Translate

Jumatatu, 1 Julai 2019

Sayyidul-Istighfaar - Dua Bora ya Kuomba Maghfirah

Du’aa hii imeitwa Sayyidul-Istighfaar (Du’aa bora au adhimu kabisa ya kuomba maghfirah kuliko istighfaar nyenginezo) kwa sababu imekusanya kukiri Tawhiyd Al-Uluwhiyyah (‘ibaadah), Tawhiyd Ar-Rubuwbiyyah (Uola), kukiri dhambi za mja, kunyenyekea mja kwa Rabb wake, kutambua neemah za Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) na kumuomba Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Amghufurie madhambi yote.

 اللّهـمَّ أَنْتَ رَبِّـي لا إلهَ إلاّ أَنْتَ، خَلَقْتَنـي وَأَنا عَبْـدُك، وَأَنا عَلـى عَهْـدِكَ وَوَعْـدِكَ ما اسْتَـطَعْـت، أَعـوذُبِكَ مِنْ شَـرِّ ما صَنَـعْت، أَبـوءُ لَـكَ بِنِعْـمَتِـكَ عَلَـيَّ وَأَبـوءُ بِذَنْـبي فَاغْفـِرْ لي فَإِنَّـهُ لا يَغْـفِرُ الذُّنـوبَ إِلاّ أَنْتَ .
Allaahumma Anta Rabbiy laa ilaaha illaa Anta Khalaqtaniy wa ana ‘abduka wa anaa ‘alaa ‘ah-dika wawa’-dika mastatwa’-tu, a’uwdhu bika min sharri maa swana’-tu, abuw-u Laka bini’-matika ‘alayya wa abuw-u bidhanbiy, faghfir-liy fainnahu laa yaghfirudh dhunuwba illaa Anta
Ee Allaah, Wewe ni Rabb wangu, hapana muabudiwa wa haki ila Wewe, umeniumba mimi na mimi ni mja Wako, nami niko juu ya  ahadi Yako, na agano Lako, kiasi cha uwezo wangu, najikinga Kwako kutokana na shari ya nilichokifanya, nakiri  Kwako kwa kunineemesha, na nakiri kwa madhambi yangu, basi nakuomba unighufurie  kwani hakuna wa kughufuria  madhambi ila Wewe.

Hadiyth ya Shaddaad bin ‘Aws (Radhwiya Allaahu ’anhu) kwamba Nabiy (Swalla Allaahu ’alayhi wa aalihi wa sallam amesema:

((مَنْ قَالَهَا مِنْ النَّهَارِ مُوقِنًا بِهَا فَمَاتَ مِنْ يَوْمِهِ قَبْلَ أَنْ يُمْسِيَ فَهُوَ مِنْ أَهْلِ الْجَنَّةِ، َنْ قَالَهَا مِنْ اللَّيْلِ وَهُوَ مُوقِنٌ بِهَا فَمَاتَ قَبْلَ أَنْ يُصْبِحَ فَهُوَ مِنْ أَهْلِ الْجَنَّةِ))
((Atakayesema mchana akiwa na yakini nayo, akafariki siku hiyo kabla kuingia jioni basi atakuwa mtu wa Jannah, na atakayesema usiku naye akiwa yakini nayo akafariki kabla hajafika asubuhi basi yeye ni mtu wa Jannah))  [Al-Bukhaariy (7/150) [2306]- Sayyid Al-Istighfaar]


Na Anasema pia ('Azza wa Jalla)  Anasema:

وَالَّذِينَ إِذَا فَعَلُوا فَاحِشَةً أَوْ ظَلَمُوا أَنفُسَهُمْ ذَكَرُوا اللَّـهَ فَاسْتَغْفَرُوا لِذُنُوبِهِمْ وَمَن يَغْفِرُ الذُّنُوبَ إِلَّا اللَّـهُ وَلَمْ يُصِرُّوا عَلَىٰ مَا فَعَلُوا وَهُمْ يَعْلَمُونَ﴿١٣٥﴾
Na wale ambao wanapofanya machafu au wakajidhulumu nafsi zao (kwa maasi), humdhukuru Allaah wakaomba maghfirah kwa madhambi yao. Na nani anayeghufuria madhambi isipokuwa Allaah. Na hawaendelei katika waliyoyafanya na wao wanajua. [Aal-‘Imraan: 135]


Na kisa cha kusisimua kuhusu kuomba tawbah katika Hdiyth ya Nabiy  (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam):

عن أَنَسُ بْنُ مَالِكٍ قَالَ: قَالَ رَسُولُ اللَّهِ صلى الله عليه وسلم: ((الَلَّهُ أَشَدُّ فَرَحًا بِتَوْبَةِ عَبْدِهِ حِينَ يَتُوبُ إِلَيْهِ مِنْ أَحَدِكُمْ كَانَ عَلَى رَاحِلَتِهِ بِأَرْضِ فَلاَةٍ فَانْفَلَتَتْ مِنْهُ وَعَلَيْهَا طَعَامُهُ وَشَرَابُهُ فَأَيِسَ مِنْهَا فَأَتَى شَجَرَةً فَاضْطَجَعَ فِي ظِلِّهَا قَدْ أَيِسَ مِنْ رَاحِلَتِهِ فَبَيْنَا هُوَ كَذَلِكَ إِذَا هُوَ بِهَا قَائِمَةً عِنْدَهُ فَأَخَذَ بِخِطَامِهَا ثُمَّ قَالَ مِنْ شِدَّةِ الْفَرَحِ: "اللَّهُمَّ أَنْتَ عَبْدِي وَأَنَا رَبُّكَ" ‏ أَخْطَأَ مِنْ شِدَّةِ الْفَرَحِ)) مسلم
((Allaah Alifurahikiwa sana na tawbah ya mja Wake  aliyekuwa katika msafara  kwenye jangwa (la joto kali  hakuna mtu) Akapotelewa na mnyama wake,  chakula  na maji, akakata tamaa ya kuvipata tena, akapumzika kidogo chini ya mti kupata kivuli chake, baada ya muda hivi mara kamuona mnyama wake kamsimamia (na vitu vyake),  kwa ile furaha akasema,  "Ee Allaah, Wewe ni mja wangu na mimi ni Rabb wako.” Alikosea (kumshukuru Rabb wake) kwa wingi wa furaha aliyokuwa nayo))  [Muslim]

Maana ya Allaah (‘Azza wa Jalla)  kuifurahia tawbah  hiyo ni kuwa anaridhika na niyyah ya mja wake huyo juu ya kuwa alikosea kutamka.

1-Allaah (‘Azza wa Jalla) Anawapenda waja Wake wanaomuomba tawbah:

Anasema Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa):

 إِنَّ اللَّـهَ يُحِبُّ التَّوَّابِينَ وَيُحِبُّ الْمُتَطَهِّرِينَ ﴿٢٢٢﴾
Hakika Allaah Anapenda wenye kutubia na Anapenda wenye kujitwaharisha. [Al-Baqarah: 222]



2-Kuomba maghfirah na tawbahnyakati za usiku hakuna shaka kuwa Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Anapokea tawbah:

 عَنْ أَبِي هُرَيْرَةَ رَضِيَ اللَّهُ عَنْهُ أَنَّ رَسُولَ اللَّهِ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ قَالَ: ((يَنْزِلُ رَبُّنَا تَبَارَكَ وَتَعَالَى كُلَّ لَيْلَةٍ إِلَى السَّمَاءِ الدُّنْيَا حِينَ يَبْقَى ثُلُثُ اللَّيْلِ الْآخِرُ يَقُولُ: مَنْ يَدْعُونِي فَأَسْتَجِيبَ لَهُ مَنْ يَسْأَلُنِي فَأُعْطِيَهُ مَنْ يَسْتَغْفِرُنِي فَأَغْفِرَ لَهُ)) البخاري و مسلم    

Imetoka kwa Abuu Hurayrah (Radhwiya Allaahu ‘anhu) kwamba Rasuli wa Allaah  (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam)  amesema: ((Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Huteremka (kwa namna inavyolingana na utukufu Wake) kila siku katika mbingu ya dunia (mbingu ya kwanza) inapobakia thuluthi ya mwisho ya usiku na Husema: Nani ananiomba Nimtakabalie? Nani Ana shida Nimtekelezee? Nani ananiomba maghfirah Nimghufurie?)) [Al-Bukhaariy, Muslim]


3-Kuomba Maghfirah Na Tawbah Kunasababisha Kujaaliwa Starehe Na Maisha Mazuri:  

Ameamrishwa Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) awaambie watu wake:  

وَأَنِ اسْتَغْفِرُوا رَبَّكُمْ ثُمَّ تُوبُوا إِلَيْهِ يُمَتِّعْكُم مَّتَاعًا حَسَنًا إِلَىٰ أَجَلٍ مُّسَمًّى وَيُؤْتِ كُلَّ ذِي فَضْلٍ فَضْلَهُ ۖ وَإِن تَوَلَّوْا فَإِنِّي أَخَافُ عَلَيْكُمْ عَذَابَ يَوْمٍ كَبِيرٍ﴿٣﴾
Na kwamba: “Mwombeni Rabb wenu maghfirah kisha tubuni Kwake, Atakustarehesheni starehe nzuri mpaka muda maalumu uliokadiriwa; na Atampa kila mwenye fadhila, fadhila Zake. Na mkikengeuka, basi hakika mimi nakukhofieni adhabu ya Siku kubwa.” [Huwd: 3]


4-Kuomba Maghfirah Na Tawbah Kunasabisha Kuletewa neema ya mvua na kuzidishiwa nguvu:


Nabiy Huwd ('Alayhis-Salaam) aliwaambia watu wake:

وَيَا قَوْمِ اسْتَغْفِرُوا رَبَّكُمْ ثُمَّ تُوبُوا إِلَيْهِ يُرْسِلِ السَّمَاءَ عَلَيْكُم مِّدْرَارًا وَيَزِدْكُمْ قُوَّةً إِلَىٰ قُوَّتِكُمْ وَلَا تَتَوَلَّوْامُجْرِمِينَ﴿٥٢﴾
 “Na enyi kaumu yangu!  Mwombeni maghfirah Rabb wenu, kisha tubieni Kwake, Atakuleteeni mbingu zenye kunyesha mvua tele ya kumiminika na Atakuzidishieni nguvu juu ya nguvu zenu, na wala msikengeuke mkawa wahalifu.” [Huwd: 52]


5-Kuomba Maghfirah Na Tawbah kunasababisha kumiminiwa mvua tele, mali na watoto, na kupewa  kila aina ya neema:


Nabiy Nuwh ('Alayhis-Salaam) alipowalingania watu wake miaka ili awatoe katika shirki, aliwanasihi waombe maghfirah na tawbah na akawatajia fadhila na faida zake:
فَقُلْتُ اسْتَغْفِرُوا رَبَّكُمْ إِنَّهُ كَانَ غَفَّارًا﴿١٠﴾
Nikasema: “Ombeni maghfirah kwa Rabb wenu; hakika Yeye ni Mwingi mno wa kughufuria.

يُرْسِلِ السَّمَاءَ عَلَيْكُم مِّدْرَارًا﴿١١﴾
 “Atakutumieni mvua tele ya kuendelea.”


وَيُمْدِدْكُم بِأَمْوَالٍ وَبَنِينَ وَيَجْعَل لَّكُمْ جَنَّاتٍ وَيَجْعَل لَّكُمْ أَنْهَارًا﴿١٢﴾
 “Na Atakuongezeeni mali na wana, na Atakupeni mabustani na Atakupeni mito.” [Nuwh: 10-12]


6-Kuomba Maghfirah Na Tawbah kunasababisha Kuingizwa Jannah:

Anasema Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa):

وَالَّذِينَ إِذَا فَعَلُوا فَاحِشَةً أَوْ ظَلَمُوا أَنفُسَهُمْ ذَكَرُوا اللَّـهَ فَاسْتَغْفَرُوا لِذُنُوبِهِمْ وَمَن يَغْفِرُ الذُّنُوبَ إِلَّا اللَّـهُ وَلَمْ يُصِرُّوا عَلَىٰ مَا فَعَلُوا وَهُمْ يَعْلَمُونَ ﴿١٣٥﴾
Na wale ambao wanapofanya machafu au wakajidhulumu nafsi zao (kwa maasi), humdhukuru Allaah wakaomba maghfirah kwa madhambi yao. Na nani anayeghufuria madhambi isipokuwa Allaah. Na hawaendelei katika waliyoyafanya na wao wanajua.

أُولَـٰئِكَ جَزَاؤُهُم مَّغْفِرَةٌ مِّن رَّبِّهِمْ وَجَنَّاتٌ تَجْرِي مِن تَحْتِهَا الْأَنْهَارُ خَالِدِينَ فِيهَا ۚ وَنِعْمَ أَجْرُ الْعَامِلِينَ ﴿١٣٦﴾
Hao jazaa yao ni maghfirah kutoka kwa Rabb wao na Jannaat zipitazo chini yake mito, ni wenye kudumu humo. Na uzuri ulioje ujira wa watendaji (wema). [Aal-‘Imraan: 135-136]


7-Kuomba Maghfirah Na Tawbah kunasababisha Kuwekewa  Nuru katika Swiraatw  Siku ya Qiyaamah ambayo itammulika mtu atakapokuwa akiivuka hiyo njia:


Anasema Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa):

يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا تُوبُوا إِلَى اللَّـهِ تَوْبَةً نَّصُوحًا عَسَىٰ رَبُّكُمْ أَن يُكَفِّرَ عَنكُمْ سَيِّئَاتِكُمْ وَيُدْخِلَكُمْ جَنَّاتٍ تَجْرِي مِن تَحْتِهَا الْأَنْهَارُ يَوْمَ لَا يُخْزِي اللَّـهُ النَّبِيَّ وَالَّذِينَ آمَنُوا مَعَهُ ۖ نُورُهُمْ يَسْعَىٰ بَيْنَ أَيْدِيهِمْ وَبِأَيْمَانِهِمْ يَقُولُونَ رَبَّنَا أَتْمِمْ لَنَا نُورَنَا وَاغْفِرْ لَنَا ۖ إِنَّكَ عَلَىٰ كُلِّ شَيْءٍ قَدِيرٌ﴿٨﴾
Enyi walioamini! Tubieni kwa Allaah tawbah ya nasuha (kwelikweli); asaa Rabb   wenu Akakufutieni maovu yenu, na Akakuingizeni Jannaat zipitazo chini yake mito. Siku ambayo Allaah Hatomfedhehesha Nabiy (Muhammad Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na wale walioamini pamoja naye. Nuru yao itatembea mbele yao na kuliani mwao, watasema: “Rabb wetu! Tutimizie Nuru yetu, na Tughufurie, hakika Wewe juu ya kila kitu ni Muweza. [At-Tahriym: 8]



8-Kuomba Maghfirah Na Tawbahni mojawapo wa Sifa Za Waja Wa Rahmaan na kunasababisha kubadilishiwa maovu ya mtu na badala yake kugezwa kuwa mema:


Anasema Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) katika kutaja sifa za ‘Ibaadur-Rahmaah (Waja wa Rahmaan):

وَالَّذِينَ لَا يَدْعُونَ مَعَ اللَّـهِ إِلَـٰهًا آخَرَ وَلَا يَقْتُلُونَ النَّفْسَ الَّتِي حَرَّمَ اللَّـهُ إِلَّا بِالْحَقِّ وَلَا يَزْنُونَ ۚ وَمَن يَفْعَلْ ذَٰلِكَ يَلْقَ أَثَامًا ﴿٦٨﴾
Na wale ambao hawaombi pamoja na Allaah mwabudiwa mwengine na wala hawaui nafsi ambayo Allaah Ameiharamisha isipokuwa kwa haki, na wala hawazini. Na atakayefanya hivyo atakutana na adhabu.

يُضَاعَفْ لَهُ الْعَذَابُ يَوْمَ الْقِيَامَةِ وَيَخْلُدْ فِيهِ مُهَانًا ﴿٦٩﴾
Ataongezewa adhabu maradufu Siku ya Qiyaamah, na mwenye kudumu humo akiwa amedhalilika.

إِلَّا مَن تَابَ وَآمَنَ وَعَمِلَ عَمَلًا صَالِحًا فَأُولَـٰئِكَ يُبَدِّلُ اللَّـهُ سَيِّئَاتِهِمْ حَسَنَاتٍ ۗ وَكَانَ اللَّـهُ غَفُورًا رَّحِيمًا ﴿٧٠﴾
Isipokuwa yule aliyetubu na akaamini na akatenda ‘amali njema; basi hao Allaah Atawabadilishia maovu yao kuwa mema.  Na Allaah daima ni Mwingi wa kughufuria, Mwenye kurehemu.

وَمَن تَابَ وَعَمِلَ صَالِحًا فَإِنَّهُ يَتُوبُ إِلَى اللَّـهِ مَتَابًا ﴿٧١﴾
Na atakayetubu na akatenda mema, basi hakika yeye anatubia kwa Allaah tawbah ya kweli.  [Al-Furqaan: 68-71]


9-Kuomba Maghfirah Na Tawbah kabla ya Alfajiri ni  ‘amali mojawapo za watakaoingia Jannah. Anasema Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa):

إِنَّ الْمُتَّقِينَ فِي جَنَّاتٍ وَعُيُونٍ﴿١٥﴾
Hakika wenye taqwa watakuwa katika Jannaat na chemchemu. 

آخِذِينَ مَا آتَاهُمْ رَبُّهُمْ ۚ إِنَّهُمْ كَانُوا قَبْلَ ذَٰلِكَ مُحْسِنِينَ﴿١٦﴾
Wakichukua yale Atakayowapa Rabb wao. Hakika wao walikuwa kabla ya hapo ni wahisani.

كَانُوا قَلِيلًا مِّنَ اللَّيْلِ مَا يَهْجَعُونَ﴿١٧﴾
Walikuwa kidogo tu katika usiku wakilala kwa raha. 
وَبِالْأَسْحَارِ هُمْ يَسْتَغْفِرُونَ﴿١٨﴾
Na kabla ya Alfajiri wakiomba maghfirah.
[Adh-Dhaariyaat: 15-18]


WabiLlaahi At-Tawfiyq



Muislamu Kufuga Rasta

Kuna aina Ngapi za Dhulma?

Hukmu ya Muislamu Anayejiua

                                                     Hukmu ya Muislamu Anayejiua





Uislamu umetukataza kujiua na yeyote mwenye kujiua atakuwa ametenda madhambi makubwa na yatakayomsababishia kuingia motoni na kuharamishiwa pepo. Isitoshe, ataadhibiwa kwa chombo kilekile alichotumia kujiulia. Allaah Aliyetukuka Atuepushe kabisa na balaa hilo la kujinyonga au kujiua kwa njia yoyote ile.

Anasema Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) kutoka katika Hadiyth iliyosimuliwa na Abu Hurayrah,
"Yeyote atakayejitupa kutoka mlimani na kujiua, atatupwa ndani ya moto milele. Atakayekunywa sumu na kujiua, basi atatupwa motoni na huko atakuwa akiinywa hiyo sumu milele. Atakayejiua kwa kipande cha chuma, atatiwamotoni akiwa na kipande hicho cha chuma akijitwanga nacho tumboni kwake humo motoni milele." Al-Bukhaariy na Muslim

Kadhaalika, mtu anayejiua, au jambazi, au aliyefariki kwa kutumia madawa ya kulevya au kuuza, mlevi n.k. wote hao watatengwa kuswaliwa na Viongozi wa Dini ili iwe funzo kwa wale wenye tabia hizo waweze kujiepusha na maovu hayo. Lakini, hata hivyo, wanaweza kuswaliwa na watu wa kawaida.


HUKUMU  YA  KUJIUA KWA SABABU YA MATESO NA MITIHANI YA KIDUNIA


Tufahamu kuwa mitihani katika hii dunia na haswa kwa Muumini ni lazima. Na kila mmoja anapimwa na Allaah Aliyetukuka kwa kiasi cha Imani yake. Allaah Aliyetukuka Anasema:
“Je! Wanadhani watu wataachwa kwa kuwa wanasema: Tumeamini. Nao wasijaribiwe? Hakika Tuliwajaribu waliokuwa kabla yao, na kwa yakini Allaah Atawatambulisha walio wa kweli na Atawatambulisha walio waongo” [Al-Ankabut [29]: 2 – 3].
Na tena:
“Mnadhani kuwa mtaingia Peponi, bila ya kukujieni kama yaliyo wajia wale waliopita kabla yenu? Iliwapata shida na madhara na wakatikiswa hata Mtume na walio amini pamoja naye wakasema: Lini nusura ya Allaah itakuja? Jueni kuwa nusura ya Allaah ipo karibu” [Al-Baqarah [2]: 214].

Mtume (Swalla Allaahu ‘Alayhi wa aalihi wa sallam) anatuelezea kuwaMuislamu mzuri ni yule anaponeemeshwa hushukuru na hiyo ikawa ni kheri kwake na anapopata mitihani husubiri, na hiyo pia ikawa ni kheri kwake. [Muslim].

Kujiua kwa sababu ya mateso ni miongoni mwa madhambi makubwa inayompeleka mwenye kufanya kitendo hicho motoni. Kwa hivyo, mwenye kujiua makaazi yake siku ya Kiyama ni Motoni.  Dalili kutoka Hadiyth zifuatazo:

Kutoka kwa Jundab kwamba Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: “Mtu alifikwa na maafa ya majeraha akajiua, hivyo Allaah Amesema: Mja wangu amejisababisha kufa mwenyewe kwa kuharakiza, hivyo Nimemharamisha Pepo.” [Al-Bukhaary]

Kutoka kwa Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu ‘anhu) kwamba Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:  “Yeyote atakayejitupa kutoka mlimani na kujiua ataingia motoni akiuangukia ambako ataishi humo milele. Na yeyote atakayekunywa sumu na kujiua nafsi yake, atabeba sumu yake mkononi mwake huku anainywa motoni ambako ataishi milele. Na yeyote atakayejiua kwa silaha ya chuma, atabeba silaha yake mkononi mwake na huku anajichinja tumbo lake motoni ambako ataishi milele.” [Al-Bukhaariy]


Anas bin Maalik ameripoti kuwaMtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: “Asiombe mmoja wenu kufa kwa sababu ya shida iliyomfika, bali ikiwa hakupata msaada aombe (du’aa) “Ee Allaah, nijaalie niishi ikiwa uhai kwangu ni kheri na nipe mauti ikiwa mauti kwangu ni kheri kwangu” [Muslim]

Kadhaalika, mtu anayejiua, au jambazi, au aliyefariki kwa kutumia madawa ya kulevya au kuuza, mlevi n.k. wote hao watatengwa kuswaliwa na Viongozi wa Dini ili iwe funzo kwa wale wenye tabia hizo waweze kujiepusha na maovu hayo. Lakini, hata hivyo, wanaweza kuswaliwa na watu wa kawaida.


Allaah Aliyetukuka Atuepushe na balaa la kujiua na mabalaa mengine kama hayo.


Na Allaah Anajua zaidi.



Vidani Vya Fedha Vinafaa kuvaliwa na Wanaume na Kuswali navyo?

SWALI


Natumai hali zenu zote ni nzuri, nimefurahi sana waislam kupata website hii inayotupa mafunzo mbalimbali ya dini yetu. Swali langu ni kuhusu vidani vya madini ya silver ambavyo vijana wengi wa kiislam wanavivaa, je ni halali kuvaliwa? Na ikiwa kuruhusiwa kuswali navyo? Au kuna uzito Fulani (grams) ni ruhusa?


JIBU


Vidani aina yoyote ile kama ni dhahabu, fedha, shaba na kadhalika havifai kwa mwanamme kwani hayo ni mapambo kwa wanawake. 


Na Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amekataza pamoja na kuwalaani wanaume wote wanaojifananisha na wanawake na kinyume chake. Mbali na hivyo uvaaji wa vidani ni ‘amali ya makafiri ambao pia sheria imetutaka tuwe tofauti nao.

Ibn ‘Abbaas (Radhwiya Allaahu ‘anhumaa) amesema: “Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amewalaani wanaume wanaojifananisha na wanawake na wanawake wanaojifananisha na wanaume” [al-Bukhaariy, Abuu Daawuwd, at-Tirmidhiy na Ibn Maajah].

Hivyo, ni vyema kabisa kwa Muislamu mwanamme aachane na kuvaa vidani. Kwa hiyo, haifai kuvivaa katika Swalaah au wakati mwingine wowote.

Na Allaah Anajua zaidi


Swalaatul-ghayb (Kumswalia Swalah Maiti Aliyefia Mbali)

                       Swalaatul-ghayb (Kumswalia Swalah Maiti Aliyefia Mbali)



SWALI

Je inafaa kwa waisilam kumsalia maiti ikiwa hayupo mbele yao?  Ama kuwa nchi nyengine au sehemu nyengine mji ulele.

   
JIBU

Wametofautiana Maulamaa kuhusu Swalaatul-Ghayb (Swalaah ya Jeneza ya Asiyekuwepo. 


Imaam Ash-Shaafi’iy na Imaam Ahmad wamekwenda kwa mtazamo wa kuwa jambo hili lafaa kishari’ah kwa kutolea dalili hoja zao kwa Hadityh hii: 


Kutoka kwa Abuu Hurayrah  (Radhwiya Allaahu 'anhu) kwamba Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam)    alitangaza kifo cha Mfalme An-Najjaashiy siku aliyokufa akatoka nao katika Mswalla akapanga safu nao akapiga Takbira nne.   [Al-Bukhaariy na Muslim].

Alimuombolezea An-Najaashiy katika siku ailiyofariki, na akatoka na Maswahaba zake kwenda kumswalia katika kiwanja, kisha akawatangulia kwenye safu na akapiga takbira nne. 

Inajulikana kuwa huyu An-Najaashiy alikuwa ni Mfalme kule Uhabashi (Ethiopia) alikuwa Mkiristo mwanzo na kisha alisilimu kwa siri na alipofariki Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam)  alijulishwa kifo chake na akamswalia.

Ama Imaam Abuu Haniyfah na Imaam Maalik wamekwenda katika msimamo kuwa Swalaatul-ghayb haifai ki-shariy’ah. Na hoja yao ni jawabu lao kuhusiana na kisa cha An Najaashiy kuswaliwa na Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) ni jambo lenye kumhusu (Khususiyaat) Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) pekee. Na inawezekana kuwa kitanda cha An-Najaashiy kilinyanyuliwa hadi kwa Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam)   na akamswalia mbele ya hadhara.

Na wakasema (upande wa Mahanafi na Maalik) kuwa, Haikupokelewa kuwa wakati wa Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam)  alikuwa akiwaswalia wale wanaokufa ambao wako mbali naye. Na wakasema kuiacha (huko kumswalia aliyefariki mbali) ni Sunnah. Na hata kuifanya kwake ni Sunnah, na hakuna njia yoyote inayowezekana ya wale baada ya Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) kubebewa na kuletewa kitanda cha Maiti aliyefia mbali ili waiswalie! Kwa hiyo kufanya Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam)  hivyo kulikuwa ni Makhsusi tu kwake yeye.

Na Imaam Ahmad katika moja ya riwaya zake mbili, ameonelea ikiwa ni mtu muhimu katika Uislam, au mwenye mchango mkubwa katika Diyn, anaweza kuswaliwa. Kasema, “Atakapokufa mtu mwema, aswaliwe.” Na muono huu pia baadhi ya ‘Ulamaa wa karibuni wameufuata.

Ama kilicho bora zaidi kwa muono wa ‘Ulamaa  wakubwa, ni kuwa, Swalaatul-Ghayb inamstahikia kishariy’ah yule ambaye amefariki katika nchi au eneo ambalo hakuna wa kumswalia (Hakuswaliwa huko alipofia). Ama yule aliyefariki na akaswaliwa huko alipofariki, basi hakuna haja ya kumswalia Swalaatul-ghayb. Na hili ndilo walilolikubali na kulipitisha ‘Ulamaa  na Ma-Imaam wakubwa wa zamani na wa sasa. Ndio msimamo wa   Al-Khatwaabiy, Ar-Rawayaaniy na amelieleza hilo Imaam Abuu Daawuwd katika Sunnan, mlango wa ‘Swalaah kwa Muislam aliye katika ardhi nyingine palipo na Washirikina.’

Na huu ndio msimamo wa Shaykhul-Islaam Ibn Taymiyyah na mwanafunzi wake hodari Ibnul Qayyim, Kasema Imaam Ibnul Qayyim katika kitabu chake maarufu cha Zaadul Ma’ad: “…Na amesema Shaykhul-Islaam Ibn Taymiyyah: Kilicho sahihi ni kuwa, ikiwa Aliyeghibu (maiti) aliyefia katika nchi au sehemu ambayo hakuswaliwa, basi ataswaliwa Swalaatul-ghayb. Kama alivyoswali Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) kumswalia An-Najaashiy kwani yeye alikufa akiwa miongoni Makafiri na hakuswaliwa. Na kama angekuwa ameswaliwa huko alipokuwa, basi asingeswaliwa tena kwani ile faradhi ya kumswalia maiti ingekuwa ishatekelezwa.”

Na kauli hiyo ya Shaykhul-Islaam kutoka kwa mwanafunzi wake, ndio pia katika riwaayah nyingine ya Imaam Ahmad.

Na muono huu unatiliwa nguvu sana na matukio wakati wa Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Makhalifa wake waongofu kwani walikufa wengi miongoni mwa Maswahaba katika sehemu na maeneo mbalimbali nje ya pale alipokuwa Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam)  na hata Makhalifa wake baadaye, na hakuna ushahidi unaoonyesha kuwa hao waliokufa maeneo ya mbali, waliswaliwa Swalaatul-ghayb. Na asili katika masuala ya ‘Ibaadah ni ‘Tawqiyfiyah’ kukifu hadi papatikane dalili ya kishariy’ah kuhusu kufanyika au kutofanyika kwa jambo.

Na Allaah Anajua zaidi


Tawheed yawafunda mahujaji watarajiwa

Taasisi ya Tawheed Development Network imeanza kutoa mafunzo kwa mahujaji watarajiwa ili kuwapa ufahamu wa ndani wa ibada ya hijja kabla ya kwenda huko Saudi Arabia

Akiongea katika Semina hiyo iliyofanyika katika ukumbi wa Karimjee, jijini Dar es swalaam, Mwenyekiti wa Kamati ya Hijja wa Taasisi hiyo ya Tawheed, Mhandisi Mussa Natty, amesema kuwa, wamekuwa wakitoa semina karibia kila wiki ili mahujaji wapate elimu ya hijja ya kutosha.

Mhandisi Natty alisema wanatoa mafunzo hayo kwa muda mrefu ili mahujaji hao watarajiwa wakienda Saudi Arabia wasipate tabu sana ya kutekeleza ibada hiyo. “Siye tunafanya semina nyingi kwa mahujaji wetu, na huwa tunafanya hivyo karibia kila wiki, na kutokana na hali hiyo ndiyo maana mahujaji wetu huwa hawapati tabu wakiwa huko Makka,” alisema mhandisi Natty.

Pia Mhandisi huyo alisema kuwa semina zinazotolewa na Tawheed si kwa ajili ya mahujaji wa taasisi hiyo bali mtu yoyote anaetarajiwa kwenda hijja anaruhusiwa kuhudhuria. Mhandisi Natty alisema kuwa semina hizo zinatolewa pia katika mikoa mingine huku akitoa wito kwa mahujaji hao watarajiwa kuhakikisha wanapata elimu ya kutosha ya ibada za hijja.

Profesa Assad

Naye muanzilishi wa taasisi hiyo, Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Fedha za Serikali, Profesa Mussa Assad amesema kuwa, taasisi hiyo inaendesha mambo yake kwa kuzingatia sheria za Kiislamu na ndiyo maana mambo yao yanakwenda vema.

“Siye tunafanya baishara na Mwenyezi Mungu, na ndiyo maana tunakikisha kila anayeenda hijja anajua mambo ya huko vizuri, na tunafanikiwa katika hilo,” alisema Prof. Assad.

Naye Mgeni rasmi katika semina hiyo, Meneja wa Shirika la Misaada Afrika (A.R.O), Samy Mohamed Elazeb, amewahimiza Waislamu kupupia ibada ya hijja akisema nguzo hiyo inapaswa kutiliwa mkazo kama nguzo zingine. “Waislamu lazima tujue ibada ya hijja ni muhimu kama zilivyo ibada zingine, hivyo hatuna budi kutumia kila kidogo tunachopata kwa ajili ya kupata uwezo wa kwenda Hijja,” alisema Meneja huyo.

Nao baadhi ya mahujaji watarajiwa wamesema semina hizo zimesaidia kuwapa elimu kubwa na wanaimani watatekeleza ibada yao wakiwa na ufahamu sahihi wa jinsi inavyofanywa ibada hiyo.



20-Hakika Shirki Ni Dhulma Kubwa Mno! - Isti’aadhah Kwa Asiyekuwa Allaah

  إِنَّ الشِّرْكَ لَظُلْمٌ عَظِيم   Hakika Shirki Ni Dhulma Kubwa Mno!   20 - Isti’aadhah  (Kuomba Kinga) Kwa Asiyekuwa Allaah   ...