Lu-ulu-un-Manthuwrun
(Mkusanyiko Wa Hadiyth Mbali Mbali Na Mafunzo Yake)
Hadiyth Ya 49
Swalaah Husafisha Madhambi Kama Anavyojisafisha Mtu Anapooga
عَنْ جَابِرٍ (رضي الله عنه) قَالَ: قَالَ رَسُولُ اللَّهِ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ: ((مَثَلُ الصَّلَوَاتِ الْخَمْسِ كَمَثَلِ نَهْرٍ جَارٍ غَمْرٍ عَلَى بَابِ أَحَدِكُمْ يَغْتَسِلُ مِنْهُ كُلَّ يَوْمٍ خَمْسَ مَرَّاتٍ)) مسلم
Kutoka kwa Jaabir (رضي الله عنه) kwamba Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema: ((Mfano wa Swalaah tano ni kama mfano wa mto uliojaa maji mengi upitao mbele ya mlango wa mmoja wenu, anaoga mara tano kwa siku)). [Muslim]
Mafunzo Na Mwongozo:
1. Bainisho la umuhimu wa Swalaah za fardhi, na Aayah nyingi zimetaja maamrisho ya Swalaah.
[Rejea: An-Nisaa (4: 103), Al-Baqarah (2: 43), An-Nuwr (24: 56), Ar-Ruwm (30: 31)].
2. Swalaah husafisha madhambi madogo madogo kama maji yanavyoondosha uchafu mwilini.
وَأَقِمِ الصَّلَاةَ طَرَفَيِ النَّهَارِ وَزُلَفًا مِّنَ اللَّيْلِ ۚ إِنَّ الْحَسَنَاتِ يُذْهِبْنَ السَّيِّئَاتِ ۚ ذَٰلِكَ ذِكْرَىٰ لِلذَّاكِرِينَ﴿١١٤﴾
Na simamisha Swalaah katika ncha mbili za mchana na sehemu ya kwanza ya usiku; hakika mema yanaondosha maovu. Hivyo ni ukumbusho kwa wanaokumbuka. [Huwd (11: 114)]
3. Muumin anahifadhika kutenda maasi, kwani siku nzima kuna vipindi vya Swalaah vinavyomsubiri asimamishe Swalaah, kwa hiyo Swalaah ni kinga ya maasi. [Al-‘Ankabuwt (29: 45)].
4. Hadiyth inatoa mfano miongoni mwa mifano ya kulingana, kubainisha, na kufahamisha jambo fulani.
5. Hikma ya maneno ya Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) katika kufunza Maswahaba zake kwa kupiga mifano mizuri iliyo sahali kufahamika kwao na kwetu sisi tunaposoma Hadiyth kama hizi.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni