Lu-ulu-un-Manthuwrun
(Mkusanyiko Wa Hadiyth Mbali Mbali Na Mafunzo Yake)
Hadiyth Ya 46
Ardhi Itashuhudia Matendo Ya Watu Siku Ya Qiyaamah
عَنْ أَبِي هُرَيْرَةَ (رضي الله عنه) قَالَ: قَرَأَ رَسُولُ اللَّهِ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ: ((يَوْمَئِذٍ تُحَدِّثُ أَخْبَارَهَا)) قَالَ: ((أَتَدْرُونَ مَا أَخْبَارُهَا)) قَالُوا: اللَّهُ وَرَسُولُهُ أَعْلَمُ. قَالَ: ((فَإِنَّ أَخْبَارَهَا أَنْ تَشْهَدَ عَلَى كُلِّ عَبْدٍ أَوْ أَمَةٍ بِمَا عَمِلَ عَلَى ظَهْرِهَا، تَقُولُ عَمِلْتَ كَذَا وَكَذَا فِي يَوْمَ كَذَا وَكَذَا فَهَذِهِ أَخْبَارُهَا)) الترمذي وقَالَ: حَدِيثٌ حَسَنٌ صحيح
Imepokelewa kutoka kwa Abuu Hurayrah (رضي الله عنه) kwamba Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) alisoma: ((Siku hiyo itahadithia khabari zake.)). Akauliza: ((Mnajua nini khabari zake?)) Wakasema: Allaah na Rasuli Wake Wanajua zaidi. Akasema: ((Khabari zake ni kwamba itashuhudia juu ya kila mja mwanamme au mwanamke waliyoyatenda juu yake, itasema: Umefanya kadhaa na kadhaa, siku kadhaa na kadhaa. Basi hii ndio habari zake)). [At-Tirmidhiy na amesema: Hadiyth Hasan Swahiyh]
Mafunzo Na Mwongozo:
1. Himizo la kutenda mema na kujiepusha na maasi.
2. Uwezo wa Allaah (سبحانه وتعالى) kujaalia kila kitu kuzungumza Siku ya Qiyaamah; ardhi, viungo vya mwili wa mtu, ngozi n.k. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):
الْيَوْمَ نَخْتِمُ عَلَىٰ أَفْوَاهِهِمْ وَتُكَلِّمُنَا أَيْدِيهِمْ وَتَشْهَدُ أَرْجُلُهُم بِمَا كَانُوا يَكْسِبُونَ ﴿٦٥﴾
Leo Tunatia vizibo juu ya vinywa vyao, na itatusemesha mikono yao, na itashuhudia miguu yao kwa yale waliyokuwa wakiyachuma. [Yaasiyn: 65]
Rejea pia: [An-Nuwr (24: 24), Ghaafir (40: 21-22)]
3. Tisho kubwa la mwenye kutenda maasi japokuwa mahali pa kutendwa maasi patakuwa ni mbali, kwani ardhi popote itamshuhudia matendo yake. [Rejea: Aal-‘Imraan (3: 30)].
4. Hakuna mtu atakayeweza kuficha maasi yake yoyote na Siku hiyo siri zote zitadhihirishwa. [Rejea: Al-Haaqah (69: 18), Atw-Twaariq (86: 9), Al-Qiyaamah (75: 13)].
5. Heshima ya Maswahaba kwa mwalimu wao, Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) kwa kusema hatujui jambo ambalo hawajui. Na si aibu kutojua jambo miongoni mwa mambo, bali ni sifa nzuri anayotakiwa kuwa nayo Muislamu.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni