Translate

Ijumaa, 10 Julai 2020

09-Hakika Shirki Ni Dhulma Kubwa Mno! - Kusujudu Na Kuinamia Kwa Asiyekuwa Allaah

 

إِنَّ الشِّرْكَ لَظُلْمٌ عَظِيمٌ

 

Hakika Shirki Ni Dhulma Kubwa Mno!

 

09 Kusujudu Na Kuinamia Kwa Asiyekuwa Allaah

 

 

 

Washirikina wa kale walimshirikisha Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) kwa namna mbali mbali; kuna walioabudu masanamu wakiyasujudia na kurukuu mbele yao. Wengine walirukuu na kusujudia mwezi, nyota na jua, jambo ambalo Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Ameliharamisha katika kauli Yake:

 

وَمِنْ آيَاتِهِ اللَّيْلُ وَالنَّهَارُ وَالشَّمْسُ وَالْقَمَرُ ۚ لَا تَسْجُدُوا لِلشَّمْسِ وَلَا لِلْقَمَرِ وَاسْجُدُوا لِلَّـهِ الَّذِي خَلَقَهُنَّ إِن كُنتُمْ إِيَّاهُ تَعْبُدُونَ﴿٣٧﴾

Na katika Aayaat (ishara, dalili) Zake, ni usiku na mchana, na jua na mwezi.  Msisujudie jua wala mwezi; bali msujudieni Allaah Ambaye Aliyeviumba ikiwa Yeye Pekee mnawambudu. [Fusw-swilat: 37]

 

 

Hali kama hii inatendwa na baadhi ya Waislamu kuinamia binaadamu wenzao katika maamkizi n.k. kwa kudhihirisha mapenzi, takrima na heshima.  Baadhi ya mila zinaamrisha watoto kuwainamia wazazi wao, au waalimu na watu wakubwa katika maamkizi. Kadhaalika, hata baadhi ya watu wa itikadi mbalimbali wenye vyeo wanapenda kusalimiwa kwa kuinamiwa! Kitendo hiki kinaingia katika kumshikirisha Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa).

 

 

Imaam Ibn Baaz (Rahimahu Allaahu) amesema: “Sujudu ni kwa ajili ya Allaah Pekee na shariy’ah ya Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ni shariy’ah kamilifu kabisa, basi haijuzu kumsujudia yeyote asiyekuwa Allaah, ikiwa ni katika maamkizi wala katika ‘ibaadah. Ama katika shariy’ah zote, sujudu ya ‘ibaadah ndio haijuzu kabisa isipokuwa kwa Allaah. Isipokuwa ilikuwa zamani (kabla ya Uislamu) sujudu ilikuwa ikitumika kama maamkizi ya kudhihirisha heshima kama alivyofanya (Nabiy Ya’quwb) baba yake Nabiy Yuwsuf na ndugu zake na kama walivyofanya Malaika kumsujudia Aadam. Hii ni katika maamkizi ya takrima wala si kusudio la ‘ibaadah. Ama katika shariy’ah ya Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), Allaah (‘Azza wa Jalla) Amekataza hivyo Akaifanya sujudu ni kwa ajili ya Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Pekee wala haijuzu kumsujudia yeyote; si Manabiy wala wengineo, hata Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amekataza asisujudiwe na yeyote na akajulisha kwamba sujudu ni kwa ajili ya Allaah (Subhaanahu wa Ta’aala) Pekee.” [Fataawaa Nuwr  ‘Alaa Ad-Darb (4/112-113)]

 

Shaykhul-Islaam Ibn Taymiyyah amenukuu katazo kama hilo katika Majmuw’ Al-Fataawaa (1/377) .     

 

Na Al-Lajnah Ad-Daaimah lil-buhuwthil-‘ilmiyyah wal-Iftaa katika Fatwa namba (4400) wamefutu ifuatavyo:

 

“Yeyote aliyeamini Risala ya Nabiy wetu Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na yale yote aliyokuja nayo katika shariy’ah, kisha baada ya hapo akamsujudia yeyote asiyekuwa Allaah; ikiwa ni walii wake au mtu kaburini, au shekhe wa Twariyqah (Masufi)  basi yeye anahesabika kuwa ni kafiri aliyeritadi kutoka katika Uislamu, ni mshirikina akimshirikisha Allaah na wengineo katika ‘ibaadah hata kama atakuwa anatamka Shahada mbili wakati wa kusujudu kwake, kwa kuleta jambo lenye kupinga kauli yake kwa kumsujudia asiyekuwa Allaah.”

 

Katazo hilo limethibiti katika Qur-aan na Sunnah: 

 

عَنْ عَبْدِ اللَّهِ بْنِ أَبِي أَوْفَى، قَالَ: "لَمَّا قَدِمَ مُعَاذٌ مِنَ الشَّامِ سَجَدَ لِلنَّبِيِّ صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ، قَالَ: ((مَا هَذَا يَا مُعَاذُ ؟)) قَالَ: أَتَيْتُ الشَّامَ فَوَافَقْتُهُمْ يَسْجُدُونَ لِأَسَاقِفَتِهِمْ وَبَطَارِقَتِهِمْ، فَوَدِدْتُ فِي نَفْسِي أَنْ نَفْعَلَ ذَلِكَ بِكَ، فَقَالَ رَسُولُ اللَّهِ صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ: ((فَلَا تَفْعَلُوا، فَإِنِّي لَوْ كُنْتُ آمِرًا أَحَدًا أَنْ يَسْجُدَ لِغَيْرِ اللَّهِ، لَأَمَرْتُ الْمَرْأَةَ أَنْ تَسْجدَ لِزَوْجِهَا، وَالَّذِي نَفْسُ مُحَمَّدٍ بِيَدِهِ، لَا تُؤَدِّي الْمَرْأَةُ حَقَّ رَبِّهَا حَتَّى تُؤَدِّيَ حَقَّ زَوْجِهَا، وَلَوْ سَأَلَهَا نَفْسَهَا وَهِيَ عَلَى قَتَبٍ لَمْ تَمْنَعْه))

Imepokelewa kutoka kwa ‘Abdullaah bin Abiy Awfaa (Radhwiya Allaahu ‘anhu) amesema: “Muaadh aliporudi kutoka Shaam alimsujudia Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akasema: ((Ee Mu’aadh! Nini hivyo?)) Akasema: “Nimekuja kutoka Shaam nikawakuta wanawasujudia Maaskofu na Mapadri wao nafsi yangu ikapenda nikufanyie hivyo.” Akasema Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam): ((Usifanye hivyo! Kwani hakika ingekuwa ni kumuamrisha mtu amsujudie asiyekuwa Allaah, basi ningeliamrisha mke amsujudie mumewe. Naapa kwa Ambaye nafsi ya Muhammad ipo Mikononi Mwake; Mke hatoweza kutimiza haki za Mola Wake mpaka atimize haki za mumewe, na hata kama atamtaka hali akiwa katika nundu la ngamia basi asimnyime)) [Riwaayah mbali mbali kama hiyo na hii ni lafdhw ya Ibn Maajah (1853) na ameisahihisha Al-Albaaniy]

 

Na Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Anasema:

 

مَا كَانَ لِبَشَرٍ أَن يُؤْتِيَهُ اللَّـهُ الْكِتَابَ وَالْحُكْمَ وَالنُّبُوَّةَ ثُمَّ يَقُولَ لِلنَّاسِ كُونُوا عِبَادًا لِّي مِن دُونِ اللَّـهِ وَلَـٰكِن كُونُوا رَبَّانِيِّينَ بِمَا كُنتُمْ تُعَلِّمُونَ الْكِتَابَ وَبِمَا كُنتُمْ تَدْرُسُونَ ﴿٧٩﴾

Ni mustahili kwa mtu kwamba Allaah Amempa Kitabu na Al-Hukma na Unabii kisha awaambie watu: “Kuweni wenye kuniabudu mimi badala ya Allaah” Bali (atawaambia): “Kuweni Wanachuoni waswalihina kwa yale mliyokuwa mkiyafundisha ya Kitabu na kwa yale mliyokuwa mkiyasoma.” 

 

 

وَلَا يَأْمُرَكُمْ أَن تَتَّخِذُوا الْمَلَائِكَةَ وَالنَّبِيِّينَ أَرْبَابًا ۗ أَيَأْمُرُكُم بِالْكُفْرِ بَعْدَ إِذْ أَنتُم مُّسْلِمُونَ ﴿٨٠﴾ 

Na wala hakuamuruni kuwachukua Malaika na Manabii kuwafanya miola. Je, anakuamrisheni ukafiri baada ya nyinyi kuwa mmejisalimisha kwa Allaah? [Aal-‘Imraan: 79-80]

 

 

 

 

 



Hakuna maoni:

Chapisha Maoni

20-Hakika Shirki Ni Dhulma Kubwa Mno! - Isti’aadhah Kwa Asiyekuwa Allaah

  إِنَّ الشِّرْكَ لَظُلْمٌ عَظِيم   Hakika Shirki Ni Dhulma Kubwa Mno!   20 - Isti’aadhah  (Kuomba Kinga) Kwa Asiyekuwa Allaah   ...