Translate

Alhamisi, 3 Oktoba 2019

34-Fadhila Za Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم): Amekubaliwa Ombi Lake Kutoka Mbingu Ya Saba Kupunguziwa Swalaah Khamsiyn Kwa Ummah Wake

 

Fadhila Za  Nabiy  (صلى الله عليه وآله وسلم)

 

34-Amekubaliwa Ombi Lake Kutoka Mbingu Ya Saba

Kupunguziwa Swalaah Khamsiyn Kwa Ummah Wake

 

www.alhidaaya.com

 

 

Juu ya kuwa Swalaah ni nguzo muhimu kabisa katika nguzo za Kiislamu, na ni msingi wa Dini, na kama alivyosema Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) kuhusu mtu asiyeswali kwamba mwenye kuiacha amekufuru kwani baina ya mtu na shirki na ukafiri ni Swalaah, lakini Allaah (عزّ وجلّ)  Alimuitikia Nabiy Wake (صلى الله عليه وآله وسلم)  ombi lake la kupunguziwa Ummah wake Swalaah hizo kutoka khamsini kwa siku hadi tano. Na fardhi hii amefaridhishwa nayo Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم)  kutoka mbingu ya saba, jambo ambalo hakuna Nabiy yeyote aliyefadhilishwa kama hivi:

 

 

قالَ أَنَسُ بْنُ مَالِكٍ وَابْنُ حَزْمٍ قَالَ رَسُولُ اللَّهِ صلى الله عليه وسلم ‏ "‏ فَرَضَ اللَّهُ عَزَّ وَجَلَّ عَلَى أُمَّتِي خَمْسِينَ صَلاَةً فَرَجَعْتُ بِذَلِكَ حَتَّى أَمُرَّ بِمُوسَى عَلَيْهِ السَّلاَمُ فَقَالَ مَا فَرَضَ رَبُّكَ عَلَى أُمَّتِكَ قُلْتُ فَرَضَ عَلَيْهِمْ خَمْسِينَ صَلاَةً ‏.‏ قَالَ لِي مُوسَى فَرَاجِعْ رَبَّكَ عَزَّ وَجَلَّ فَإِنَّ أُمَّتَكَ لاَ تُطِيقُ ذَلِكَ ‏.‏ فَرَاجَعْتُ رَبِّي عَزَّ وَجَلَّ فَوَضَعَ شَطْرَهَا فَرَجَعْتُ إِلَى مُوسَى فَأَخْبَرْتُهُ فَقَالَ رَاجِعْ رَبَّكَ فَإِنَّ أُمَّتَكَ لاَ تُطِيقُ ذَلِكَ ‏.‏ فَرَاجَعْتُ رَبِّي عَزَّ وَجَلَّ فَقَالَ هِيَ خَمْسٌ وَهِيَ خَمْسُونَ لاَ يُبَدَّلُ الْقَوْلُ لَدَىَّ ‏.‏ فَرَجَعْتُ إِلَى مُوسَى فَقَالَ رَاجِعْ رَبَّكَ فَقُلْتُ قَدِ اسْتَحْيَيْتُ مِنْ رَبِّي عَزَّ وَجَلَّ ‏"‏ ‏.‏

 

Imepokelewa kutoka kwa Anas bin Maalik na Ibn Hazmi kwamba Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema:  “Allaah (عزّ وجلّ) Amefaridhisha kwa Ummah wangu Swalaah khamsini, nikarudi nikiwa nimezikubali mpaka nikafikia kwa Muwsaa (عليه السلام) akauliza: Rabb wako Amefaridhisha nini kwa Ummah wako? Nikasema: Amewafaridhisha Swalaah khamsini.  Akaniambia: Rudi kwa Rabb wako Allaah (عزّ وجلّ) kwani ummah wako hawataziweza. Nikarudi kwa Rabb wangu Allaah (عزّ وجلّ) Akapunguza idadi fulani nikarudi kwa Muwsaa na kumjulisha akasema: Rejea kwa Rabb wako kwani Ummah wako hawataziweza. Nikarudi kwa Rabb wangu Allaah (عزّ وجلّ) mwisho Akasema: Hizo ni tano lakini (thawabu zake) ni khamsini; Haibadilishwi Kwangu kauli. Nikarudi kwa Muwsaa akasema: Rejea kwa Rabb wako, nikasema: Hakika ninamstahi Rabb wangu Allaah (عزّ وجلّ) [An-Nisaaiy, Ibn Maajah]

 

 



34-Sifa Na Akhlaaq Za Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم): Unyenyekevu Wake: Akimhudumia Yeyote Aliyemuomba Njiani

 

Sifa Na Akhlaaq Za Nabiy  (صلى الله عليه وآله وسلم)

34-Unyenyekevu Wake Akimhudumia Yeyote Aliyemuomba Njiani

www.alhidaaya.com

 

 

 

  عَنْ أَنَسِ بْنِ مَالِكٍ أَنَّ امْرَأَةً لَقِيَتِ النَّبِيَّ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ فِي طَرِيقٍ مِنْ طُرُقِ الْمَدِينَةِ فَقَالَتْ: يَا رَسُولَ اللَّهِ إِنَّ لِي إِلَيْكَ حَاجَةً؟ قَالَ: يَا أُمَّ فُلَانٍ اجْلِسِي فِي أَيِّ نَوَاحِي السِّكَكِ شِئْتِ أَجْلِسْ إِلَيْكِ، قَالَ: فَقَعَدَتْ فَقَعَدَ إِلَيْهَا رَسُولُ اللَّهِ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ حَتَّى قَضَتْ حَاجَتَهَا  

Kutoka kwa Anas bin Maalik (رضي الله عنه) kwamba mwanamke mmoja alikutana na Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) katika njia mojawapo ya Madiynah akasema: Ee Rasuli wa Allaah, hakika mimi nnakuhitaji jambo. Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) Akasema:  “Ee Ummu fulani, kaa kitako upande wowote ule wa njia nami nitakaa pamoja nawe.”  Anas akasema:  Akakaa kitakao, naye Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) akakaa kitako (akamsikiliza) hadi akamtimizia haja yake.” [Abuu Daawuwd, ameisahihisha Al-Albaaniy  - Swahiyh Abiy Daawuwd (4818),  Swahiyh Al-Jaami’ (7857)]

 

 



Jumanne, 1 Oktoba 2019

Husnul Khuluq (Tabia Njema)



Sifa njema zote Anastahiki Allaah Mola wa viumbe wote na rehma na amani zimfikie Mtume wetu Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam), Jamaa na Swahaba zake wote.


Hivi unajua ndugu yangu Muislam, Allaah Akulinde na Akuhifadhi, kwamba 'amali iliyo bora zaidi na inayopendwa na Allaah Mtukufu na Mtume wake ni tabia njema?

Katika Hadiyth sahihi: Kutoka kwa Sa'ad bin Abiy Waqqaas (Radhiya Allaahu 'anhu) amesema Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam): "Hakika Allaah Anapenda tabia njema na Anachukia tabia mbaya"

Na tabia njema tumefahamishwa kuwa ni ukunjufu wa uso kutenda wema  na kujizuia na maovu." 
     
Hakika sisi Waislam wa zama hizi tumo katika tatizo kubwa la tabia, tabia za Kiislam ambazo watu wengi wa kheri wamezikosa, na zimekua kwa baadhi yao ni kama mazungumzo ya kawaida na wala hazihitaji kutekelezwa.

Tabia njema zinauweka Uislam kwenye daraja ya juu kabisa. Je, Hujui kwamba Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: "Kwa hakika nimeletwa ili nikamilishe tabia njema" kulingana na maneno haya inaonyesha Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amekusanya umuhimu wote alIokuja nao kwa jambo la tabia njema na Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) Akamsifu Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) katika Qur-aan Tukufu: Amesema:

"Kwa hakika una tabia njema mno" Qur-aaan 68:4

Kwa hakika yamethibiti mambo matukufu makubwa kutokana na tabia njema, baadhi ya mambo hayo ni:

1- Wema haupatikani ila kwa tabia njema, kasema Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) katika hadithi ilyopokelewa na Nawwaas bin Sam'aan (Radhiya Allaahu 'anhu): "Wema ni tabia njema na dhambi "uovu" Ni ile iliyojificha kwenye moyo (inakutia wahka) ukachukia watu wajue. (Imepokelewa na Muslim)

2- Na tabia njema ni 'amali itakayo mpelekea mtu kuingia peponi kwa wingi kama aliyvosema Mtume(Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) katika Hadiyth iliyopokewa na Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu 'anhu) Amesema: Na aliulizwa ni kitu gani kitakachowaingiza watu kwa wingi peponi? Akasema: "Kumcha Allaah na tabia njema" Na akaulizwa tena ni kitu gani kitakachowaingiza watu wengi kwa wingi motoni? Akasema "kinywa (mdomo) na utupu. (Imepokelewa na At-Tirmidhiy na akasema Hadiyth nzuri na sahihi)

3- Tabia njema ni katika 'amali nzito atakayoikuta Muislam katika miradi ya matendo yake siku ya Qiyaama.

Katika Hadiyth iliyopokelewa na Abu Dardaa (Radhiya Allaahu 'anhu), Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) kasema: "Hakuna kitu kizito katika mizani ya Muumin siku ya Qiyaama kuliko tabia njema. Hakika Allaah Humchukia mtu muovu mwenye tabia mbaya." (Imepokelewa na At-Tirmidhiy, na ni Hadiyth Hasan)

4- Mwenye kujipamba na kusifika na tabia njema  Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amemdhamini nyumba katika pepo ya juu kabisa.
Kama ilivyopokewa kutoka kwa Abu Umaamah (Radhiya Allaahu 'anhu) kuwa Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: "Mimi ni mdhamini wa nyumba "iliyopo" katikati ya pepo kwa yule mwenye kuacha mijadala (ubishani) japo akiwa ana haki, Na nitakua mdhamini wa nyumba katika pepo ya juu kwa mwenye Tabia njema."

5- Imepokelewa kutoka kwa mama wa waumini 'Aaishah (Radhiya Allaahu 'anha) akisema, nimemsikia Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akisema: "Hakika Muumin hupata kwa tabia yake njema daraja za aliyefunga na anayesimama usiku kufanya ibada."

6- Katika Hadiyth waliyoafikiana ma-Imaam Al-Bukhaariy na Muslim kutoka kwa 'Abdullaah bin Amru bnil-'Aaswi (Radhiya Allaahu 'anhuma) amesema, alikuwa Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akisema "Hakika aliye bora kati yenu ni yule mwenye tabia njema"

Hakika mwenye tabia mbaya ni mwenye kuzungumza maneno mabaya na vilevile Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) anasema: "Hakika Allaah Huwarehemu waja wake wenye huruma, basi wahurumieni walio katika ardhi na Atawahurumia aliye mbinguni"

Hivyo basi, tabia njema inafuatana na kuhurumiana na Iymaan iliyokamilika.

Mwenye kuangalia hali ya hivi sasa utakuta ni mtihani kwetu na mbele ya Allaah (Subhanahu wa Ta'ala), utaona mambo ya ajabu, utaona uongo badala ya ukweli, utaona nguvu zikitumika badala ya upole, utaona khiyana badala ya uaminifu, utaona ghadhabu badala ya subira na kuondosha ghadhabu na kusameheana baina ya watu, utaona maudhi badala ya hisani, utaona ubakhili badala ya ukarimu, utaona uchoyo katika kuchukua sehemu ya kukaa au kufanya ibada, au katika vinywaji au chakula, badala ya kuathirika na kuwatanguliza wengine kabla yake, utaona kiburi badala ya unyenyekevu, kisha mtu atajiuliza katika nafsi yake hivi hawa ni Waislam kweli? Uko wapi uchaji Allaah? Iko wapi Iymaan? Kuko wapi kuoneana hayaa? Iko wapi huruma kwa maskini, yako wapi mapenzi na huruma  kati ya Waislam???

Je, tuwafanye nini watu hawa? Tuwalipe uovu kwa uovu tukawaadhibu hapo hapo? Tukifanya hivyo hatutowazuia kitu, bali tutakuwa tumeshirikiana nao katika kueneza tabia mbaya. Lililo wajibu kwetu mimi na wewe juu ya watu hawa ni kufuata muongozo wa Allaah Mtukufu, nao ni; kuwasamehe na kufuta kabisa nyoyoni mwetu yale wanayotufanyia, na kubadilisha baya kwa kutenda jema na Allaah Mtukufu Anasema:

Na wazuiao ghadhabu zao na kuwasamehe watu na Allaah Anawapenda wafanyao hisani" Qur-aan 3:134

Na Akasema tena Allaah Mtukufu kuwasifu waumini:
"Na wakayaondoa maovu kwa mema, hao ndio watakaopata malipo "mema" ya nyumba ya Aakhirah" Qur-aan 13:22

Na Amesema Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala):
"
Na wala haulingani sawa wema na uovu. Lipiza (uovu ulilotendewa) kwa ambalo ni zuri zaidi; tahamaki yule ambaye baina yako na baina yake kuna uadui, atakuwa kama ni rafiki mwandani.
." Qur-aan 41:34

Na Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: katika Hadiyth iliyopokewa na Abu Dharr Jundub bin Junaadah na Abu Abdur-Rahmaan Mu'aadh bin Jabal (Radhiya Allaahu 'anhum) kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) kuwa kasema " Muogope Allaah popote ulipo, na lifutishe ovu (baya) kwa jema, na tangamana na watu kwa tabia zilizo njema

Na hakika Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) Amesema: "Hakika ya mema yanaondosha mabaya". Qur-aan 11:114

Pamoja na hayo yote Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) hakulipiza kisasi kwa maudhi aliyofanyiwa yeye binafsi, ila yatakapovunjwa maamrisho ya Allaah au makatazo (maharamisho) Basi huadhibu kwa ajili ya Allaah.

ALLAH ATUWAFIQISHE KWA ANAYOYAPENDA NA KUYARIDHIA NA AJAALIE TUWE WENYE KUYAFANYA YALIO MEMA. AAMIIN.

WA ALLAHU A'LAM


Jumatatu, 30 Septemba 2019

Facebook Au Fitnah-Book?

Kwanza kabisa, ijulikane wazi kwamba kusudio la makala hii si kutoa fatwa wala hukumu. Lengo ni kuweka wazi manufaa na madhara ya Facebook ili mtu binafsi atoe hukumu yake mwenyewe.
Je, ni Facebook au Fitnabook? Hili ni suali ambalo watu wengi wameanza kujiuliza baada ya kujionea vitimbi na kashfa kadhaa katika huu mtandao ambao unazidi kujipatia umaarufu kila pembe ya dunia. Naam, kuna vitimbi kadhaa vinafanyika kwa jina la Facebook. Na ndio kuna vijana wengi ambao wametumbikia katika janga la fitna katika Facebook lakini nini suluhisho la hili?
Kabla hatujatazama hebu kwanza tuangalie manufaa na madhara ya Facebook.

Manufaa
Kama ilivyo kawaida ya vitu vingi, Facebook ina faida yake. Lakini je, hizo faida ni nyingi kuliko madhara? Katika sehemu hii tutaja manufaa ambayo yanasemwa na watumiaji wa Facebook. Manufaa hayo ni kama yafuatayo:
1. Kufanya Da’wah (kuwalingania watu kwenye Uislam)
Madaa’iyah kadhaa pamoja na baadhi ya Mashaykh hutumia Facebook kwa kazi za da’wah. Huwekwa na kutumwa vitu mbalimbali vya kufikisha mafunzo mbalimbali ya Dini kama: mawaidha, makala za Kiislamu na njia mbalimbali za kunufaisha wasomaji.

2. Kutangaza shughuli na harakati za Kiislam
Mambo mbalimbali yanayowahusu Waislamu mara nyingi huwa yanatangaziwa kwa kutumia Facebook.

Madhara
Ijapokuwa kunaonekana kuna baadhi ya manufaa kadhaa juu ya utumiaji wa Facebook, kuna madhara mengi na fitnah nyingi hupatikana humo, kadhalika watu wengi wanaitumia kwa njia mbaya. Katika madhara ya Facebook ni haya:

1. Kukashifiwa Mtume na Uislam.
Kubwa zaidi na baya zaidi na la hatari zaidi, ni hili lililotokea siku za nyuma, la kukashiwa kwa Mtume kwenye Facebook, jambo ambalo limewasikitisha wengi wetu na tuna kila haki ya kuhuzunika juu ya hilo. Picha mbalimbali za kashfa na za kumlinganisha Mtume wetu mtukufu Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na mambo maovu na machafu, zimewekwa huko kwa kuchorwa vikatuni vinavyodaiwa kuwa ni yeye. Na yamejitokeza makundi tofauti yaliyoungana huko kwenye Facebook ili kuukashifu Uislamu na Waislamu na kumdhalilisha Mtume wetu (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam). Haya yote ni matunda ya hiyo Facebook.

2. Kuweka mapicha na kujitangaza na kujionesha na zaidi ni Riyaa ima kwa kukusudia au kutojitambua. Haya yanafanywa hata na wanaoonekana wana elimu ya Dini kama Madu’aat na Masheikh.

3. Mchanganyiko wa wanaume na wanawake.
Ada kuu iliyoshamiri na kuenea kati ya watumiaji ya Facebook ni kutazama na kuongea na watu wasio Mahram zao.

4. Utakuta hata wanaojiita Madu'aat au kujinasibisha na ulinganiaji, wanapiga soga na wanawake wasio mahram zao, kuwepo mapicha ya wanawake tena yasiyo na stara na wakiwa ni marafiki wa hao Madu'aat!! Wa Allaahul Musta'aan.

5. Mijadala isiyo na tija. Kunazuka mijadala mingi ya kiitikadi, kimadhehebu na mfano wake, na makundi potofu na watu wa bid'ah na hawaa. Matokeo ni ubishi usio na tija na hakuna faida inayopatikana, ila kinachoshuhudiwa aghlabu ni matusi na kukufurishana.

6. Kupoteza muda kwa mambo ya upuuzi.
Watu wengi hasa vijana hupoteza masaa juu ya Facebook wakati wangeliutumia muda ule kwa kufanya kitu cha muhimu

7. Kutokuwepo kwa hayaa na heshima.
Uislamu umekuja kulinda heshima ya binaadam lakini cha ajabu vijana wengi wa Kiislamu hutokwa na hayaa na huvuruga heshima zao kupitia Facebook. Wasichana wangapi wameweka picha zao bila ya hijaab kwenye Facebook kwa kutaka kujionyesha? Wanawake wangapi wameharibu heshima zao na za familia zao kwa kutuma maasi yao kwenye Facebook?

Suluhisho
Baada ya kujionea na kutafakari juu ya madhara na manufaa yaliyomo kwenye Facebook, lilobakia ni kujiamulia mwenyewe. Ikiwa utaona kwamba Facebook madhara yake ni makubwa kuliko faida, basi ni juu yako kujihadhari juu ya kuitumia na bora zaidi kujiepusha nayo.
Ikiwa utaona kwamba manufaa yamezidi basi ni pia juu yako kujichunga na madhara yaliyomo huko. Inawezekana kitu ukakiona kina manufaa kadhaa lakini madhara yake ni mengi zaidi. Allaah Anasema kuhusu ulevi na kamari

يَسْأَلُونَكَ عَنِ الْخَمْرِ وَالْمَيْسِرِ قُلْ فِيهِمَا إِثْمٌ كَبِيرٌ وَمَنَافِعُ لِلنَّاسِ وَإِثْمُهُمَآ أَكْبَرُ مِن نَّفْعِهِمَا
Wanakuuliza kuhusu ulevi na kamari, sema ndani yake yamo madhara mengi na manufaa kwa watu, lakini madhara ni makubwa kuliko manufaa.”  [Al-Baqarah 2: 219]
Isitoshe, pahala ambapo anatukanwa Allaah au Mtume Wake, au Qur-aan au Sunnah au jambo lolote la Dini, basi sehemu hiyo inapaswa kuhamwa au kutengwa hadi itakapojirudi au kuomba radhi na kubadili mwelekeo wako. Na ikiwa Facebook imeomba radhi kwa matendo yake ya kumtusi na kumdhalilisha Mtume wetu (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), hapo tena Muislamu ana khiyari ya kutumia ukumbi huo kwa manufaa yaliyotajwa au kuuacha na kuutenga kwa madhara yaliyoelezwa. Na bila shaka madhara na uadui waliouonyesha kwa Uislamu na Waislamu, unamtosha Muislamu kuwa mbali na ukumbi kama huo au mwengine wowote unaofanana na huo.

Kwahiyo, tujihadhari, hasa katika mambo ambayo yana utata ili tuweze kulinda Dini yetu na heshima yetu.

Imeandaliwa na: Iliyaasah.


Jumamosi, 28 Septemba 2019

Majuto Ya Nafsi - 1

Utulivu Wa Nafsi (Sakiynatun-Nafs) - 3

Imekusanywa na Ukht Haliymah ‘Abdullaah




7. Muumin Anaishi Pamoja Na Urafiki (Suhba) Ya Manabii Na Wakweli 

Muumin hahisi kwamba ametengeka na nduguze Waumini, hakika wao ikiwa hawapo naye msikitini au nyumbani kwake daima wanaishi katika dhamira yake. Akiswali hata akiwa peke yake anaongea kwa jina lao:

“hakika Wewe Ndiye tunayekuabudu na Wewe tu Ndiye tunayekutaka msaada” Al-Faatihah: 5.

Akiomba du’aa anaomba kwa jina lao (tuongoze njia iliyonyooka), akijikumbuka nafsi yake anawakumbuka (amani iwe juu yetu na juu ya waja wema wa Allaah).

Muumin haishi na nduguze Waumini wa wakati wake tu bali anaishi na Waumini wa karne zote hata ikiwa imepita baina yao miaka anasema waliyosema watu wema:

Mola wetu! Tusamehe sisi na ndugu zetu waliotutangulia (kufa) katika Uislam.” Al-Hashr: 10.

Muumin anahisi anaishi kwa imani yake na matendo yake mema pamoja na Manabii wa Allaah na Mitume Wake. Na pamoja na kila mkweli, shahiyd, mtu mwema katika kila umma na kila zama:

“Na wenye kumtii Allaah na Mtume, basi hao watakuwa pamoja na wale Aliowaneemesha Allaah, Manabii na Mashahidi na Swaalihiyn (watu wema). Na uzuri ulioje (kwa mtu) watu hao kuwa rafiki (zake). An-Nisaa: 69.

Ni nani ana furaha zaidi ya yule anayefungamana na hawa? Mafungamano haya si ya kimwili na sura tu bali ni mafungamano ya kiroho, kifikra na kimoyo.


8. Swalah Na Du’aa Ni Vinavyopelekea Utulivu  

Katika sababu ya utulivu wa nafsi ambayo wamenyimwa wenye kuabudia mali wakaneemeshwa nayo Waumini wakawa wanaongea na Mola wao kila siku katika Swalah na dua …

Swalah ni fursa ya mtu kuisafisha nafsi yake na shughuli za kidunia asimame mbele ya Mola wake kwa kumtukuza hali akimuomba. Katika kuwasiliana na Allaah (katika Swalah) kunaipa nafsi nguvu na matumaini kwa roho nayo ni silaha ya Muumin anayoitumia katika vita vya kimaisha na kupambana na balaa zake na vyenye kutia uchungu. Anasema Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala):

“Enyi mlioamini jisaidieni (katika mambo yenu) kwa subira na Swalah, bila shaka Allaah yu pamoja na wanaosubiri.” Al-Baqarah: 153.

Alikuwa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) likimtingisha jambo lolote anakimbilia Swalah na haikuwa Swalah yake ni picha tu bali ilikuwa ni katika kuwa faragha na kunong’ona na Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala), mpaka ikawa ikifika wakati wa Swalah anamwambia muadhini wake Bilaal (Radhiya Allaah ‘anhu):

“Tufurahishe kwayo ewe Bilaal”
na alikuwa akisema,

“Nimejaaliwa kitulizo cha macho yangu katika Swalah”.

Anasema Deen Carnegie katika kitabu chake ‘Acha yanayokutatiza na uanze maisha’:

“…Swalah inakuhakikishia mambo matatu haijalishi uwe ni Muumin au Mulhid (anayeitoa kasoro dini na kutoiamini).

1.     Swalah ni usaidizi katika kuelezea yanayoshughulisha nafsi yako na yaliyo mazito, wamebainisha wema waliopita kwamba haiwezekani kukabiliana na tatizo ambalo halijulikani, Swalah ni sawa na kitabu ambayo anaelezea mwenye fani ya Adab (Adiyb)  matatizo yake (humuum), tukitaka suluhisho la matatizo yetu ni wajibu kwetu iwe wazi katika ndimi zetu na hivi ndivyo tunavyofanya tukimuelezea matatizo yetu Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala).

2.     Swalah inakufanya uhisi huko peke yako katika kutatua matatizo yako na yanayokuhuzunisha (humuum), mara nyingi matatizo yatukutayo ya kibinafsi tunashindwa kuwaelezea hata watu walio karibu yetu lakini kwa mapana tunamuelezea Allaah ‘Azza wa Jalla katika Swalah.


Madaktari wa nafsi wanakubaliana kwamba tiba ya maradhi ya kinafsi (Tawaatur Al-‘Aaswab) kwa kuwaelezea marafiki wa karibu sana na ndugu mpenzi sababu ya matatizo uliyonayo, tusipopata wa kumueleza anatutosha Allaah kuwa msaidizi wetu.

3.     Swalah ni hatua ya mwanzo kuiendea kazi. Inawezekana mtu akawa anaswali siku baada ya siku bila ya kupata faida yaani haiboreshi hali yake na kutatua yamkumbayo.

Ikiwa hii ni hali ya Swalah kwa ujumla (kwa wasio Waislamu) basi Swalah katika Uislamu ina athari zaidi ya hivi ndani yake kuna twahara inayochangamsha mwili, Qur-aan isomwayo nacho ni Kitabu cha kudumu, kuhuisha jama’ah ambayo imesisitiza na kuhimiza Uislam.

Utulivu ulioje anaohisi Muumin pindi anapomwelekea Mola wake wakati wa matatizo na siku ya shida anamuomba kama alivyoomba Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam):

“Ewe Allaah, Mola wa mbingu saba, na Mola wa ‘arshi tukufu, Mola wetu na Mola wa kila kitu, Mwenye kuichanua tembe ya mbegu na kokwa, na Aliyeteremsha Tawraat na Injiyl na Qur-aan, najikinga Kwako kutokana na shari ya kila kitu, Wewe Ndiye mwenye kukamata utosi wake, Ewe Allaah Wewe Ndiye wa mwanzo, hakuna kabla Yako kitu, na Wewe Ndiye uliye wazi, hakuna juu yako kitu chochote, na Wewe Ndiye uliyefichika, hakuna kilichojificha chini Yako, tulipie madeni yetu, na utuepushe na ufakiri.” Muslim

Dokezo: Du’aa hii pia ni katika du’aa za kusoma wakati wa kulala usiku ipo katika kitabu kidogo cha du’aa ‘Hiswnul Muslim.’

Na ni ipi matumaini kama aliyoshushiwa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) moyoni mwake alipokuwa anarudi kutoka Twaaif miguu miwili ikiwa inavuja damu, amejeruhiwa moyo kutokana na mabaya aliyokumbana nayo kwa watu hao, haikuwa kwake ila kunyanyua mikono yake mbinguni huku moyo wake ukiwa baridi na salama na kusema:

“Ewe Allaah mimi nashtakia udhaifu wa moyo wangu na uchache wa hila yangu na kudharauliwa na watu. Ewe mwenye kurehemu mwingi wa rehma, Wewe Ndiye Mola wa wenye kutiwa udhaifu (Mustadhw’afiyn), nawe Ndiye Mola wangu…”


9. Muumin Haishi Baina Ya ‘Lau’ Na ‘Layta’

Sababu kubwa ya matatizo (Qalaq) ambayo anakosa mwanaadamu utulivu wa nafsi, amani, radhi ni kujutia wakati uliopita na kukasirikia wakati uliopo na khofu ya wakati ujao.

Baadhi ya watu inawashukia misiba anabaki nayo miezi na miaka anajikumbushia maumivu yake wakati mwengine akijuta na wakati mwengine akiwa na matumaini laiti ningefanya, laiti ningeacha, lau ningefanya vile ingekuwa hivi.

Madaktari wa nafsi wao pamoja na waelekezaji wa kijamii na watu wa malezi na kazi, wanatoa nasaha kwamba mwanaadamu asahau maumivu yaliyopita na aishi sanjari na wakati uliopo Kwani wakati uliopita haurudi.

Udhaifu wa mwanaadamu unawakumba wengi unawajaalia watwange unga uliokwishatwangwa wanalilia wakati uliopita wanang’ata vidole vyao kujutia yaliyopita. Muumin wa kweli amesalimika na hisia hizi Kwani anaamini Uwezo na makadirio ya Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) hajisalimishi nafsi yake kutokana na matukio yaliopita anaitakidi kwamba jambo Analotaka Allaah  huwa.

Muumin anaelewa Alilokadiria Allaah huwa hivyo, kwanini akasirike?
Anasema Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala):

“Hautokei msiba katika ardhi wala katika nafsi zenu ila umekwishaandikwa katika Kitabu (cha Allaah) kabla Hatujaumba. Kwa yakini hilo ni sahali kwa Allaah.
“Ili msihuzunike sana juu ya kitu kilichokupoteeni (na kinachokupoteeni), wala msifurahi sana kwa Alichokupeni (na kwa Anachokupeni). Na Allaah Hampendi kila ajivunaye,ajifakharishaye.” Al-Hadiyd: 22-23.

Katika vita vya Uhud ambapo waliuawa Waislamu sabini, Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) Alielezea hali za wanafiki wenye maradhi ya moyo na madhaifu wa imani walioishi baina ya ‘lau’ na kujutia kwa kusema ‘layta’ laiti..

“Na kulikuwa kundi jingine nafsi zao zimewashughulisha (hawajijui hawajitambui); wakimdhania Allaah dhana zisizokuwa ndizo, dhana za ujinga; wakisema “Ah! Tuna amri sisi katika jambo hili?” Sema: “Mambo yote ni ya Allaah. Wanaficha katika roho zao (hao wanafiki) wasiyokubainishia. Wanasema: “Tungekuwa na chochote katika jambo hili tusingeuawa hapa”. Sema: “Hata mngalikuwa majumbani mwenu, basi wangelitoka wale walioandikiwa kufa, wakenda mahali pao pa kuangukia wafe.” Al-‘Imraan: 154.

Akawarudi (Allaah) hao waliowaambia Ndugu zao hali wao hawakwenda:

“Wale waliosema juu ya Ndugu zao na (wao wenyewe) wamekataa kwenda (hawakwenda) vitani: “Wangalitutii wasingeuawa.” Sema: “Jiondoleeni mauti (nyinyi wenyewe msife maisha) ikiwa mnasema kweli.”  Al-‘Imraan: 168.


Muumin hawi kama hawa wanafiki wala Ndugu zake makafiri ambao Qur-aan imekataza kujifananisha nao katika kujuta kwao na matamanio yao ya kihuzuni.

Anasema Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala):

“Enyi mlioamini! Msiwe kama wale waliokufuru na wakasema juu ya Ndugu zao waliposafiri katika nchi au walipopigana (wakafa): “Wangalikuwa kwetu wasingalikufa wala wasingaliuawa.” (Amewatia Allaah dhana hii) ili Afanye hayo kuwa majuto katika nyoyo zao. Na Allaah Anahuisha na kufisha na Allaah Anaona yote mnayotenda.
“Na kama mkiuawa katika njia ya Allaah au mkifa (si khasara kwenu) Kwani msamaha na rehema zinatoka kwa Allaah (kukujieni) ni bora kuliko vile wanavyokusanya (hapa ulimwenguni.” Al-‘Imraan: 156-157.

Alama (shi’aar) ya Muumin daima ni kusema “Amekadiria Allaah na Analotaka huwa, Namshukuru Allaah kwa kila hali”. Na kwa hilo hatajutia yaliyopita wala haishi kwa kukumbukia machungu inamtosha kusoma neno lake Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala):

“Haufiki msiba wowote ila kwa idhini ya Allaah, na anayemuamini Allaah Huuongoza moyo wake (kwendea maliwaza mazuri). Na Allaah ni Mjuzi wa kila kitu.” At-Taghaabun: 11. 


WabiLlaahi At-Tawfiyq               


20-Hakika Shirki Ni Dhulma Kubwa Mno! - Isti’aadhah Kwa Asiyekuwa Allaah

  إِنَّ الشِّرْكَ لَظُلْمٌ عَظِيم   Hakika Shirki Ni Dhulma Kubwa Mno!   20 - Isti’aadhah  (Kuomba Kinga) Kwa Asiyekuwa Allaah   ...