Translate

Jumatano, 13 Novemba 2019

Mambo Yanayosababisha Katika Kumpwekesha Allaah (Tawhiyd) Kwenye 'Ibaadah


Inasikitisha kuona kuwa hadi wakati huu, bado wapo Waislamu wenye itikadi isiyokuwa sahihi na wenye kusema maneno ambayo huenda yakawatia katika shirki.
Watu wa aina hiyo wengi wao niyyah zao ni nzuri, na ni katika watu wamchao Allaah (Subhaanahu Wa Ta’aala) sana, wanaswali na kufunga na kutimiza nguzo zote tano za kiislamu. Lakini itikadi zao hizo pamoja na kuvuka kwao mipaka katika kuwasifia na kuwatukuza watu wema au Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) katika Rusul wa Allaah ('Alayhis Salaam Ajmaiyn), huwafanya kutoa kauli zinazoweza kuwatia katika shirki na kuwatoa katika Tawhyid ambayo juu yake Dini hii tukufu imesimama.
Allaah Anasema:

وَإِذْ قَالَ لُقْمَانُ لِابْنِهِ وَهُوَ يَعِظُهُ يَا بُنَيَّ لَا تُشْرِكْ بِاللَّـهِ ۖ إِنَّ الشِّرْكَ لَظُلْمٌ عَظِيمٌ ﴿١٣﴾
Na Luqmaan alipomwambia mwanawe huku akimuwaidhi: “Ee mwanangu! Usimshirikishe Allaah, hakika shirki ni dhulma kubwa mno!” [Luqmaan: 13]

Na Akasema:

إِنَّ اللَّـهَ لَا يَغْفِرُ أَن يُشْرَكَ بِهِ وَيَغْفِرُ مَا دُونَ ذَٰلِكَ لِمَن يَشَاءُ ۚ وَمَن يُشْرِكْ بِاللَّـهِ فَقَدْ ضَلَّ ضَلَالًا بَعِيدًا ﴿١١٦﴾
Hakika Allaah Haghufurii kushirikishwa; lakini Anaghufuria yasiyokuwa hayo kwa Amtakae. Na yeyote atakayemshirikisha Allaah basi kwa yakini amepotoka upotofu wa mbali. [An-Nisaa: 116]

Kabla ya kuendelea mbele, ni bora tufafanue kidogo nini maana ya Tawhiyd:
Tawhiyd - ambayo kinyume chake ni Shirki; maana yake ni: "kupwekesha" au kuelekeza ‘ibaadah zote mahali pamoja tu. Nako ni kwake Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala). Tawhiyd inakanusha aina yoyote ya kumshirikisha Allaah.

Dini ya Kiislamu ndiyo dini pekee ulimwenguni inayohubiri Tawhiyd. Kwasababu dini nyengine zote zinamnasibisha Allaah na washirika wengine.
Ma’ulamaa wameigawa elimu hii ya Tawhiyd sehemu tatu, nazo ni:
  1. Tawhiyd Ar-Rubuubiyyah
  2. Tawhyid Al-Uluuhiyyah
  3. Tawhiyd Al-Asmaa Was-Swifaat

1.    Tawhiyd Ar-Rubuubiyyah

Nayo ni kuamini kwamba Allaah.  Allaah Ndiye aliyeumba kila kitu bila ya msaidizi. Itikadi hiyo pekee haimuingizi mtu Peponi, kwasababu washirikina wa Makkah wote walikuwa wakiamini kwamba Allaah ndiye Aliyeumba kila kitu bila ya msaidizi.
Allaah Anasema:
قُلْ مَن يَرْزُقُكُم مِّنَ السَّمَاءِ وَالْأَرْضِ أَمَّن يَمْلِكُ السَّمْعَ وَالْأَبْصَارَ وَمَن يُخْرِجُ الْحَيَّ مِنَ الْمَيِّتِ وَيُخْرِجُ الْمَيِّتَ مِنَ الْحَيِّ وَمَن يُدَبِّرُ الْأَمْرَ ۚ فَسَيَقُولُونَ اللَّـهُ ۚ فَقُلْ أَفَلَا تَتَّقُونَ﴿٣١﴾
Sema: “Nani anayekuruzukuni kutoka mbinguni na ardhini. Au nani anayemiliki kusikia na kuona; na nani anayemtoa aliye hai kutoka mfu, na anayemtoa mfu kutoka aliye uhai; na nani anayeendesha mambo (yote)?”  Watasema: “Ni Allaah”; basi sema: “Je basi hamuwi na taqwa?” [Yuwnus: 31]

Hata Ibliys aliyelaaniwa na Allaah, alikuwa anayo Tawhiyd hii.

Allaah Anasema:
قَالَ رَبِّ فَأَنظِرْنِي إِلَىٰ يَوْمِ يُبْعَثُونَ﴿٣٦﴾
Akasema: “Rabb wangu! Nipe muhula mpaka Siku watakayofufuliwa.” [Al-Hijr: 36]

Kutokana na Aayah zilizotangulia, utaona kuwa Maquraysh waliokuwa wakiabudu masanamu, pamoja na Ibliys wao, walikuwa wakiamini kuwa Allaah ndiye Mola wao, na ndiye aliyeumba na ndiye Mwenye kumiliki kila kitu. Lakini imani yao hiyo hakuwasaidia kitu, kwa sababu ya kutoamini sehemu nyingine za Tawhiyd.

Kwa hivyo, hata kama utaamini kwamba Allaah Ndiye aliyeumba na ndiye mwenye kumiliki kila kitu, lakini ikiwa hujaamini sehemu ya pili na ya tatu ya Tawhiyd, basi iymaan yako hiyo haitokusaidia kitu.

2.    Tawhyid Al-Uluuhiyyah

Nayo ni kuamini kwamba ‘ibaadah zote lazima zielekezwe kwake tu Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala).

‘Ibaadah kama vile kuswali, kuhijji, kuomba du’aa, kuchinja, kuweka nadhiri, kuhukumu n.k., zote hizo pamoja na niyyah ya mtu katika kutenda tendo lolote lile la kidunia au la kiakhera lazima zielekezwe kwake tu (Subhaanahu wa Ta’ala), na asiingizwe mshirika wa aina yeyote ndani yake.

Allaah Anasema:
قُلْ إِنَّ صَلَاتِي وَنُسُكِي وَمَحْيَايَ وَمَمَاتِي لِلَّـهِ رَبِّ الْعَالَمِينَ ﴿١٦٢﴾
Sema: “Hakika Swalaah yangu, na kuchinja kafara na ‘ibaadah zangu na uhai wangu na kufa kwangu ni kwa ajili ya Allaah Pekee Rabb wa walimwengu.” [Al-An’aam: 162]


3.    Tawhiyd Al-Asmaa Was-Swifaat

Nayo ni kuamini na kukubali kila kilichoandikwa katika Qur-aan Tukufu na katika Hadiyth zilizo sahihi za Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) zikielezea sifa tukufu za Allaah au majina Yake matukufu, bila ya kukisia kisia, wala kuchelewesha, wala kubadilisha maana yake.

Kwa mfano unapokutana na kauli ya Allaah isemayo:
يَدُ اللَّـهِ فَوْقَ أَيْدِيهِمْ ۚ
Mkono wa Allaah Uko juu ya mikono yao… [Al-Fat-h: 10]

Kubadilisha neno mkono tukasema nguvu, tutakuwa tumebadilisha maana.

Na Shaytwaan anapojaribu kutaka kukuchezea kwa kutaka ufananishe au ugeuze maana ya sifa, au majina ya Allaah kumbuka kauli Yake (Subhaanahu wa Ta’ala):

لَيْسَ كَمِثْلِهِ شَيْءٌ ۖ  
Hakuna chochote kinachofanana Naye… [Ash-Shuwraa: 11]

Shirki

Shirki katika lugha ya Kiarabu maana yake ni Ushirika. Nako ni kumjaalia mmoja au zaidi, awe na sehemu kubwa au ndogo, katika jambo lolote lile aloshirikiana na mwenziwe au wenziwe.

Kumshirikisha Allaah katika kuamini kwamba anaye mshirikia katika kuumba chochote kile (Tawhiyd Ar-Rubuubiyyah) au kuamini kwamba yuko mwenye uwezo au sifa kama Zake (Tawhiyd Al-Asmaa Was-Swifaat), au kuamini kwamba ‘ibaadah ya aina yoyote ile, inaweza ikaelekezwa au kupitia kwa mwengine asiyekuwa Allaah (Tawhyid Al-Uluuhiyyah), basi huko ni kwenda kinyume na mafundisho ya dini yetu tukufu ya Tawhiyd na kumkadhibisha Allaah, na kwa sababu hii, dhambi yake haisameheki [kwa ukubwa wake].

Allaah Anasema:

شَهِدَ اللَّـهُ أَنَّهُ لَا إِلَـٰهَ إِلَّا هُوَ
Allaah Ameshuhudia kwamba hapana muabudiwa wa haki ila Yeye… [Aal-‘Imraan: 18]

Na Anasema:
فَاعْلَمْ أَنَّهُ لَا إِلَـٰهَ إِلَّا اللَّـهُ
Basi jua kwamba laa ilaaha illa-Allaah, hapana muabudiwa wa haki ila Allaah… [Muhammad: 19]


Tofauti Baina Ya Shirki Na Kufru

Shirki inahitilafiana na kufru. Kwani kuna shirki nyengine hazikupeleki kwenye kufru, kama vile Shirki ndogo (Ash-Shirkul-Asghar) au Shirki iliyojificha (Ash-Shirkul-Khafiy).
Pia kutenda au kutamka neno la shirki bila kujua, hakumpeleki mtu katika kufru. Isipokuwa mara tu baada ya kutambua, inampasa Muislam akiache kitendo hicho haraka sana.  Dalili ya maneno haya ni Hadiyth zifuatazo:

Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), aliulizwa juu ya watu ambao wanapokuwa mbele ya wenzao hujionyesha kuwa ni watu wema na wanapokuwa peke yao hufanya kinyume na hayo. Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) hakuwakufurisha watu wa aina hiyo, bali alisema: “Ninachokuogopeeni sana ni Shirki ndogo”. Maswahaabah wakauliza: "Ni nini hii Shirki ndogo, ewe RAsuli wa Allaah?" Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akasema: ((Riyaa (kujionyesha). [Imepokewa na Imaam Ahmad]


Dalili nyengine ni pale Swahaabah mmoja alipomwambia Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam): “Kama alivyotaka Allaah na ulivyotaka. Maa shaa Llaahu wa shi-ita.” Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akamwambia: “Umenigeuza kuwa mshirika wa Allaah? Sema: 'Alivyotaka Allaah peke Yake' Qul Maa shaa-Llaahu wahdahu”. [Imepokewa na Imaam Ahmad, Addarmy na Ibni Maajah]

Zipo dalili nyingi juu ya maudhui haya, lakini hapa nitamaliza kwa kutoa dalili ifuatayo:
Siku moja Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) aliwasikia baadhi ya watu wakisema: "Njooni tuombe, tuelekeze du’aa zetu kwa Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam).” Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alipowasikia, akawaambia: “Nani huyu mnafiki? Du’aa hazielekezwi kwangu, bali zinaelekezwa kwa Allaah”. [Imepokewa na Imaan Ahmad na At-Twabaraaniy]

Ingawaje maneno yaliyotamkwa hapo juu na baadhi ya Maswahaabah, yalikuwa na dalili ya shirki ndani yake; lakini Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) hakuwahukumu waliotenda au kutamka maneno hayo kuwa ni makafiri. Bali aliwasahihisha itikadi yao, na hii ni kwasababu ya kutokujua kwao kosa lao, kisha akawafahamisha hatari ya makosa hayo.

Kwa hivyo mwenye itikadi kama hiyo ya kumuomba Rasuli katika Rusul ya Allaah ('Alayhis Salaam Ajmaiyn) au Waliy katika Mawaliy wa Allaah n.k., hatuhumiwi kuwa ni kafiri. Isipokuwa mtendaji au msemaji wa kauli kama hizi ikiwa anafanya inadi na kushikilia, pamoja na kuendelea kutenda au kutamka maneno mfano wa haya kwa inadi na kutakabari tu, basi hapo ndipo anapokuwa katika hatari ya kuingia katika kufru.

Je, Inajuzu Kumuomba Rasuli (Swalla Allaahu ‘Alayhi Wa Aalihi Wa Sallam)?

Suala sasa linakuja: "Jee inajuzu kuelekeza du’aa yako kumuomba Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam)?"

Jawabu: "Haijuzu".

Kwa sababu Rasuli mwenyewe (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amebainisha aliposema: “Du’aa ndiyo ‘ibaadah”. [Imepokewa na Imaam Ahmad na Imaam At-Tirmidhiy]

Nini ‘Ibaadah?

Anasema Ibnu Qayyim Al-Jawziyyah (Rahimahu Allaah): "’Ibaadah ni jina lililokusanya kila Anachokipenda Allaah na kuridhika nacho ikiwa ni kitendo au kauli, zilizojificha au zilizodhihirika.”

Kwa hivyo kitendo chochote kinachokukaribisha kwa Allaah kama vile kuswali, kufunga, kuhijji, kutoa Zakkah, kutoa Swadaqah, kusoma Qur-aan, kuomba du’aa n.k. ni ‘ibaadah.
Ushahidi kwamba du’aa ni ‘ibaadah unatokana na kauli yake (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) iliyotajwa hapo juu; aliposema katika Hadiyth sahihi iliyosimuliwa na Imaam Ahmad pamoja na Imaam At-Tirmidhiy: “Du’aa ndiyo ‘ibaadah”.

Kwa hivyo atakayemuomba yeyote asiyekuwa Allaah iwapo ni Malaika mtukufu, au Rasuli katika Rusul ya Allaah ('Alayhis Salaam), au Waliy katika mawaliy wa Allaah au jinni au kiumbe chochote kile kihai au kilichokufa, atakuwa amekwisha fanya kitendo cha ushirikina.
Allaah Anasema:

وَلَا تَدْعُ مِن دُونِ اللَّـهِ مَا لَا يَنفَعُكَ وَلَا يَضُرُّكَ ۖ فَإِن فَعَلْتَ فَإِنَّكَ إِذًا مِّنَ الظَّالِمِينَ﴿١٠٦﴾
Na wala usiombe badala ya Allaah visivyokufaa wala visivyokudhuru. Na ukifanya, basi hakika utakuwa miongoni mwa madhalimu.

وَإِن يَمْسَسْكَ اللَّـهُ بِضُرٍّ فَلَا كَاشِفَ لَهُ إِلَّا هُوَ ۖ وَإِن يُرِدْكَ بِخَيْرٍ فَلَا رَادَّ لِفَضْلِهِ ۚ يُصِيبُ بِهِ مَن يَشَاءُ مِنْ عِبَادِهِ ۚ وَهُوَ الْغَفُورُ الرَّحِيمُ﴿١٠٧﴾
Na Allaah Akikugusisha dhara, basi hakuna wa kuiondosha isipokuwa Yeye. Na Akikutakia kheri, basi hakuna wa kurudisha fadhila Zake, Anasababisha kumfikia kwayo (fadhila Yake) Amtakaye katika waja Wake. Naye ni Mwingi wa kughufuria, Mwenye kurehemu. [Yuwnus: 106-107]

Na Anasema:
قُلْ إِنِّي لَا أَمْلِكُ لَكُمْ ضَرًّا وَلَا رَشَدًا﴿٢١﴾
Sema: “Hakika mimi sikumilikieni dhara na wala uongofu.” [Al-Jinn: 21]

Na pia Anasema:

قُل لَّا أَمْلِكُ لِنَفْسِي نَفْعًا وَلَا ضَرًّا إِلَّا مَا شَاءَ اللَّـهُ ۚ وَلَوْ كُنتُ أَعْلَمُ الْغَيْبَ لَاسْتَكْثَرْتُ مِنَ الْخَيْرِ وَمَا مَسَّنِيَ السُّوءُ ۚ إِنْ أَنَا إِلَّا نَذِيرٌ وَبَشِيرٌ لِّقَوْمٍ يُؤْمِنُونَ ﴿١٨٨﴾
Sema: “Siimilikii nafsi yangu manufaa yoyote wala dhara yoyote isipokuwa Apendavyo Allaah. Na lau ningekuwa najua ya ghayb, bila shaka ningelijikithirishia ya khayr, na wala lisingelinigusa ovu. Mimi si chochote isipokuwa ni mwonyaji na mbashiriaji kwa watu wanaoamini.” [Al-‘Aaraaf: 188]

Ukizichunguza Aayah nyingi, utaona kwamba Allaah Anamwambia Rasuli wake (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam): sema, waambie, wafahamishe, wajuulishe kwamba hakuna awezae kudhuru au kunufaisha isipokuwa Allaah, na kwamba hapana ajuae ghayb isipokuwa Allaah tu. Lakini kinachosikitisha ni kwamba bado wapo wasiotaka kufahamu wala kuambiwa.

Inafaa mtu ajiulize suali hili: "Je Rasuli mwenyewe (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) aliwahi kudai au kutufundisha kwamba du’aa zielekezwe kwake?"

Bila shaka hakupata hata siku moja kudai hayo, bali kauli zake zote ni dalili ya kuyakanusha hayo. Ndiyo maana siku ile Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alipopanda mnyama pamoja na Ibni ‘Abbaas (Radhwiya Allaahu ‘anhu) akamwambia:

“Ewe kijana, mimi ninakufundisha maneno: Muhifadhi Allaah naye atakuhifadhi, muhifadhi Allaah siku zote atakuwa na wewe, ukiomba du’aa umuombe Allaah ukitaka msaada umuombe Allaah  na ujue ya kwamba Ummah wote ukikusanyika ili wakunufaishe na kitu basi hawawezi kukunufaisha ila kwa kile ambacho Allaah ameshakuandikia, na wakikusanyika ili wakudhuru kwa jambo, basi hawawezi kukudhuru ila kwa kile ambacho Allaah  keshakuandikia; kalamu zimekwishanyanyuliwa na wino umekwishakauka juu ya karatasi”. [Imepokewa na At-Tirmidhiy]

Hakumwambia Ibn ‘Abbaas (Radhwiya Allaahu ‘anhu) kwamba: "Ukiomba du’aa niombe mimi, na ukitaka msaada niombe mimi." Bali alimwelekeza kule kule kwa Mwenye Nguvu, Mwenye Uwezo Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala).

Anasema Imaam Ibn Qayyim Al-Jawziyyah (Rahimahu Allaah) katika kitabu chake kiitwacho Zaad al-Maad, ukurasa wa tatu:

"Ninashuhudia kwamba Rasuli Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ameletwa na Mola wake kama Rasul mingine, akiwa kiongozi wa wamchao Allaah ni rahmah kwa walimwengu. Akawaongoza watu katika njia iliyo sahihi na iliyonyooka. Allaah akawafaradhishia waja wake kumtii Rasuli huyu (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), kumuheshimu, kumpenda na akajaalia njia ya kuelekea kwenye Jannah yake ni moja tu, nayo ni kufuata njia yake Rasuli huyu mtukufu (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam).

Akajaalia kudhalilika na kudharaulika kumfikie kila atakayekwenda kinyume na Rasuli huyu mtukufu (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam).

Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: “Na akajaalia kudhalilika na kudharaulika kwa kila atakayekwenda kinyume na amri yangu na atakayejifananisha na kundi keshakuwa pamoja nao”. [Imepokewa na Imaam Ahmad]

Kwa hivyo watadhalilika waliomuasi na wataheshimika watakaomtwii na kumfuata Rasuli huyu (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam).

Allaah Anasema:
وَلَا تَهِنُوا وَلَا تَحْزَنُوا وَأَنتُمُ الْأَعْلَوْنَ إِن كُنتُم مُّؤْمِنِينَ ﴿١٣٩﴾ 
Na wala msilegee na wala msihuzunike na ilhali nyinyi mko juu mkiwa ni Waumini. [Aali-‘Imraan: 139]

Na Akasema:
وَلِلَّـهِ الْعِزَّةُ وَلِرَسُولِهِ وَلِلْمُؤْمِنِينَ وَلَـٰكِنَّ الْمُنَافِقِينَ لَا يَعْلَمُونَ﴿٨﴾
Na hali utukufu ni wa Allaah na wa Rasuli Wake na wa Waumini, lakini wanafiki hawajui. [Al-Munafiquun: 8]


Kutosheleza Na Kufuata

Anaendelea kuelezea Imaam Ibnu Qayyim Al-Jawziyyah katika kitabu chake hicho akisema: Allaah Anasema:

Na Akasema:
يَا أَيُّهَا النَّبِيُّ حَسْبُكَ اللَّـهُ وَمَنِ اتَّبَعَكَ مِنَ الْمُؤْمِنِينَ﴿٦٤﴾
Ee Nabiy! Anakutosheleza Allaah na anayekufuata miongoni wa Waumini. [Al-Anfaal: 62]
Anaendelea kueleza Ibnul-Qayyim kwamba; katika Aayah hizi Allaahh Anamjuulisha Rasuli wake (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kwamba Allaah pekee anamtosheleza yeye pamoja na waliomfuata, na kwamba hawahitajii msaada wa yeyote mwengine isipokuwa wake Subhaanahu wa Ta’ala.

Katika Aayah nyengine Akasema:


الَّذِينَ قَالَ لَهُمُ النَّاسُ إِنَّ النَّاسَ قَدْ جَمَعُوا لَكُمْ فَاخْشَوْهُمْ فَزَادَهُمْ إِيمَانًا وَقَالُوا حَسْبُنَا اللَّـهُ وَنِعْمَ الْوَكِيلُ ﴿١٧٣﴾
Wale walioambiwa na watu: “Hakika watu wamejumuika dhidi yenu, basi waogopeni.” Lakini iliwawazidishia iymaan wakasema: “Hasbuna-Allaah! (Allaah Anatutosheleza) Mzuri Alioje Mdhamini Anayetegemewa kwa yote.” [Aal-‘Imraan: 173]


Ukiichunguza Aayah hii utaona kuwa Waislamu hawakusema "Anatutosheleza Allaah na Rasuli wake". Bali walisema: "Allaah Anatutosha. Naye ni mlinzi bora kabisa".

Na ukiichunguza kauli ya Allaah (Subaahanahu wa Ta’aalaa) katika Suuratut-Tawbah: 59 Aliposema:

وَلَوْ أَنَّهُمْ رَضُوا مَا آتَاهُمُ اللَّـهُ وَرَسُولُهُ وَقَالُوا حَسْبُنَا اللَّـهُ سَيُؤْتِينَا اللَّـهُ مِن فَضْلِهِ وَرَسُولُهُ إِنَّا إِلَى اللَّـهِ رَاغِبُونَ﴿٥٩﴾
Na lau wangeliridhiya yale Aliyowapa Allaah na Rasuli Wake, na wakasema: “Anatutosheleza Allaah, karibuni Allaah Atatupa katika fadhila Zake na Rasuli Wake (pia); hakika sisi kwa Allaah tuna raghba.”  [At-Tawbah: 59]

Tazama jinsi Allaah Alivyomnasibisha Rasuli wake (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) katika ‘kutoa’. Akatumia neno (Allaah Atatupa katika fadhila zake na Mtume wake) kama katika kauli nyengine aliposema:
وَمَا آتَاكُمُ الرَّسُولُ فَخُذُوهُ وَمَا نَهَاكُمْ عَنْهُ فَانتَهُوا ۚ
Na lolote analokupeni Rasuli (صلى الله عليه وآله وسلم) basi lichukueni, na analokukatazeni, basi acheni. [Al-Hashr: 7]

Lakini katika neno ‘kutosha’, utaona kwamba amejinasibisha Yeye peke yake Subhaanahu wa Ta’ala. Hakusema: ‘Anatutoshea Allaah  na Rasuli wake’ bali amesema: ‘Anatutoshea Allaah’. Akakamilisha kwa kauli yake: ‘Hakika sisi tunaelekea kwa Allaah’. Akajaalia ‘kuelekea’ kuwe kwake tu, kama Alivyosema katika Suuratun-Nashrah:
فَإِذَا فَرَغْتَ فَانصَبْ ﴿٧﴾
Basi utakapopata faragha fanya juhudi katika ‘ibaadah.


وَإِلَىٰ رَبِّكَ فَارْغَب ﴿٨﴾
Na kwa Rabb wako elemea kwa raghba (kutakabaliwa). [Ash-Sharh: 7-8]

Kwa hivyo, kutegemea, kutosheleza, kuelekea ni kwake Allaah tu peke yake. Pia kusujudu, kuweka nadhiri, kuapa, yote haya yanaelekezwa kwake tu Subhaanahu wa Ta’ala. Ushahidi wa haya ni kauli yake Allaaah (Subhaanahu wa Ta’alaa):
أَلَيْسَ اللَّـهُ بِكَافٍ عَبْدَهُ ۖ
Je, kwani Allaah si Mwenye kumtosheleza mja Wake? [Az-Zumar: 36]

Kwa hayo tunatambua kuwa, kumshirikisha Allaah katika ‘ibaadah zake zozote zile, na kiumbe chochote kile baada ya kuzijua dalili zilizotangulia na zilizowazi kabisa, ni jambo lililo baatwil na la ufisadi.

Kwa ufupi, Allaah Anatutaka tumtegemee Yeye tu na Kumuomba Yeye tu, pamoja na kuelekeza ‘ibaadah zetu zote kwake Yeye tu, na Anatutaka tumfuate Rasuli Wake (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ndipo utakapopatikana ushindi na utukufu na kusaidiwa na Allaah pamoja na maisha mema hapa duniani na Aakhera.

Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) aliapa akasema:
“Hatoamini mmoja wetu mpaka mapenzi yake kwa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) yawe makubwa kupita mapenzi ya nafsi yake, na ya watoto wake na ampende Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kuliko watu wote”.

Na Allaah Akaapa Akasema:

فَلَا وَرَبِّكَ لَا يُؤْمِنُونَ حَتَّىٰ يُحَكِّمُوكَ فِيمَا شَجَرَ بَيْنَهُمْ ثُمَّ لَا يَجِدُوا فِي أَنفُسِهِمْ حَرَجًا مِّمَّا قَضَيْتَ وَيُسَلِّمُوا تَسْلِيمًا ﴿٦٥﴾
Basi Naapa kwa Rabb wako, hawatoamini mpaka wakufanye wewe ni mwamuzi katika yale wanayozozana baina yao, kisha wasipate katika nyoyo zao karaha katika yale uliyohukumu na wajisalimishe, kwa kujisalimisha kikamilifu. [An-Nisaa: 65]

Katika Aayah hii, Allaah Anatukataza kufuatwa amri isiyokuwa Yake Subhaanahu wa Ta’ala au ya Rasuli wake (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam).

Muislamu hana hiari ya kuchagua, kufuata au kutofuata baada ya kuijua hukumu ya Allaah au ya Rasuli wake (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam). Bali Muislamu, lengo lake lote pamoja na mapenzi yake yote, yawe katika kufuata amri za Allaah na za Rasuli wake (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam).

Mwisho wa maneno ya Ibnul-Qayyim (Rahimahu Allaah).

Wasiylah
Nini maana ya Wasiylah?
Majibu:
Wasiylah katika lugha ya Kiarabu, maana yake ni njia au sababu inayoweza kukufikisha utakapo.
Na asili yake ni kauli yake Mwenyezi Mungu katika Qur-aan aliposema:

يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا اتَّقُوا اللَّـهَ وَابْتَغُوا إِلَيْهِ الْوَسِيلَةَ وَجَاهِدُوا فِي سَبِيلِهِ لَعَلَّكُمْ تُفْلِحُونَ ﴿٣٥﴾
Enyi walioamini! Mcheni Allaah na tafuteni njia za kumkurubia; na fanyeni jihaad katika njia Yake ili mpate kufaulu. [Al-Maaidah: 35]

Na katika Hadiythul-Qudusy Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Anasema:

“Hatojikurubisha kwangu mja wangu kwa jambo nilipendalo kuliko yale niliyomfaradhishia. Na mja wangu angali anaendelea kujikurubisha kwangu kwa ‘ibaadah za Sunnah mpaka nimpende...”  [Imepokewa na Al-Bukhaariy]

Ama katika lugha ya Dini (katika Fiq-hi), neno 'Wasiylah' pia huwa na maana ya ‘amali njema anayoitanguliza mja kwa Mola wake, kabla hajaomba du’aa au pamoja na du’aa ili du’aa yake ikubaliwe.

Katika kujisogeza huku kwa Mola wao, baadhi ya Waislamu wakavumbua njia zisizo za kishari’ah ambazo badala ya kuwasogeza karibu na Mola wao, huwa zinawabaidisha Naye. Kuna Wasiylah inayompeleka mtu katika shirki, na nyengine inampeleka mtu katika uzushi (bida’ah).


Mambo Yanayowababaisha Watu

Kujikurubisha Kwa Jaha (Heshima) Ya Rasuli (Swalla Allaahu ‘Alayhi Wa Aalihi Wa Sallam)

Kwanza kabisa; nini maana ya Jaha:

Jaha, katika lugha ya Kiarabu maana yake ni hishima. Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Anasema juu ya Nabii ‘Iysa ('Alayhis Salaam):

 إِذْ قَالَتِ الْمَلَائِكَةُ يَا مَرْيَمُ إِنَّ اللَّـهَ يُبَشِّرُكِ بِكَلِمَةٍ مِّنْهُ اسْمُهُ الْمَسِيحُ عِيسَى ابْنُ مَرْيَمَ وَجِيهًا فِي الدُّنْيَا وَالْآخِرَةِ وَمِنَ الْمُقَرَّبِينَ ﴿٤٥﴾
Na pale Malaika waliposema: “Ee Maryam! Hakika Allaah Anakubashiria Neno (la Kun!) kutoka Kwake (umzae mtoto), jina lake ni Al-Masiyhu ‘Iysaa mwana wa Maryam, mwenye taadhima katika dunia na Aakhirah na ni miongoni mwa waliokurubishwa (kwa Allaah). [Aali ‘Imraan: 45]

Na juu ya Nabii Muusa ('Alayhis Salaam), Allaah (Subhaanahu Wa Ta’aalaa) Anasema:

يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا لَا تَكُونُوا كَالَّذِينَ آذَوْا مُوسَىٰ فَبَرَّأَهُ اللَّـهُ مِمَّا قَالُوا ۚ وَكَانَ عِندَ اللَّـهِ وَجِيهًا ﴿٦٩﴾
Enyi walioamini! Msiwe kama wale waliomuudhi Muwsaa, lakini Allaah Akamtoa tuhumani kutokana na yale waliyoyasema. Na alikuwa mbele ya Allaah mwenye kuheshimika. [Al-Ahzaab: 69]

Bila shaka (Jaha) hishima ya Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) mbele ya Mola wake ni kubwa kabisa. Lakini kumuomba Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) akukubalie jambo lako kwa hishima ya Rasuli wake (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) badala ya kumuomba akukubalie kwa nguvu Zake Allaah au kwa uwezo Wake au kwa ukarimu Wake n.k. huku ni kuyakimbia yale majina na sifa Zake tukufu Subhaanahu wa Ta’ala.

Kujikurubisha Kwa Baraka Za Mawalii

Nako ni kujisogeza kwa Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) kwa njia ya kwenda makaburini (makaburi ya mawalii) au njia zilizo kama hizo.

Hapana anayepinga kuwepo kwa Mawalii wa Allaah (Subhaanahu wa ta’aalaa), pamoja na makarama yao pale walipokuwa hai. Qur-aan na Sunnah zimezungumzia juu ya yote hayo. Lakini kwenda makaburini na kuwaomba maiti hao ili kupitia kwao uweze kuondolewa shida zako na Mola wako, jambo hilo halijuzu kabisa na pana hatari ya kukuingiza katika kumshirikisha Allaah (Subhaahu wa Ta’aalaa) na kiumbe.


Kujisogeza Kwa Du’aa Iitwayo ‘Wasiylah’

Kuna baadhi ya watu hujisogeza kwa kusoma ‘Wasiylah’ - nayo ni du’aa maarufu iitwayo Asw-Swalaatu-Nnaariyah. Husomwa mara 4,444 ili kuondoa shida au dhiki. Inasemekana kwamba mmoja katika watu wema alioteshwa na kufundishwa du’aa hii.
Swalah yenyewe inasomwa hivi:

"Allahumma swalliy swalaatan kaamilah, wa sallim salaaman taammah ‘alaa Sayyidina Muhammad, alladhiy tanhallu bihil ‘uqad, watanfarij bihil kurab, watanqadhiy bihil hawaaij...” mpaka mwisho wake.

Maana yake ni: "Mola wangu Swali Swalah iliyokamilika na umsalimie salaam iliyotimia Bwana wetu Muhammad, ambaye kwake yeye fundo zinafunguka na dhiki zinaondoka na haja zinatimia…” mpaka mwisho wa du’aa.

Ukiichunguza Swalah hii, utaona kwamba badala ya kuelekeza du’aa kwa Mwenyezi Mungu, inaelekezwa kwa Rasuli wake (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), na kumpa Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) sifa za Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa). Hasa pale inaposemwa ‘kwake yeye fundo zinafunguka na dhiki zinaondoka’, na huku ni kumpa kiumbe sifa za Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa).

Baadhi ya Ma’ulamaa wamesema laiti pale paliposemwa, alladhiy tanhallu bihil ‘uqad na maana yake ni ‘kwake yeye fundo zinafunguka’ pangesemwa tanhallu bihal ‘uqad; hapo maana yake inabadilika na kuwa ‘kwa kumswalia na kumsalimia Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ndiyo dhiki na shida zinaondoka’; na kwa vile kumswalia Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ni ‘ibaadah ambayo Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Ametuamrisha.

Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Anasema:

إِنَّ اللَّـهَ وَمَلَائِكَتَهُ يُصَلُّونَ عَلَى النَّبِيِّ ۚ يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا صَلُّوا عَلَيْهِ وَسَلِّمُوا تَسْلِيمًا ﴿٥٦﴾
Hakika Allaah na Malaika Wake wanamswalia Nabiy. Enyi walioamini mswalieni na msalimieni kwa mamkizi ya amani na kwa tasliymaa. [Al-Ahzaab: 56]

Na kwa vile inajuzu kujikurubisha kwa Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) kwa ‘ibaadah iliyo sahihi, kwa hivyo inajuzu kujikurubisha Kwa kumswalia Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam).

Ama kuielekeza du’aa yako kwa Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) moja kwa moja au kumpa Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) sifa katika sifa za Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa), hiyo haijuzu.

Kujisogeza Kwa Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Kwa Amali Njema

Inajuzu kujisogeza kwa Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) (Kutawassal) kwa ‘amali njema. Kwa mfano, mtu aseme:

"Ee Mola wangu siku moja nilifanya jambo fulani jema, na sikulifanya jambo hilo ila kwa ajili ya kutaka ridhaa yako tu, kwa hivyo kwa ajili ya kitendo changu kile chema nakuomba unikubalie du’aa yangu hii".

Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alitufundisha hayo katika Hadiyth iliyopokewa kutoka kwa Al-Bukhaariy na Muslim. Hadiyth hiyo imo katika kitabu cha Imaam An-Nawawiy kiitwacho Riyaadhus-Swaalihiyn (Hadiyth nambari 13) juu ya wale watu watatu walioingia pangoni kisha jiwe kubwa sana likaanguka na kuifunga njia yao ya kutokea. Kila mmoja wao aliomba kwa ‘amali njema yake na Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Akawafungulia njia yao.

Toba Ya Aadam ('Alayhis Salaam)
Kuhusu usemi wa baadhi ya watu kw
amba Nabii Aadam ('Alayhis Salaam) alipotubu aliomba asamehewe kwa Jaha ya Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam). Hadiyth zilizoegemewa katika kuithibitisha hoja hii ni zile ambazo Ma’ulamaa wa Hadiyth wamezitaja kuwa ni maudhui (za uongo na hazina msingi wowote).


Qur-aan imekweshatujulisha juu ya du’aa aliyoiomba Aadam ('Alayhis Salaam). Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Anasema:

فَدَلَّاهُمَا بِغُرُورٍ ۚ فَلَمَّا ذَاقَا الشَّجَرَةَ بَدَتْ لَهُمَا سَوْآتُهُمَا وَطَفِقَا يَخْصِفَانِ عَلَيْهِمَا مِن وَرَقِ الْجَنَّةِ ۖ وَنَادَاهُمَا رَبُّهُمَا أَلَمْ أَنْهَكُمَا عَن تِلْكُمَا الشَّجَرَةِ وَأَقُل لَّكُمَا إِنَّ الشَّيْطَانَ لَكُمَا عَدُوٌّ مُّبِينٌ ﴿٢٢﴾
Basi akawachota (wote wawili) kwa ghururi. Walipoonja mti ule zikawafichukia sehemu zao za siri; na wakaanza kujibandika majani ya Jannah. Na Rabb wao Akawaita: “Je, kwani Mimi Sikukukatazeni mti huo na kukuambieni kwamba shaytwaan ni adui bayana kwenu?”

قَالَا رَبَّنَا ظَلَمْنَا أَنفُسَنَا وَإِن لَّمْ تَغْفِرْ لَنَا وَتَرْحَمْنَا لَنَكُونَنَّ مِنَ الْخَاسِرِينَ ﴿٢٣﴾
Wakasema: “Rabb wetu! Tumedhulumu nafsi zetu, na basi Usipotughufuria na Ukaturehemu; bila shaka tutakuwa miongoni mwa waliokhasirika.” [Al-‘Aaraf: 22-23]

Natumai inafahamika hapa kwamba; Aadam na mkewe ('Alayhimas Salaam) waliomba toba moja kwa moja kwa Mola wao bila kupitia njia nyingine.

Hadiyth Ya Kipofu

Kipofu mmoja alimwendea Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akamwambia: "Niombee du’aa ili Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) anijaalie niweze kuona.” Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akamwambia: “Ukitaka nitakuombea na kama ukitaka subiri, kwani hiyo ni khayr kwako”. Yule kipofu akasema: "Bora niombee ili nipone". Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akamuamrisha atawadhe vizuri na aswali raka’ah mbili kisha aombe ifuatavyo: ”Mola wangu mimi nakuomba na ninaelekea kwako pamoja na Rasuli wako, Rasuli wa Rahmah, Ee Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) mimi naelekea Kwa Mola wangu pamoja nawe katika haja yangu hii ili ikubaliwe. Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) mkubalie du’aa yake kwa ajili yangu.)) [Imepokewa na At-Tirmidhiy na Ahmad]. Hadiyth inaendelea: "Baada ya kuomba du’aa hii mtu yule akapona".

Jawabu

Baadhi ya watu imewakanganya Hadiyth hii, wakaona kwamba labda inajuzu kuomba kwa baraka au kwa Jaha ya Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) hasa kwa vile kipofu yule alitumia neno: "Atawassal ilayka binabiyyika Muhammad, nabiyyi rahma".  Maana yake ni: "Ninajisogeza kwako pamoja na Mtume wako Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), Rasuli wa Rahmah".

Ukiichunguza, utaona kwamba; tawassul hii imepangika kwa mambo mengi, na haiwi sahihi ila baada ya kupatikana kwa mambo hayo, na baadhi ya mambo hayo hayawezi kupatikana hivi sasa baada ya kufa kwa Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam). Mambo yenyewe ni haya yafuatayo:

a.     Iwapo wakati huu mtu ataomba aseme:
"Ee Rasuli wa Allaah, muombe Mola wako anikidhie haja yangu".
Kauli yake hiyo itakuwa ni batwili na ya upotevu. Kwasababu Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) hamsikii wala hamuoni na wala hatoweza kumuombea kama alivyoombewa kipofu yule.

b.     Iwapo mmoja wetu atasema:

"Mola wangu ninakuomba na ninaelekea kwako pamoja na Rasuli wako.”
Mtu huyo atakuwa muongo, maana Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) hayupo ili aelekee naye na aombe du’aa pamoja naye. Kwasababu maneno hayo husemwa na aliyesimama na Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) mfano wa yule kipofu.
Kwa hivyo tawassul hiyo haifai, kwasababu ya kukosekana kwa nguzo muhimu, nayo ni du’aa ya Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kwa muombaji wa wasiylah.

Hadiyth Ya Kuomba Mvua

Hadiyth ifuatayo pia imewakanganya baadhi ya watu. Hadiyth hiyo inasema hivi:
’Umar bin Khattwaab (Radhwiya Allaahu ‘anhu), alikuwa akimuomba Al-‘Abbaas Ammi yake Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) wakati wa ukame na mvua ilikuwa ikinyesha.
Hadiyth inaendelea:
‘Umar bin Khattwaab (Radhwiya Allaahu ‘anhu) alikuwa wakati wa ukame akimuomba Al’Abbaas Ibn ‘Abdul-Muttwalib na kusema:

"Mola wetu tulikuwa tukikuomba kupitia kwa Rasuli wetu na ukituletea mvua, na sasa tunakuomba kwa njia ya Ammi yake ili utuletee mvua - Walikuwa wakinyeshewa mvua". [Imepokewa na Al-Bukhaariy]

Wamebabaika kwa kudhani kuwa kwa vile ‘Umar (Radhwiya Allaahu ‘anhu) alisema:

"Sisi tulikuwa tukikuomba kupitia kwa Rasuli wetu (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na ukituletea mvua". Wakaona kuwa huu ni ushahidi kwamba ‘Umar (Radhwiya Allaahu ‘anhu) alikuwa akitawassal kwa jaha ya ‘Ammi yake Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam). Kwa hivyo, haina lazima sisi kumuomba Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa). Na kwa vile hapo mwanzoni ‘Umar (Radhwiya Allaahu ‘anhu) alikuwa akitawassal kwa Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), kwa nini basi na sisi tusiuombe kwa njia ya Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam)?

Jibu:

Kule kutawassal kwa Maswahaba wakati wa Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kulikuwa ni kwa kumuomba Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) awaombee du’aa. Naye Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa akiomba, na du’aa yake ilikuwa ikikubaliwa. Hadiyth hiyo kwa ukamilifu inasema hivi:

"Siku moja Mabedui walimuendea Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na kumtaka awaombee du’aa ili mvua inyeshe, maana hata wanyama wao walikuwa wakifa kwa ukame. Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akanyanyua mikono yake juu na kuomba, kabla ya kuishusha chini, mvua kali ilinyesha."

Shaykh Abuu Bakar Al-Jazairiy katika kuisherehesha Hadiyth hii katika kitabu chake kiitwacho “Itikadi ya Muislam” Aqiydatul-Muumin alisema:

Maswahaabah hawakuwa wakiomba kwa kuelekeza du’aa zao kwa Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) mwenyewe, au kwa dhati yake au kwa jaha yake kama wanavyofikiria.

Kwa sababu ingelikuwa ni hivyo basi ‘Umar (Radhwiya Allaahu ‘anhu) asingemuomba Al-‘Abbaas (Radhwiya Allaahu ‘anhu) ili awaombee du’aa. Bali angeomba kwa Jaha ya Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ambaye alikuwa amezikwa pale pale msikitini, karibu yake.

Lakini alielewa kuwa hivyo si sawa na sivyo alivyofundishwa na Rasuli wake (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam). Ndiyo maana baada ya kufa kwake (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), akaona ni vizuri kumtaka ‘Ammi yake Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) awaombee, na alikuwa akiwaombea na kukubaliwa du’aa yao.

Na hii ni dalili kuwa inakubaliwa kumtanguliza mtu mwema ili aombe du’aa na wengine waitikie. Lakini haikubaliwi kumtanguliza maiti au asiyekuwepo na kusema: "Mola wetu tunatawassal kwako kwa jaha ya fulani".

Maana huyo atakayetangulizwa anatakiwa awepo na anyanyue mikono yake juu na kuomba, wakati maiti au asiyekuwepo hawezi kufanya hivyo."

Mwisho wa maneno ya Shaykh Abu Bakar Al-Jazairiy.

Tunamaliza kwa kauli yake Subhaanahu wa Ta’ala katika Suuratul-‘Imraan, aayah ya 79 Aliposema:

مَا كَانَ لِبَشَرٍ أَن يُؤْتِيَهُ اللَّـهُ الْكِتَابَ وَالْحُكْمَ وَالنُّبُوَّةَ ثُمَّ يَقُولَ لِلنَّاسِ كُونُوا عِبَادًا لِّي مِن دُونِ اللَّـهِ وَلَـٰكِن كُونُوا رَبَّانِيِّينَ بِمَا كُنتُمْ تُعَلِّمُونَ الْكِتَابَ وَبِمَا كُنتُمْ تَدْرُسُونَ ﴿٧٩﴾
Ni mustahili kwa mtu kwamba Allaah Amempa Kitabu na Al-Hukma na Unabii kisha awaambie watu: “Kuweni wenye kuniabudu mimi badala ya Allaah” Bali (atawaambia): “Kuweni Wanachuoni waswalihina kwa yale mliyokuwa mkiyafundisha ya Kitabu na kwa yale mliyokuwa mkiyasoma.” [Al-‘Imraan: 79-80]


Jumatatu, 11 Novemba 2019

003-Hiswnul-Muslim: Du’aa Ya Kuvaa Nguo Mpya

[6] 

اللّهُـمَّ لَـكَ الحَـمْـدُ أنْـتَ كَسَـوْتَنيهِ، أَسْأَلُـكَ مِـنْ خَـيرِهِ وَخَـيْرِ مَا صُنِعَ لَـه، وَأَعوذُ بِكَ مِـنْ شَـرِّهِ وَشَـرِّ مـا صُنِعَ لَـهُ.

Allaahumma Lakal Hamdu Anta Kaswtaniyhi. As-aluka min khayrihi wa khayri maa swuni’a lahu, wa a’uwdhu bika min sharrihi wa sharri maa swuni’a lahu

Ee Allaah, Himdi ni Zako, Wewe Ndiye Uliyenivisha, nakuomba kheri ya nguo hii, na kheri ya kila ambacho nguo hii imetengenezewa, na najikinga Kwako kutokana na shari yake, na shari ambayo nguo hii imetengenezewa[1]



 
[1]Hadiyth ya Abu Sa’iyd Al-Khudriyy, Sa’ad bin Maalik (رضي الله عنهما) - Abu Daawuwd na At-Tirmidhiy na Al-Baghaawiy na angalia: Mukhtaswar Shamaail At-Tirmidhiy ya Al-Albaaniy (رحمه الله) (Uk. 47).


Simu Katika Shariy'ah Ya Kiislamu-2

Imekusanywa Na: Sulaymaan ‘Iysaa



4-Dakika na muda wa maongezi

Kipimo chake ni maneno ya kiusuli yasemayo:
  • Kila sehemu pana mazungumzo husika.
  • Na kila mazungumzo yana kipimo husika.
  • Katika kipindi cha nyuma kidogo na mpaka sasa baadhi ya mitandao ya simu imekuwa ikitoa ofa ya kuongea muda mrefu kwa gharama ndogo, na mtu bila kujali kuwa huu ni wakati wa kazi au usiku watu wamelala na kadhalika, anarefusha mazungumzo kisa na mkasa ni kwamba leo ana ofa ya kuongea bure masaa 24 au 12 kwa thamani ndogo ya vocha alizoingiza katika simu yake.

5-Maamkizi ya Kiislamu kwa mwenye kufanya mawasiliano mwanzo na mwisho

Mpigaji simu ni kama vile mjaji katika adabu za ziara, hivyo, atakaporuhusu au kupokea simu nduguyo fanya haraka kumtolea salamu ya Kiislamu “Assalaamu ‘Alaykum” kwani maamkizi haya ni nembo kuu za Uislamu na ni ufunguo wa amani na salama si hivyo tu bali ni sharaf ya Ummat Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) katika mambo yanayowauma sana wasiokuwa Waislamu na haswa Mayahudi ni kuwaona Waislamu na kuwasikia wakitoleana salaam hii “Assalamu ‘Alaykum wa RahmatuLlaahi wa Barakaatuh” na ni lazima kujibu kwa kusema “Wa ‘Alaykumus Salam wa RamatuLlaahi wa Barakaatuh” kwa atakayesikia salaam hii. 

Pamepokelewa katika Sunan Abiy Daawuud kutoka kwa Rabiu (Radhiya Allaahu ‘anhu) anasema, alitueleza mtu mmoja katika kabila la bani Aamir kwamba yeye alitaka idhini kwa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akiwa ndani kwake – akasema yule mtu wakati anabisha hodi, “niingie?” Akasema Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kumwambia mfanyakazi wake: “Toka na umfundishe mtu huyu kubisha hodi – mwambie aseme – Assalaamu ‘Alaykum – Je. niingie? Akasikia yule mtu  akasema, “Assalaamu ‘Alaykum, je, ningie?” Akakaribiswa na Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akaingia. 
Inafahamisha Hadiyth hii juu ya kutanguliza salamu kwa mwenye kufanya ziara – hiyo pia kwa mwenye kufanya mawasiliano na atangulize salaam ya kishari’ah – si kunyamaza au kuanza kwa kusema ‘hallo’ au ‘khabari’, ‘mambo’, n.k.


Hata hivyo baadhi ya salaam ni vizuri
Amepokea Imaam Muslim katika sahihi yake na Abuu Daawuud katika Sunnan yake kuwa Jaabir (Radhwiya Allaahu ‘anhu) amesema: 
“Nilitaka idhini ya kuingia kwa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akasema ni nani huyu anayebisha hodi? Nikasema, “mimi”. Akasema Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), “mimi”, “mimi” – kama kwamba neno hilo lilimkera.”

Ikiwa itatokea mpokea simu hatakufahamu, akataka kujua nani anawasiliana naye, basi taja jina au sifa ya ujumla mfano ‘jina lako’ au ‘kun-yah yako’ na mfano wa hayo. 
 
Kadhalika kujifahamisha kwa jina lako la Kun-yah kama kusema, “mimi Abuu Hannaan” au “mimi Abuu Hasan” au “Abuu Maryam” na kadhalika ikiwa jina kama hilo wewe si maarufu nalo si vyema, bali wema waliotangulia hawakuwa wakijitambulisha hivyo – hili ni kwa wale hayakua majina yao ni maarufu –,  lakini waliojulikana sana kwa Kun-yah zao si vibaya kuyatumia kama ambayo alivyokuwa Abuu Bakr na Abuu Dharr na Ummu Haaniy (Radhwiya Allaahu ‘anhum) ambao walikuwa wakijulikana zaidi kwa majina hayo ya Al-kunaa kuliko majina yao ya asili.

Kisha kama ulivyoanza mazungumzo kwa salaam, kamilisha au funga mazungumzo yako kwa salaam. Ansema Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam):
“Pindi atakapofika mmoja wenu katika kikao chochote basi atoe salaam na atakapo kuamka ili aondoke basi atoe salaam tena, kwani salaam ya mwanzo si kwenye haki (si bora zaidi) kuliko ya mwisho.” Amepokea Abuu Daawuud.


6-Simu na mwanamke

Pindi awapo mmoja kati ya wenye kufanya mawasiliano ni mwanamke, basi na achukue tahadhari yake ya Kiislamu kutolainisha na kuiremba sauti yake, kwani Allaah (Subhanahu wa Ta’ala) Aliwakataza wake wa Nabii Wake (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) mama wa Waumini (Radhiya Allaahu ’anhunna) ambao hakuna yeyote awezae kuwatamani! (kwani kuna yeyote awezae kumtamani mama yake? Ila aliye punguwani) na walikatazwa kulainisha na kuremba sauti zao pindi waongeapo na Maswahaba (Radhiya Allaahu ‘anhum) katika zama tukufu na bora, zama za Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Maswahaba (Radhiya Allaahu ‘anhum). Anasema Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala):
“Na wala msilainishe sauti zenu kwa neno lolote mlisemalo akatamani yule ambaye katika moyo wake pana maradhi ya kutamani. Na semeni maneno mema.” Al-Ahzaab: 32

Vipi kwa wanawake wa zama zetu? Uongeavyo na mumeo; mumeo mrembee na umpambie sauti na maneno pia. Zama zisizo bora, zama zilizojaa uovu na uchafu wa kila aina? Hakika kulainisha na kuremba sauti zao kunakatazwa zaidi. Hivyo mcheni Mola wenu enyi wanawake wa Kiislamu msilainishe wala kuziremba sauti zenu pindi muongeapo na watu wasi Mahrim zenu (ajnabiy) iwe ndani ya simu au laa; kwa ufupi usiongee na mwanaume yeyote kama

Kadhalika si vizuri kuchukua muda mrefu kuongea na kutoa sauti kubwa isiyokuwa na haja ya kunyanyuliwa isipokuwa kiasi cha kusikilizana wao wawili tu.  Na itakapokuwa hali ni kama hivi tulivyoeleza (yaani mwanamke anaongea kwa sauti laini iliyojaa kila aina za kurembwa, inakuwa ni haramu mwanaume kwa kuhofia fitna kuendelea kumsikiliza na kuongea nae hata kama mwanamke huyo anasoma Qur-aan kwa sauti iliyo jaa mahaba na kadhalika).

Na hapa tunajifunza pia, kwa mwanaume mwenye wivu na mwenye kuijua dini yake vizuri mchunga wa familia yake kimaadili na kitabia, kama anavyojihifadhi kiafya – basi na aijifadhi na yaliyo haramu, asiwe mwanamke ni wa kwanza kupokea simu, kuitikia, na kukaribisha mbisha hodi pindi awapo mwaname nyumbani.

Tumeona  katika sehemu ya (5) Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ndiye aliyekuwa akiuliza nani mbisha hodi? Na si wake zake au watoto wake wa kike.

Imetukuka kimaadili nyumba ile ambayo ipo chini ya msimamizi, mchunga, mwenye akili na mwenye elimu, si mkali wala mwenye hasira, ila mwenye kumuudhi Allaah. Na imepata hasara nyumba ile ambayo haina msimamizi, mchunga mwenye akili, wala elimu. Simu ya baba mwenye nyumba kila mtu ni yake; ikiita tu mara mtoto kapokea, au mke wake, au mfanyakazi wake wa ndani, na kila mmoja kati ya wao aigombea si mdogo wala mkubwa!! Maskini aliyepiga hajulikani au ajulikana basi akiipokea mke ataongea kama vile anamjua, au kama ni baba yake mzazi aliyepotezana nae muda mrefu – Ya Allaah Mola wetu – ni mara ngapi matatizo hutokea katika majumba yetu kwa sababu hizi? Ee Mola wetu kwa upole Wako na sitara Yako tusitiri wewe ni Mwingi wa rahma na huruma tuhurumie, Aamiyn, Aamiyn.


7-Simu na miito (kengele) au miziki

Watu (watumia simu) katika hili wamegawanyika pande mbili zenye kupingana:
(1) Kuna watu ambao simu zao zikiita au ukiwapigia patasikika zikiita kwa kutoa sauti za pumbao miongoni mwa nyimbo na muziki na kadhalika, hili ni haramu.

(2) Na kuna watu ambao simu zao zikiita au ukiwasiliana nao patasikika katika simu zao sauti za Qur-aan ikisomwa au dhikri na kadhalika na pindi iitapo simu hapawezekani kabisa kusubiri mpaka msomaji afike mwisho wa Aayah wala dhikri au Hadiyth iishe. Hivyo, panatokeya kusimamisha au kupokea simu katika Aayah kabla ya jumla (sentensi) haijakamilika; kwani ni vigumu mno kusubiri kwa kuzingatia yafuatayo:

(a) Ikiwa aliyepiga simu mtu anayemdai muda mrefu na aliahidi kuwa leo saa fulani atawasiliana nawe ili mkutane sehemu apate kukulipa deni lako, kwa tamaa na hamu ya kulipwa deni lako, hutoweza kusubiri mpaka Aayah imalizwe!

(b)  Ikiwa aliyepiga simu mathalani ni mmoja kati ya jamaa zako aliyekuwa amebaki na mgonjwa wenu hospitalini au nyumbani na hali yake haikuwa nzuri bali yu hoi taabani kadhalika katika hali kama hii pia hapawezekani kusubiri mpaka msomaji afike mwishoni mwa Aayah au jumla au pia Hadiyth iishe.
Hivyo kutampelekea kusimama au kupokea simu sehemu isiyoridhiwa kishariy’ah mfano Suwratul Anfaal Aayah 1:
يَسْأَلُونَكَ عَنِ الْأَنفَالِ 
“Wanakuuliza kuhusu ngawira…”
Akipokea simu kabla jumla haijaisha: يَسْأَلُونَكَ عَنِ الْأَنف 
Maana inakua:  “Wanakuuliza kuhusu pua”, na si “wanakuuliza kuhusu ngawira” (mali igawiwayo baada ya vita), hili nalo halifai (yaani kujaalia Qur-aan ndiyo mwito wa kukuita ili upokee simu au dhikri au mawaidha au du'aa na kadhalika).  

Bali Qur-aan haikuletwa ila iwe ni mawaidha na kuwaonya na kuwaelekeza watu wazuri na kuwakataza watu mabaya tazama Suwrat Yaasiyn (69–70) haikuwa Qur-aan ila ni ukumbusho na Kitabu kibainishacho kila yanayohitajiwa ili imwonye aliye hai hai na ihakikike kauli (ya kuadhibiwa) juu ya Makafiri. 

Hivyo kuifanya Qur-aan ndio mwito wa wewe kupokelea simu ni jambo baya kabisa mbele ya Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) ni madharau ya Kitabu Chake na ni kejeli na maneno Yake.

Watu wema walikuwa wakiheshimu mno maneno ya Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) bali hata ya Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) mfano mmoja tu katika hilo kisa cha Imaam Daarul Hijrah, Imaam Maalik (Rahimahu Allaah) alipokuwa akidarisisha (akifundisha) Hadiyth za bwana Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) katika kitabu chake “Al-Muwatwaa” katika Msikiti wa Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) huko Madiynah, ghafla akang’atwa na nge (mdudu mkali mwenye sumu kali mno – baadhi ya watu wakiumwa na mdudu huyu hupoteza fahamu, wengine hutokwa na povu jingi mdomoni, wengine hubaki na maumivu muda wa masaa 12 na wakati mwengine masaa 24) nge huyo alimng’ata Imaam Maalik (Rahimahu Allaah) mara tatu! Na kila mara Imaam anashtuka kidogo lakini hakatishi Hadiyth ya Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) baada ya kumaliza akawaambia wanafunzi wake, angalieni hapa chini kuna nini? Wakafungua na kunyanyua tandiko alilokalia tahamaki wanamuona nge. (Imaam Maalik (Rahimahu Allaah) akawaonyesha sehemu alizomuuma mara wanazikuta ni tatu!
Wakasema wanafunzi kwanini  Imaam usikatize Hadiyth mara alipokuuma tu, tukamuua kisha ukaendelea na Hadiyth? Akawajibu Imaam maneno yenye maana: “Haikuwa kwangu ni rahisi kukatisha maneno ya bwana Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kwa sababu ya nge aliyening’ata!

Ona hiyo heshima waliyokuwa nayo, kisha tazama hali tulizo nazo sisi na maneno ya Allaah!! Tazama hali tulizonazo sisi na Hadiyth za Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam)!! Kwetu ni miito ya kutujulisha kwa kuna mtu kakupigia simu!! Yaa Allaah ya Kariym, Kwake pekee twashtakia unyonge wetu – tutengeneze Yaa Allaah hali zetu.


8-Kutorekodi maneno ya mwenzio

Adabu ya nane na ya mwisho, ni kutorekodi maneno ya mwenzio vyovyote yatakayokuwa maneno – ya kidini au kidunia ila kwa idhini yake au kwa kumjuilisha kabla –, hakika pamethibiti Hadiyth sahihi kama ilivyokuja katika Sunnan At-Tirmidhiy au Abuu Daawuud na Musnad Ahmad bin Hanbal (Rahimahum Allaah) kutoka kwa Jaabir bin Abdillaah Al-Answaariy (Radhwiya Allaahu 'anhu) kuwa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:
“Pindi atakapozungumza mtu na mtu kabla ya kuzungumza akatazama huku na huku basi hiyo ni dalili tosha kuwa hiyo ni amana.”
Imamu Raaghib (Rahimahu Allaah) anasema, siri zipo aina mbili:

(1) Ni ili aisemayo mwana mwana Aadam akataka ifichwe kwa kusema kwake mwishoni mwa mazungumzo: “Hii ni siri baina yangu mimi na wewe” au “ficha siri hii” au “usimwambie mtu haya.”

(2) Siri ijulikanayo bila kuambiwa bali mazingira yanatosha kukufahamisha hii ni siri usiitoe kama kujitahidi mzungumzaji maneno yenu yawe yenu tu – kwa kutoka pembeni au kukunong’oneza au kwa kuangalia huku na huku… na kadhalika.

Na simu inaingia katika hali zote hizi mbili, hivyo kusajili au kurekodi bila idhini yake ni khadaa na makosa, bali kosa kubwa kabisa ni kule kurekodi bila idhini yake na kumjuilisha kisha ukayaeneza yale mliyoongea naye kwa watu wengine, Hilo ni baya mno na ni kubomoa amana.

Allaah Atuhifadhi na yote mabaya Allaahumma Aamiyn.


Mwisho


Nimekusanya Adabu hizi toka sehemu tofauti, lakini kubwa zaidi nimerejea sana katika risala ya Shaykh Bakr bin 'Abdillaah Abuu Zayd (Rahimahu Allaah) aliyoiita “Aadabul-Haatwif.”


20-Hakika Shirki Ni Dhulma Kubwa Mno! - Isti’aadhah Kwa Asiyekuwa Allaah

  إِنَّ الشِّرْكَ لَظُلْمٌ عَظِيم   Hakika Shirki Ni Dhulma Kubwa Mno!   20 - Isti’aadhah  (Kuomba Kinga) Kwa Asiyekuwa Allaah   ...