Sifa njema zote Anastahiki Allaah Mola wa viumbe wote na rehma na amani zimfikie Mtume wetu Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam), Jamaa na Swahaba zake wote.
Hivi unajua ndugu yangu Muislam, Allaah Akulinde na Akuhifadhi, kwamba 'amali iliyo bora zaidi na inayopendwa na Allaah Mtukufu na Mtume wake ni tabia njema?
Katika Hadiyth sahihi: Kutoka kwa Sa'ad bin Abiy Waqqaas (Radhiya Allaahu 'anhu) amesema Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam): "Hakika Allaah Anapenda tabia njema na Anachukia tabia mbaya"
Na tabia njema tumefahamishwa kuwa ni ukunjufu wa uso kutenda wema na kujizuia na maovu."
Hakika sisi Waislam wa zama hizi tumo katika tatizo kubwa la tabia, tabia za Kiislam ambazo watu wengi wa kheri wamezikosa, na zimekua kwa baadhi yao ni kama mazungumzo ya kawaida na wala hazihitaji kutekelezwa.
Tabia njema zinauweka Uislam kwenye daraja ya juu kabisa. Je, Hujui kwamba Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: "Kwa hakika nimeletwa ili nikamilishe tabia njema" kulingana na maneno haya inaonyesha Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amekusanya umuhimu wote alIokuja nao kwa jambo la tabia njema na Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) Akamsifu Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) katika Qur-aan Tukufu: Amesema:
"Kwa hakika una tabia njema mno" Qur-aaan 68:4
Kwa hakika yamethibiti mambo matukufu makubwa kutokana na tabia njema, baadhi ya mambo hayo ni:
1- Wema haupatikani ila kwa tabia njema, kasema Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) katika hadithi ilyopokelewa na Nawwaas bin Sam'aan (Radhiya Allaahu 'anhu): "Wema ni tabia njema na dhambi "uovu" Ni ile iliyojificha kwenye moyo (inakutia wahka) ukachukia watu wajue. (Imepokelewa na Muslim)
2- Na tabia njema ni 'amali itakayo mpelekea mtu kuingia peponi kwa wingi kama aliyvosema Mtume(Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) katika Hadiyth iliyopokewa na Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu 'anhu) Amesema: Na aliulizwa ni kitu gani kitakachowaingiza watu kwa wingi peponi? Akasema: "Kumcha Allaah na tabia njema" Na akaulizwa tena ni kitu gani kitakachowaingiza watu wengi kwa wingi motoni? Akasema "kinywa (mdomo) na utupu. (Imepokelewa na At-Tirmidhiy na akasema Hadiyth nzuri na sahihi)
3- Tabia njema ni katika 'amali nzito atakayoikuta Muislam katika miradi ya matendo yake siku ya Qiyaama.
Katika Hadiyth iliyopokelewa na Abu Dardaa (Radhiya Allaahu 'anhu), Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) kasema: "Hakuna kitu kizito katika mizani ya Muumin siku ya Qiyaama kuliko tabia njema. Hakika Allaah Humchukia mtu muovu mwenye tabia mbaya." (Imepokelewa na At-Tirmidhiy, na ni Hadiyth Hasan)
4- Mwenye kujipamba na kusifika na tabia njema Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amemdhamini nyumba katika pepo ya juu kabisa.
Kama ilivyopokewa kutoka kwa Abu Umaamah (Radhiya Allaahu 'anhu) kuwa Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: "Mimi ni mdhamini wa nyumba "iliyopo" katikati ya pepo kwa yule mwenye kuacha mijadala (ubishani) japo akiwa ana haki, Na nitakua mdhamini wa nyumba katika pepo ya juu kwa mwenye Tabia njema."
5- Imepokelewa kutoka kwa mama wa waumini 'Aaishah (Radhiya Allaahu 'anha) akisema, nimemsikia Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akisema: "Hakika Muumin hupata kwa tabia yake njema daraja za aliyefunga na anayesimama usiku kufanya ibada."
6- Katika Hadiyth waliyoafikiana ma-Imaam Al-Bukhaariy na Muslim kutoka kwa 'Abdullaah bin Amru bnil-'Aaswi (Radhiya Allaahu 'anhuma) amesema, alikuwa Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akisema "Hakika aliye bora kati yenu ni yule mwenye tabia njema"
Hakika mwenye tabia mbaya ni mwenye kuzungumza maneno mabaya na vilevile Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) anasema: "Hakika Allaah Huwarehemu waja wake wenye huruma, basi wahurumieni walio katika ardhi na Atawahurumia aliye mbinguni"
Hivyo basi, tabia njema inafuatana na kuhurumiana na Iymaan iliyokamilika.
Mwenye kuangalia hali ya hivi sasa utakuta ni mtihani kwetu na mbele ya Allaah (Subhanahu wa Ta'ala), utaona mambo ya ajabu, utaona uongo badala ya ukweli, utaona nguvu zikitumika badala ya upole, utaona khiyana badala ya uaminifu, utaona ghadhabu badala ya subira na kuondosha ghadhabu na kusameheana baina ya watu, utaona maudhi badala ya hisani, utaona ubakhili badala ya ukarimu, utaona uchoyo katika kuchukua sehemu ya kukaa au kufanya ibada, au katika vinywaji au chakula, badala ya kuathirika na kuwatanguliza wengine kabla yake, utaona kiburi badala ya unyenyekevu, kisha mtu atajiuliza katika nafsi yake hivi hawa ni Waislam kweli? Uko wapi uchaji Allaah? Iko wapi Iymaan? Kuko wapi kuoneana hayaa? Iko wapi huruma kwa maskini, yako wapi mapenzi na huruma kati ya Waislam???
Je, tuwafanye nini watu hawa? Tuwalipe uovu kwa uovu tukawaadhibu hapo hapo? Tukifanya hivyo hatutowazuia kitu, bali tutakuwa tumeshirikiana nao katika kueneza tabia mbaya. Lililo wajibu kwetu mimi na wewe juu ya watu hawa ni kufuata muongozo wa Allaah Mtukufu, nao ni; kuwasamehe na kufuta kabisa nyoyoni mwetu yale wanayotufanyia, na kubadilisha baya kwa kutenda jema na Allaah Mtukufu Anasema:
Na wazuiao ghadhabu zao na kuwasamehe watu na Allaah Anawapenda wafanyao hisani" Qur-aan 3:134
Na Akasema tena Allaah Mtukufu kuwasifu waumini:
"Na wakayaondoa maovu kwa mema, hao ndio watakaopata malipo "mema" ya nyumba ya Aakhirah" Qur-aan 13:22
Na Amesema Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala):
"
Na wala haulingani sawa wema na uovu. Lipiza (uovu ulilotendewa) kwa ambalo ni zuri zaidi; tahamaki yule ambaye baina yako na baina yake kuna uadui, atakuwa kama ni rafiki mwandani.
|
." Qur-aan 41:34
Na Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: katika Hadiyth iliyopokewa na Abu Dharr Jundub bin Junaadah na Abu Abdur-Rahmaan Mu'aadh bin Jabal (Radhiya Allaahu 'anhum) kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) kuwa kasema " Muogope Allaah popote ulipo, na lifutishe ovu (baya) kwa jema, na tangamana na watu kwa tabia zilizo njema
Na hakika Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) Amesema: "Hakika ya mema yanaondosha mabaya". Qur-aan 11:114
Pamoja na hayo yote Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) hakulipiza kisasi kwa maudhi aliyofanyiwa yeye binafsi, ila yatakapovunjwa maamrisho ya Allaah au makatazo (maharamisho) Basi huadhibu kwa ajili ya Allaah.
ALLAH ATUWAFIQISHE KWA ANAYOYAPENDA NA KUYARIDHIA NA AJAALIE TUWE WENYE KUYAFANYA YALIO MEMA. AAMIIN.
WA ALLAHU A'LAM
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni