Translate

Ijumaa, 27 Septemba 2019

Utulivu Wa Nafsi (Sakiynatun-Nafs) - 1

Imekusanywa na Ukht Haliymah ‘Abdullaah


Anasema Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala):

“Yeye ndiye Aliyeshusha utulivu katika nyoyo za waumini ili waongezeke imani juu ya imani yao.”Al-Fath: 4.

Anasema mmoja wa daktari mashuhuri Marekani, “Nilipokuwa kijana niliweka ratiba ya vitu vizuri vinavyokubalika katika maisha, nikaandika hali nimejawa na matamanio ya kidunia, navyo ni: afya, mapenzi, ujuzi (kipaji), nguvu, utajiri, umashuhuri. Nikampelekea mzee mwenye hekima.

“Akaniambia huyo mzee, ratiba nzuri imepangika vilivyo lakini inaonesha umesahau kipengele muhimu akapiga mstari katika ratiba yote na kuandika maneno mawili ‘Utulivu (wa) Nafsi’.

Akasema hii ni zawadi ambayo Anamhifadhia Allaah Aliyemchagua (katika waja wake) Anawapa wengi akili na afya, mali, ama utulivu wa nafsi , Anatoa kwa kukadiria.

“Akasema: haya nisemayo si mawazo yangu ila nimenakili kutoka kwa wenye hekima wanasema: (Ewe mola acha neema ya dunia chini ya miguu ya wajinga, na unipe moyo usiotetereka (usiotatizika).

“Niliona tabu wakati huo kukubali hayo, lakini sasa baada ya nusu karne nimekiri katika majaribio niliyopitia na mazingatio niliyopata, nimejua utulivu wa nafsi ndio lengo la mwongozo wa maisha yenye kupigiwa mfano, na mimi nimejua sasa jumla ya mambo mengine sio lazima yampatie mtu utulivu, nimeona utulivu huu unachanua bila usaidizi wa mali, wala afya. Katika nguvu za utulivu inabadilisha banda kuwa kasri, ama kunyimwa utulivu inabadilisha kasri la mfalme kuwa kiota.”


Haya ni maneno ya mtu anayeishi Marekani nchi ya starehe na utajiri, nchi ya uhuru kufanya utakacho. Anayasema haya baada kupitia maisha, hakupata katika maisha neema bora na ghali kama utulivu wa nafsi.


HAKUNA UTULIVU BILA IMANI

Utulivu wa nafsi ndio chimbuko la furaha (sa’ada), vipi itafikiwa ikiwa haitokani na akili wala elimu, afya, nguvu, mali, utajiri, umashuhuri, wala neema nyingine ya kimaisha.

Jibu lenye matumaini ni Kumuamini Allaah na siku ya mwisho.

Imetufundisha maisha kwamba watu wengi wenye wasiwasi, kukosa msimamo, hisia za upungufu na kupotea ni walionyimwa neema ya imani na yakini.

Utulivu huu ni matunda ya daraja za Imani na Tawhiyd.

Anashusha Allaah (Subhaanah wa Ta’ala) katika mioyo ya waumini waliopo duniani wawe na msimamo watakapopata matatizo watu, waridhike watakapokasirika watu, wawe na yakini watakapotilia shaka watu, wasubiri watakapotetereka watu, wawe wapole watakapokuwa wajinga.

Utulivu huu ndio uliojaa moyo wa Mtume (Swalla Allahu ‘alayhi wa sallam) siku aliyohama. Anasema Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala):

“…basi Allaah Alimnusuru walipomtoa wale waliokufuru, alipokuwa (mmoja tu na mwenziwe) wa pili wake, (peke yao) walipokuwa wote wawili katika pango, (Mtume) alipomwambia sahibu yake, usihuzunike kwa yakini Allaah Yu pamoja nasi.” At-Tawbah: 40

Ulimpata uoga Abu Bakr (Radhiya Allaahu ‘anhu) juu ya Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) na uendelevu wa Da’awah na kusema, “Ewe Mtume wa Allaah lau mmoja wao akitizama chini atatuona.” Akasema Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam), “unafikiria nini wawili watatu wao Allaah.”


SABABU ZA UTULIVU KWA MUUMINI

1.    Muumin Kuutikia Wito Kimaumbile

Mwanzo wa sababu ya utulivu kwa Muumin ni kwamba ameongozwa katika umbile Alilomuumba nalo Allaah, linaloshikamana na kuwepo kwake na kumuwezesha kuishi kwa amani na upendo sio ugomvi na vita.

Anasema Ibnul Qayyim (Rahimahu Allaah) katika kitabu chake Madaarij As-Saalikiyn:
“Katika moyo kuna mtawanyiko (sha’itha) huwezi kukusanya ila kuelekea kwa Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala). Na kuna ubaya hauondoki ila kujibembeleza kwa Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala). Na kuna huzuni haiondoki ila kufurahika kwa kumjua (Allaah), kuwa mkweli katika matendo.

Na kuna wasiwasi hautotulia ila kwa kukutana Naye na Kuwa kimbilio lako.
Na kuna moto wa majuto hauzimiki ila kwa kuridhia Amri Yake, makatazo, na Qadhwaa Yake, na kuikumbatia subra juu ya hilo mpaka utakapokutana Naye.

Na kuna uwazi hauzibiki ila kwa kumpenda, kurejea Kwake na kumtaja daima, ukweli wa kumtakasa. Lau mtu atapewa dunia na vilivyomo hautoziba huo uwazi.”


Hilo ndilo umbile la mwanaadamu la asili hapati utulivu ila kwa kumfuata Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala), kumuamini na kumuelekea.
Ni umbile (fitwrah) walilokiri washirikina enzi za ujahiliya. Anasema Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala):

“Na kama ukiwauliza, ni nani aliyeumba mbingu na ardhi na akalitiisha jua na mwezi? Bila shaka watasema, Allaah. Wapi basi wanakogeuziwa?”Al-‘Ankabuut: 61.

Akipatwa mwanaadamu na shida mara anamkimbilia Allaah kisha akiondoshewa matatizo anamsahau kama vile hakumuomba.

Kwa ajili ya kupata utulivu huu ikawa kazi ya Mitume kuamrisha ‘Ibaada ya Allaah na kujiepusha na twaaquut.


2.    Muumin Kuongoka Kutokana Na Siri Ya Kuwepo Duniani

Ndani ya kila mwanaadamu kuna sauti iliyojificha inamuita, na maswali yanayompitia kutaka jawabu litakalomuondoshea hofu na kumtuliza nafsi, ni nini ulimwengu? Nani mwanaadamu, amekuja kutoka wapi? Nani kamtengeneza? Nani anamsimamia mambo yake? Nini lengo lake? Vipi ameanza na ataishia vipi? Ni nini maisha na mauti? Ni nini kinamsubiri baada ya maisha haya? Je, inapatikana kitu baada ya maisha haya? Na ni nini uhusiano wake na kudumu (al-khuluud)?

Maswali haya yaliyomsumbua mwanadamu tangu kuumbwa kwake mpaka yatakapomalizika maisha hayakupata na hayatopata majibu yanayotosheleza ila katika Dini.

Uislam ndio Dini bora inayotupa majibu.

Qur-aan imeeleza kwamba hii dini ni ya kimaumbile, Anasema Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala):

“Basi uelekeze uso wako katika Dini iliyo sawasawa ndilo umbile Allaah Alilowaumbia watu …” Ar-Ruum: 30


Itaendelea In shaa Allaah…


Alhamisi, 26 Septemba 2019

33-Fadhila Za Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم): Ana Ujira Usiokatika Anasifika Na Maarufu Mno

 

Fadhila Za  Nabiy  (صلى الله عليه وآله وسلم)

 

33-Ana Ujira Usiokatika Anasifika Na Maarufu Mno

 

www.alhidaaya.com

 

 

 

Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):

وَإِنَّ لَكَ لَأَجْرًا غَيْرَ مَمْنُونٍ ﴿٣﴾

 

Na hakika wewe bila shaka una ujira usiokatika. [Al-Qalam: 3]

 

Na Anasema pia Allaah (سبحانه وتعالى):

وَرَفَعْنَا لَكَ ذِكْرَكَ ﴿٤﴾

 

Na Tukanyanyulia juu utajo wako (ukawa mwenye kusifika mno)?  [Ash-Sharh: 4]

 

Allaah (سبحانه وتعالى)  Amemfadhilisha na kumkirimu Nabiy Wake (صلى الله عليه وآله وسلم) kwa kutajwa mno na kusifiwa na akawa maarufu ulimwenguni.  Hutajwa katika kila Adhaana ya Swalaah, katika Iqaamah, katika khutbah za Ijumaa, katika kutamka Shahaadah, na hutajwa ndani ya Swalaah na kila zinapotajwa Hadiyth zake, na anaswaliwa katika kuomba du’aa ambapo du’aa haitaqabaliwi bila ya kumswalia yeye kwanza, na huswaliwa pia inapomalizika du’aa, na katika hali nyingi mbali mbali, na Hadiyth zifuatazo zinathibitisha:

 

عن ابي سعيد الخدري رضي الله عنه ان رسول الله صلى الله عليه وسلم قال: أتاني جبريلُ فقال: إنَّ ربِّي وربَّك يقولُ لك: كيف رفَعْتُ ذِكْرَك ؟ قال: اللهُ أعلَمُ قال: إذا ذُكِرْتُ ذُكِرْتَ معي

Imepokelewa kutoka kwa Sa’idy Al-Khudriyy (رضي الله عنه) kwamba Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema:  “Amenijia Jibriyl akasema: Hakika Rabb wangu na Rabb Wako Anasema: Vipi umenyanyuliwa juu utajo wako? Akasema: Allaah Anajua zaidi. Akasema: (Allaah Anasema): Kila nnapotajwa, nawe unatajwa pamoja nami.” [Ibn Jariyr, Ibn Abiy Haatim, Ibn Hibbaan na Ameisahihisha Al-Albaaniy katika Swahiyh Ibn Hibbaan 3382]

 

Ibn ‘Abbaas (رضي الله عنهما) amesema ) (kuhusu maana ya):  “Sitajwi isipokuwa unatajwa pamoja Nami”;  katika Adhaan, Iqaamah, Tashahhud, Siku ya Ijumaa, kwenye Minbari (khutbah), Siku ya ’Iydul-Fitwr, Siku ya ’Iydul- Adhw-haa, Ayyaamut-Tashriyq, Siku ya ’Arafah, katika Jamarah, katika Swafaa Wal Marwah, katika Khutbah za Nikaah, Mashariki ya ardhi na Magharibi, na kwamba lau mtu akamwabudu Allaah akaamini Jannah na Moto na kila kitu lakini hashuhudii  kwamba Muhammad ni Rasuli wa Allaah,  basi hakuna kitakachomfaa na atakuwa ni kafiri. [Tafsiyr Al-Qurtwubiy]

 

Naye Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema:

 ((الْبَخِيلُ مَنْ ذُكِرْتُ عِنْدَهُ فَلَمْ يُصَلِّ عَلَيَّ))

((Bakhili ni yule ambaye nikitajwa haniswalii))  [Hadiyth ya ‘Aliy bin Abi Twaalib (رضي الله عنه)   - At-Tirmidhiy (5/551) [3546], na wengineo na angalia: Swahiyh Al-Jaami’ (3/25) [2787] na Swahiyh At-Tirmidhiy (3/177)]

 



33-Sifa Na Akhlaaq Za Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم): Unyenyekevu Wake Akinyenyekea Kwa Ahli Zake

 

Sifa Na Akhlaaq Za Nabiy  (صلى الله عليه وآله وسلم)

 

33-Unyenyekevu Wake Akinyenyekea Kwa Ahli Zake

 

www.alhidaaya.com

 

 

عَنِ ابْنِ عَبَّاسٍ، عَنِ النَّبِيِّ ـ صلى الله عليه وسلم ـ قَالَ ‏ "‏ خَيْرُكُمْ خَيْرُكُمْ لأَهْلِهِ وَأَنَا خَيْرُكُمْ لأَهْلِي ‏"‏ ‏ رواه الترمذي

Imepokelewa kutoka kwa Ibn ‘Abbaas (رضي الله عنهما) kwamba Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema:  ((Mbora wenu ni yule aliye mbora kwa mke wake, na mimi ni mbora kwa watu wangu wa nyumbani [ahli])) [Ibn Maajah na Ad-Daarimiy].



103-Aayah Na Mafunzo: Allaah Anaridhia Mshikamane Kwa Kamba Yake Msifarikiane

Aayah Na Mafunzo

Aal-‘Imraan

Allaah Anaridhia Mshikamane Kwa Kamba Yake Msifarikiane

 

Alhidaaya.com

 

 

 

Anasema Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa):

 

 

وَاعْتَصِمُوا بِحَبْلِ اللَّـهِ جَمِيعًا وَلَا تَفَرَّقُوا ۚ وَاذْكُرُوا نِعْمَتَ اللَّـهِ عَلَيْكُمْ إِذْ كُنتُمْ أَعْدَاءً فَأَلَّفَ بَيْنَ قُلُوبِكُمْ فَأَصْبَحْتُم بِنِعْمَتِهِ إِخْوَانًا وَكُنتُمْ عَلَىٰ شَفَا حُفْرَةٍ مِّنَ النَّارِ فَأَنقَذَكُم مِّنْهَا ۗ كَذَٰلِكَ يُبَيِّنُ اللَّـهُ لَكُمْ آيَاتِهِ لَعَلَّكُمْ تَهْتَدُونَ ﴿١٠٣﴾ 

103. Na shikamaneni kwa kamba ya Allaah nyote pamoja, wala msifarikiane. Na kumbukeni neema ya Allaah juu yenu, pale mlipokuwa maadui (kati yenu); kisha Akaunganisha nyoyo zenu, mkawa kwa neema Yake ndugu; na mlikuwa ukingoni mwa shimo la moto Akakuokoeni humo. Hivyo ndivyo Allaah Anavyokubainishieni Aayaat Zake mpate kuongoka.

 

 

Mafunzo:

 

Abuu Hurayrah (رضي الله عنه) amehadithia kwamba Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema: “Hakika Allaah Anawaridhia mambo matatu na Anachukia kwenu mambo matatu; Anawaridhia mumwabudu Yeye, wala msimshirikishe kwa chochote, na mshikamane nyote na kamba ya Allaah wala msifarikiane. Na anachukia kwenu uvumi, kuuliza sana na   kupoteza mali.” [Muslim, na katika riwayaah: “Na muwanasihi wenye kuwatawalia mambo yenu.” Swahiyh Adaab Al-Mufrad (343)].

 

 

 



049-Asbaabun-Nuzuwl: Al-Hujuraat: 9

 أسْبابُ النُّزُول

Asbaabun-Nuzuwl

Sababu Za Kuteremshwa (Baadhi Ya  Suwrah Na Aayaat Za Qur-aan)

 

Imekusanywa na: Alhidaaya.com

 

049-Al-Hujuraat  Aayah 9

 

Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):

 

  وَإِن طَائِفَتَانِ مِنَ الْمُؤْمِنِينَ اقْتَتَلُوا فَأَصْلِحُوا بَيْنَهُمَا ۖ فَإِن بَغَتْ إِحْدَاهُمَا عَلَى الْأُخْرَىٰ فَقَاتِلُوا الَّتِي تَبْغِي حَتَّىٰ تَفِيءَ إِلَىٰ أَمْرِ اللَّـهِ ۚ فَإِن فَاءَتْ فَأَصْلِحُوا بَيْنَهُمَا بِالْعَدْلِ وَأَقْسِطُوا ۖ إِنَّ اللَّـهَ يُحِبُّ الْمُقْسِطِينَ﴿٩﴾

Na ikiwa makundi mawili ya Waumini yakipigana, basi suluhisheni baina yao. Lakini mojawapo likikandamiza jengine, basi piganeni na ambalo linakandamiza mpaka lielemee kwenye amri ya Allaah. Likishaelemea, basi suluhisheni baina yao kwa uadilifu, na timizeni haki. Hakika Allaah Anapenda wanaotimiza haki.

 

إِنَّمَا الْمُؤْمِنُونَ إِخْوَةٌ فَأَصْلِحُوا بَيْنَ أَخَوَيْكُمْ ۚ وَاتَّقُوا اللَّـهَ لَعَلَّكُمْ تُرْحَمُونَ﴿١٠﴾

Hakika Waumini ni ndugu, basi suluhisheni baina ya ndugu zenu. Na mcheni Allaah ili mpate kurehemewa.  [Al-Hujuraat: 9-10]

 

 

Sababun-Nuzuwl: 

 

عَنْ أَنَسِ بْنِ مَالِكٍ قَالَ قِيلَ لِلنَّبِيِّ صلى الله عليه وسلم لَوْ أَتَيْتَ عَبْدَ اللَّهِ بْنَ أُبَىٍّ قَالَ فَانْطَلَقَ إِلَيْهِ وَرَكِبَ حِمَارًا وَانْطَلَقَ الْمُسْلِمُونَ وَهِيَ أَرْضٌ سَبِخَةٌ فَلَمَّا أَتَاهُ النَّبِيُّ صلى الله عليه وسلم قَالَ إِلَيْكَ عَنِّي فَوَاللَّهِ لَقَدْ آذَانِي نَتْنُ حِمَارِكَ ‏.‏ قَالَ فَقَالَ رَجُلٌ مِنَ الأَنْصَارِ وَاللَّهِ لَحِمَارُ رَسُولِ اللَّهِ صلى الله عليه وسلم أَطْيَبُ رِيحًا مِنْكَ - قَالَ - فَغَضِبَ لِعَبْدِ اللَّهِ رَجُلٌ مِنْ قَوْمِهِ - قَالَ - فَغَضِبَ لِكُلِّ وَاحِدٍ مِنْهُمَا أَصْحَابُهُ - قَالَ - فَكَانَ بَيْنَهُمْ ضَرْبٌ بِالْجَرِيدِ وَبِالأَيْدِي وَبِالنِّعَالِ - قَالَ - فَبَلَغَنَا أَنَّهَا نَزَلَتْ فِيهِمْ ‏   ((وَإِنْ طَائِفَتَانِ مِنَ الْمُؤْمِنِينَ اقْتَتَلُوا فَأَصْلِحُوا بَيْنَهُمَا))

Imepokelewa kutoka kwa Anas bin Maalik (رضي الله عنه) kwamba Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) aliambiwa: Unaonaje umwendee ‘Abdullaah bin Ubayy (umlinganie Uislamu). Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) akamwendea akiwa amepanda punda, na (kundi la) Waislamu walienda (naye) wakitembea katika ardhi kavu iliyo na chumvi. Pindi Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) alipomfikia, (‘Abdullaah bin Ubayy) alisema:  “Jiepushe mbali nami! Naapa kwa Allaah harufu mbaya ya punda wako imenikera.”  Mtu mmoja katika Answaariy akasema (kumwambia ‘Abdullaah bin ‘Ubayy): “Naapa kwa Allaah punda wa Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) ana harufu nzuri zaidi kulikoni yako!” Hapo mtu mmoja katika kabila ya ‘Abdullaah akaghadhibika kwa ajili ya aliyoaambiwa ‘Abdullaah, kisha hao watu wawili wakawa wanashutumiana ikasababisha maswahibu wa hao wawili kughadhibika. Makundi mawili ya watu hao  yakaanza kupigana kwa vitawi, viatu na makofi.  Tukajulishwa kwamba imeteremshwa:

 

وَإِن طَائِفَتَانِ مِنَ الْمُؤْمِنِينَ اقْتَتَلُوا فَأَصْلِحُوا بَيْنَهُمَا ۖ  

Na ikiwa makundi mawili ya Waumini yakipigana, basi suluhisheni baina yao….

 

  

 

 



033-Lu-ulu-un-Manthuwrun: Kutaja Jina La Allaah Katika Chakula Na Kula Kilichoko Mbele Yako

 

Lu-ulu-un-Manthuwrun

 

(Mkusanyiko Wa Hadiyth Mbali Mbali Na Mafunzo Yake)

 

Hadiyth Ya 33

 

Kutaja Jina La Allaah Katika Chakula Na Kula Kilichoko Mbele Yako

 

Alhidaaya.com

 

 

 

عَنْ عُمَرَ بْن أَبِي سَلَمَةَ عَبْدُ الله رَبيب رَسُولِ اللَّهِ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ قَال:  كُنْتُ غُلاَمًا فِي حَجْرِ رَسُولِ اللَّهِ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ وَكَانَتْ يَدِي تَطِيشُ فِي الصَّحْفَةِ  فَقَالَ لِي رَسُولُ اللَّهِ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ: ((يَا غُلاَمُ سَمِّ اللَّهَ تَعَالى، وَكُلْ بِيَمِينِكَ،  وَكُلْ مِمَّا يَلِيكَ)) فَمَا زَالَتْ تِلْكَ طِعْمَتِي بَعْدُ. متفق عليه

Imepokelewa kutoka kwa ‘Umar bin Abi Salamah, ambaye ni mwanakambo wa Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema: Nilikuwa kijana mdogo chini ya ulezi wa Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم), na mkono wangu ulikuwa ukizungukazunguka katika sinia (ya chakula). Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) akaniambia: ((Ee ghulamu! Taja jina la Allaah (Ta’aalaa) na kula kwa mkono wako wa kulia, na ule kilicho mbele yako)). Basi huo ukawa ndio mtindo wangu wa kula baadaye.   [Al-Bukhaariy, Muslim]

 

 

Mafunzo na Mwongozo:

 

 

1. Kuwajibika kuwafunza watoto kila aina mojawapo wa tabia njema za Kiislamu na kuwatanabahisha makosa yao wanapoanza kuyatenda.

 

 

 

2. Miongoni mwa adabu za kuanza jambo lolote, kama kula chakula ni kuanza kwa ‘BismiLlaah’ (Naanza kwa Jina la Allaah), na kula kwa mkono wa kulia, na kula kilicho mbele ya sahani.

 

 

 3. Ruhusa ya kula pamoja au pekee. Lakini Hadiyth inaashiria kula katika sahani moja ni bora zaidi, na bila shaka inaleta baraka katika chakula. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):

 

لَّيْسَ عَلَى الْأَعْمَىٰ حَرَجٌ وَلَا عَلَى الْأَعْرَجِ حَرَجٌ وَلَا عَلَى الْمَرِيضِ حَرَجٌ وَلَا عَلَىٰ أَنفُسِكُمْ أَن تَأْكُلُوا مِن بُيُوتِكُمْ أَوْ بُيُوتِ آبَائِكُمْ أَوْ بُيُوتِ أُمَّهَاتِكُمْ أَوْ بُيُوتِ إِخْوَانِكُمْ أَوْ بُيُوتِ أَخَوَاتِكُمْ أَوْ بُيُوتِ أَعْمَامِكُمْ أَوْ بُيُوتِ عَمَّاتِكُمْ أَوْ بُيُوتِ أَخْوَالِكُمْ أَوْ بُيُوتِ خَالَاتِكُمْ أَوْ مَا مَلَكْتُم مَّفَاتِحَهُ أَوْ صَدِيقِكُمْ ۚ لَيْسَ عَلَيْكُمْ جُنَاحٌ أَن تَأْكُلُوا جَمِيعًا أَوْ أَشْتَاتًا ۚ فَإِذَا دَخَلْتُم بُيُوتًا فَسَلِّمُوا عَلَىٰ أَنفُسِكُمْ تَحِيَّةً مِّنْ عِندِ اللَّـهِ مُبَارَكَةً طَيِّبَةً ۚ كَذَٰلِكَ يُبَيِّنُ اللَّـهُ لَكُمُ الْآيَاتِ لَعَلَّكُمْ تَعْقِلُونَ ﴿٦١﴾

 Si vibaya kwa kipofu, na wala si vibaya kwa kilema, na wala si vibaya kwa mgonjwa, na wala nyinyi wenyewe kama mtakula majumbani mwenu, au majumbani mwa baba zenu, au majumbani mwa mama zenu, au majumbani mwa kaka zenu, au majumbani mwa dada zenu, au majumbani mwa ‘ammi zenu, au majumbani mwa shangazi zenu, au majumbani za wajomba wenu, au majumbani mwa makhalati zenu au za mliowashikia funguo zao, au rafiki yenu. Hakuna ubaya kama mkila pamoja au mbali mbali. Mtakapoingia majumbani toleaneni salaam; maamkizi kutoka kwa Allaah, yenye Baraka, mazuri. Hivyo ndivyo Anavyokubainishieni Allaah Aayaat ili mpate kutia akilini. [An-Nuwr (24: 61)]

 

 

4. Hima ya Maswahaba kufuata Sunnah, maamrisho na muongozo wa Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) tokea udogoni mwao.

 

 

5. Umuhimu wa kumfunza mtoto angali mdogo.

 

 

6. Kurekebisha kosa pale pale linapotokea kwa wakati wake munaasib na kwa upole.

 

 

7. Kutumia utaratibu na mfumo mzuri wa kumrekebisha mtu bila ya yeye kujihisi vibaya au kumfedhehesha. Hapa tunaona kuwa tatizo la mtoto lilikuwa ni mkono kuzungukazunguka katika sahani, lakini hilo lilitajwa mwisho na Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم).

 

 

8. Kuwa makini katika kurekebisha jambo na kujali hisia za mtu japo za mtoto mdogo.

 

 

9. Maswahaba walikuwa makini katika kuyafikisha waliyopewa, kufundishwa na kunasihiwa na Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم), kwani walifahamu kuwa hayo hayakuwa yao pekee yao bali ni kwa Ummah wote.

 

 

10. Hadiyth inatupatia fundisho kujuzu kwa mwanamme kuwalea watoto wa mke wake aliyezaa na mume mwengine.

 

 

11. Mwanamme anayelea watoto wa kambo anatakiwa awalee kwa njia nzuri kama watoto wake wa uhusiano wa damu.   

 



Jumatano, 25 Septemba 2019

Kila Nafsi Itaonja Mauti Na Hakuna Atakayebakia Isipokuwa Allaah سبحانه وتعالى

Anasema Allaah سبحانه وتعالى:

  كُلُّ نَفْسٍ ذَآئِقَةُ الْمَوْتِ وَإِنَّمَا تُوَفَّوْنَ أُجُورَكُمْ يَوْمَ الْقِيَامَةِ فَمَن زُحْزِحَ عَنِ النَّارِ وَأُدْخِلَ الْجَنَّةَ فَقَدْ فَازَ وَما الْحَيَاةُ الدُّنْيَا إِلاَّ مَتَاعُ الْغُرُور   
((Kila nafsi itaonja mauti. Na bila ya shaka mtapewa ujira wenu kamili Siku ya Qiyaamah. Na atakayeepushwa na Moto na akatiwa Peponi basi huyo amefuzu. Na maisha ya dunia si kitu ila ni starehe ya udanganyifu)) [Al-'Imraan: 185]

Tokea kuumbwa kwa Nabii Aadam عليه السلام   hadi  leo na mpaka siku ya Qiyaamah hakuna kiumbe kitakachobakia isipokuwa Mwenyewe Mola Mtukufu kama Anavyosema:
 كُلُّ شَيْءٍ هَالِكٌ إِلَّا وَجْهَهُ
((Kila kitu kitaangamia isipokuwa Yeye)) [Al-Qaswas: 88]

Vile vile Anasema Allaah سبحانه وتعالى :

 ((كُلُّ مَنْ عَلَيْهَا فَانٍ))
 ((وَيَبْقَى وَجْهُ رَبِّكَ ذُو الْجَلَالِ وَالْإِكْرَام))

((Kila kilioko juu Yake kitatoweka))
((Na Atabakia Mwenyewe Mola wako  Mwenye utukufu na ukarimu)) [Ar-Rahmaan: 26-27]

Baada ya kupulizwa Swuur (baragumu) siku ya Qiyaamah viumbe vyote vitakufa kwa mpangilio Anaoutaka Mwenyewe Allaah سبحانه وتعالى. Kisha mwisho atabakia Malakul Mawt (Malaika mtoaji roho) na Allaah سبحانه وتعالى. Kisha Allaah سبحانه وتعالى  Atamuamrisha Malakul Mawt ajitoe roho yake mwenyewe. Atakapokufa Malakul Mawt Atabakia Allaah سبحانه وتعالى   Pekee wa Mwanzo na wa Mwisho, Al-Hayyul-Qayyuum (Mwenye uhai wa maisha, Msimamia kila jambo). Allaah سبحانه وتعالى  Siku hiyo Atazikusanya ardhi na mbingu katika Mikono Yake,

  ((وَالْأَرْضُ جَمِيعًا قَبْضَتُهُ يَوْمَ الْقِيَامَةِ وَالسَّماوَاتُ مَطْوِيَّاتٌ بِيَمِينِهِ))

((Na Siku ya Qiyaamah ardhi yote itakuwa mkononi Mwake, na mbingu zitakunjwa katika mkono wake wa kuume)) [Az-Zumar: 67]

Na Hadiyth kutoka kwa Ibn 'Umar رضي الله عنه   kwamba:

  ((يطوي السموات والأرض بيده، ثم يقول: أنا الملك، أنا الجبار، أنا المتكبر، أين ملوك الأرض؟ أين الجبارون؟ أين المتكبرون؟))  مسلم

((Allaah Atazikunja mbingu kwa Mikono Yake, kisha Atasema, Mimi ni Mfalme, Mimi ni Al-Jabbaar (Mwenye Kushurutisha), wako wapi wafalme wa dunia? Wako wapi majabbaar (wanaolazimisha), wako wapi wanaotakabari?)) [Muslim]

Hapo tena Atauliza mara tatu: 
  ((لِّمَنِ الْمُلْكُ الْيَوْمَ))
((Ufalme ni wa nani leo?)) [Ghaafir:16]

Hakutakuwa na mtu wa kujibu, basi Atajibu Mwenyewe,
  ((لِلَّهِ الْوَاحِدِ الْقَهَّار))  

((Ni wa Allaah Mmoja Mtenda Nguvu)) [Ghaafir 16]

Na hapo tena ndipo kila mtu atakuta hesabu yake ya matendo aliyoyatenda duniani ikiwa ni mema au mabaya, hakuna atakayedhulumiwa hata chembe, kwani Allaah سبحانه وتعالى  Atahukumu kwa uadilifu baina ya viumbe Vyake. Kila jema Atalilipa kwa mara kumi na kila ovu atahesabiwa mja kwa ovu moja.

  ((الْيَوْمَ تُجْزَى كُلُّ نَفْسٍ بِمَا كَسَبَتْ لَا ظُلْمَ الْيَوْمَ إِنَّ اللَّهَ سَرِيعُ الْحِسَابِ))  

((Leo kila nafsi italipwa kwa iliyochuma. Hapana dhulma leo. Allaah  ni Mwepesi wa kuhisabu)) [Ghaafir: 17]


************



20-Hakika Shirki Ni Dhulma Kubwa Mno! - Isti’aadhah Kwa Asiyekuwa Allaah

  إِنَّ الشِّرْكَ لَظُلْمٌ عَظِيم   Hakika Shirki Ni Dhulma Kubwa Mno!   20 - Isti’aadhah  (Kuomba Kinga) Kwa Asiyekuwa Allaah   ...