Translate

Jumapili, 8 Desemba 2019

Buluwgh Al-Maraam: Kitabu Cha Chakula


كِتَاب اَلْأَطْعِمَةِ
01-Kitabu Cha Chakula



1134.

عَنْ أَبِي هُرَيْرَةَ  رضى الله عنه  عَنْ اَلنَّبِيِّ  صلى الله عليه وسلم قَالَ: {" كُلِّ ذِي نَابٍ مِنْ اَلسِّبَاعِ، فَأَكَلَهُ حَرَامٌ"} رَوَاهُ مُسْلِمٌ
وَأَخْرَجَهُ: مِنْ حَدِيثِ اِبْنِ عَبَّاسٍ بِلَفْظٍ: نَهَى.‏ وَزَادَ: {" وَكُلُّ ذِي مِخْلَبٍ مِنْ اَلطَّيْرِ"}
Kutoka kwa Abuu Hurayrah (رَضِيَ اللهُ عَنْهُ) amesema kuwa Nabiy (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) amesema: “Kila mnyama mwenye kuwinda kwa meno, kumla kwake ni haraam.”[1] [Imetolewa na Muslim]
Pia amepokea kutoka katika hadiyth ya ‘Abdullaah ibn ‘Abbaas kwa tamshi hili: “Amekataza.” Na akaongeza: “Na kila ndege anayewinda kwa kucha.”



1135.
وَعَنْ جَابِرٍ  رضى الله عنه  قَالَ: {نَهَى رَسُولُ اَللَّهِ  صلى الله عليه وسلم يَوْمَ خَيْبَرَ عَنْ لُحُومِ اَلْحُمُرِ اَلْأَهْلِيَّةِ، وَأْذَنْ فِي لُحُومِ اَلْخَيْلِ} مُتَّفَقٌ عَلَيْهِ.‏ ‏ وَفِي لَفْظِ اَلْبُخَارِيِّ: {وَرَخَّصَ}
Kutoka kwa Jaabir (رَضِيَ اللهُ عَنْهُ) amesema: “Rasuli wa Allaah (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) amekataza nyama za punda kihongwe (wa mjini)[2] siku ya Vita vya Khaybar, akaruhusu nyama za farasi.” [Al-Bukhaariy, Muslim]
Na katika tamshi la Bukhaariy: “Na ameruhusu.”



1136.
وَعَنْ اِبْنِ أَبِي أَوْفَى قَالَ: {غَزَوْنَا مَعَ رَسُولِ اَللَّهِ  صلى الله عليه وسلم سَبْعَ غَزَوَاتٍ، نَأْكُلُ اَلْجَرَادَ} مُتَّفَقٌ عَلَيْهِ
Kutoka kwa Ibn Abiy Awfaa amesema: “Tumepigana pamoja na Rasuli wa Allaah (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) vita saba, tunakula nzige.” [Al-Bukhaariy, Muslim]



1137.
وَعَنْ أَنَسٍ  فِي قِصَّةِ اَلْأَرْنَبِ  {قَالَ: فَذَبَحَهَا، فَبَعَثَ بِوَرِكِهَا إِلَى رَسُولِ اَللَّهِ  صلى الله عليه وسلم فَقَبِلَهُ} مُتَّفَقٌ عَلَيْهِ
Kutoka kwa Anas katika kisa cha sungura: “…akamchinja, akampelekea Rasuli wa Allaah (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) paja lake naye akalikubali.”[3] [Al-Bukhaariy, Muslim]



1138.
وَعَنْ اِبْنِ عَبَّاسٍ رَضِيَ اَللَّهُ عَنْهُمَا قَالَ: {نَهَى رَسُولُ اَللَّهِ  صلى الله عليه وسلم عَنْ قَتْلِ أَرْبَعِ مِنْ اَلدَّوَابِّ: اَلنَّمْلَةُ، وَالنَّحْلَةُ، وَالْهُدْهُدُ، وَالصُّرَدُ} رَوَاهُ أَحْمَدُ، وَأَبُو دَاوُدَ، وَصَحَّحَهُ اِبْنُ حِبَّانَ
Kutoka kwa Ibn ‘Abbaas (رَضِيَ اللهُ عَنْهُمَا) amesema: “Rasuli wa Allaah (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) amekataza kuuwa wanyama wanne sisimizi, nyuki, hudihudi na kipwe (ndege).” [Imetolewa na Ahmad na Abuu Daawuwd na akaisahihisha Ibn Hibbaan]



1139.
وَعَنْ اِبْنِ أَبِي عَمَّارٍ قَالَ: {قُلْتُ لِجَابِرٍ: اَلضَّبُعُ صَيْدُ هِيَ  ؟ قَالَ: نِعْمَ.‏ قُلْتُ: قَالَهُ رَسُولُ اَللَّهِ  صلى الله عليه وسلم قَالَ: نِعْمَ} رَوَاهُ أَحْمَدُ، وَالْأَرْبَعَةَ ‏ وَصَحَّحَهُ اَلْبُخَارِيُّ، وَابْنُ حِبَّانَ
Kutoka kwa Ibn Abiy ‘Ammaar[4] amesema: “Nilimuuliza Jaabir fisi analiwa? Akasema Ndiyo.[5] Nikasema Rasuli wa Allaah (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) amesema hivyo? Akasema ndiyo.” [Imetolewa na Ahmad na Al-Arba’ah (At-Tirmidhiy, An-Nasaaiy, Abuu Daawuwd, Ibn Maajah) na akaisahihisha Al-Bukhaariy na Ibn Hibbaan]



1140.
وَعَنْ اِبْنِ عُمَرَ  رضى الله عنه  ، أَنَّهُ سُئِلَ عَنْ اَلْقُنْفُذِ، فَقَالَ: ﴿ قُلْ لَا أَجدُ فِي مَا أُوحِيَ إِلَيَّ مُحَرَّمًا عَلَى طَاعِمٍ ﴾ ‏ فَقَالَ شَيْخٌ عِنْدَهُ: سَمِعْتَ أَبَا هُرَيْرَةَ يَقُولُ: {ذَكَرَ عِنْدَ اَلنَّبِيِّ  صلى الله عليه وسلم فَقَالَ: خِبْثَةَ مِنْ اَلْخَبَائِثِ"} أَخْرَجَهُ أَحْمَدُ، وَأَبُو دَاوُدَ، وَإِسْنَادُهُ ضَعِيفٌ
Kutoka kwa Ibn ‘Umar (رَضِيَ اللهُ عَنْهُ) amesema: “Aliulizwa kuhusu nungu akasema kwa kusoma Aayah hii: (Sema: Sipati katika yale niliyofunuliwa Wahyi kwangu kilichoharamishwa kwa mlaji…) Qur-aan 6: 145. Mzee mmoja aliye kwake akasema: ‘Nilimsikia Abuu Hurayrah anasema alitajwa mbele ya Nabiy (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) akasema: “Ni mchafu miongoni mwa vichafu’.” [Imetolewa na Ahmad na Abuu Daawuwd na isnaad yake ni dwaifu]



1141.
وَعَنْ اِبْنِ عُمَرَ رَضِيَ اَللَّهُ عَنْهُمَا قَالَ: {نَهَى رَسُولُ اَللَّهِ  صلى الله عليه وسلم عَنْ اَلْجَلَّالَةِ وَأَلْبَانِهَا} أَخْرَجَهُ اَلْأَرْبَعَةِ إِلَّا النَّسَائِيُّ، وَحَسَّنَهُ اَلتِّرْمِذِيُّ
Kutoka kwa Ibn ‘Umar (رَضِيَ اللهُ عَنْهُمَا) amesema: “Rasuli wa Allaah (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) amekataza kula mnyama anayekula uchafu na kunywa maziwa yake.”[6] [Imetolewa na Al-Arba’ah (At-Tirmidhiy, Abuu Daawuwd, Ibn Maajah) isipokuwa An-Nasaaiy, na akaisahihisha At-Tirmidhiy]



1142.
وَعَنْ أَبِي قَتَادَةٌ  رضى الله عنه  {فِي قِصَّةِ اَلْحِمَارِ اَلْوَحْشِيِّ فَأَكَلَ مِنْهُ اَلنَّبِيُّ  صلى الله عليه وسلم} مُتَّفَقٌ عَلَيْهِ
Kutoka kwa Abiy Qataadah (رَضِيَ اللهُ عَنْهُ) amesema katika kisa cha punda milia: “Nabiy (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) akamla.” [Al-Bukhaariy, Muslim]



1143.
وَعَنْ أَسْمَاءِ بِنْتِ أَبِي بَكْرٍ رَضِيَ اَللَّهُ عَنْهَا قَالَتْ: {نَحَرْنَا عَلَى عَهْدِ رَسُولِ اَللَّهِ  صلى الله عليه وسلم فَرَساً، فَأَكَلْنَاهُ} مُتَّفَقٌ عَلَيْهِ
Kutoka kwa Asmaa bint Abiy Bakr (رَضِيَ اللَّهُ عَنْهَا) amesema: “Katika zama za Rasuli wa Allaah (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) tulichinja farasi na tukamla.”[7] [Al-Bukhaariy, Muslim]



1144.
وَعَنْ اِبْنِ عَبَّاسٍ رَضِيَ اَللَّهُ عَنْهُمَا قَالَ: {أَكُلَّ اَلضَّبِّ عَلَى مَائِدَةِ رَسُولُ اَللَّهِ  صلى الله عليه وسلم} مُتَّفَقٌ عَلَيْهِ
Kutoka kwa Ibn ‘Abbaas (رَضِيَ اللهُ عَنْهُمَا) amesema: “Kenge aliliwa katika meza ya Rasuli wa Allaah (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ).”[8] [Al-Bukhaariy, Muslim]



1145.
وَعَنْ عَبْدِ اَلرَّحْمَنِ بْنِ عُثْمَانَ اَلْقُرَشِيُّ  رضى الله عنه  {أَنَّ طَبِيباً سَأَلَ رَسُولَ اَللَّهِ  صلى الله عليه وسلم  عَنْ اَلضِّفْدَعِ يَجْعَلُهَا فِي دَوَاءٍ، فَنَهَى عَنْ قَتْلِهَا} أَخْرَجَهُ أَحْمَدُ، وَصَحَّحَهُ اَلْحَاكِمُ
Kutoka kwa ‘Abdir-Rahmaan bin ‘Uthmaan Al-Qurashiyy (رَضِيَ اللهُ عَنْهُ) amesema: “Kuwa tabibu mmoja alimuuliza Rasuli wa Allaah (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ)  kuhusu chura kumfanya dawa. Nabiy (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) akakataza kuuwa chura.”[9] [Imetolewa na Ahmad na akaisahihisha Al-Haakim]
 
[1] Hadiyth hii inatoa maelezo kwamba kila mnyama mwenye kula mnyama na mwenye chonge ni haraam kuliwa. Vivyo kwa ndege anayenyofoa kiwindwa chake na kutumia ukucha ndege wa aina hiyo ni haraam kuliwa.
[2] Punda wa porinini (Pundamilia) ni halaal kuliwa.
[3] Sungura ni halaal kwa mujibu wa ‘Ulamaa wengi.
[4] Huyu ni ‘Abdur-Rahmaan bin ‘Abdillaah bin Abuu ‘Ammaar Al-Qurayshiy Al-Makkiy. Alikuwa ni Mwenye Taqwa na An-Nasaaiy anamthibitisha kuwa ni madhubuti.

[5] Hadiyth inaonesha kuwa kumla fisi kumeruhusiwa. Kulingana na baadhi ya Maimaam (kama vile Shaafi’y) ni halaal. Wengine kama Hanafiy wanaona kuwa ni haraam. Sababu ya kuwa kwake ni haraam ni kuwa anapenda kula nyama ya mwana Aadam na kuichimbia chini.
[6] Katika lugha ya Kiarabu Jallaala ina maana ya wanyama wenye kula kwenye vinyaa, uchafu, awe mnyama huyo ni ngamia jike, ng’ombe au mbuzi. Hata ikiwa ni halaal kutumia nyama au maziwa yake, hili ni jambo lenye tofauti ya rai kati ya Wanazuoni tokea awali. Baadhi ya Wanazuoni wanaona kwamba ni halaali na wengine wakiona kuwa ni haraam. Mnyama ataonekana kuwa ni Jallaala ikiwa kiasi kikubwa cha chakula chake ni uchafu wa mwana Aadam. Ama ikiwa kiwango kikubwa cha chakula chake ni kinachoruhusiwa basi hatoingia katika kundi hili la Jallaala.
[7] Kuna Hadiyth iliyotangulia kabla ya hii ikisisitiza kuwa kula farasi ni halaal. Na hadiyth hii inathibitisha jambo hilo hilo.
[8] Tunajifunza katika baadhi ya Hadiyth kuwa Dhabbu (mburukenge) analiwa, pamoja na kuwa Rasuli wa Allaah (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) mwenyewe hakumla, lakini Maswahaba wake walimla mbele yake katika meza yake. Alialikwa kumla lakini hakushiriki. Hakuwakataza watu kumla. Wanazuoni wanataja katika maandiko yao kuwa ni chukizo la Tanzihi (vile vilivyokuwa chini ya daraja la makatazo).

[9] Tunajifunza katika Hadiyth hii kuwa ni haraam kuuwa chura na kadhalika kumla.


01-Matendo Mema Na Athari Yake Katika Utajiri Na Ukunjufu Wa Rizki: Utangulizi

Utangulizi
 
Shukrani zote zinamstahiki Allaah, tunamtukuza na tunamtegemea, tunaomba msamaha kwake, tunataka kinga kwa Allaah kutokana na shari ya nafsi zetu na matendo maovu yetu aliyeongozwa na Allaah hakuna wa kumpoteza na aliyepotea hakuna wa kumuongoza. Tunashuhudia hakuna mola wa kuabudiwa kwa haki ila Allaah Pekee na tunashuhudia kwamba Muhammad ni Mja Wake na Mtume Wake.
 
Ama baada, ametaja Allaah rizki ya viumbe katika Qur-aan Tukufu sehemu nyingi, na hii ni dalili ya ukubwa wa Allaah Aliyetukuka na nguvu Zake, kwani Ameumba viumbe na Akatawalia rizki zao, pia ni dalili juu ya rehma kwa waja Wake na ukarimu Wake mkubwa, Naye ni Tajiri hahitaji kitu kwa viumbe, Naye ni Mtoaji kwa wote.
 
Amesema Allaah:
 
“Sikuwaumba majini na watu illa wapate kuniabudu, Sitaki kwao rizki wala Sitaki wanilishe, kwa yakini Allaah Ndiye Mtoaji wa riziki, Mwenye nguvu, madhubuti.” Adh-Dhariyaat: 57
 
Na Amejaalia AllaahAllaah matendo memayanaendana na imani na ni sharti ya kupata maisha mazuri na malipo mazuri zaidi Akhera, Amesema Allaah :
 
“Mwenye kutenda mema katika mwanaume au mwanamke naye ni Muumin, Tutamuhuisha maisha mema na Tutawalipa ujira wao kwa mema waliyokuwa wakiyatenda.”
 
Hakika maisha yamewahadaa watu wakatopea nafsi zao katika mali, wakawa wanakimbizana kutafuta rizki kwa njia yoyote iwe halali au haramu, wakafuata nafsi zao maisha yao yakawa dhalili, wakasahau kitabu cha Allaah na Sunnah, ambavyo ndani yake kuna ponyo (tatuzi) na kila kheri, navyo ni njia ya maisha mazuri na rizki pana na kheri nyingi katika dunia na Akhera.
 
Na sababu ya riziki na baraka ni matendo mema.


Jumamosi, 7 Desemba 2019

00-Hakika Shirki Ni Dhulma Kubwa Mno! Utangulizi


إِنَّ الشِّرْكَ لَظُلْمٌ عَظِيمٌ
 
Hakika Shirki Ni Dhulma Kubwa Mno!
 
 00-Utangulizi
 
 
 
بِسْمِ الله الرَّحْمنِ الرَّحِيم
 
الْحمْدُ لِلَّه وَالصَّلاةُ وَالسِّلامُ عَلى خَاتم الأنْبِيَاء وَالْمُرْسَلِين، الْمَبْعُوثُ رَحْمَةً لِلْعَالَمِين، مُحَمَّد وَعَلى آلِه وَأصْحابِه أجْمَعِين وَمَنْ تَبِعَهُمْ بِإِحْسَانٍ إِلَى يَوْمِ الدِّينِ.
Himdi Anastahiki Allaah, Swalaah na salaam zimfikie Nabiy na Rasuli wa mwisho, aliyetumwa awe rahmah kwa walimwengu, Muhammad, pamoja na ahli zake na Maswahaba zake wote, na wanaowafuata kwa ihsaan mpaka Siku ya Malipo.
 
 
Anasema Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa):
إِنَّ الشِّرْكَ لَظُلْمٌ عَظِيمٌ ﴿١٣﴾
hakika shirki ni dhulma kubwa mno [Luqmaan: 13]
 
 
Kinyume ya shirki ni Tawhiyd ambayo ni kumpwekesha Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) katika Rubuwbiyyah (Uola) Uluwhiyyah (‘ibaadah) Yake na katika Asmaa na Swifaat (Majina na Sifa nzuri) Zake.  Anasema Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa):
 
وَلَقَدْ أُوحِيَ إِلَيْكَ وَإِلَى الَّذِينَ مِن قَبْلِكَ لَئِنْ أَشْرَكْتَ لَيَحْبَطَنَّ عَمَلُكَ وَلَتَكُونَنَّ مِنَ الْخَاسِرِينَ﴿٦٥﴾
Kwa yakini umefunuliwa Wahy na kwa wale walio kabla yako kwamba: “Ukifanya shirki bila shaka zitaporomoka ‘amali zako na bila shaka utakuwa miongoni mwa waliokhasirika.”
 
بَلِ اللَّـهَ فَاعْبُدْ وَكُن مِّنَ الشَّاكِرِينَ﴿٦٦﴾
Bali Allaah Pekee mwabudu, na uwe miongoni mwa wenye kushukuru. [Az-Zumar: 65-66]
 
 
Waislamu wengi wako katika hali ya kumshirikisha Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa); wengine wakiwa wanatambua hatari zake, na wengine wakiwa hawatambui kuwa wanamshirikisha Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa), kwa sababu baadhi ya ‘amali zinazotendwa zinaonekana kuwa kama ni nzuri na hali zimeingia shirki ndani yake.
 
Imaam Muhammad bin ‘Abdil-Al-Wahhaab amesema katika Al-Qawaaid Al-Arba’: “Kwamba washirikina wa zama zetu ni waovu zaidi (shirki zao ni kubwa zaidi) kuliko washirikina wa awali, kwa sababu, wa awali walimshirikisha Allaah katika raha, lakini wakizitakasa ‘Ibaadah zao wakati wa shida. Ama washirikina wa sasa, shirki zao ni wakati wote, wakiwa katika raha au katika shida … na dalili ni kauli Yake Ta’aalaa:
 
فَإِذَا رَكِبُوا فِي الْفُلْكِ دَعَوُا اللَّـهَ مُخْلِصِينَ لَهُ الدِّينَ فَلَمَّا نَجَّاهُمْ إِلَى الْبَرِّ إِذَا هُمْ يُشْرِكُونَ ﴿٦٥﴾
Wanapopanda merikebu humwomba Allaah wakiwa wenye kumtakasia Yeye Dini, lakini Anapowaokoa katika nchi kavu, tahamaki hao wanamshirikisha. [Al-‘Ankabuwt: 65]
 
Kwa hiyo, kuna umuhimu mkubwa wa Waislamu kujifunza somo hili ili kujitahadharisha na hatari zake ili waweze kufunga milango na njia zote kubwa na ndogo za shirki. Makala hizi In Shaa Allaah zitaweza kutambulisha na kubainisha matendo mengi yanayomshirikisha Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) na namna ya kuyaepuka, ili Muislamu abakie katika amri ya Muumba wake Ambaye Ameamrisha kuabudiwa Yeye Pekee bila ya kumshirikisha. Kumshirikisha Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) ni katika dhambi kubwa mno kama alivyobainisha Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam):
 
عَنْ اِبْنِ مَسْعُودٍ ‏ رضى الله عنه ‏ قَالَ سَأَلْتُ رَسُولَ اَللَّهِ صلى الله عليه وسلم: أَيُّ اَلذَّنْبِ أَعْظَمُ؟ قَالَ: ((أَنْ تَجْعَلَ لِلَّهِ نِدًّا, وَهُوَ خَلَقَكَ))‏  
Imepokelewa kutoka kwa ibn Mas-‘uwd (Radhwiya Allaahu ‘anhu) ambaye amesema: “Nilimuuliza Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam): Je, dhambi ipi kubwa mno?” Akasema: ((Kumfanyia Allaah mlinganishi (wa kumshirikisha) na hali Yeye Amekuumba)) [Al-Bukhaariy, Muslim]
 
Nukta chache zifuatazo ni mukhtasari wa hatari za kumshirikisha Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa):
 
 
1. Shirki inaharibu ‘amali za mtu. Dhambi hii kubwa walitahadharishwa Rasuli wa Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) kwa ukali mno pale Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Anaposema:
 
وَلَوْ أَشْرَكُوا لَحَبِطَ عَنْهُم مَّا كَانُوا يَعْمَلُونَ ﴿٨٨﴾
Na kama wangemshirikisha bila shaka yangeporomoka yale waliyokuwa wakitenda. [Al-An’aam: 88]
 
 
2. Shirki ni dhambi pekee ambayo Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Haisamehe isipokuwa tu mtu akirudi kutubia Kwake. Anasema Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa):
 إِنَّ اللَّـهَ لَا يَغْفِرُ أَن يُشْرَكَ بِهِ وَيَغْفِرُ مَا دُونَ ذَٰلِكَ لِمَن يَشَاءُ ۚ وَمَن يُشْرِكْ بِاللَّـهِ فَقَدْ ضَلَّ ضَلَالًا بَعِيدًا﴿١١٦﴾
Hakika Allaah Haghufurii kushirikishwa; lakini Anaghufuria yasiyokuwa hayo kwa Amtakae. Na yeyote atakayemshirikisha Allaah basi kwa yakini amepotoka upotofu wa mbali. [An-Nisaa: 116]
 
 
3. Shirki inamtoa mtu nje ya Uislamu!
 
Imeelezwa shirki kuwa ni miongoni mwa matendo yanayomtoa mtu nje ya Uislamu, kama ilivyo katika Nawaaqidhw Al-Islaam cha Imaam Muhammad ibn Al-Wahhaab (Rahimahu-Allaah).
 
Na miongoni mwa mengi wanayotenda baadhi ya Waislamu ni kumwendea kahini anayetabiri mambo ya ghayb; elimu ambayo hakuna aijuae isipokuwa Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa). Hatari ya tendo hili ni kama alivyotahadharisha Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam):   
 
وَعَنْ أَبِي هُرَيْرَةَ (رَضِيَ اللَّهُ عَنْهُ) عَنِ النَّبِيِّ (صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ) قَالَ: ((مَنْ أَتَى كَاهِنًا، فَصَدَّقَهُ بِمَا يَقُولُ فَقَدْ كَفَرَ بِمَا أُنْزِلَ عَلَى مُحَمَّدٍ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ)) رَوَاهُ أَبُو دَاوُدَ
Imepokewa toka kwa Abu Hurayrah (Radhwiya Allaahu ‘anhu) kutoka kwa Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: ((Atakayemkaribia kahini na kuamini anayoyasema basi amekanusha aliyoteremshiwa Muhammad صلى الله عليه وآله وسلم))  [Abu Daawuwd]
 
 
4-Mwenye kumshirikisha Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) ni mwenye hatima mbaya mno ya makazi ya Moto. Ametahadharisha hilo Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa):
إِنَّهُ مَن يُشْرِكْ بِاللَّـهِ فَقَدْ حَرَّمَ اللَّـهُ عَلَيْهِ الْجَنَّةَ وَمَأْوَاهُ النَّارُ  وَمَا لِلظَّالِمِينَ مِنْ أَنصَارٍ﴿٧٢﴾
Hakika mwenye kumshirikisha Allaah bila shaka Allaah Atamharamishia Jannah, na makazi yake yatakuwa ni motoni. Na madhalimu hawatopata yeyote mwenye kunusuru.” [Al-Maaidah: 72]
 
Tunataraji tawfiyq ya Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) makala hizi ziwazidishie elimu yenye manufaa Waislamu kuhusiana na somo hili na Atuepushe sote kumshirikisha Yeye Subhaanahu wa Ta’aalaa. 
 


Dalili Za Watu Wa Matamanio Ni Moja Kati Ya Aina Tatu

Shukrani zote ni za Muumba wa ulimwengu. Kwa hakika, mwisho mwema ni wa wenye taqwa, hakuna uadui isipokuwa kwa madhalimu. Rahmah na amani ziwe juu ya yule aliyetumwa kama ni Rahmah kwa ulimwengu, watu wake wa nyumbani na Maswahaba zake.
Kwa kuendelea,

Kuna nukta tatu ambazo ni hoja kuu za kupotoka na kutoongoka kwa watu wa matamanio ambao wanaegemea matamanio yao na bila ya kuwa na ‘ilmu kuzua mambo ndani ya Dini ambayo hayamo.

Sababu hizi ni:

1-Kutokuwa na dalili kwa yale wanayoyazungumza;

2- Dalili zao hazina usahihi;
3- Dalili zao ni sahihi lakini hazinasibiani na hoja husika.

Kwa kuomba msaada wa Allaah na kumtegemea Yeye; nitachambua kwa kina hayo hapo juu:

Awali ya yote, Maana ya Uzushi

Uzushi ni kuanzisha kitu kipya ndani ya Dini ambacho mzushi anazua kwa utashi wake binafsi na bila ya kuwa na msingi kutoka katika Qur-aan au Sunnah kwa minajili ya kuwa karibu na Allaah. Kuanzisha mambo mapya ndani ya Dini ni dhambi kubwa. Ukweli ni kwamba, ni miongoni mwa madhambi (makubwa ni) kumfanya Allaah kuwa na mshirika kama ambavyo Allaah Mtukufu amesema:

أَمْ لَهُمْ شُرَكَاءُ شَرَعُوا لَهُم مِّنَ الدِّينِ مَا لَمْ يَأْذَن بِهِ اللَّـهُ ۚ

“Au Wanao washirika [wa Allaah] waliowawekea dini asiyoitolea Allaah ruhusa [Yake]?” [Ash-Shuwraa: 21].

Na kwa sababu ya hili, Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amefafanua uzushi kuwa “jambo ovu kabisa” kama alivyosema ndani ya Hadiyth ambayo imesimuliwa na Jaabir (Radhiya Allaahu ‘anhu):

إنُّ َشَرُّ الْأُمُورِ مُحْدَثَاتُهَا

“Kwa hakika, mambo yaliyo maovu kabisa ni yale mambo yanayozushwa.” [Muslim na pia katika Swahiyhul-Jaami’, 1353].

Na uzushi ni sehemu ya ushirikina (shirk). Hutamuona mzushi aliyebobea katika uzushi, isipokuwa yumo katika shirki aidha katika mambo (madhambi) makubwa au madogo. Au utamuona kutokuwa tofauti dhidi ya ushirikina na kutafuta hoja kwa watu wa shirk.

Sufyaan Ath-Thawriy amesema:

“Uzushi unapendwa zaidi na Ibliys kuliko upotofu. Mtu anaweza kuomba msamaha kwa kupotoka, lakini hawezi kuomba msamaha kwa uzushi.” [Chanzo; ‘Aqiydah Ya Ahlus-Sunnah cha Al-Lalakaa’iy 1/132].


Ndugu yangu mpenzi ambaye unasoma makala hii,

Elewa, tambua vyema na hifadhi yafuatayo na yachukue kama ni silaha yako dhidi ya wazushi:

Yeyote anayedai tendo la ‘ibaadah kuwa ni sahihi basi analazimika kuleta mbele dalili na kuthibitisha kwamba imethibiti katika Shari’ah. Jukumu la kuthibitisha litakuwa ni juu yake na si juu yako. Usihadaiwe kwa maneno ya mzushi “ushahidi gani kwamba lile na lile ni uzushi?”  Mjibu: “Ushahidi wako upi kwamba tendo hili ni la ki-Shari’ah”.

Na inatosha kwa watu wa Sunnah kudai ushahidi kwamba uzushi si sahihi, na kumwabudu Allaah katika hilo haliruhusiki, kwa sababu hakuna ushahidi katika hilo. Haiwezekani kupatikana dalili ya kila uzushi ili tupingane nayo, isipokuwa, kuna ushahidi wa jumla unaokataza uzushi wote kama ilivyo ndani ya Hadiyth iliyosimuliwa na Jaabir (Radhiya Allaahu ‘anhu):

كل بدعة ضلالة

“Kila uzushi ni upotofu.” [Muslim na pia katika Swahiyhul-Jaami’, 1353].

Na Hadiyth katika Al-Bukhaariy na Muslim:

مَنْ أَحْدَثَ فِي أَمْرِنَا هَذَا مَا لَيْسَ مِنْهُ فَهُوَ رَدٌّ

”Yeyote anayezua jambo katika jambo letu (Dini) ambalo halimo litakataliwa.”

Hivyo, kama mzushi akisema kwa uongo na usingiziaji: “Haikatazwi watu kumdhukuru Allaah katika mtindo ambao wameuanzisha wenyewe alimuradi tu haupingani na Shari’ah ya Kiislamu.”  Basi mwambie: “Umesema uongo bali imekatazwa hilo.” Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam)   aliposema:

إِيَّاكُمْ وَمُحْدَثَاتِ الأُمُورِ
“Tahadharini na mambo ya uzushi”

Na Allaah Mtukufu amekamilisha Dini na Akatimiza Neema kwa hivyo hairuhusiki kuzua dhikri wala Swalah wala kitu chengine chochote. Na mwambie (huyo mzushi): “Kwa nini useme alimuradi tu haipingani na Shari’ah hali ya kuwa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amekataza uzushi ambao ni kwenda kinyume na Shari’ah na misingi yake. Ungelitia akilini, hayo unayosema, basi usingelitamka tamko kama hilo lenye utata”


Ndugu yangu ambaye unasoma hii,

Namna gani wazushi wanajiamini kuchupa mpaka pale linapokuja suala la Allaah, Mtume Wake (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Dini ya Uislamu. Sikiliza yale anayosema mzushi:

“Kuonesha furaha kwa kuzaliwa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ni tendo la ki Shari’ah na kuna dalili nyingi kuhusu  hilo”

Subhaana Allaah! (Ametakasika Allaah!) Je ziko wapi hizo dalili nyingi?  Hawezi kutaja hata dalili moja juu ya madai yake kuwa ziko dalili nyingi.   Lakini lile alilonalo na matamanio yake ndivyo yanavyotumika, kutetea kwa uzushi katika madai mepesi bila ya kuweka wazi ushahidi. Lakini sisi tunaona kwamba Allaah Mtukufu Ameweka bayana dalili nyingi za Tawhiyd [Kumpwekesha Yeye], kwa Aayah za kawniyyah [kiulimwengu] na Shari’ah.  Ameweka pia dalili nyingi kusadikisha Wajumbe Wake na kuwaunga mkono kwa Aayah nyingi. Hali ya kuwa tunaona wazushi wakizua uzushi ambao hauna ushahidi na kubadili ukweli kwa uongo. Lile tu analoweza kusema ni “Kuna dalili nyingi.”


Msomaji wangu mwema,

Tambua, Allaah Anilinde mimi na wewe kutokana na uzushi na watu wake, kwamba watu wa uzushi na matamanio yake hawana ushahidi kwa uzushi wao na hii ndio njia yao ya jumla jamala pale wanapoliendea jambo lao la uzushi na upotofu.

Na iwapo watu watawakana na kuwataka wathibitishe ushahidi wao, basi watataja simulizi ambazo hazina usahihi kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam). Simulizi hizo ima za uongo au ambazo isnadi yake imekatika, au hawana ushahidi au wana ushahidi ambao si sahihi.

Hii ndio maana tunaona kwamba Wenye kuihami Dini na ‘Aqiydah sahihi wa zama zilizopita na sasa wamesimama kidete dhidi ya simulizi zisizo sahihi na zile zenye wasimulizi wepesi, wakathibitisha yale yaliyo sahihi na yale yasiyo sahihi. Na hii ni sifa nzuri ambayo watu wa Hadiyth wamekuwa nayo peke yao, si kama walivyo watu wa uzushi na wa matamanio ambao hawajui lipi ni sahihi na lipi lisilo sahihi. Wakathibitisha ‘Aqiydah na ‘ibaadah zao kwa masimulizi ya uongo na ubatilifu. Hivyo wamepotoka na wamepotoa wengine. Hizo ndizo sababu mbili za upotofu wa watu wa uzushi, kutokuwa na ushahidi na kuwa na thibati zisizokuwa sahihi.

Ama sababu ya tatu na hii ndio iliyokuwa ni hoja ya hatari zaidi kwa wapotofu wa watu wa upotofu na uzushi, matumizi yao ya dalili sahihi ambazo hazihusiani katika hoja zao au wanazo dalili lakini zipo nje ya mada.


Kwa ndugu yangu ambaye anasoma hii,

Tambua, Allaah Awe na Rahmah juu yangu na yako; wengi katika viumbe vya Allaah miongoni mwa wanaadamu na majini wamezifasiri sivyo Aayah kisha baadaye wakaja na uzushi wao na upotofu. Pamoja na hayo, hoja ya kuwa na mapenzi kwa mawalii na waja wema wao wakaanza kuwaabudu ghairi ya Allaah. Na hoja ya kuwatukuza Ahlul-Bayt na kuwaitakidi yasiyostahiki isipokuwa kwa Allaah. Na hoja ya kumdhukuru Allaah na kumswalia Mtume wakazusha Mawlid, kuimba mashairi, kucheza na nyimbo za jazba; kupandisha hamasa wakidai kwamba ni katika ‘ibaadah kwa Allaah.  

Na hoja ya Jihaad wakamwaga damu ya wasio na hatia. Na hoja ya kumtukuza Muumba kwa kumfananisha Naye kwa viumbe Vyake, wakaanza kuzikanusha Sifa Zake kwa hoja ya kuwa na wivu wa Dini, wakawakufurisha Waislamu kuwatoa nje ya Dini, na kwenda kinyume na mikataba na makubaliano. Na hoja ya kujifanya wachaji na kujiweka mbali na machafu, wakaharamisha mazuri Aliyoyahalisha Allaah kwa waja Wake. Na hoja ya kutafuta mibadala, wakazua ndani ya Dini yale ambayo Allaah Hajaruhusu.

Wanatumia dalili zisizokatazwa bila ya vikwazo, dalili zisizojieleza bila ya kuwa na maelezo, na wanatumia dalili za jumla bila ya kuzihusisha. Wametumia Shari’ah za wale ambao walikuwa kabla yetu badala ya Shari’ah zetu. Na hili ndilo ambalo Ibliys amefanya kabla yao pale aliposema:

  أَنَا خَيْرٌ مِّنْهُ خَلَقْتَنِي مِن نَّارٍ وَخَلَقْتَهُ مِن طِينٍ  

“Mimi ni bora kuliko yeye. (Mimi) Umeniumba kwa moto, naye Umemuumba kwa udongo.” [Al-A’raaf: 12].

Kisha baada yake walikuwa ni makafiri wa awali na kusema:

لَوْ شَاءَ اللَّـهُ مَا أَشْرَكْنَا وَلَا آبَاؤُنَا

“Angalipenda Allaah tusingalimshirikisha sisi wala baba zetu.” [Al-An’aam: 148].

Hivyo kuwa muangalifu, Allaah Akulinde, ni namna gani maneno ya wale wanaokusanya pamoja ukweli na uongo. Ni kweli kwamba Ibliys aliumbwa kutokana na moto, na Aadam ('Alayhis Salaam) aliumbwa kutokana na udongo, lakini haikubaliki kutumia kwake Ibliys kwa Aayah hizi kama ni ushahidi kwamba yeye ni bora kuliko Aadam.

Na makafiri walisema: “Angalipenda Allaah tusingalimshirikisha” na hili ni kweli. Kwa sababu Atakalo Allaah huwa, na Asilolitaka haliwezekani. Na hakuna yeyote atakayeweza kumshirikisha bila ya uwezo wa Allaah, lakini hii ni kuruhusu Kwake [iwezekane] kwa Qadar [makadirio] Yake ya kawniyyah na si kwamba Ameiwekea ruhusa katika Shari’ah.  Kwa hilo, ingawa Allaah Amemwezesha kafiri kutokuamini, lakini Hakuruhusu hivyo wala Haridhii kwalo kama Anavyosema:  

إِن تَكْفُرُوا فَإِنَّ اللَّـهَ غَنِيٌّ عَنكُمْ ۖ وَلَا يَرْضَىٰ لِعِبَادِهِ الْكُفْرَ ۖ  

“Mkikufuru, basi Allaah hana haja nanyi; lakini Haridhii kufuru kwa waja Wake.” [Az-Zumar: 7].

Na ndivyo ilivyo kwa wazushi, anachanganya haki pamoja na batili. Lau ingelikuwa uzushi wake ni ubatili mtupu asingeliweza kuusambaza. Anafanya tendo la Ahlul-Kitaab (Mayahudi na Manaswara) ambao wamechanganya haki na batili, au tendo la mfanya biashara anayeghushi kwa kuchanganya bidhaa mbaya pamoja na bidhaa nzuri. Na laiti angeliweka wazi bidhaa zake mbovu, asingeliweza kuiuza na kupata pesa mara moja.

Basi tahadharini enyi watu wa Tawhiyd na Sunnah, tahadharini na njia za watu wa uzushi na matamanio. Na ni lazima mpigane nao kwa silaha ya ‘ilmu yenye kunufaisha. Ni uzuri ulioje maneno ya Shaykhul-Islaam al-Mujaddid Muhammad bin ‘Abdil-Wahhaab (Rahimahu Allaah) katika katika Kashf Shubuhaat uk. 11:

“Mjinga miongoni mwa watu wa Tawhiyd anaweza kuwashinda maelfu ya wasomi wa kikafiri kama Allaah Mtukufu alivyosema:

وَإِنَّ جُندَنَا لَهُمُ الْغَالِبُونَ
“Na kwa hakika jeshi Letu ndilo litakaloshinda.” [As-Swaafaat: 173,

Amesema kweli (Rahimahu Allaah), kwani mzushi hatoweza kumkabili mtu wa Sunnah. Atahiyari kumkwepa kama anavyomkwepa mbwa mwitu. Mzushi ataitema sumu yake maeneo mengi na hata nyuma za kuta. Utawadhania wako pamoja lakini nyoyo zao zimegawanyika; makundi, madhehebu na ‘Aqiydah mbali mbali. Hawawatendi ila kizani, na mwishowe hudhihirika mambo yao. Huenda watu walikuwa hawatambui uhakika wao hapo zamani, lakini watu wa leo wameziona kanda na picha zao walizopiga wenyewe wakifanya ‘matambiko’ au wanazoona ni ‘ibaadah kwao. Tunamuomba Allaah kutughufuria na kutuokoa.


Muhtasari

Sababu za kupotoka kwa watu wa uzushi ni aidha; kutokuwa na dalili, au kuwa na dalili ambayo si sahihi au kuwa na dalili sahihi ambayo haiendani pamoja na hoja zao.

Ninamuomba Allaah Mtukufu Anithibitishe katika haki bayana pamoja na kila Sunni (Ahlus Sunnah wal Jama’aah) na Atuepushe na fitna za dhahiri na zilofichika. Na Sifa Njema ni za Allaah mwanzo na mwisho wake. Na Swalah na amani ziwe juu ya Mjumbe Wake (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), nyumba yake na Maswahaba zake.



Katika Uislam - 5 Masuala Kumi Yanayoeleweka Vibaya Katika Uislam - 5

Suala Nambari 5 Linaloeleweka Vibaya


Uislamu unamkataa Yesu kwa sababu:
·                     Yesu hakubaliki kuwa ni ‘mtoto wa Mungu’

JIBU:
Zote mbili; Qur-aan na Sunnah zinatufundisha kwa msisitizo na bila ya wasiwasi kwamba Muumba Anatambua tamko la Utatu kuwa ni uongo ulio mkubwa mno. Qur-aan inaeleza (iliyotafsiriwa):
 [19:88-93]]

Hata hivyo, suala hilo linaloeleweka vibaya haliendani na hoja zinazotolewa hapo juu kwamba Yesu (‘Iysaa) anakataliwa (moja kwa moja). Ni vyema kutanabahisha kwa kusema kwamba inakataliwa kumueleza Yesu (‘Iysaa) kama ni ‘mtoto wa Mungu’. Kwa kuwa ni Mtume wa Allaah, Yesu anatunukiwa cheo chake cha heshima namna walivyopewa Mitume wote, kama ambavyo Aayah ifuatayo inavyotamka (tafsiri):
 [2:136]

Itaendelea In Shaa Allaah...


20-Hakika Shirki Ni Dhulma Kubwa Mno! - Isti’aadhah Kwa Asiyekuwa Allaah

  إِنَّ الشِّرْكَ لَظُلْمٌ عَظِيم   Hakika Shirki Ni Dhulma Kubwa Mno!   20 - Isti’aadhah  (Kuomba Kinga) Kwa Asiyekuwa Allaah   ...