Lu-ulu-un-Manthuwrun
(Mkusanyiko Wa Hadiyth Mbali Mbali Na Mafunzo Yake)
Hadiyth Ya 30
Mwanamke Asifunge (Swawm)
Au Kumuingiza Mtu Kwenye Nyumba Bila Ya Idhini Ya Mumewe
عَنْ أَبِي هُرَيْرَةَ (رضي الله عنه) أَنَّ رَسُولَ اللَّهِ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ قَالَ: ((لاَ يَحِلُّ لِلْمَرْأَةِ أَنْ تَصُومَ وَزَوْجُهَا شَاهِدٌ إلاَّ بِإِذْنِهِ. وَلاَ تَأْذَنَ فِي بَيْتِهِ إلاَّ بِإِذْنِهِ)) متفق عليه وهذا لفظ البخاري
Imepokelewa kutoka kwa Abuu Hurayrah (رضي الله عنه) kwamba Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema: ((Si halali kwa mwanamke kufunga Swawm [ya Sunnah] ilhali mumewe yupo [hakusafiri] ila kwa idhini yake. Wala asimruhusu mtu kuingia nyumbani kwake ila kwa idhini yake)). [Al-Bukhaariy na Muslim kwa lafdhi ya Al-Bukhaariy]
Mafunzo na Mwongozo:
1. Mwanamke hatakiwi kufunga Swawm ya Sunnah yoyote ila kwanza apate ruhusu ya mumewe, kwani huenda akawa anamhitajia kwa kitendo cha ndoa.
2. Mwanamke hapasi kumuingiza mtu yeyote nyumbani kwake bila ya ruhusa ya mumewe. Akumbuke kauli ya Allaah (سبحانه وتعالى):
فَالصَّالِحَاتُ قَانِتَاتٌ حَافِظَاتٌ لِّلْغَيْبِ بِمَا حَفِظَ اللَّـهُ ۚ﴿٣٤﴾
Basi wanawake wema ni wale watiifu wenye kujihifadhi katika hali ya kutokuweko waume zao kwa kuwa Allaah Ameamrisha wajihifadhi [An-Nisaa (4: 34)]
3. ‘Ibaadah za Sunnah zinashinda haki ya bin Aadam.
4. Mke kufuata Shariy’ah kama hii itamzuia mume kufanya zinaa.
5. Umuhimu wa kuhifadhi haki baina ya mke na mume. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):
وَلَهُنَّ مِثْلُ الَّذِي عَلَيْهِنَّ بِالْمَعْرُوفِ ۚ وَلِلرِّجَالِ عَلَيْهِنَّ دَرَجَةٌ ۗ
Nao wake wana haki kama ambayo (ya waume zao) iliyo juu yao kwa mujibu wa shariy’ah. Na wanaume wana daraja zaidi juu yao [Al-Baqarah (2: 228)]
Na Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema:
((لو كنتُ آمرًا أحدًا أن يسجدَ لغيرِ اللهِ ، لأمرتُ المرأةَ أن تسجدَ لزوجِها، و الذي نفسُ محمدٍ بيدِه ، لا تؤدِّي المرأةُ حقَّ ربِّها، حتى تؤدِّيَ حقَّ زوجِها كلَّه، حتى لو سألها نفسَها و هي على قَتَبٍ لم تمنَعْه))
((Ningeliweza kumuamrisha mtu amsujudie asiyekuwa Allaah, ningelimuamrisha mke amsujudie mume wake. Naapa kwa Ambaye nafsi ya Muhummad imo Mikononi Mwake, mwanamke hatotimiza haki za Rabb Wake mpaka atimize haki zote za mumewe. Akimtaka (kujamii naye) hata kama yuko katika kipando cha ngamia, basi asimkatalie)) [Hadiyth ya ‘Abdullaah bin Abiy Awfaa - Sunan Ibn Maajah na ameisahihisha Al-Albaaniy katika Swahiyh Ibn Maajah (1515), Swahiyh Al-Jaami’ (5295)
Rejea pia Hadiyth namba (29), (128),
6. Umuhimu wa kujilinda na maasi kwa jinsi ya kwamba hata ‘ibaadah ya Sunnah kama hiyo ya Swawm haitakiwi kutekelezwa juu ya kwamba ni ‘ibaadah yenye malipo makubwa kabisa ambayo Allaah (سبحانه وتعالى) Amesema kuwa ‘ibaadah hii ni kwa ajili Yake na kwamba Yeye Ndiye Atakayemlipa mja kama ilivyotajwa katika Hadiyth: ((Kila ‘amali njema ya mwana Aadam inalipwa mara kumi na inaongezewa thawabu kutoka kumi hadi mia saba, na Allaah Anasema isipokuwa Swawm, kwani hiyo ni kwa ajili Yangu na Mimi Ndiye Nitakayemlipa))].[Al-Bukhaariy na Muslim]
7. Mke kufuata amri ya kutokumuingiza mtu yeyote yule nyumbani kwake. Na kufanya hivyo kutazuia fitna na hatari ya maasi ya zinaa.
8. Utekelezaji wa Uislamu ni nidhamu kamili ya maisha hata katika mas-alah ya nyumba na unyumba. Nidhamu hii ikitofuatwa, basi kunatokea matatizo mengi katika utangamano baina ya mume na mke.
9. Kila Shariy’ah iliyoletwa na Uislamu ina hikma yake kubwa na hivyo Muislamu mwema na mzuri ni yule mwenye kuzifuata bila ya kuwa na uzito au kuchagua baadhi na kuacha baadhi yake. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):
وَمَا كَانَ لِمُؤْمِنٍ وَلَا مُؤْمِنَةٍ إِذَا قَضَى اللَّـهُ وَرَسُولُهُ أَمْرًا أَن يَكُونَ لَهُمُ الْخِيَرَةُ مِنْ أَمْرِهِمْ ۗ وَمَن يَعْصِ اللَّـهَ وَرَسُولَهُ فَقَدْ ضَلَّ ضَلَالًا مُّبِينًا ﴿٣٦﴾
Na haiwi kwa Muumini mwanamme na wala kwa Muumini mwanamke, Anapohukumu Allaah na Rasuli Wake jambo lolote, iwe wana hiari katika jambo lao. Na anayemuasi Allaah na Rasuli Wake, basi kwa yakini amepotoka upotofu bayana. [Al-Ahzaab (33: 36)]
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni