Lu-ulu-un-Manthuwrun
(Mkusanyiko Wa Hadiyth Mbali Mbali Na Mafunzo Yake)
Hadiyth Ya 33
Kutaja Jina La Allaah Katika Chakula Na Kula Kilichoko Mbele Yako
عَنْ عُمَرَ بْن أَبِي سَلَمَةَ عَبْدُ الله رَبيب رَسُولِ اللَّهِ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ قَال: كُنْتُ غُلاَمًا فِي حَجْرِ رَسُولِ اللَّهِ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ وَكَانَتْ يَدِي تَطِيشُ فِي الصَّحْفَةِ فَقَالَ لِي رَسُولُ اللَّهِ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ: ((يَا غُلاَمُ سَمِّ اللَّهَ تَعَالى، وَكُلْ بِيَمِينِكَ، وَكُلْ مِمَّا يَلِيكَ)) فَمَا زَالَتْ تِلْكَ طِعْمَتِي بَعْدُ. متفق عليه
Imepokelewa kutoka kwa ‘Umar bin Abi Salamah, ambaye ni mwanakambo wa Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema: Nilikuwa kijana mdogo chini ya ulezi wa Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم), na mkono wangu ulikuwa ukizungukazunguka katika sinia (ya chakula). Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) akaniambia: ((Ee ghulamu! Taja jina la Allaah (Ta’aalaa) na kula kwa mkono wako wa kulia, na ule kilicho mbele yako)). Basi huo ukawa ndio mtindo wangu wa kula baadaye. [Al-Bukhaariy, Muslim]
Mafunzo na Mwongozo:
1. Kuwajibika kuwafunza watoto kila aina mojawapo wa tabia njema za Kiislamu na kuwatanabahisha makosa yao wanapoanza kuyatenda.
2. Miongoni mwa adabu za kuanza jambo lolote, kama kula chakula ni kuanza kwa ‘BismiLlaah’ (Naanza kwa Jina la Allaah), na kula kwa mkono wa kulia, na kula kilicho mbele ya sahani.
3. Ruhusa ya kula pamoja au pekee. Lakini Hadiyth inaashiria kula katika sahani moja ni bora zaidi, na bila shaka inaleta baraka katika chakula. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):
لَّيْسَ عَلَى الْأَعْمَىٰ حَرَجٌ وَلَا عَلَى الْأَعْرَجِ حَرَجٌ وَلَا عَلَى الْمَرِيضِ حَرَجٌ وَلَا عَلَىٰ أَنفُسِكُمْ أَن تَأْكُلُوا مِن بُيُوتِكُمْ أَوْ بُيُوتِ آبَائِكُمْ أَوْ بُيُوتِ أُمَّهَاتِكُمْ أَوْ بُيُوتِ إِخْوَانِكُمْ أَوْ بُيُوتِ أَخَوَاتِكُمْ أَوْ بُيُوتِ أَعْمَامِكُمْ أَوْ بُيُوتِ عَمَّاتِكُمْ أَوْ بُيُوتِ أَخْوَالِكُمْ أَوْ بُيُوتِ خَالَاتِكُمْ أَوْ مَا مَلَكْتُم مَّفَاتِحَهُ أَوْ صَدِيقِكُمْ ۚ لَيْسَ عَلَيْكُمْ جُنَاحٌ أَن تَأْكُلُوا جَمِيعًا أَوْ أَشْتَاتًا ۚ فَإِذَا دَخَلْتُم بُيُوتًا فَسَلِّمُوا عَلَىٰ أَنفُسِكُمْ تَحِيَّةً مِّنْ عِندِ اللَّـهِ مُبَارَكَةً طَيِّبَةً ۚ كَذَٰلِكَ يُبَيِّنُ اللَّـهُ لَكُمُ الْآيَاتِ لَعَلَّكُمْ تَعْقِلُونَ ﴿٦١﴾
Si vibaya kwa kipofu, na wala si vibaya kwa kilema, na wala si vibaya kwa mgonjwa, na wala nyinyi wenyewe kama mtakula majumbani mwenu, au majumbani mwa baba zenu, au majumbani mwa mama zenu, au majumbani mwa kaka zenu, au majumbani mwa dada zenu, au majumbani mwa ‘ammi zenu, au majumbani mwa shangazi zenu, au majumbani za wajomba wenu, au majumbani mwa makhalati zenu au za mliowashikia funguo zao, au rafiki yenu. Hakuna ubaya kama mkila pamoja au mbali mbali. Mtakapoingia majumbani toleaneni salaam; maamkizi kutoka kwa Allaah, yenye Baraka, mazuri. Hivyo ndivyo Anavyokubainishieni Allaah Aayaat ili mpate kutia akilini. [An-Nuwr (24: 61)]
4. Hima ya Maswahaba kufuata Sunnah, maamrisho na muongozo wa Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) tokea udogoni mwao.
5. Umuhimu wa kumfunza mtoto angali mdogo.
6. Kurekebisha kosa pale pale linapotokea kwa wakati wake munaasib na kwa upole.
7. Kutumia utaratibu na mfumo mzuri wa kumrekebisha mtu bila ya yeye kujihisi vibaya au kumfedhehesha. Hapa tunaona kuwa tatizo la mtoto lilikuwa ni mkono kuzungukazunguka katika sahani, lakini hilo lilitajwa mwisho na Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم).
8. Kuwa makini katika kurekebisha jambo na kujali hisia za mtu japo za mtoto mdogo.
9. Maswahaba walikuwa makini katika kuyafikisha waliyopewa, kufundishwa na kunasihiwa na Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم), kwani walifahamu kuwa hayo hayakuwa yao pekee yao bali ni kwa Ummah wote.
10. Hadiyth inatupatia fundisho kujuzu kwa mwanamme kuwalea watoto wa mke wake aliyezaa na mume mwengine.
11. Mwanamme anayelea watoto wa kambo anatakiwa awalee kwa njia nzuri kama watoto wake wa uhusiano wa damu.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni