Adabu Kabla ya Kuingia Msikitini
Assallaam Aleykum WarahmatulLaah Wabarakatuh
1. Muislamu anapaswa kutambua kuwa lengo kuu la Misikiti ni kwa ajili ya kuabudiwa Allaah (ndani yake. Kwa kuzingatia hili, inafaa kwa mtu kuweka niyyah sahihi kabla ya kuingia katika nyumba hii ya ‘ibaadah.
Allaah (Azza wa Jalla) amesema katika Qur-aan kuhusiana na Misikiti:
فِي بُيُوتٍ أَذِنَ اللَّـهُ أَن تُرْفَعَ وَيُذْكَرَ فِيهَا اسْمُهُ يُسَبِّحُ لَهُ فِيهَا بِالْغُدُوِّ وَالْآصَالِ
“Katika nyumba (Misikiti) Ameidhinisha Allaah zitukuzwe, na litajwe humo Jina Lake; humsabihi Pekee humo asubuhi na jioni.” [An-Nuwr: 36].
Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema kuhusiana na Misikiti:
“Kwa hakika nyumba za Allaah zimejengwa kwa ajili ya kumkumbuka (kumtaja) Allaah, kuswalia, na kusomea Qur-aan.” [Swahiyh Muslim].
Kwa hiyo ni wajibu kwa Muislamu kutambua kuwa lengo la Misikiti si kwa ajili ya mikusanyiko ya kijamii na mazungumzo (yasiyohusiana na Msikiti), bali ni eneo lililoteuliwa na Allaah (Azza wa Jalla) kwa ajili ya kuabudiwa Yeye, kutajwa jina Lake, na kusomwa kitabu Chake. Mtu anyeingia Msikitini na akatoka, anatakiwa kujihisi ongezeko hasa la kiimani. Baada ya kuondoka Msikitini, kiwango chake cha imani na taqwa (Uchaji Allaah) kinatakiwa kuwa juu kuliko mwanzoni alipoingia Msikitini. Allaah (Azza wa Jalla) Amesema katika Kitabu Chake kitukufu:
إِنَّ الصَّلَاةَ تَنْهَىٰ عَنِ الْفَحْشَاءِ وَالْمُنكَرِ
“Kwa hakika Swalah huzuilia (mtu kutokana na) mambo maovu na machafu (munkar)” [Al-‘Ankabuwt: 45].
2. Ni lazima kwa mtu anayetaka kwenda Msikitini kuhakikisha kuwa hana (hatoi) harufu mbaya. Hii ni kutokana na kauli ya Allaah katika Qur-aan:
يَا بَنِي آدَمَ خُذُوا زِينَتَكُمْ عِندَ كُلِّ مَسْجِدٍ
“Enyi wana Aadam! Chukueni mapambo yenu katika kila Masjid (mnapokwenda Misikitini kwa ajili ya ‘ibaadah)” [Al-A‘raaf: 31].
Pia, maneno ya Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam):
“Yeyote aliyekula vitunguu vyeupe (vitunguu thaumu) au vitunguu vya kawaida (vitunguu maji) asihudhurie Msikitini.” [Swahiyh Al-Bukhaariy na Swahiyh Muslim].
Ushahidi tulioutoa hapo juu unatudhihirishia kuwa ni wajibu kwa Muislamu kuhakikisha kuwa hatowaudhi watu wengine kutokana na harufu (mbaya) ya mwili (wake) anapohudhuria Msikitini, na kwa hiyo, anapaswa kujitahidi kadiri awezavyo kujisafisha kabla ya kuhudhuria Swalah katika nyumba ya Allaah. Wanachuoni wa Kiislamu wanasisitiza juu ya katazo hilo tulilolitaja na kwamba linaenea zaidi pia kwa uvutaji sigara, kutokana na harufu mbaya ya sigara anayobaki nayo mvuta sigara mara tu amalizapo kuvuta sigara. Harufu hii (ya sigara), bila shaka, ina madhara na huwasumbua wanaoswali katika Msikiti, na pia huwasumbua (huwaumiza) Malaika. Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:
“Kwa hakika Malaika huumia kwa kile ambacho huwaumiza bin Aadam.”[Swahiyh Muslim].
3. Wakati wa kwenda Msikitini, haifai kwa mtu kuharakisha na kukimbia, bali aende kwa mwendo wa kawaida. Hii ni kutokana na kauli ya Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam):
“Utakaposikia adhana (mwito wa Swalah) utembee kuelekea Msikitini katika hali ya utulivu, kwa amani, na usiharakishe. Utakachodiriki (katika Swalah), basi swali, na kile ambacho utakikosa, kimalizie.”[Swahiyh Al-Bukhaariy na Swahiyh Muslim].
Na Allaah anajua zaidi
from fisabilillaah.com http://bit.ly/2VktKJO
via IFTTT
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni