦٢﴾
Sema: “Hakika Swalaah yangu, na kuchinja kafaara na ‘ibaadah zangu na uhai wangu na kufa kwangu ni kwa ajili ya Allaah Pekee Rabb wa walimwengu.” [Al-An’aam: 162]
Na Rasuli wa Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) amelaani mwenye kuchinja kwa ajili ya asiyekuwa Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa). Hadiyth ya ‘Aliy bin Abiy Twaalib (Radhwiya Allaahu ‘anhu):
عَنْ عَلِيِّ بن أبي طالب (رضي الله عنه) قَالَ: حَدَّثَنِي رَسُولُ اللَّهِ (صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ) بأرْبَعِ كَلِمَاتٍ: ((لَعَنَ اللَّهُ مَنْ ذَبَحَ لِغَيْرِ اللَّهِ, وَلَعَنَ اللَّهُ مَنْ لَعَنَ وَالِدَيْهِ, وَلَعَنَ اللَّهُ مَنْ آوَى مُحْدِثًا, وَلَعَنَ اللَّهُ مَنح مَنَارَ الأَرْضِ ))
Imepokewa kutoka kwa ‘Aliy bin Abiy Twaalib (Radhwiya Allaahu ‘anhu) kwamba: Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alinihadithia maneno manne: ((Allaah Amemlaani anayechinja kwa ajili ya asiyekuwa Allaah, na Allaah Amemlaani anayewalaani wazazi wake, na Allaah Amelaani anayemkaribisha na kumhami mhalifu, na Allaah Amelaani anayemlaani mzazi wake, na Allaah Amelaani anayebadilisha mipaka ya ardhi [anayomiliki])) [Muslim]
Pia:
حديث ثَابِتُ بْنُ الضَّحَّاكِ قَالَ : نَذَرَ رَجُلٌ عَلَى عَهْدِ رَسُولِ اللَّهِ صلى الله عليه وسلم أَنْ يَنْحَرَ إِبِلاً بِبُوَانَةَ فَأَتَى النَّبِىَّ صلى الله عليه وسلم فَقَالَ: إِنِّى نَذَرْتُ أَنْ أَنْحَرَ إِبِلاً بِبُوَانَةَ. فَقَالَ النَّبِىُّ -صلى الله عليه وسلم : ((هَلْ كَانَ فِيهَا وَثَنٌ مِنْ أَوْثَانِ الْجَاهِلِيَّةِ يُعْبَدُ)) قَالُوا: لاَ. قَالَ: ((هَلْ كَانَ فِيهَا عِيدٌ مِنْ أَعْيَادِهِمْ )) قَالُوا : لاَ. قَالَ رَسُولُ اللَّهِ صلى الله عليه وسلم: ((أَوْفِ بِنَذْرِكَ فَإِنَّهُ لاَ وَفَاءَ لِنَذْرٍ فِى مَعْصِيَةِ اللَّهِ وَلاَ فِيمَا لاَ يَمْلِكُ ابْنُ آدَمَ )). وصححه الألباني
Imepokelewa kutoka kwa Thaabit ibn Adhw-Dhwahhaak (Radhwiya Allaahu ‘anhu) kwamba: “Mtu mmoja aliweka nadhiri kuchinja ngamia sehemu ya Buwaanah. Akaja kwa Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akasema: “Nimeweka nadhiri kuchinja ngamia Buwaanah”. Akasema Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam): ((Je kuliweko masanamu ya kijaahiliyyah (kabla Uislamu) yakiabudiwa?”. Wakasema: “Hapana” Akasema: ((Je kuliweko sherehe za kijaahiliyyah zikifanywa hapo?)). Wakasema: “Hapana” Rasuli wa Allaahh (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akasema: ((Timiza nadhiri yako, kwani hakuna kutimiza nadhiri katika kumuasi Allaah, wala katika ambayo hayamiliki bin Aadam)). [Abuu Daawuwd na ameisahihisha Al-Albaaniy]
Al-Lajnah Ad-Daaimah (1/226) wamefutu: “Kuchinja kwa ajili ya asiyekuwa Allaah ni shirki na hukmu ya kichinjo ni hukmu ya nyamafu (mzoga) haijuzu kuliwa nyama yake hata kama imetajwa Jina la Allaah ikiwa imehakiki kuwa imechinjwa ghairi ya Allaah.”
Na Imaam Ibn ‘Uthaymiyn (Rahimahu Allaah) amesema katika Majmuw' Fataawa Ibn ‘Uthaymiyn (2/148): “Kuchinja kwa ajili kwa ajili ya aisyekuwa Allaah ni shirki kubwa kwa sababu kuchinja ni ‘ibaadah, kwa hiyo anayechinja kwa ajili (niyyah) asiyekuwa Allaah ni mshirikina ambaye shirki yake inamtoa nje ya Uislamu – tunajikinga na Allaah – ikiwa amechinja kwa ajili ya Malaika au kwa ajili ya Nabiy yeyote au kwa ajili ya Khaliyfah yeyote au kwa ajili ya awliyaa (waja wema) au kwa ajili ya Mwanachuoni yeyote. Yote ni kumshirikisha Allaah (Subhanaahu wa Ta’aalaa) na inamtoa nje ya Uislamu. Na kuhusu kula nyama ya vichinjo hivyo ni haraam kwa sababu amechinjwa kwa ajili ya asiyekuwa Allaah na kila kinachochinjwa kwa ajili ya chochote ghairi ya Allaah au amechinjwa juu ya jiwe la madhabahu (mizimwi) ni haraam.”
Hadiyth ifuatayo inadhihirisha kwamba hata ikiwa ni kiasi kidogo vipi kitu kinachokurubishwa pasi na Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) kwa kuchinja, huwa ni shirki na hatari yake humuingiza mtu Motoni:
((دَخَلَ الْجَنَّةَ رَجُلٌ فِي ذُبَاب، وَدَخَلَ النَّار رَجُلٌ فِي ذُبَاب)): قَالُوا: وَكَيْفَ ذَلِكَ يَا رَسُولَ الله؟ قَالَ: ((مَرَّ رَجُلانِ علَى قَوْمٍ لَهُمْ صَنَمٌ لاَ يَجُوزُهُ أحَدٌ حَتَّى يُقَرِّبَ لَهُ شَيْئاً، فَقَالُوا لإَحَدِهِمَا: قَرِّبْ، قَالَ: لَيْسَ عِنْدِي شَيْءٌ أُقَرِّبَهُ، قَالُوا بِه: قَرِّبْ وَلَوْ ذُباَبًا، فَقَرَّبَ ذُبَاباً، فَخَلُّوا سَبِيْلَهُ، فَدَخَلَ النَّارَ، وَقَالُوا لِلآخر: قَرِّبْ، فَقَالَ: مَا كُنْتُ لأُقَرِّبَ لأحَدٍ شَيْئًا دُونَ الله عَزَّ وَجَلَّ. فَضَرَبُوا عُنقَهُ، فَدَخَلَ الْجَنَّةَ))
((Mtu mmoja ameingia Jannah kwa nzi, na ameingia Motoni mtu kwa ajili ya nzi)). Wakasema: Vipi hivyo ee Rasuli wa Allaah? Akasema: ((Watu wawili walipitia mbele ya watu walikuwa na sanamu lao, hapiti mtu hadi ajikurubishe kwa kuchinja. Wakamwambia mmoja wao: Jikurubishe! [Chinja!] Akasema: Sina kitu cha kujikurubisha. Wakasema: Jikurubishe japo kwa nzi. Akajikurubisha kwa nzi. Wakamwachia apite njia akaingia Motoni. Wakawambia mwengine: Jikurubishe! Akasema: Sikuwa najikurubisha [nachinja] kwa yeyote pasi na Allaah ‘Azza wa Jalla. Wakampiga shingo [wakamuua] akaingia Jannah)). [Ahmad, Fataawaa Shaykh Ibn Baaz]
Shaykh Fawzaan bin Fawzaan akifafanua Hadiyth hiyo anasema:
“[Mtu wa kwanza] Ametoa udhuru kutokuwa na kitu. Hakusema “hakika kuchinja pasi na Allaah haijuzu au ni munkari” – Tunajikinga kwa Allaah. Na hii inafahamika kwamba lau angelikuwa ana mnyama wa kuchinja angelichinja. Wakamwambia: “Jikurubishe walau kwa nzi!” Akajikurubisha kwa nzi, yaani akafanya hivyo kwa ajili ya sanamu wakamwachia apite njia, akaingia Motoni kwa sababu ya shirki. Amejikurubisha pasi na Allaah, na 'ibra (zingatio) hapa ni niyyah na kusudio wala sio kuhusu kinachochinjwa. Na kwamba hakuchukia jambo hili wala hakujiepusha nalo, bali ametoa udhuru kutokuwa na kitu na kwa hivyo amengia Motoni – Tunajikinga kwa Allaah.
Na wakamwambia mwengine: “Jikurubishe!” Akasema: “Sikuwa ni mwenye kuchinja chochote kwa ajili ya asiyekuwa Allaah ‘Azza wa Jalla.” Amejiepusha na amechukia shirki. Wakampiga shingo yake, kwa maana wamemuua akaingia Jannah kwa sababu ya Tawhiyd.
Hivyo basi katika Hadiyth hii tukufu kuna mafunzo muhimu:
Kwanza: Hadiyth inaruhusu kuelezea habari za ummah zilizopita na kuelezea ilivyothibiti kwa ajili ya kuwaidhi na zingatio.
Pili: Katika Hadiyth kuna dalili ya kuharamishwa kujikurubisha kwa kuchinja pasi na Allaah, na mwenye kujikurubisha pasi na Allaah, atakuwa ametenda shirki kwa sababu mtu aliyeua nzi ameingia Motoni hata ikiwa ni kitu kichafu cha kutemwa (kidogo, duni mno). Na mtu wa pili amechukia shirki na amejiepusha japokuwa ilikuwa ni kitu cha kuchukizwa (duni) akaingia Jannah.
Tatu: Kama alivyosema Shaykh (Rahimahu Allaah) kuhusu mas-alah ya niyyah ya 'amali za moyo, japokuwa ni kitu kichafu cha kutemwa (kidogo, duni mno) lakini itambulike kuwa niyyah ni 'amali ya moyo.
Nne: Kama alivyosema Shaykh (Rahimahu Allaah) kuhusu wepesi wa bin Aadam kukaribia Jannah na Moto ni kama alivyosema Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam): ((Jannah iko karibu zaidi kwa mmoja wenu kuliko nyuzi za viatu vyake, na Moto kama hivyo)). [Al-Bukhaariy]
Huyu amepigwa shingo yake (ameuliwa) akaingia Jannah. Na yule wamemwachia njia akaingia Motoni.
Tano: Kwamba mtu aliyeua nzi alikuwa Muumini, akaingia Motoni kwa sababu ya kujikurubisha kwake kwa nzi, kwa sababu angelikua kafiri, angeliingia Motoni kwa kufru yake si kwa kujikurubisha kwa nzi. Akadhihirisha kwamba alikuwa Muumini, na mas-alah haya ni khatari sana!
Basi wako wapi wanaochinja kwa ajili ya makaburi, na majini, na mashaytwaan, na kwa ajili ya ardhi, na wachawi?
Akaonyesha kwamba shirki kubwa kabisa inamtoa mtu nje ya Dini japokuwa ikiwa ni kitu chepesi. Hivyo basi, suala la Tahwiyd na ‘Aqiydah hayasamehe hayo.” [Sharh Kitaab At-Tawhiyd – Baab maa jaa-a fiy adhdhab-h li-ghayri-LLaah]
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni